Wednesday, June 17, 2020

WAZIRI MKUU ATIA SANI KITABU CHA MAOMBOLEZO KIFO CHA NKURUNZIZA


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Juni 17, 2020 ametia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza na kutoa pole kwa wananchi wa nchi hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

“Kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli nimekuja hapa kutoa pole na salamu za rambirambi kwa Serikali na wananchi wa Burundi kufuatia kifo cha aliyekuwa rais wa nchi ya Burundi. Mheshimiwa Rais na Watanzania wote tumepokea kwa mshituko na masikitiko makubwa taarifa za kifo chake.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Juni 17, 2020) akiwa katika Ofisi za Ubalozi wa Burundi, Upanga jijini Dar es Salaam baada ya kusaini kitabu cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza aliyefariki Juni 9, 2020 kutokana na mshituko wa moyo.

Amesema Tanzania na Burundi ni nchi zenye historia ndefu na mshikamano wa muda mrefu, hivyo ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wa Burundi wawe watulivu katika kipindi hiki cha majonzi. “Serikali ya Tanzania itaendelea kudumisha umoja na mshikamano kati yake na Burundi.”

Awali, Balozi wa Burundi nchini Tanzania, Balozi Abayeho Gervais ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa ushirikiano mkubwa anaoutoa kwa Taifa hilo na kwamba anatarajia umoja na mshikano huo utadumu milele na milele.

“Tunamshukuru Rais wa Tanzania amepeleka ujumbe mkubwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete nchini Burundi kwa ajili ya kushuhudia uapishwaji wa Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye ambaye anatarajiwa kuapishwa kesho Juni 18.

Akizungumzia kuhusu kifo cha aliyekuwa rais wa nchi hiyo Balozi Gervais amesema wamepokea kwa mshtuko mkubwa kwa sababu alikuwa bado ni kijana akiendelea kufanya shughuli zake. “Hii yote ni mipango ya Mwenyezi Mungu na sote tupo safarini.”

Mwisho.
Read More

MAJALIWA ATIA SAINI KITABU CHA MAOMBOLEZO YA KIFO CHA ALIYEKUWA RAIS WA BURUNDI, PIERRE NKURUNZIZA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitia saini katika kitabu cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Burundi, Pierre  Nkurunziza kwenye Ubalozi wa Burundi, Upanga jijini Dar es salaam, Juni 17, 2020. Wa pili kulia ni Balozi wa Burundi nchini, Mhe. Abayeho Gervais.  
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akitoa heshima baada ya kutia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza kwenye Ubalozi wa Burundi, Upanga jijini Dar es salaam, Juni 17, 2020. Wa pili kulia ni Balozi wa Burundi nchini, Mhe. Abayeho Gervais.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa Burundi nchini , Mhe. Abayeho Gervais  baada ya kutia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha  aliyekuwa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza kwenye Ubalozi wa Burundi, Upanga jijini Dar es salaam, Juni 17, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa Burundi nchini , Mhe. Abayeho Gervais  baada ya kutia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha  aliyekuwa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza kwenye Ubalozi wa Burundi, Upanga jijini Dar es salaam, Juni 17, 2020.

Read More

Monday, June 15, 2020

MAJALIWA ASOMA HOTUBA YA KUKAMILIKA KWA SHUGHULI ZA BUNGE




Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma Hotuba ya  Kukamilika kwa  Shughuli za Mkutano wa Kumi na Tisa wa Bunge,  Bungeni Jijini Dodoma, Juni 15, 2020.

Read More

WAZIRI MKUU ATAJA MAFANIKIO MAKUBWA YA AWAMU YA TANO


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika kipindi cha miaka mitano imepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kurekebisha nidhamu kwa watumishi wa umma na uwajibikaji Serikalini, hivyo kuwezesha watumishi kutambua majukumu yao na kuwatumikia Watanzania.

Amesema mambo mengi ya kujivunia yamefanywa na tumekuwa tukiyaeleza katika maeneo mengi kupitia mikutano ya hadhara, vyombo vya habari, nyaraka mbalimbali, uwepo wa miradi mingi ya kimkakati hadi kwa wananchi wa kawaida, yakiwemo mapambano dhidi ya rushwa ndani ya Serikali na nje ya Serikali ili kulinda mali na fedha za umma. “Hatua hii ni endelevu, lengo ni kung’oa mizizi ya rushwa nchini.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Juni 15, 2020) Bungeni jijini Dodoma wakati akihitimisha mkutano wa 19 wa Bunge, Bungeni jijini Dodoma. Ametaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama, mhimili wa Bunge na Mahakama.

