Tuesday, May 21, 2019

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI WAZIRI MKUU AONGOZA MAZISHI YA ASKOFU MMOLE MTWARA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania wote wamuenzi marehemu Askofu Mstaafu Gaberiel Mmole (80) wa Jimbo Katoliki Mtwara kwa wema, upole  na utumishi mwema aliouonesha wakati wote wa maisha yake.

Ametoa wito huo leo (Jumanne, Mei 21, 2019) wakati wa mazishi ya Askofu Mmole yaliyofanyika katika Kanisa Katoliki Mtwara na kuhudhuriwa na viongozi, waumini wa Kanisa Katoliki pamoja na wakazi wa mkoa wa Mtwara 

Askofu Mmole alizaliwa Januari Mosi, 1939 katika Parokia ya Nangoo, ambapo alibatizwa na kupata kipaimara Oktoba 5, 1952. Mwaka 1971 alipata daraja ya upadre na kuwa Askofu kuanzia mwaka 1988, alifariki Mei 15, 2019 Mkoani Mtwara baada ya kuugua kwa muda mrefu. 

Maeneo aliyoyatumikia tangu apate daraja la padri ni Paroko msaidizi wa Mnero (1972), Pastoral Institute GABA-Uganda (1973), Gombera Namupa seminari (1974 hadi Mei 1988), alitangazwa kuwa askofu wa Jimbo la Mtwara Machi 12, 1988 na alisimikwa kuwa askofu wa Jimbo la Mtwara Mei 25, 1988.

Mwaka 1951 hadi 1954 alipata elimu ya singi katika shule ya msingi Ndanda, 1955 alisoma Nyangao Middle School, 1956 akahamia Lukuledi ambako alihitimu 1958. Alienda chuo cha ualimu Peramiho 1959 hadi 1960, ambapo 1962 alijiunga na seminari ndogo ya Namupa na alihitimu 1964. 

1965 hadi 1966 alichukua masomo ya falsafa kwenye seminari kuu ya Peramiho na mwaka 1967 hadi 1971 alichukua masomo ya theolojia katika seminari hiyo hiyo ya Peramiho. 1971 alifanya mitihani ya Baccalaureate inayotoka chuo kikuu cha Kipapa Urbaniana Roma na kupata shahada ya theolojia.

Ibada ya mazishi imeongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo la Songea, Mhashamu Askofu Damian Dallu ambaye alitumia muda huo kuwaasa Watanzania kuishi katika maadili mema na kuheshimiana.

Waziri Mkuu amesema enzi za uhai wake Askofu Mmole alitoa kipaumbele katika masuala muhimu ya maendeleo ya jamii ikiwemo elimu ambapo alisaidia sana watawa waliomaliza darasa la saba na kuwasaidia wajiunge na shule za sekondari.

“Hata uanzishwaji wa chuo kikuu cha STEMMUCO ambacho ni tawi la SAUT hapa Mtwara ni moja ya jitihada zake alizozifanya katika kuhakikisha anawapa elimu bora vijana na jamii. 

Kifo chake ni pigo kubwa kwa Taifa kwa sababu tumepoteza kiongozi wa kiroho aliyesimamia kwa uadilifu ustawi wa jamii ya Kitanzania.”

Kwa upande wake, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Mhashamu Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Kuu la Mbeya amesema wamepata simanzi kubwa kufuatia kifo cha Askofu Mmole kwani walitegemea hekima zake katika Baraza la Maaskofu.

Ameongeza kuwa Askofu Mmole alikuwa kielelezo cha dhamira njema na alilitumikia kanisa katika hali yoyote, hivyo yatupasa kumuombea apumzike kwa amani.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwaaliwashukuru viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini mkoani Mtwara kutokana kwa ushirikiano mzuri anaopata unaomwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Mazishi hayo yamehudhuriwa na maelfu ya wananchi, maaskofu wa majimbo mbalimbali nchini, Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa na mkewe Mama Anna Mkapa, Waziri wa Nchi OR-Utumishi na Utawala Bora Mheshimiwa Huruma George Mkuchika.
Read More

