Tuesday, February 21, 2017

BARABARA ZA LAMI KUUFUNGUA MKOA WA MANYARA

*Ni kutoka Karatu-Mbulu-Haydom-Sibiti-Lalago hadi Meatu
*Nyingine ni ya kutoka Haydom hadi Katesh
*Limo pia daraja la Magara linalounganisha Mbulu na Babati

SERIKALI imepanga kujenga barabara mbili kuu za lami ambazo zikikamilika zitasaidia kuunganisha mikoa mitano ya Arusha, Singida, Simiyu, Shinyanga na Manyara.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa kauli hiyo jana (Jumatatu, Februari 20, 2017) kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Haydom na Mbulu Mjini kwenye mikutano wa hadhara iliyofanyika wilayani Mbulu, mkoani Manyara.

Waziri Mkuu amezitaja barabara hizo kuwa ni ya kutoka Karatu-Mbulu-Haydom-Sibiti-Lalago- Meatu hadi Maswa yenye urefu wa km. 389 (maarufu kama Serengeti Southern Bypass) na nyingine ni ya kutoka Haydom hadi Katesh yenye urefu wa km. 74. Pia limo daraja la Magara linalounganisha Mbulu na Babati.

Amesema anatambua umuhimu wa barabara hizo na kwamba kukamilika kwake kutaharakisha kuufungua mkoa huo na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wakazi wake.

“Fedha kwa ajili ya upembuzi wa awali imeshatolewa na kazi imeshaanza kwa ajili ya barabara ya kutoka Karatu-Mbulu-Haydom-Sibiti-Lalago hadi Meatu na Maswa lakini hii ya Katesh hadi Haydom itaombewa fedha kwenye bajeti tunayoiandaa hivi sasa.”

“Lengo letu ni kuona hospitali ya rufaa ya Haydom inafikiwa kwa urahisi zaidi.La sivyo wagonjwa watakaoletwa hapa watafika wakiwa hoi zaidi,” ameongeza.

Akizungumzia kuhusu hoja ya ujenzi wa daraja la Maraga ambayo iligusiwa na wabunge wote wa mkoa huo, Waziri Mkuu alisema: “Waheshimiwa wabunge wasemea vikali kuhusu daraja la Maraga. Napenda kuwathibitishia kwamba Serikali imeshatoa kiasi cha sh. milioni 950 kwa ajili ya ujezi wa daraja hili muhimu ambalo linaunganisha wilaya zetu za Mbulu na Babati.”

Akizungumzia ahadi ya Mheshimiwa Rais Dk. John Pombe Magufuli kuhusu ujenzi wa barabara ya lami wa km. 5 Haydom, km. 6 Dongobesh na km. 5 mji wa Mbulu, Waziri Mkuu alisema analibeba suala na kulipekea kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa ili alifuatilie.

Kuhusu tatizo la maji, Waziri Mkuu alisema Serikali imeshatoa kiasi cha milioni 200 kwa ajili ya Mamlaka ya Maji ya Mji wa Mbulu ili wafanye utafiti wa vyanzo vya maji vya uhakika na pia imetoa sh. milioni 300 kwa ajili ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ili watafute maeneo ya uhakika ya kuchimba visima.

“Huku kwenye Halmashauri vijiji ni vingi. Kwa hiyo tumetoa sh. Milioni 300 ili watafute ni wapi wanaweza kuchimba visima virefu na vya kati ili kuondoa tatizo hili kwa wananchi wetu. Mkurugenzi wa Halmashauri sisitiza wataalamu wako watafute vyanzo hivina watumie fedha hizi vizuri,” alisisitiza.

Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake ya kikazi ya siku sita mkoani Manyara kwa kutembelea wilaya ya Hanang ambako atapokea taarifa ya wilaya hiyo atazungumza na watumishi wa umma, na kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.