WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaasa wanaume wa wilaya ya Tarime
kujiepusha na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto pamoja na kuachana
na kilimo cha bangi.
Alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumatano, Januari 17, 2018) wakati
akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa
Serengeti, wilayani Tarime.
Waziri Mkuu alisema vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na
watoto pamoja na kilimo cha bangi vinaitia doa wilaya hiyo, hivyo hawana budi wakaepukana
navyo.
“Serikali inakemea vitendo vya ukatili, achaneni navyo. Mtu
unamchapa mtoto makofi hadi anazimia, kitendo hicho hakiwezi kuvumilika na pia
kinaitia doa wilaya yenu.”
Wakati Huo huo, Waziri Mkuu alimuagiza
Mkuu wa wilaya hiyo, Bw. Glorious Luoga kuendelea na msako wa mashamba ya bangi
na mirungi na kuchukua hatua kwa watakaobainika kuendesha kilimo hicho.
Alisema ardhi ya wilaya hiyo ni nzuri na inahimili kilimo cha mazao
mbalimbali ya chakula na biashara kama mahindi, mihogo, ndizi, kahawa, pamba,
ni marufuku kulima bangi.
Pia Waziri Mkuu aliagiza kuchukuliwa hatua kwa wakandarasi
waliotekeleza ujenzi wa maji mkoani Mara kwa sababu miradi hiyo wameijenga
chini ya kiwango.
Waziri Mkuu aliyasema hayo baada ya kupokea malalamiko ya
wananchi kupitia mabango wakidai kutonufaika na miradi ya maji katika maeneo
yao licha ya Serikali kutoa fedha.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.