Tuesday, February 28, 2017

WAZIRI MKUU ANUSA MADUDU MINADA YA MADINI

*Amuagiza Kamishna wa Madini aende Mererani
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema anafuatilia kwa makini minada ya madini inayofanyika nchini kwa sababu anazo taarifa za kukiukwa utaratibu kwenye minada hiyo.

Amesema ukiukwaji huo unachangia kutobadilika kwa mapato ya mauzo yatokanayo na mnada hata kama kuna vito viliyokakatwa au havijakatwa.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Februari 27, 2017) wakati akihitimisha kikao alichokiitisha kwenye makazi yake Oysterbay jijini Dar es Salaam kilichojumuisha Mawaziri wa Fedha pamoja na Nishati, Mkuu wa Mkoa wa Manyara na watendaji wake, Mbunge wa Simanjiro, wamiliki wa mgodi wa Tanzanite One, watumishi waliofukuzwa kazi na wachimbaji wadogo. 

Alisema licha ya kuwa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito cha Wizara ya Nishati na Madini (TANSORT) kinasifiwa kwa kuongeza mapato ya madini, bado kuna kazi ya ziada inabidi ifanyike kwenye minada hiyo ili Serikali iweze kunufainika na madini hayo.

“Uzoefu wa kwenye minada ya korosho unaonyesha kuwa wanaushirika ndiyo wanaiba fedha za wakulima. Nimekuwa ninafuatilia kwa muda sasa uendeshaji wa hii minada na sijaridhishwa na uendeshaji wake. Hakuna tofauti ya bei madini ya Tanzanite yanapokuwa yamekatwa au la,” alisema.

Kwa mujibu wa wataalamu wa madini na vito, inapotokea kuna madini yamekatwa bei inapaswa kuwa juu ikilinganishwa na madini ghafi yanapouzwa moja kwa moja.

Amemuagiza Kaimu Kamishna wa Madini, Bw. Benjamini Mchwampaka (ambaye alihudhuria kikao hicho kwa niaba ya Kamishna wa Madini) aende Mererani na kufuatilia utendaji kazi wa mgodi wa Tanzanite One na suala zima la teknolojia zinazotumika kiwandani hapo.

Waziri mkuu aliitisha kikao hicho kufuatia ahadi aliyoitoa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Mererani, wilayani Simanjiro, mkoani Manyara Februari 16, 2017 kwamba akimaliza ziara ya mkoa huo ataitisha kikao na wawekezaji wa Tanzanite One baada ya kupokea malalamiko kwamba hali ya watumishi ilikuwa nafuu wakati kampuni hiyo ilipokuwa inamilikiwa na wazungu kuliko ilivyo hivi sasa.

Ili kuhakikisha ukusanyaji wa mapato katika sekta ya madini unaongezeka, Waziri Mkuu amemwagiza Kamishna wa Mamlaka ya Mapato (TRA) aimarishe ukaguzi kwenye viwanja wa ndege vya Arusha na Kilimanjaro (KIA),

“Kamishna wa TRA na watu wako inabidi mjipange kwa sababu kuna njia nyingi za ukwepaji kodi zinafanyika kwenye sekta ya madini wakiwemo hata hawa wachimbaji wadogo. Simamieni utaratibu wa kufuatilia kodi, nendeni kule walipo, msisubiri waje kuwaletea malipo ofisini. Wasipokuja je? Au wakija wakakuta mmetoka ofisini je?” Alihoji Waziri Mkuu.

Akizungumzia kuhusu uelewa wa sheria miongoni mwa wachimbaji wadogo, Waziri Mkuu alisema Wizara ya Nishati na Madini kupitia kwa Kamishna wa Madini wanapaswa kutoa elimu na uelewa wa kisheria kwa wachimbaji hao ili kupunguza migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza kwenye maeneo mengi nchini.