Akiorodhesha mafanikio hayo, Waziri Mkuu amesema Serikali imefanikiwa katika mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya ambayo yanalenga kujihakikishia kuwa na Taifa lenye nguvukazi inayofanya kazi na kwamba mapambano hayo bado yanaendelea nchini kote.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa mafanikio mengine ni utambuzi wa watumishi hewa ambapo katika zoezi hilo wamepata mafanikio makubwa na kuokoa sh. bilioni 19.83 kwa kuwaondoa kwenye mfumo wa malipo watumishi hewa 19,708 na wenye vyeti vya kugushi 15,411.

Amesema Serikali imefanikiwa katika suala la ukusanyaji wa mapato ulioiwezesha Serikali kujenga miradi na kutoa huduma muhimu. “Ukusanyaji wa mapato umeongezeka kutoka wastani wa sh. bilioni 800 kwa mwezi mwaka 2015 hadi wastani wa sh. trilioni 1.5 kwa mwezi katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020.”

“Tumefanikiwa kuimarisha uwekezaji kwa kujenga viwanda. Hadi Aprili 2020 jumla ya viwanda vipya 8,477 vikiwemo vidogo, vya kati na vikubwa vimeanzishwa katika maeneo mbalimbali nchini na hivyo kuwezesha ongezeko la ajira za viwandani zipatazo 482,601.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imefanikiwa kuimarisha masoko na kilimo cha mazao makuu, kama korosho, pamba, chai, tumbaku, kahawa, michikichi na mkonge. Aidha, Serikali imeimarisha uzalishaji wa mazao ya chakula ili kuwa na uhakika wa usalama wa chakula.

Mafanikio mengine yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Tano ni pamoja na kuimarisha ushirika wa kilimo na upatikanaji wa pembejeo pamoja na huduma za ugani ili kuwafanya wakulima kuzalisha kwa tija.

Amesema marekebisho ya Sheria ya madini yamefanyika sambamba na kuanzisha masoko ya madini 28 na vituo 12 vya ununuzi wa madini katika maeneo ya uchimbaji na hivyo kuongeza makusanyo ya Serikali, kupunguza biashara haramu na utoroshaji wa madini kwenda nje. Pia, Waziri Mkuu amesema kuanzia Machi hadi Septemba, 2019 jumla ya kilo za dhahabu 4,680.28 zenye thamani ya shilingi bilioni 432.49 zimezalishwa na Serikali imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 30.27.

Vilevile, Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha miaka mitano, Serikali imefanikiwa kuhamishia Makao Makuu ya Serikali Dodoma ambapo tayari Watumishi wapatao 15,361 wamehamia Dodoma na sasa fursa za uwekezaji zimeongezeka katika Jiji la Dodoma.

“Tumefanikiwa kuboresha miundombinu na taaluma ya sekta ya elimu kwa ngazi zote kuanzia awali hadi elimu ya juu ikiwemo ujenzi na ukarabati wa madarasa, maktaba, maabara, nyumba za walimu na mabweni. Kwa upande wa Sera ya Elimu bila Ada tumetumia zaidi ya sh. bilioni 20.8 kila mwezi kwa ajili ya fidia ya ada, posho ya madaraka kwa walimu wakuu, wakuu wa shule na waratibu kata kila mwezi tangu 2016 na tutaendelea. Hii imesaidia kuongeza uandikishaji na mahudhurio shuleni,” ameongeza.

Amesema mafanikio mengine ya Serikali ya Awamu ya Tano ni pamoja na kuimarisha huduma za afya kwa kujenga zahanati, vituo vya afya, kujenga Hospitali za Wilaya, Mikoa, Kanda na za Kitaifa, huduma za Madawa na Vifaa Tiba.

Waziri Mkuu amesema Serikali imejenga Zahanati 1,198 Vituo vya Afya 487, Hospitali za Wilaya 71, Hospitali za Rufaa za Mikoa 10, na Hospitali za Kanda tatu za Kusini – Mtwara, Magharibi – Tabora na Kanda ya Ziwa - Burigi.

“Ujenzi wa miradi ya maji vijijini na mijini tumefikia asilimia 84 mijini na asilimia 70.1 vijijini. Pia tumefufua Shirika la Ndege kwa kununua ndege mpya 11, ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege kwenye mikoa isiyo na viwanja vya ndege pamoja na ununuzi wa rada nne mpya za kuongoza ndege za kiraia zilizo Mwanza, Mbeya, Dar-es-Salaam na Kilimanjaro.”

Waziri Mkuu ametaja mafanikio mengine ni ujenzi wa mradi mkubwa wa kufua umeme (Mwalimu Nyerere Dam) utakaozalisha Mw 2,115 ambao kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 40, gharama za ujenzi huo ni sh. trilioni 6.5

Amesema usambazaji wa umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umefikia asilimia 80 ambapo hadi Aprili 2020 sh. trilioni 2.27 zimetumika na kufanikisha jumla ya vijiji 9,112 kati ya 12,268 vya Tanzania Bara kuunganishwa na umeme kutoka vijiji 2,118 mwaka 2015.

