Tuesday, February 14, 2017

MAMA MAGUFULI NA MAMA MAJALIWA WATEMBELEA GEREZA TABORA


MKE wa Rais Mheshimiwa Mama Janeth Magufuli pamoja na Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa wametembelea Gereza la Mahabusu Tabora na kutoa zawadi mbalimbali kwa wafungwa na mahabusu gerezani hapo.

Wake wa viongozi wametembelea gereza hilo leo (Jumanne, Februari 14, 2017)  wakiwa katika ziara  mkoani Tabora, ambapo Mama Janeth amesema wameamua kuwatembelea wafungwa na mahabusu hao kwa nia ya kuwafariji kwa kuwa wao ni sehemu ya jamii.

“Vitabu vitakatifu vinasema kwamba ukiwasaidia watu wenye mahitaji utakuwa umetoa sadaka kubwa kwa Mwenyezi Mungu, hivyo tumeamua kuja kutembea  wafungwa na mahabusi kwenye gereza hili na kuwapa zawadi kwa kuwa nanyi mnahitaji faraja,” amesema.

Amesema wameamua kwenda kuwaona wafungwa na mahabusu hao kwa lengo la kuwafariji na kuwatia moyo kwa sababu wanaimani kwamba wakitoka watakuwa raia wema na hayo wanayopitia ni sehemu ya kufanya marekebisho ya tabia.

“Ni siku kubwa kwangu, nimejifunza mengi baada ya kufika hapa. Kitendo cha kwenda kuwaona wenye mahitaji wakiwemo wagonjwa, wafungwa ni jambo jema tunaamini hizi zawadi tulizozitoa zitawasaidia kwa sababu tunajua mnamahitaji mengi,” amesema.

Katika gereza hilo wake hao wa viongozi wamekabidhi zawadi mbalimbali kwa wafungwa na mahabusu, ambapo mwakilishi wa wafungwa hao Deo Kitave aliwashukuru kwa niaba ya wenzake. “Tunawashukuru kwa kutukumbuka, tunamuomba Mwenyezi Mungu muendelee kuwa na moyo huo,”.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.