MAJALIWA AIWAKILISHA SERIKALI KATIKA MAZISHI YA ASKOFU MSTAAFU WA JIMBO KATOLIKI LA MTWARA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza katika  Mazishi ya Askofu Mstaafu wa Jimbo Katoliki la Mtwara,Mhashamu Gebriel Mmole kwenye Kanisa Kuu la Watakatifu Wote mjini Mtwara, Mei 21, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpa pole Askofu wa Jimbo Katoliki la Mtwara, Titus Joseph Mdoe katika mazishi ya Askofu Mstaafu wa Jimbo Katolki la Mtwara, Mhashamu Gabriel Mmole yaliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Watakatifu Wote mjini Mtwara, Mei 21, 2019.
Waombolezaji wakiuweka kaburini mwili wa Askofu Mstaafu wa Jimbo Katoliki la Mtwara, Mhashamu Gabriel Mmole katika mazishi yaliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Watakatifu  Wote mjini Mtwara, Mei 21, 2019.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka udongo  kwenye kaburi la Askofu Mstaafu wa Jimbo la Mtwara, Mhashamu Gebriel Mmole katika mazishi yaliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Watakatifu Wote mjini  Mtwara, Mei 21, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa  wakishiriki katika Ibada ya mazishi ya Askofu Mstaafu wa Jimbo Katoloki la Mtwara, Mhashamu, Gabriel Mmole  iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo la Mtwara,Titus  Mdoe (kushoto)  kwenye Kanisa Kuu la Watakatifu Wote mjini Mtwara, Mei 21, 2019.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akiweka shada la maua kwenye kaburi la Askofu Mstaafu wa Jimbo Katoliki la Mtwara, Mhashamu, Gabriel Mmole katika mazishi yaliyofanyika kwenye Kanisa la Watakatifu Wote mjini Mtwara, Mei 21, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha Askofu Mstaafu wa Jimbo Katoliki la Mtwara, Mhashamu Gabriel Mmole katika mazishi yaliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Watakatifu Wote Mjini Mtwara, Mei 21, 2019. Kulia ni Askofu wa Jimbo la Geita na  Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Flavian Kasalla.

Read More

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA ZOEZI LA KUPIMA UTAYARI WA KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MLIPUKO MIPAKANI KWA DHANA YA AFYA MOJA

Mkurugenzi wa Kitengo cha Dharura na Majanga, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto, Dkt. Eliasi Kwesi, akiendesha kikao leo Jijini Dodoma,  cha maandalizi ya  zoezi la Kupima Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani, litakalofanyika mpakani mwa Tanzania na Kenya kwenye eneo la Namanga,  kuanzia tarehe 11 hadi 14 Juni.

Na. OWM, DODOMA.

Kufuatia nchi za Kanda ya Afrika Mashariki kuwa katika hatari ya kuathirika na magonjwa ya mlipuko kama Homa ya Bonde la Ufa, Mafua Makali ya Ndege na Ebola, na kwa kuwa magonjwa hayo husambaa kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine, Tanzania inatarajia kuandaa zoezi la Kupima Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani, litakalofanyika mpakani mwa Tanzania na Kenya kwenye eneo la Namanga,  kuanzia tarehe 11 hadi 14 Juni mwaka huu.

Zoezi hilo, litazingatia Dhana ya Afya moja ambayo hujumuisha sekta ya afya ya binadamu, wanyamapori, mifugo na  mazingira katika kujiandaa, kufuatilia  na kukabili magonjwa yanayoathiri binadamu. Jumla ya washiriki 150 ambao watatoka Sekretarieti ya Afrika Mashariki, Kenya na Tanzania washiriki 130 kutoka ngazi ya taifa, mkoa na wilaya katika mpaka wa Namanga; pamoja na nchi nyingine wanachama ambapo watakuwa watazamaji ikiwa ni Uganda, Burundi, Rwanda na Sudani Kusini wanatarajiwa kushiriki zoezi hilo.

Akiongea, mjini Dodoma leo, katika kikao cha maandalizi ya zoezi hilo kwa ngazi ya Taifa, Mkurugenzi wa Kitengo cha Dharura na Majanga, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto, Dkt. Eliasi Kwesi,  amefafanua kuwa zoezi  hilo linalenga kufanyia majaribio ya utekelezaji wa Mipango ya Dharura ya Taifa na Kanda, Miongozo ya Utendaji na kuwapa washiriki fursa ya kujifunza namna sekta zingine zinavyotekeleza majukumu katika kuzuia na kupunguza madhara pamoja na kujiandaa kukabiliana na maafa ya magonjwa ya mlipuko.