Amesema ujenzi wa Mradi wa Reli ya Kimataifa (SGR) wa kilomita 300 Dar-es-Salaam–Morogoro, umefikia asilimia 78 huku kipande cha Morogoro hadi Makutupora chenye urefu wa kilomita 422 mradi wake umefikia asilimia 30 ya kazi. “Lengo ni kukamilisha mradi huu ifikapo Juni 2021 kwa gharama ya sh. trilioni 7.5.”

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana kwenye miradi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zikiwemo barabara kuu, barabara za mikoa na za wilaya zenye thamani ya zaidi ya sh. trilioni 7.6, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kujenga barabara ya njia nne kutoka Kimara hadi Kibaha (km 19.2).

Ujenzi wa madaraja: ujenzi wa daraja la juu la Mfugale (Dar es Salaam), daraja la Furahisha (Mwanza) na daraja la Magufuli (mto Kilombero) umekamilika; ujenzi wa barabara ya pete (Ubungo interchange) umefikia asilimia 77 kwa shilingi bilioni 247; Aidha,  ujenzi unaendelea kwa daraja la New Selander (Dar es Salaam) kwa shilingi Bilioni 270. Daraja la Kigongo- Busisi shilingi Bilioni 699.2”.

Kuhusu, ujenzi wa Bandari, Waziri Mkuu amesema uboreshaji na upanuzi wa bandari za Tanga, Dar-es-Salaam na Mtwara umegharimu zaidi ya sh. trilioni 1.2. Pia Waziri Mkuu amezungumzia ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Victoria na ujenzi wa chelezo; ukarabati wa meli ya MV Victoria na MV Butiama ambapo katika kipindi cha mwaka 2015/2016 hadi Aprili, 2020 jumla ya sh. bilioni 111.7 zimetumika.

Vilevile, Serikali imekamilisha ujenzi wa meli moja mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 200 za mizigo katika Ziwa Nyasa; na ukarabati wa meli ya mafuta ya MV Sangara katika Ziwa Tanganyika. Ujenzi wa vivuko vya MV Kigamboni, MV Pangani, Kigongo -Busisi, MV Sengerema na Nyamisati.

“Tumefanikiwa katika suala zima la urejeshaji na usimamizi wa mali za Ushirika zilizokuwa zimechukuliwa kinyume na utaratibu, kama NYANZA, SHIRECU, KNCU na Mamlaka ya Mkonge Tanzania. Pia tumeweza kusimamia maboresho kwenye sekta ya uvuvi na mifugo kwa kuvua na kufuga kisasa, kujenga viwanda na masoko yake.”

Kwa namna ya pekee kabisa nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kutokana na fikra na uongozi makini katika ujenzi wa Taifa letu. Ni dhahiri kuwa maono yake katika kuongoza na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015 - 2020 na mipango ya Serikali, zimeleta mafanikio makubwa ambayo hivi sasa wote tunayaona.

“…nyote mtakubaliana nami kwamba Mheshimiwa Rais na Makamu wake Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanawafikia Watanzania, wanawasikiliza na kutatua kero zao.”

Amesema lengo la ziara hizo, pamoja na mambo mengine lilikuwa ni kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 ikiwemo kukagua miradi ya maendeleo; kuzungumza na watumishi na kuwafahamisha kuhusu falsafa ya Serikali ya awamu ya tano ya Hapa Kazi Tu.

Amesema ziara hizo zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha utendaji wa watumishi wa umma. “Hivi sasa, wananchi wanapokwenda katika ofisi za umma wanapokewa, wanasikilizwa na kuhudumiwa vizuri. Aidha, usimamizi wa miradi ya maendeleo umeimarika sambamba na kuakisi thamani halisi ya fedha katika utekelezaji wa miradi hiyo”.

Read More

MAJALIWA: MAAMBUZI YA COVID-19 YAMEPUNGUA NCHINI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) kwa sasa yamepungua na idadi ya wagonjwa waliopo nchini hadi leo ni 66.

“Anayestahili sifa katika hili ni Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa msimamo wake usiotetereka na maono ya mbali aliyokuwa nayo ambayo yamekuwa chachu katika kupunguza maambukizi ya COVID-19 na kulinda uchumi wa nchi.”

Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Juni 15, 2020) wakati akihitimisha shughuli za Mkutano wa 19 wa Bunge jijini Dodoma. “Mheshimiwa Rais ameifanya Tanzania iwe ya kupigiwa mfano duniani kwa namna alivyoshughulikia ugonjwa huu”.

Waziri Mkuu amesema “nchi nyingi duniani zikiwemo nchi za bara la Afrika zilichukua hatua kadhaa za kudhibiti maambukizi zikiwemo watu kutotoka ndani ya nyumba zao (Lockdown), kuzuia mikusanyiko kwa kufunga shule, vyuo, michezo, aina zote za usafiri wa ndani na nje, maeneo ya ibada na shughuli za uzalishaji mali na viwanda vilifungwa.”