“STAMICO na Kamishna wa Madini fanyeni kazi pamoja, waelewesheni wachimbaji wadogo kuwa uwepo wa vitalu maana yake kuna mipaka ambayo pia inajumisha utoaji wa leseni kwa wenye vitalu hivyo. Kwa hiyo, waelimisheni kuwa mtu hapaswi kwenda upande wa pili wa mtu mwenye leseni, akifanya hivyo atakuwa anavunja sheria.” 

“Ninyi ni wadau wakubwa wa sekta hii kwa hiyo mnapaswa kushiriki katika zoezi la kutoa elimu. Mnayo maeneo mengi ya uchimbaji lakini yana migogoro, mfano ni kule Ngaka na Kiwira. Maeneo yote haya yanahitaji usimamizi mzuri. Mnayo Bodi, Mwenyekiti yupo kwa hiyo mnatosha kuifanya kazi hii,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wamiliki wa mgodi wa Tanzanite One waboreshe mahusiano yao na vijiji vilivyo jirani na mgodi huo. “Kuweni karibu na wananchi ili wajue umuhimu wenu na uwepo wenu na waweze kusaidia kulinda mali zenu. Shirikianeni na Halmashauri na Baraza la Madiwani, tangazeni kazi zenu za CSR ili wananchi wajue mmechangia nini katika kusaidia maendeleo yao,” alisema.

Kuhusu suala la watumishi waliofukuzwa kazi kwenye mgodi huo, Waziri Mkuu amemwagiza Katibu Mkuu (OWM-Kazi, Ajira na Vijana), Bw. Erick Shitindi asimamie suala lao na kuwapatia majibu kuhusu hatma ya suala hilo.

Watumishi hao walikuwa wanawakilisha wenzao 201 ambao walifukuzwa kazi Februari 8, 2016 kwa sababu ya kufuatilia maslahi yao vikiwemo malipo ya saa za kazi za ziada (overtime), mishahara ya miezi miwili, malipo ya NSSF, vitendea kazi na usalama wa kazi migodini.


Read More

WAZIRI MKUU ANUSA MADUDU MINADA YA MADINI

Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika kikao alichokiitisha kuhusu masuala ya madini kati yake na viongozi wa Serikali, viongozi wa kampuni ya uchimbaji madini ya Tanzanite One na baadhi ya wachimbaji wadogo,kwenye makazi yake, Oysterbay jijini Dar es salaam jana  Februari 27, 2017.
Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa akisisitiza jambo katika kikao alichokiitisha kuhusu masuala ya madini kati yake na viongozi wa Serikali, viongozi wa kampuni ya uchimbaji madini ya Tanzanite One na baadhi ya wachimbaji wadogo ,kwenye Makazi yake Oysterbay jijini Dar es salaam jana  Februari 27, 2017
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimsikiliza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipokuwa akifafanua jambo katika kikao kilichoitishwa na Waziri Mkuu kwenye Makazi yake Oysterbay jijini Dar es salaam Februari 27, 2017, kwa ajili ya kujadili masuala ya madini. Watatu kushoto ni Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango na  ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dkt. Joel Bendera.

Read More

Sunday, February 26, 2017

MIAKA 100 YA USKAUTI TANZANIA IFANYIKE DODOMA - MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekiagiza Chama cha Maskauti (TSA) nchini kifanye sherehe zake za maadhimisho ya miaka 100 ya uskauti Tanzania Makao Makuu Dodoma.

Ameiagiza pia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupitia Halmashauri zote iandae utaratibu wa kuwezesha watoto nchini washiriki maadhimisho hayo kwa gharama zake ili waweze kuona na kujifunza (live) kuhusu uskauti na iwe rahisi kuueneza kwa wenzao.

Alitoa maagizo hayo mwishoni mwa wiki katika hafla ya chakula cha hisani kuchangia maadhimisho ya Siku ya Skauti Afrika na miaka 100 ya Uskauti Tanzania.

Awali, chama hicho kilipanga sherehe za Siku ya Uskauti Afrika zifanyike Machi 8-11 Jijini Arusha na Maadhimisho ya Miaka 100 ya Uskauti Tanzania zifanyike Juni 24 hadi Julai 1 mwaka huu katika eneo ambalo lingetajwa baadaye.