“Zoezi hili tunalenga kutathmini utaratibu wa kutuma kikosi cha taifa cha dharura cha kukabili lakini pia  kuhakiki matumizi ya maabara zinazohamishika, kutathmini uwezo wa uchunguzi na usimamizi wa magonjwa ya mlipuko kwa vituo vilivyopo mpakani kwa magonjwa ya mifugo na binadamu; kupima hatua za kujiandaa kukabiliana katika viwanja vya kimataifa vya Jomo Kenyatta na Kilimanjaro.” Alisisitiza Dkt. Kwesi.

Kwesi alibainisha kuwa zoezi litaandaliwa kwa kuhusisha mlipuko wa virusi vinavyoshabihiana na Homa ya Bonde la Ufa katika eneo la mpakani, ambapo washiriki watahitajika kuonesha utayari wa kukabiliana na ugonjwa huo kwa kuzingatia mfumo wa Afya Moja.

Zoezi hilo linafanyika nchini Tanzania kufuatia Kikao cha 11 cha Kawaida cha Mawaziri wa Sekta ya Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofanyika mwezi Machi, 2015, ambapo kilielekeza Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuandaa Zoezi la Nadharia la kukabiliana na magonjwa ya mlipuko katika mpaka wa Tanzania na Kenya kwenye eneo la Namanga. Zoezi hilo ambalo litafanyika hapa nchini  linaratibiwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na nchi wanachama kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani la GIZ na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa.
MWISHO.

Baadhi ya Wataalamu kutoka Wizara, Taasisi na Idara za serikali wakifuatilia kikao leo Jijini Dodoma,  cha maandalizi ya  zoezi la Kupima Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani, litakalofanyika mpakani mwa Tanzania na Kenya kwenye eneo la Namanga,  kuanzia tarehe 11 hadi 14 Juni. 2019.
Baadhi ya Wataalamu kutoka Wizara, Taasisi na Idara za serikali wakifuatilia kikao leo Jijini Dodoma,  cha maandalizi ya  zoezi la Kupima Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani, litakalofanyika mpakani mwa Tanzania na Kenya kwenye eneo la Namanga,  kuanzia tarehe 11 hadi 14 Juni. 2019.
Baadhi ya Wataalamu kutoka Wizara, Taasisi na Idara za serikali wakifuatilia kikao leo Jijini Dodoma,  cha maandalizi ya  zoezi la Kupima Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani, litakalofanyika mpakani mwa Tanzania na Kenya kwenye eneo la Namanga,  kuanzia tarehe 11 hadi 14 Juni. 2019.

Read More

Sunday, May 19, 2019

WADAU WAOMBWA KUJITOKEZA KUSAIDIA MAANDALIZI YA MASHINDANO YA SOKA KWA WENYE ULEMAVU AFRIKA MASHARIKI

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati waliokaa) pamoja na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye ulemavu Mhe. Stella Ikupa (wa pili kutoka kushoto waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wabungu wa kamati iliyojitolea kuhamasisha ushiriki wa Watanzania katika mashindano hayo, mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)kuhusu mashindano ya Shirikisho la mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu Afrika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika  mwishoni mwa mwezi Juni mwaka na kushirikisha nchi 5 wanachama.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri mkuu Wenye Ulemavu mhe. Stella Ikupa akisisitiza jambo wakati wa mkutano wa waandishi wa habari  kuhusu mashindano ya Shirikisho la mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu Afrika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika  mwishoni mwa mwezi Juni mwaka na kushirikisha nchi 5 wanachama wakati wa mkutano huo.
Mbunge wa Sengerema mhe. William Ngeleja,ambaye pia ni mwenyekiti wa klabu ya michezo ya Bunge akichangia jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari ili kuhamasisha jamii kushiriki katika mashindano ya Shirikisho la mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu Afrika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika  mwishoni mwa mwezi Juni mwaka na kushirikisha nchi 5 wanachama.