Waziri Mkuu aliongeza kuwa Tanzania ilianza kuchukua hatua kadhaa ili kukabiliana na maambukizi kwa kuunda Kamati tatu za ngazi ya Mawaziri, Watendaji na Wataalam wa Afya kwa lengo la kufanya tathmini ya hatua za kuchukua ili kupunguza maambukizi na kulinda anguko la kiuchumi. Hatua zilizochukuliwa ni kupunguza misongamano kwa kufunga shule, vyuo, mikutano, kunawa maji, matumizi ya vitakasa mikono na kuvaa barakoa.

“Siku ya tarehe 22 Machi, 2020 Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, akiwa Jijini Dodoma na tarehe 03 Mei, 2020 akiwa Chato aliwataka Watanzania wawe watulivu waondoe hofu ya ugonjwa huu na waone ni ugonjwa kama magonjwa mengine, kama vile Malaria, UKIMWI, Kifua Kikuu na akawataka Watanzania wachukue tahadhari na kuendelea na shughuli za uzalishaji mali, kufanya kazi ofisini, viwandani, mashambani na kutofunga nyumba za ibada.”

Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli alihutubia tena Taifa tarehe 16 Aprili, 2020 kwa kutoa maelekezo na kusisitiza mambo matano ambayo ni pamoja na kuwasihi Watanzania kuondoa hofu kwa kuwa Mwenyezi Mungu yupo nasi na hivyo, waendelee kuchapa kazi ili kunusuru uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla na kuzingatia kanuni za afya.

Pia, aliwataka Watanzania watumie siku tatu kumuomba na kumlilia Mwenyezi Mungu kwani Mungu yu pamoja nao na atawasikia huku akiendelea kusimamia kauli yake ya kuwataka Watanzania wafanye kazi kwa bidii na kumtegemea Mungu bila kujali kauli za kebehi na ukosoaji kutoka pande mbalimbali za dunia.

Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli aliwahimiza Watanzania wamtegemee Mwenyezi Mungu na kwamba Mwenyezi Mungu pekee ndiye atakayewavusha na kuwaepusha na janga hilo. Pia, aliwahimiza Watanzania kutopuuza umuhimu wa tiba mbadala katika mapambano dhidi ya COVID-19. “Kauli hii, imekuwa chachu katika kuimarisha tafiti za dawa za asili ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika kupambana na maradhi mbalimbali ikiwemo COVID-19”. Amesema Waziri Mkuu.

Vilevile, Waziri Mkuu amesema Mei 20, 2020 akiwa Singida, Rais Dkt. Magufuli aliwaomba Watanzania watumie siku tatu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa maajabu aliyoyafanya kwa Taifa la Tanzania kwa kuliepusha na kusambaa kwa virusi vya COVID-19.

Amesema suala la kudhibiti maambukizi ya COVID-19 litaendelea kuwa kipaumbele cha Serikali kwa sasa sambamba na malengo ya muda mrefu ya kumaliza ugonjwa huo hususan katika kipindi hiki ambacho WHO imebainisha kwamba si wa kuondoka mara moja watu wajifunze kuishi nao.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Juni 9, 2020 Bunge lilipitisha Azimio la kumpongeza na kumuunga mkono Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna alivyomudu kuivusha nchi katika janga la COVID-19. Waswahili husema mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni.

“Katika hili, nami naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa hotuba zake zote zilizohusu ugonjwa huu ambapo alihimiza masuala muhimu kwa Watanzania katika kukabiliana na janga hili na hivyo, kuondoa hofu na taharuki iliyokuwa imetanda kwa Watanzania.”

“…leo tunaona idadi ya wagonjwa wanaougua imepungua sana. Kwa mfano, taarifa ya leo, Jumatatu tarehe 15 Juni, 2020 inaonesha kuwa tuna wagonjwa 66 kutoka katika mikoa 10 huku mikoa mingine 16 ikiwa haina wagonjwa.”

Pia, Waziri Mkuu ametoa pongezi maalum kwa Viongozi wa dini kwa namna walivyoshirikiana na waumini katika mapambano ya ugonjwa wa COVID-19. Wakati wote viongozi hao wamekuwa wakiwapatia faraja waumini na wagonjwa kwamba Mwenyezi Mungu atawaponya. “Hatua hizo zimekuwa mhimili mkubwa wa upendo, umoja, mshikamano na ujasiri miongoni mwa Watanzania. Tunawashukuru sana.”

Amesema taarifa iliyotolewa na Taasisi ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (Organisation for Economic Cooperation and Development - OECD) inabashiri kuwa kitendo cha kuwafungia watu ndani yaani “Lockdown” kitasababisha kusinyaa kwa uchumi wa nchi zilizoendelea kwa asilimia mbili kila mwezi.