Agizo hilo la Waziri Mkuu limetaka sherehe hizo mbili ziunganishwe kuwa moja na ifanyike Makao Makuu Dodoma, pamoja na mambo mengine, kuenzi uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma.

“Nashauri muone uwezekano wa kuunganisha matukio haya mawili yaani Maadhimisho ya miaka 100 na Siku ya Skauti Afrika yafanyike kwa pamoja na kwa bajeti ndogo, ili fedha zitakazookolewa ziweze kutumika kwenye program mbalimbali za kuhamasisha uskauti kote nchini.”

Pia aliwashauri wabuni njia nyingine za kupata michango kama vile kuwa na mechi ya mpira wa miguu, mabonanza ya muziki, bahati nasibu au hata kampeni ya uchangiaji kupitia makampuni ya simu za mkononi ili waweze kukusanyafedha za kutosha kwa ajili ya maandalizi ya tukio hilo kubwa.

Waziri Mkuu alisema kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, nusu ya Watanzania ni vijana na kama Taifa linataka kuwa lenye ustawi, kila mwananchi hana budi kuwekeza kwenye makuzi mema ya vijana. “Natamani sana watoto wote wa Tanzania wangepitia kwenye mafunzo ya uskauti ili wawe wakakamavu na wazalendo kwa nchi yao,” alisema.

“Serikali inapopambana  na uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya, matumizi holela ya pombe za viroba, mimba za utotoni na  mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ili kuboresha huduma za kijamii, lengo lake ni kujenga kesho iliyo bora ya vijana wetu,” alisisitiza.

“Chama cha Skauti kama moja ya taasisi kongwe hapa nchini inayojihusisha na malezi ya vijana ni mdau muhimu sana wa kushirikiana na Serikali katika malezi ya vijana wetu. Tunaposhuhudia makundi kama ‘Panya Road’, ongezeko la vijana wenye uraibu wa dawa za kulevya na ongezeko la mimba za utotoni ni lazima tuhoji nafasi ya wazazi kwenye malezi ya watoto wetu,” alisema.

“Sambamba na kuhoji huko, tunadhani ni wakati muafaka pia kwa Chama cha Skauti nacho kijitathmini endapo bado kina ushawishi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, na endapo kuna jambo linaweza kufanyika ili kurekebisha hali hiyo,” alisisitiza.

Alitumia fursa hiyo kuiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iweke msisitizo kwa kila shule nchini kuhakikisha watoto wanafundishwa ukakamavu na malezi ya uskauti.

Katika hafla hiyo, Waziri Mkuu alifanikiwa kuchangisha jumla ya sh. 265,170,500.00 zikiwa ni ahadi na fedha taslimu.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzumgumza na wageni waalikwa, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, ambaye pia ni Rais wa Skauti Tanzania, aliwaomba Watanzania na makampuni binafsi wachangie ili kukiwezesha Chama cha Maskauti nchini kufanikisha sherehe hizo muhimu.

Alisema chama hicho kimepanga kukusanya shilingi milioni 600 ili kufanikisha sherehe hizo.

Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa Maskauti Tanzania, Bw. Abdulkarim Shah wakati maskauti wa Tanzania watakuwa wakiadhimisha miaka 100 ya Uskauti Tanzania, mwaka huu wamepewa heshima ya kuwa wenyeji sherehe za Siku ya Uskauti ya Bara la Afrika.

Alisema lengo la chama hicho ni kuwalea watoto wa Kitanzania na kuwakuza kimaadili, kiakili, kielimu na kiroho. Alisema kaulimbiu ya mwaka huu ni “Kuwahamasisha Vijana Kuwa Raia Bora Wenye Kuwajibika na Kuhimiza Ustawi wa Amani, Utamaduni, Maadili na Maendeleo Endelevu  kwa ajili ya Dunia Bora Zaidi.”
Read More