Read More

Thursday, May 9, 2019

ASKOFU MKUU DK. SHOO AWAONYA VIONGOZI, MATAJIRI

* Asema wasitumie nafasi zao kunyanyasa wengine, akemea ubaguzi
*Ataka wajitoe kusaidia wasionacho kama njia ya kumuenzi Dk. Mengi

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Mkuu Dk. Ferdinand Shoo amewaonya viongozi wa Tanzania na kuwataka watumie nafasi zao kuwasaidia wengine hasa wale wenye uhitaji.

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Mei 9, 2019) wakati akitoa mahubiri kwenye ibada ya mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni za IPP, Dkt. Reginald Mengi iliyofanyika kwenye kanisa la KKKT, Usharika wa Moshi mjini.

Amesema kuna watu wakipata vyeo ama utajiri kidogo tu, wanatumia nafasi zao kunyanyasa wengine na akaonya Watanzania wasie wepesi wa kuhukumu, kunyanyasa wengine au kubagua wengine.

Katika mahubiri yake, Dk. Shoo amesema kama kuna dhambi ambayo binadamu anapaswa kuifanyia toba ni ile ya kubaguana na kama Watanzania wanahitaji Taifa lipokee baraka kutoka kwa Mungu, ni vema wakaacha kufanya hivyo. Amesema dhambi nyingine inayopaswa kufanyiwa toba ni ile ya watu wenye nafasi kuwakanyaga wengine.

“Ndugu zangu tukiwa na cheo, tukiwa matajiri, tukiwa na uwezo tuvitumie kuwasaidia wengine, tuache ubinafsi, tuache kiburi, tuache kujitutumua hasa kwa viongozi wa umri mdogomdogo. Kuna mahali mmefika mnajitutumua kama chatu, acheni kabisa. Naomba tuwe unyenyekevu ndugu zangu.”

“Wale wanaopata utajiri, acheni kukumbatia mali zenu, toeni na kuwasaidia wenye uhitaji kwani mnapata satisfaction kwa kufanya hivyo. Huu ni ujumbe kwetu sote na Mungu atusaidie tulishike hili. Muendelee kuiombea familia na yale mazuri mengi tuliyojifunza kwake tukayatende tukayatende, tuyaenzi,” amesema.

Akimuelezea Dkt. Mengi, Askofu Mkuu huyo amesema: “Aliwahi kusema kuwa, mali na utajiri ambao Mungu amempatia siyo kwa sababu yeye ni bora kuliko wengine, bali alimpa ili awe kama bomba la kufikisha baraka kwa wengine.”


“Leo mtu anapata vimilioni kadhaa tu anataka atembee juu ya migongo ya watu, anapata ka-cheo sijui ni diwani, Mkuu wa Mkoa au wa Wilaya, halafu unaona wenzako si kitu. Tuache na tutubu, acha kiburi namuomba Mungu atujalie roho hiyo ya unyenyekevu,” amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Dkt. Mengi atakumbukwa kwa kitendo chake cha kuuchukia umaskini na zaidi kwa kazi mbalimbali ambazo alishiriki.

“Bila shaka kila mmoja wetu ameguswa kwa namna ya kipekee na mchango wa Dkt. Mengi. Kiukweli, marehemu Dkt. Mengi, atakumbukwa kama mwanahabari, mwanaviwanda na mfanyabiashara maarufu ambaye alitumia elimu, maarifa na utajiri wake kwa ajili ya manufaa ya wote hususan watu wenye mahitaji maalum,” amesema Waziri Mkuu.

Amewaomba wanafamilia wasimamie makampuni ambayo Dkt. Mengi aliyaanzisha na kama watakwama wasisite kuomba msaada serikalini kwani iko pamoja nao.

Akielezea wasifu wa baba yake, mtoto wa marehemu, Bw. Abdiel mengi alisema siyo rahisi kuyazungumzia yote kwa wakati mmoja mambo ambayo yamefanywa na Dkt. Mengi bali aliwashukuru waombolezaji wote, viongozi wa Serikali na wafanyakazi wa makampuni ya IPP kwa upendo wao.

“Mambo yote aliyoyafanya naweza kumwelezea katika sifa tatu kubwa ambazo ni alikuwa mzalendo, mwenye uthubutu na mwenye kupenda breakthrough. Alikuwa nafikiria tofauti na wengine. Kwanza anajiuliza kwa nini nifanye jambo hili, na nifanyeje ilikuwa ni suala la pili,” alisema.