“Hivi sasa, nchi nyingi zinakubaliana kuwa “Lockdown” si hatua sahihi ya kukabiliana na COVID-19. Vilevile, kisayansi inakadiriwa kuwa nchi ambazo ziliwafungia watu wake na mipaka yake zipo katika hatari ya kukumbwa na madhara makubwa ya ugonjwa huo pindi utakapotokea mlipuko wa pili na hata wa tatu.”

“…kwa mantiki hiyo, mtizamo na hatua zilizochukuliwa na Tanzania katika kupambana na COVID-19 zinaonesha upekee tulionao kama nchi. Serikali, inayo kila sababu ya kuwapongeza Watanzania ambao si tu walipokea maelekezo ya Serikali lakini pia walifanya hivyo kwa uaminifu mkubwa na kwa hiari yao wenyewe bila kushurutishwa na mamlaka yoyote ya nchi.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Katibu Mkuu, Mganga Mkuu wa Serikali pamoja na wataalamu wa afya kwa usimamizi wa tatizo hilo kwani walitekeleza majukumu yao bila kujali hatari ya virusi hivyo kwa maisha yao na wapendwa wao.

Vievile, Waziri Mkuu ameishukuru sekta binafsi, mtu mmoja mmoja na wadau wote ambao waliitikia wito wa Serikali kwa kutoa michango ya hali na mali katika kufanikisha vita dhidi ya COVID-19 nchini. Pia wamiliki wa viwanda ambao waliitikia wito wa Mheshimiwa Rais na kuanza kuzalisha vifaa kinga hapa nchini.

Mwisho
Read More

SERIKALI ITAKAMILISHA MIRADI YOTE YA KIPAUMBELE-MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itatoa msukumo wa kipekee katika kukamilisha miradi ya kipaumbele na kimkakati inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano ili wananchi waendelee kupata huduma bora.

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali itashirikiana na sekta binafsi kuleta mageuzi kwa kutekeleza kwa kasi mpango wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini (yaani Blue Print for Business Environment).

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Juni 15, 2020) wakati akihitimisha mkutano wa 19 wa Bunge. Amesema, lengo ni kuhakikisha shughuli za uchumi na biashara zinashamiri na kuchangia kuondoa umaskini nchini.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi shupavu wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli imejipanga vizuri kutekeleza mipango yote iliyowekwa katika Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya mwaka 2020/2021. “Serikali itaendelea kuboresha huduma za jamii pamoja na kuhakikisha kwamba ulinzi na usalama unaimarishwa.”

“Nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge na Madiwani waendelee kushirikiana na Serikali katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu. Aidha, natoa wito kwa sekta binafsi, wadau wa maendeleo na wananchi wote waendelee kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa mpango na bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha.”

Waziri Mkuu amesema, Serikali itaendelea kutekeleza Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/2021 kwa kuzingatia athari na changamoto za ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (COVID-19).

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali itakamilisha mchakato wa shughuli zilizobaki za maandalizi ya uchaguzi mkuu wa ubunge, urais na udiwani na kuiwezesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kusimamia kikamilifu shughuli zote za uchaguzi huo kwa uhuru na haki.

Amesema sambamba na maandalizi ya uchaguzi mkuu, utekelezaji wa kazi za Serikali utaendelea. “Hivyo, watumishi wote wa umma wanashauriwa waendelee kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uaminifu na kutoa huduma bora kwa wananchi kwa ufanisi na tija wakati wote.”

Wabunge wamepitisha kwa kishindo Bajeti ya Serikali ya mwaka 2020/2021 ya jumla ya sh. trilioni 34.88, kati ya fedha hizo, sh. trilioni 21.98 ni za matumizi ya kawaida na sh. trilioni 12.90 ni za miradi ya maendeleo sawa na asilimia 37 ya bajeti yote.


Mwisho.

Read More

IDADI YA WAPIGAKURA YAONGEZEKA UCHAGUZI MKUU 2020


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema idadi ya wananchi waliojiandikisha kupiga kura imeongezeka ambapo wapiga kura halali kwa mwaka huu ni 29,804,992 ikilinganishwa na wapiga kura 23,161,440 wa mwaka 2015.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Tume inaendelea na uchambuzi wa taarifa za wapiga kura waliojiandikisha na baada ya zoezi hilo kukamilika, Daftari la mwisho litakalotumika katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 litaandaliwa na kuwekwa wazi.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Juni 15, 2020) bungeni jijini Dodoma wakati akihitimisha mkutano wa 19 wa Bunge, ambapo amesema kwa sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea vema na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Amesema takwimu za awamu ya kwanza na ya pili, zinaonesha kuwa wapiga kura wapya walioandikishwa ni 7,326,552, wapiga kura walioboresha taarifa zao ni 3,548,846 na wapiga kura 30,487 wamepoteza sifa.