Wednesday, February 22, 2017

MAJALIWA AZUNGUMZA NA WATUMISHI NA KUHUTUBIA MKUTANO WA HADHARA MJINI BABATI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akihutubia Mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Kwaraa mjini Babati  kuhitimisha  ziara ya mkoa wa Manyara, Februari 22, 2017.
Baadhi ya  watumishi wa serikali na Halmashauri za mkoa wa Manyara wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao kwenye viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Februari 22, 2017.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa serikali na Halmashauri za mkoa wa Manyara kwenye viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Februari 22, 2017. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt. Joel Bendera.
Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa akiwapungia wananchi wa Babati wakati alipowasili kwenye uwanja wa Kwaraa mjini Babati kuhutubia mkutano wa hadhara, Februari 22, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na wazee  wakati alipoingia kwenye uwanja wa Kwaraa mjini Babati,  kuhutubia mkutano wa hadhara Februari 22, 2017.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akihutubia Mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Kwaraa mjini Babati  kuhitimisha  ziara ya mkoa wa Manyara, Februari 22, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na wazee  wakati alipoingia kwenye uwanja wa Kwaraa mjini Babati,  kuhutubia mkutano wa hadhara Februari 22, 2017.


Read More

ZIARA YA MAJALIWA BABATI

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la Msingi la daraja la Bonga- Endanachan wilayani Babati,  Februari 22, 2017.  Kulia ni Mkoa wa Manyara, Dkt, Joel Bendera na kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Babati, Raymound Mushi.
Baba mmoja ambaye jina lake halikupatikana akiwa amembeba mwanae kwa mtindo wa 'Kangaroo Style' wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipozungumza na wanakijiji  wa Singu wilayani  Babati, Februari  21, 2017.

Read More

Tuesday, February 21, 2017

MAJALIWA AZINDUA MADARASA NA KUHUTUBIA MKUTANO WA HADHARA MJINI KATESH

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua madarasa ya Shule ya Msingi ya Mogitu wilayani Hanang Februari 21, 2017. Kulia kwake ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Eliakim Maswi na wapili kulia kwake ni Mbunge wa hanang, Dkt. Mary Nagu.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia Mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Katesh wilayani Hanang, Februari 21, 2017.
Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akimkabidhi zawadi ya Shilingi 500,000/= mzee Giloya Semhonda  ikiwa ni shukurani kwa usimamizi wake mzuri wa ujenzi na ukarabati wa madarasa ya shule ya msingi ya Mogitu wilayani Hanang baada ya uzindu madarasa hayo Februari 21, 2017.  Fedha hizo zilitolewa na Mkuuu wa Mkoa wa Manyara,  Dkt. Joel Bendera.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika apicha ya pamoja na Walimu wa Shule ya Msingi ya Mogitu wilayani Hanang baada ya kuzindua madarasa ya shule hiyo, Februari 21, 2017. Watatu kulia ni Mbunge wa Hanang, Dkt. Mary Nagu.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na Walimu wa Shule ya Msingi ya Mogitu Wilayani Hanang baada ya kuzindua madarasa ya shule hiyo  Februari 21, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama ngoma ya asili ya kabila la Wanyaturu kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Katesh wilayani Hanang Februari 21, 2017.


Read More

BARABARA ZA LAMI KUUFUNGUA MKOA WA MANYARA

*Ni kutoka Karatu-Mbulu-Haydom-Sibiti-Lalago hadi Meatu
*Nyingine ni ya kutoka Haydom hadi Katesh
*Limo pia daraja la Magara linalounganisha Mbulu na Babati

SERIKALI imepanga kujenga barabara mbili kuu za lami ambazo zikikamilika zitasaidia kuunganisha mikoa mitano ya Arusha, Singida, Simiyu, Shinyanga na Manyara.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa kauli hiyo jana (Jumatatu, Februari 20, 2017) kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Haydom na Mbulu Mjini kwenye mikutano wa hadhara iliyofanyika wilayani Mbulu, mkoani Manyara.