Dkt. Mengi ambaye alifariki dunia alfajiri ya Mei 2, mwaka huu akiwa kwenye matibabu huko Dubai, Falme za Kiarabu, amezikwa katika makaburi ya familia huko Nkuu Sinde - Kisereni, Machame, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro. Ameacha mke na watoto wanne.






Read More

SERIKALI YAIPONGEZA TOTAL KWA KUWEKEZA SH. 460 BILIONI

* Yasaidia wajasiriamali wadogo kwa kuwatengea sh. milioni 200 kila mwaka
                  
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameipongeza kampuni ya TOTAL Tanzania kwa kuwekeza hapa nchini mtaji wa dola za Marekani milioni 200 (sawa na sh. bilioni 460) ndani ya miaka mitatu.

Alitoa pongezi hizo jana usiku (Alhamisi, Mei 9, 2019) kwenye sherehe za kutimiza miaka 50 kwa kampuni ya TOTAL hapa nchini, zilizofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, mabalozi, Rais wa TOTAL Africa, wakandarasi na wafanyabiashara mbalimbali.

“Tangu mwaka 2015, kampuni ya TOTAL imewekeza hapa nchini mtaji mkubwa wa zaidi ya dola za Marekani milioni 200 ili kutoa huduma za uagizaji, uuzaji na usambazaji wa bidhaa za mafuta ikiwemo mafuta ya dizeli, petrol, vilainishi mbalimbali pamoja na bidhaa za nishasti mbadala (solar products),” alisema.

Sambamba na uwekezaji huo, Waziri Mkuu alisema, Watanzania zaidi ya 800 wamenufaika na ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kutoka TOTAL ambapo kampuni hiyo imekuwa ikichangia sh. milioni 25 kila mwaka kwa ajili ya masuala ya usalama barabarani.

Shughuli nyingine za kijamii ambazo zimenufaika na uwepo wa kamuni hiyo nchini ni ujenzi wa madarasa (sh. milioni 45), ujenzi wa vituo vya afya (sh. milioni 80) na uchangiaji wa madawati 3,000 kwa baadhi ya shule za mkoa wa Dar es Salaam.

“Serikali ya awamu ya tano inaipongeza kampuni ya TOTAL kwa kuendelea kuwekeza nchini katika kipindi hicho cha miaka 50. Hongereni sana kwa ubunifu wenu na uwekezaji wa zaidi ya shilingi milioni 200 ili kusaidia wajasiriamali kupitia mpango ujulikanao kama The African Start Upper Challenge.”

“Nimearifiwa kuwa tayari Watanzania sita wamenufaika na mpango huo kwa kupatiwa zaidi ya shilingi milioni 25 za kuanzisha shughuli mbalimbali za ujasiriamali,” alisema Waziri Mkuu akielezea mpango huo ulioanzishwa mwaka 2016.

Kuhusu uwekezaji, Waziri Mkuu alisema Rais Dkt. John Pombe Magufuli kupitia Baraza la Biashara nchini amekuwa akikutana na jumuiya ya wafanyabiashara ili kujadili na kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Alisema Rais Magufuli alianzisha Wizara ya Uwekezaji na kuiweka chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ili iwe rahisi kwake kukutana na wawekezaji na kuzungumza nao moja kwa moja kuhusu vikwazo vya kibiashara wanavyokutana navyo.

“Tumeanza utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji na Biashara nchini (blueprint) na tunafanya mapitio ya vivutio mbalimbali vya uwekezaji ikiwemo vivutio vya kikodi, kupitia timu maalumu,” alisema.

Aliwataka wawekezaji waliohudhuria sherehe hizo, waangalie Jiji la Dodoma kama fursa nyingine ya uwekezaji na njia ya kuunga mkono mkakati wa Serikali kuhamia Dodoma. “Sasa hivi Serikali tumetengeneza fursa nyingine ya uwekezaji, nayo ni Dodoma. Milango ya uwekezaji iko wazi na fursa za uwekezaji zipo. Ukitaka kujenga viwanda, majumba, mahoteli, njoo Dodoma. Ardhi tunayo, tutakupa,” alisisitiza.