Amesema zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wa awamu ya kwanza lilianza rasmi Julai 18, 2019 na kukamilika Februari 23, 2020 kwa nchi nzima wakati awamu ya pili ilianza Aprili 17, 2020 na kukamilika Mei 5, 2020.

“Hivi sasa, pamoja na mambo mengine Tume imekamilisha matakwa ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ya kufanya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili kati ya uchaguzi mkuu mmoja na mwingine.”

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi wazingatie Katiba, sheria, kanuni na miongozo iliyopo katika uendeshaji wa shughuli za uchaguzi.

Vilevile, Waziri Mkuu amewasihi viongozi na wanachama wa vyama vyote vya siasa na wananchi kwa ujumla waendelee kulinda amani na kuendeleza mshikamano katika kipindi hiki na wakati wa uchaguzi mkuu.

(Mwisho)
Read More

Sunday, June 14, 2020

MAJALIWA:TUTAENDELEA KUCHUKUA HATUA KWA WATAKAOKATISHA MASOMO KWA WATOTO WA KIKE


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa watu wote watakaothibitika kufanya vitendo vya kuwakatisha watoto wa kike ndoto za masomo ikiwemo kuwafunga jela miaka 30.

Pia amewaagiza Wakuu wa Wilaya wote nchini wahakikishe wanaendelea kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama hadi ngazi za kata kusimamia Sheria ya Elimu ya kuwalinda watoto wote wa kike walio chini ya umri wa miaka 18.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Juni 14, 2020) wakati alipoweka jiwe la msingi na kukabidhiwa shule ya sekondari ya wasichana ya Bunge High School iliyojengwa na wabunge katika Kata ya Kikombo jijini Dodoma kwa thamani ya zaidi ya sh. bilioni moja.

 “Sekta ya elimu ni wakala wa mabadiliko katika jamii kiuchumi, kiteknolojia na kiutamaduni katika kuleta maendeleo ya nchi. Ninawapongeza sana waheshimiwa wabunge kwa kuamua kuwa sehemu ya wadau muhimu katika sekta ya elimu .”

Amesema utoaji wa elimu bora kwa Watanzania ni moja ya vipaumbele vya nchi katika kuleta maendeleo na kufikia malengo ya Milenia 2025, Elimu kwa wote (EFA) na Mkakati wa Kupambana na Kupunguza Umasikini Tanzania (MKUKUTA).

Waziri Mkuu amesema ili kuweza kufanikisha hayo wanahitaji sekta hiyo iwe bora, imara, inayokidhi mahitaji ya jamii kwa kuwapa vijana maarifa na ujuzi wa kukabiliana na matatizo ya kijamii, kitaifa na kimataifa.

Amesema Serikali kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali imepata mafanikio makubwa sana kwa upatikanaji wa huduma za jamii ikiwemo elimu, afya na maji, ambapo kwa sasa kuna shule za msingi 17,659 na shule za sekondari 4,883 nchi nzima zikiwemo shule za sekondari za Serikali za wasichana 156.

”Idadi hii ya shule imesaidia kutoa fursa kwa wanafunzi wengi kupata elimu nchini katika ngazi mbalimbali.  Hivi sasa kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi tunatekeleza mpango wa elimu bila ada kwa kutoa shilingi bilioni 22.8 kila mwezi kwa lengo la kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule anapata fursa bila vikwazo.”

Amesema Serikali, itaendelea kusimamia utekelezaji wa sera ya Elimumsingi Bila Ada kwa lengo la kuwawezesha watoto wa kike kupata elimu ya sekondari na stadi za kazi, kuondoa vikwazo kwa watoto wa kike kupata elimu ya sekondari, kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji pamoja na uratibu, usimamizi na tathmini ya ubora wa elimu ya sekondari.

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali imeweka mikakati maalum ya kuwasaidia watoto wa kwa kuhakikisha  wanapata elimu bora na kutokana na mikakati hiyo idadi ya wanafunzi wa kike wanaosoma Elimu ya Juu imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka katika ngazi mbalimbali.

Mfano idadi ya wanafunzi wa kike katika Elimu ya Juu wameongezeka kutoka wanafunzi 49,959 kati ya wanafunzi 139,638 waliodahiliwa mwaka 2010/2011 hadi kufikia wanafunzi 90,159 kati ya wanafunzi 230,339 waliodahiliwa mwaka 2017/2018. “Niwahakikishie kuwa Serikali itaendelea kuwekeza kwa elimu ya mtoto wa kike.”

 Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Elimu isimamie kufungua madawati ya malalamiko katika vyuo vikuu kuhusu unyanyasaji wa kijinsia. “Serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa wahadhiri watakaobanika kujihusisha na  unyanyasaji wa kijinsia katika vyuo chini ya sheria ya Mahusiano ya kulazimisha.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) watumie shule hiyo kuwatambua wasichana wenye vipaji  hususan kwa tahasusi za sayansi na kuwasaidia kuvikuza na kuviendeleza.

Amesema kwa kufanya hivyo, watakuwa wakitoa motisha kwa wanafunzi hasa wa kike na kuwatia moyo ili wayapende masomo ya sayansi na teknolojia na hatimaye kuongeza idadi ya wataalamu wa kike. Shule hiyo ni ya mchepuo wa sayansi.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge Job Ndugai amesema ujenzi wa shule hiyo ni alama kubwa iliyowekwa na wabunge wa bunge la 11 kwani wamefanya jitihada kubwa katika kujitolea kuchangia fedha zilizowezesha ujenzi wa shule hiyo.

“…Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwezesha wabunge wa bunge la 11 kuweza kufanikisha ujenzi wa shule ya Wasichana ya Bunge ambayo itakuwa ya kidato cha tano na sita kwa mchepuo wa sayansi.”

Awali, Mwenyekiti wa Umoja wa Wapunge Wanawake Tanzania (TWPG), Margaret Sitta alitumia fursa hiyo kumshukuru Spika Ndugai kwa kuunga mkono juhudi za wabunge wanawake na hatimaye kufanikisha ujenzi wa shule hiyo.

Pia, alimshukuru na kumpongeza Spika Ndugai kwa kuhakikisha usawa wa kijinsia unaendelea kuwepo bungeni. Hata hivyo ameiomba Serikali iangalie namna ya kuwawezesha wanawake wengi kuingia bungeni kwa kupitia majimbo kwani waliopo ni asilimia tisa tu ya wabunge wote wa majimbo.


Mwisho.

Read More

Thursday, June 11, 2020

BUNGENI DODOMA,11.06.2020

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Bumbuli, January Makamba,  Bungeni jijini Dodoma, Juni 11, 2020. 
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, akiwasilisha hali ya uchami nchini, Bungeni jijini Dodoma. Juni 11, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Paramagamba Kabudi, Bungeni jijini Dodoma, Juni 11, 2020. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifurahia jambo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (kushoto) na Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia , Profesa Joyce Ndalichako (katikati), Bungeni jijini Dodoma, Juni 11, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Viti Maalum, Vicky Kamata, née ya jengo la  Bunge jijini Dodoma, Juni 11, 2020.


Read More

Tuesday, June 9, 2020

MAJALIWA AMTEMBELEA MBOWE HOSPITALI YA NTYUKA ALIKOLAZWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpa pole Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye amelazwa katika  hospitali ya Ntyuka jijini Dodoma, kwa matibabu Juni 9, 2020. Mbowe anatibiwa majeraha aliyoyapata baada ya kushambuliwa  na watu ambao bado hawajajulikana wakati akiingia nyumbani kwake jijini Dodoma usiku wa kuamkia   leo. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpa pole Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye amelazwa katika  hospitali ya Ntyuka jijini Dodoma, kwa matibabu Juni 9, 2020. Mbowe anatibiwa majeraha aliyoyapata baada ya kushambuliwa  na watu ambao bado hawajajulikana wakati akiingia nyumbani kwake jijini Dodoma usiku wa kuamkia   leo. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpa pole Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye amelazwa katika  hospitali ya Ntyuka jijini Dodoma, kwa matibabu Juni 9, 2020. Mbowe anatibiwa majeraha aliyoyapata baada ya kushambuliwa  na watu ambao bado hawajajulikana wakati akiingia nyumbani kwake jijini Dodoma usiku wa kuamkia   leo. 


Read More

Monday, June 8, 2020

MHESHIMIWA WAZIRI MKUU BUNGENI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Katiba na Sheria, Mwigulu Nchemba,  Bungeni jijini Dodoma, Juni, 8, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Mwigulu Nchemba,  Bungeni jijini Dodoma, Juni, 8, 2020.


Read More

MHESHIMIWA WAZIRI MKUU BUNGENI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Katiba na Sheria, Mwigulu Nchemba,  Bungeni jijini Dodoma, Juni, 8, 2020. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Mwigulu Nchemba,  Bungeni jijini Dodoma, Juni, 8, 2020.

Read More

Tuesday, June 2, 2020

WAZIRI MKUU AKABIDHI NYUMBA 103 KWA IDARA YA UHAMIAJI


*Ni utekelezaji wa uamuzi wa Rais Dkt. John Magufuli

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameikabidhi Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi nyumba 103 zenye gharama ya zaidi ya sh. bilioni tano kwa ajili ya makazi ya Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji nchini zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika eneo la Iyumbu jijini Dodoma ikiwa ni utekelezaji wa uamuzi ulitolewa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Baada ya kukabidhi nyumba hizo, Waziri Mkuu amesema kwamba makazi hayo yawe chachu kwa Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji nchini katika kutambua wajibu wao wa kutoa huduma iliyobora na inayokidhi matarajio ya wateja ambao ndiyo waajiri wao.