Waziri Mkuu amezitaja barabara hizo kuwa ni ya kutoka Karatu-Mbulu-Haydom-Sibiti-Lalago- Meatu hadi Maswa yenye urefu wa km. 389 (maarufu kama Serengeti Southern Bypass) na nyingine ni ya kutoka Haydom hadi Katesh yenye urefu wa km. 74. Pia limo daraja la Magara linalounganisha Mbulu na Babati.

Amesema anatambua umuhimu wa barabara hizo na kwamba kukamilika kwake kutaharakisha kuufungua mkoa huo na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wakazi wake.

“Fedha kwa ajili ya upembuzi wa awali imeshatolewa na kazi imeshaanza kwa ajili ya barabara ya kutoka Karatu-Mbulu-Haydom-Sibiti-Lalago hadi Meatu na Maswa lakini hii ya Katesh hadi Haydom itaombewa fedha kwenye bajeti tunayoiandaa hivi sasa.”

“Lengo letu ni kuona hospitali ya rufaa ya Haydom inafikiwa kwa urahisi zaidi.La sivyo wagonjwa watakaoletwa hapa watafika wakiwa hoi zaidi,” ameongeza.

Akizungumzia kuhusu hoja ya ujenzi wa daraja la Maraga ambayo iligusiwa na wabunge wote wa mkoa huo, Waziri Mkuu alisema: “Waheshimiwa wabunge wasemea vikali kuhusu daraja la Maraga. Napenda kuwathibitishia kwamba Serikali imeshatoa kiasi cha sh. milioni 950 kwa ajili ya ujezi wa daraja hili muhimu ambalo linaunganisha wilaya zetu za Mbulu na Babati.”

Akizungumzia ahadi ya Mheshimiwa Rais Dk. John Pombe Magufuli kuhusu ujenzi wa barabara ya lami wa km. 5 Haydom, km. 6 Dongobesh na km. 5 mji wa Mbulu, Waziri Mkuu alisema analibeba suala na kulipekea kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa ili alifuatilie.

Kuhusu tatizo la maji, Waziri Mkuu alisema Serikali imeshatoa kiasi cha milioni 200 kwa ajili ya Mamlaka ya Maji ya Mji wa Mbulu ili wafanye utafiti wa vyanzo vya maji vya uhakika na pia imetoa sh. milioni 300 kwa ajili ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ili watafute maeneo ya uhakika ya kuchimba visima.

“Huku kwenye Halmashauri vijiji ni vingi. Kwa hiyo tumetoa sh. Milioni 300 ili watafute ni wapi wanaweza kuchimba visima virefu na vya kati ili kuondoa tatizo hili kwa wananchi wetu. Mkurugenzi wa Halmashauri sisitiza wataalamu wako watafute vyanzo hivina watumie fedha hizi vizuri,” alisisitiza.

Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake ya kikazi ya siku sita mkoani Manyara kwa kutembelea wilaya ya Hanang ambako atapokea taarifa ya wilaya hiyo atazungumza na watumishi wa umma, na kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara.

Read More

MAJALIWA AWASALIMIA WANANCHI WA BASHNET

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi wa kijiji cha Bashnet wilayani Mbulu wakati aliposimama kijijini hapo akitoka Mbulu kwenda Hanang Februari 21, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi wa kijiji cha Bashnet wilayani Mbulu wakati aliposimama kijijini hapo akitoka Mbulu kwenda Hanang Februari 21, 2017.

Read More

MAJALIWA AHUTUBIA MKUTANO WA HADHARA MBULU

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimiana wanakwaya wa Shule ya Sekondari ya Singiland wilayani Mbulu wakati alipowasili kwenye uwanja wa michezo wa Mbulu kuhutubia Mkutano wa hadhara, Februari 20, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa michezo wa Mbulu mkoani Manyara, Februari 20, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa michezo wa Mbulu mkoani Manyara, Februari 20, 2017.
Read More

Monday, February 20, 2017

WAZIRI MKUU: HOSPITALI YA HAYDOM KUPANDISHWA HADHI

Waziri MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haina kipingamizi na wazo la kuifanya hospitali ya rufaa ya Haydom kuwa ya kanda kwani hatua hiyo itaupunguzia mzigo Serikali.