Mapema, akielezea utendaji wa kampuni hiyo, Rais kampuni ya TOTAL Africa anayeshughulikia masoko na huduma, Bw. Stanislas Mittelman alisema kampuni hiyo ilianzishwa mwaka 1969 na siku zote wamekuwa wakiamini kuwa uimara wa mahusiano yao na Serikali, utatokana na uvumilivu na uaminifu wao kwa jamii ya Watanzania.

Alisema uwekezaji wanaoufanya ni sehemu ya ukuaji wao lakini pia ni njia yao ya kushiriki kuchangia azma ya Serikali ya ukuzaji wa viwanda ili kuelekea “Tanzania ya Viwanda”. “Tumeitikia wito wa Rais Magufuli wa kuongeza uwekezaji hapa nchini, tuliamua kuwa wabia Wakuu (leading partner) kwenye mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta litakalosafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda kuja Tanga, Tanzania,” alisema.

“Pia tumewekeza mtaji wa dola za marekani milioni 200 hasa kwenye ununuzi wa kampuni ya GAPCO, jambo ambalo limetusaidia tuongeze mtandao wetu mara tatu zaidi na kufikisha vituo zaidi ya 100 vya kuuzia mafuta hapa nchini. Pia tumezindua mtambo wa kisasa wa kusafishia mafuta ambao umetuwezesha kuingiza bidhaa mpya kwenye soko la Tanzania,” alisema.

“Kampuni ya TOTAL itaendelea kuwashirikisha Watanzania ubunifu tunaoupata kwnye Nyanja za kimataifa na hii inadhihirishwa na mabadiliko tuliyoyafanya kwenye kituo chetu cha kuhifadhia mafuta (fuel storage terminal) na utoaji wa mafuta bora ya kusafishia injini ya TOTAL Excellium,” alisema.

(mwisho)
Read More

WAZIRI MKUU KUONGOZA MAZISHI YA DK. MENGI LEO

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa anatarajiwa kuongoza mazishi ya Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dkt. Reginald Mengi yatakayofanyika leo Mei 9, 2019 kijijini kwake, Kisereni, Machame, wilayani Hai, Kilimanjaro.

Waziri Mkuu anatarajiwa kuongoza mazishi hayo kwa niaba ya Serikali. Ibada ya mazishi itafanyika kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) la Kisereni, Machame.

Mwili wa Dkt. Mengi ambaye alifariki dunia alfajiri ya Mei 2, mwaka huu akiwa kwenye matibabu huko Dubai, Falme za Kiarabu, umewasili Moshi leo ukitokea Dar es Salaam na kupokekelewa na mamia ya wananchi waliojipanga barabarani.

Juzi, (Jumanne, Mei 6, 2019) Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wa Serikali, waliongoza maelfu ya wananchi kutoa heshima za mwisho wakati wa shughuli za kuaga mwili huo katika ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam.

Hadi mauti yanamfika, Dkt. Mengi alikuwa Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo Vya Habari Tanzania (Chairman of the Media Owners Association of Tanzania - MOAT). Pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (Tanzania Private Sector Foundation – TPSF).

Baadhi ya nyandhifa ambazo Dkt. Mengi aliwahi kushika ni pamoja na Kamishna wa kamati inayoshughulikia mishahara (Salary Review Commission); Mwenyekiti wa Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi Tanzania (NBAA); Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mazingira Tanzania (NEMC); Mwenyekiti wa vyombo vya habari vya Jumuia ya Madola Tanzania (Chairman of the Tanzania Chapter-Commonwealth Press Union-CPU); Kamishna wa TACAIDS na Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki.

(mwisho)
Read More

Sunday, May 5, 2019

DHANA YA AFYA MOJA KUTUMIKA KUDHIBITI MAGONJWA AMBUKIZI MAENEO YA MIPAKANI

Mwezeshaji wa Mafunzo ya kuimarisha udhibiti wa magonjwa ambukizi kati ya Binadamu na wanyama, kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, Profesa, Rudovick Kazwala, akifundisha kwa vitendo namna ya kutumia Vifaa vya kitaalam vya Kinga Binafsi, wakati wa mafunzo hayo kwa wataalamu wa sekta za Afya  kutoka Mkoa wa Songwe na Mbeya katika Halmashauri zilizopo mipakani, Mafunzo hayo yamefadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa na Kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Dawati la Kuratibu Afya moja, tarehe 29 Aprili hadi 3Mei, 2019, mkoani Songwe.