Akikabidhi nyumba hizo leo (Jumanne, Juni 2, 2020), Waziri Mkuu amesema “Uamuzi huu wa Mheshimiwa Rais ambao leo hii tunashuhudia utekelezaji wake kupitia makabidhiano haya, utasaidia kuwafanya Maafisa na Askari wa Uhamiaji kukaa katika makazi yao tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo waliishi uraiani.”

Ameongeza kuwa “Ni ukweli usiofichika kuwa makabidhiano ya nyumba hizi baina ya Shirika la Nyumba la Taifa na Idara ya Uhamiaji ni moja kati ya vielelezo vya utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuwapatia Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji nyumba 103.”

Pia, Waziri Mkuu amesema “Nyote mtakubaliana nami kwamba leo ni siku muhimu kwa sekta ya nyumba kwani ujenzi wa nyumba za namna hii ni muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa huduma bora kwenye Taasisi za Serikali sambamba na kuboresha ufanisi wa wafanyakazi wetu.”

“Vilevile, utekelezaji wa mradi huu umetoa ajira zipatazo 1,000 ikiwa ni sawa na ajira 800 za mafundi na ajira 200 kwa watoa huduma za chakula yaani mama lishe. Upatikanaji wa ajira hizo umechangia kuongeza kipato kwa walengwa na kusaidia kujikwamua dhidi ya umaskini.”

Amesema ujenzi wa majengo hayo ni mwendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 inayosisitiza ujenzi wa majengo ya ofisi na makazi kwa watumishi wa umma kwa lengo la kuipunguzia Serikali gharama kubwa ya kodi ya pango pamoja na kuimarisha utendaji na uwajibikaji wa watumishi wa umma katika kuwahudumia Watanzania.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Shirika la Nyumba la Taifa, kuendelea na kazi nzuri ya ujenzi wa nyumba za makazi pamoja na biashara kwani lengo la Ilani ya CCM ya mwaka 2015 ni kuliwezesha Shirika la Nyumba la Taifa kuwa Mwendelezaji Miliki Mkuu.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema watendaji wa shirika hilo wanapaswa kuongeza kasi ya ukusanyaji kodi ili kuongeza mapato ya shirika. “Serikali kwa upande wake, itaendelea kutoa Ushirikiano wa karibu kwa Shirika katika kutatua changamoto zinazokabili utekelezaji wa malengo ya shirika hili.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Idara ya Uhamiaji kwa kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka pamoja na kufanikisha maboresho mbalimbali kama vile Uhamiaji Mtandao ambapo sasa huduma za pasipoti, vibali vya ukaazi, viza, usimamizi na udhibiti wa mipaka vinafanyika kwa njia ya kielektroniki. “Utekelezaji mzuri wa mageuzi ya Uhamiaji Mtandao umewezesha idara hii kupata tuzo ya ushindi wa pasipoti yenye ubora duniani kwa mwaka 2019.”

Waziri Mkuu amesema ushindi huo, umelipatia sifa na heshima kubwa Taifa Kimataifa. “Halikadhalika, nimefurahishwa na taarifa kuwa ujenzi wa Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji, Dodoma nao unaendelea vizuri. Ninawahimiza endeleeni hivyo kwa mustakabali wa ustawi wa Taifa letu.”

Awali, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwezesha Idara ya Uhamiaji, kupata nyumba 103 za makazi kwa ajili ya Maafisa na Askari wa Uhamiaji kwani hatua hiyo ni kielelezo cha vipaumbele vya Serikali katika kuboresha makazi ya askari wa vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama pamoja na wananchi kwa ujumla.

“Aidha, tunalipongeza pia Shirika la Nyumba la Taifa, kwa kubuni mradi mkubwa kwa ajili ya kuboresha mazingira ya makazi ya Wananchi kwa kujenga na kuuza nyumba kwa bei nafuu, ambapo nasi tumekuwa wanufaika wa mradi huu. Gharama za nyumba 103 za makaazi ya watumishi wa Idara ya Uhamiaji, ni kiasi cha sh. 5,306,000,000.”

Alisema upatikanaji wa nyumba hizo utasaidia Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji kuishi katika maeneo yao maalum, badala ya ilivyokuwa hapo awali ambapo walilazimika kutafuta nyumba za makazi uraiani. Sambamba na hilo, itasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi yetu, kwani itakuwa ni rahisi kuwapata askari walio katika eneo moja mara wanapohitajika.

Makabidhiano hayo yameshuhudiwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Dkt. Maulid Banyani, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mary Makondo  na Maafisa wengine wa Serikali.  


MWISHO

Read More