“Serikali hii ni sikivu, na kuifanya hospitali hii kuwa ya kanda ni kazi ndogo. Kwa hiyo nitamleta Waziri wa Afya aje awaongoze kusimamia vigezo vya kuifanya hospitali hii iwe ya kanda,” amesema.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumatatu, Februari 20, 2017) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa kata ya Haydom kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa kata.

"Serikali haina kipingamizi na wazo lenu, cha msingi ni vigezo muhimu vifuatwe. Kwa hiyo, nitamleta Waziri wa Afya awasaidie kuangalia vigezo," amesisitiza.

“Kama vigezo havipo, tushirikiane kuvikamilisha kwa sababu uwepo wa hospitali hii kwa hadhi ya kanda kunaisadia Serikali kutokana na nafasi yake kijiografia,” amesema Waziri Mkuu

“Nia yetu ni kupunguza gharama kwa mgonjwa anayelazimika kutoka Simiyu hadi Bugando (Mwanza) au kutoka Arusha hadi Muhimbili (Dar es Salaam).  Hapa ni katikati na nimearifiwa kuwa wagonjwa kutoka mikoa mitano ya Tabora, Simiyu, Arusha, Singida na Manyara wanafika hapa kupatiwa matibabu,” amesema.

Amesema Serikali imepokea maombi kwa ajili ya watumishi wanaotakiwa kwenye hospitali hiyo na kwamba hivi karibuni itaajiri watumishi kati ya 5,000 hadi 6,000 wa sekta ya afya peke yake. “Tumekwishaanza kuajiri, tumeanza na sekta ya elimu kwa kuajiri walimu 4,693 ambao wote ni wa fani ya sayansi. Na sekta inayofuata ni ya afya, kwa hiyo hao watumishi 90 wanaohitajika watapatikana kwenye kundi hilo hilo,” amesema.

Hospitali hiyo inahudumia wananchi kutoka wilaya nane za Mbulu, Hanang, Babati, Karatu, Mkalama, Iramba, Kondoa na Meatu.

Wakati huohuo, Balozi wa Norway nchini Tanzania, Bibi Hannamarie Kaarstad ambaye alikuwepo kwenye mkutano huo, alisema amefarijika na mchango unaotolewa na Serikali ya Tanzania kusaidia juhudi zinazofanywa na marafiki wa hospitali walioko Norway.

“Hospitali ya Haydom ni mahali thabiti ambapo mshikamano baina ya Tanzania na Norway unaweza kuonekana kwa dhahiri. Nawashukuru watumishi wa hospitali kwa moyo wao wa kujitoa kuwahudumia wananchi wa wilaya ya Mbulu na maeneo ya jirani,” amesema.

Hospitali hiyo ambayo inaendeshwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mbulu kwa ufadhili kutoka Serikali za Tanzania na Norway, ilianzishwa mwaka 1955 ikiwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 50. Hivi sasa ina uwezo wa kulaza wagonjwa 420 kwa wakati mmoja.

Pia inatoa huduma za upasuaji, magonjwa ya macho, tiba ya mifupa na mazoezi ya viungo. Ilipandishwa hadhi kuwa ya rufaa baada ya mkoa wa Manyara kuanzishwa.

Mapema, akisoma taarifa kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa Tiba wa hospitali hiyo, Dk. Emanuel Q. Nuwass alisema wameomba kibali cha ajira kwa watumishi 90 kupitia bajeti ya mwaka 2016/2017.

“Tumeomba pia hospitali ipandishwe hadhi na kuwa ya rufaa ya kanda (Kaskazini kati au Kanda maalum) ili iweze kutoa huduma bora kwa mkoa wa Manyara na mikoa jirani kwani wahisani wa maendeleo wako tayari kuchangia ujenzi wa miundombinu,” alisema.

Pia aliomba waongezewe ruzuku ya dawa ikilinganishwa na ya sasa hivi ambayo ni asilimia 15 na pia waongezwe malipo ya on call allowance kwa ajili ya madaktari na watumishi wengine wa hospitali hiyo.

Read More