Na. OWM, SONGWE.

Dhana ya Afya moja ambayo hujikita katika kujumuisha sekta zote za Afya katika kujiandaa, kufuatilia  na kukabili magonjwa yanayomuathiri binadamu imeendelea kufundishwa kwa Wataalamu wa sekta hizo za Afya, ikiwa ni Sekta ya Afya  ya Binadamu, Wanyamapori, Mifugo, Kilimo na Mazingira, ili wataalamu hao watumie dhana hiyo kuimarisha udhibiti wa magonjwa ambukizi kati ya Binadamu na wanyama  ambayo hutokea mara kwa mara katika maeneo ya mipakani kutokana na kuwepo kwa  mwingiliano mkubwa kati ya  watu na wanyama katika mazingira yao.

Pamoja na Mwingiliano huo wenye faida kubwa kiuchumi lakini pia unasababisha kuenea kwa vimelea   kwa uharaka zaidi na kusababisha magonjwa kwa binadamu, wanyama na mimea katika mazingira yao, hivyo ili kuimarisha Afya ya binadamu, Shirika la Chakula na Kilimo  la Umoja wa Mataifa (FAO), pamoja  na watalaamu kutoka Wizara ya Mifugo na  Uvuvi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine wamewapa mafunzo wataalamu wa sekta za Afya wanao toka katika Halmashauri za Mkoa wa Mbeya na Songwe zilizo mipakani juu ya namna ya kujiandaa na kukabili magonjwa ambukizi kama  vile Ugonjwa wa Kimeta kwa kutumia Dhana ya Afya  moja.

Akiongea wakati wa kufunga mafunzo hayo yaliyofanyika kuanzia tarehe 29 Aprili hadi,tarehe 3 Mei, 2019, Mkoani Songwe, Mkurugenzi wa Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe, ambaye aliwakilishwa na Mratibu Kitaifa, Dawati la Kuratibu Afya Moja, Ofisi ya Waziri Mkuu, Harrison Chinyuka,  alibainisha kuwa ushirikiano wa wataalam na sekta za Afya  kwa kutumia dhana ya Afya Moja hivi sasa ni agenda ya dunia nzima. Aidha, alieleza kuwa Dhana hiyo imekusudiwa kutumika maeneo ya mipakani   ambapo mwingiliano huo huchochewa na wasafiri kutoka eneo moja kwenda jingine, ongezeko la watu duniani, mabadiliko ya tabia nchi,  utandawazi, ongezeko la mahitaji ya maji na chakula.

Awali akiongea katika mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo nchini, Dkt. Hezron Nonga alibainisha kuwa  sekta za Afya zikishirikiana katika Kudhibiti magojwa zitasaidia kuimarisha Afya ya Binadamu kwa kuwa kila sekta itakuwa inachukuwa tahadhri kwa wakati. Aidha alibainisha kuwa  vimelea vingi vinavyo sabababisha magonjwa kwa binadamu asilimia (60%) vinatoka  kwa wanyama pori na mifugo na maambukizi yanatokea pale binadamu anapoingilia maskani ya wanyama hao bila tahadhari, hivyo Afya moja ikitumika maeneo ya mipakani itasaidia kuimarisha udhibiti wa magonjwa ambukizi yanayotokana na shughuli za mwingiliano wa wanyama na binadamu zinazofanyika sana maeneo ya mipakani.

Katika kuhakikisha watalaam hao kutoka sekta za Afya wanaweza kutumia Dhana  hiyo katika kudhibiti magonjwa katika maeneo ya mipakani wameweza kujengewa uwezo wa namna ya kutoa taarifa za milipuko ya magonjwa ambukizi kama vile ugonjwa wa Kimeta, pindi unapotokea maeneo ya mipakani, Namna ya kuunda vikosi vya kufuatilia na kukabili Ugonjwa, Mawasiliano wakati wa kufuatilia na kukabili magonjwa hayo kwa kutumia Dhana ya Afya moja,  pamoja na masuala ya kutumia vifaa Kinga Binafsi vya Kitaalamu.

Tarehe 13 Februari 2018, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alizindua Dawati la Uratibu la Afya moja chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, likiwa na lengo la kusimamia na kuratibu shughuli za Afya moja nchini. Kwa kutambua umuhimu huo  Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia Dawati la Uratibu wa Afya moja  kwa kushirikiana Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) waliandaa na kuratibu mafuzo hayo.

MWISHO.

Baadhi ya wataalamu wa sekta za Afya  kutoka Mkoa wa Songwe na Mbeya kwa Halmashauri zilizopo mipakani wakiwa wamevaa vifaa vya Kitaalamu vya Kinga Binafsi, wakati wa  Mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa na Kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Dawati la Kuratibu Afya moja, tarehe 29 Aprili hadi 3Mei, 2019, mkoani Songwe.
Mratibu wa Kitaifa, Dawati la Afya moja, lililopo Ofisi ya Waziri Mkuu, Harrison Chinyuka, akisisitiza  umuhimu wa sekta za Afya kushirikiana wakati wa mafunzo ya kuimarisha udhibiti wa magonjwa ambukizi kati ya Binadamu na wanyama kwa wataalamu wa sekta za Afya  kutoka Mkoa wa Songwe na Mbeya katika Halmashauri zilizopo mipakani, Mafunzo hayo yamefadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa na Kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Dawati la Kuratibu Afya moja, tarehe 29 Aprili hadi 3Mei, 2019, mkoani Songwe
Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo nchini, Dkt. Hezron Nonga akisisitiza  umuhimu wa kutumia Dhana ya Afya moja wakati wa mafunzo ya kuimarisha udhibiti wa magonjwa ambukizi kati ya Binadamu na wanyama kwa wataalamu wa sekta za Afya  kutoka Mkoa wa Songwe na Mbeya katika Halmashauri zilizopo mipakani, Mafunzo hayo yamefadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa na Kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Dawati la Kuratibu Afya moja, tarehe 29 Aprili hadi 3Mei, 2019, mkoani Songwe
Mwezeshaji wa Mafunzo ya kuimarisha udhibiti wa magonjwa ambukizi kati ya Binadamu na wanyama, kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, Niwael Mtui,  akifundisha namna ya kudhibiti magonjwa ambukizi maeneo ya mipakani wakati wa mafunzo hayo kwa wataalamu wa sekta za Afya  kutoka Mkoa wa Songwe na Mbeya katika Halmashauri zilizopo mipakani, Mafunzo hayo yamefadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa na Kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Dawati la Kuratibu Afya moja, tarehe 29 Aprili hadi 3Mei, 2019, mkoani Songwe.
Mwezeshaji wa Mafunzo ya kuimarisha udhibiti wa magonjwa ambukizi kati ya Binadamu na wanyama, kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Emmanuel Swai, akifundisha namna ya kudhibiti magonjwa ambukizi maeneo ya mipakani, wakati wa mafunzo hayo kwa wataalamu wa sekta za Afya  kutoka Mkoa wa Songwe na Mbeya katika Halmashauri zilizopo mipakani, Mafunzo hayo yamefadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa na Kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Dawati la Kuratibu Afya moja, tarehe 29 Aprili hadi 3Mei, 2019, mkoani Songwe.

Baadhi ya wataalamu wa sekta za Afya  kutoka Mkoa wa Songwe na Mbeya katika Halmashauri zilizopo mipakani, wakiwa katika makundi ya majadiliano wakati wa mafunzo ya Kuimarisha Udhibiti wa magonjwa ambukizi kwa kutumia Dhana ya Afya moja kwa maeneo ya mipakani, Mafunzo  hayo yamefadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa na Kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Dawati la Kuratibu Afya moja, tarehe 29 Aprili hadi 3Mei, 2019, mkoani Songwe.

Washiriki wa Mafunzo ya Kuimarisha Udhibiti  wa  magonjwa ambukizi kati ya Binadamu na wanyama kwa kutumia Dhana ya Afya moja wakiwa katika picha ya pamoja. Mafunzo hayo yamefadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa na Kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Dawati la Kuratibu Afya moja, tarehe 29 Aprili hadi 3Mei, 2019, mkoani Songwe.








Read More