Sunday, February 26, 2017

MIAKA 100 YA USKAUTI TANZANIA IFANYIKE DODOMA - MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekiagiza Chama cha Maskauti (TSA) nchini kifanye sherehe zake za maadhimisho ya miaka 100 ya uskauti Tanzania Makao Makuu Dodoma.

Ameiagiza pia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupitia Halmashauri zote iandae utaratibu wa kuwezesha watoto nchini washiriki maadhimisho hayo kwa gharama zake ili waweze kuona na kujifunza (live) kuhusu uskauti na iwe rahisi kuueneza kwa wenzao.

Alitoa maagizo hayo mwishoni mwa wiki katika hafla ya chakula cha hisani kuchangia maadhimisho ya Siku ya Skauti Afrika na miaka 100 ya Uskauti Tanzania.

Awali, chama hicho kilipanga sherehe za Siku ya Uskauti Afrika zifanyike Machi 8-11 Jijini Arusha na Maadhimisho ya Miaka 100 ya Uskauti Tanzania zifanyike Juni 24 hadi Julai 1 mwaka huu katika eneo ambalo lingetajwa baadaye.

Agizo hilo la Waziri Mkuu limetaka sherehe hizo mbili ziunganishwe kuwa moja na ifanyike Makao Makuu Dodoma, pamoja na mambo mengine, kuenzi uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma.

“Nashauri muone uwezekano wa kuunganisha matukio haya mawili yaani Maadhimisho ya miaka 100 na Siku ya Skauti Afrika yafanyike kwa pamoja na kwa bajeti ndogo, ili fedha zitakazookolewa ziweze kutumika kwenye program mbalimbali za kuhamasisha uskauti kote nchini.”

Pia aliwashauri wabuni njia nyingine za kupata michango kama vile kuwa na mechi ya mpira wa miguu, mabonanza ya muziki, bahati nasibu au hata kampeni ya uchangiaji kupitia makampuni ya simu za mkononi ili waweze kukusanyafedha za kutosha kwa ajili ya maandalizi ya tukio hilo kubwa.

Waziri Mkuu alisema kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, nusu ya Watanzania ni vijana na kama Taifa linataka kuwa lenye ustawi, kila mwananchi hana budi kuwekeza kwenye makuzi mema ya vijana. “Natamani sana watoto wote wa Tanzania wangepitia kwenye mafunzo ya uskauti ili wawe wakakamavu na wazalendo kwa nchi yao,” alisema.

“Serikali inapopambana  na uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya, matumizi holela ya pombe za viroba, mimba za utotoni na  mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ili kuboresha huduma za kijamii, lengo lake ni kujenga kesho iliyo bora ya vijana wetu,” alisisitiza.

“Chama cha Skauti kama moja ya taasisi kongwe hapa nchini inayojihusisha na malezi ya vijana ni mdau muhimu sana wa kushirikiana na Serikali katika malezi ya vijana wetu. Tunaposhuhudia makundi kama ‘Panya Road’, ongezeko la vijana wenye uraibu wa dawa za kulevya na ongezeko la mimba za utotoni ni lazima tuhoji nafasi ya wazazi kwenye malezi ya watoto wetu,” alisema.

“Sambamba na kuhoji huko, tunadhani ni wakati muafaka pia kwa Chama cha Skauti nacho kijitathmini endapo bado kina ushawishi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, na endapo kuna jambo linaweza kufanyika ili kurekebisha hali hiyo,” alisisitiza.

Alitumia fursa hiyo kuiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iweke msisitizo kwa kila shule nchini kuhakikisha watoto wanafundishwa ukakamavu na malezi ya uskauti.

Katika hafla hiyo, Waziri Mkuu alifanikiwa kuchangisha jumla ya sh. 265,170,500.00 zikiwa ni ahadi na fedha taslimu.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzumgumza na wageni waalikwa, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, ambaye pia ni Rais wa Skauti Tanzania, aliwaomba Watanzania na makampuni binafsi wachangie ili kukiwezesha Chama cha Maskauti nchini kufanikisha sherehe hizo muhimu.

Alisema chama hicho kimepanga kukusanya shilingi milioni 600 ili kufanikisha sherehe hizo.

Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa Maskauti Tanzania, Bw. Abdulkarim Shah wakati maskauti wa Tanzania watakuwa wakiadhimisha miaka 100 ya Uskauti Tanzania, mwaka huu wamepewa heshima ya kuwa wenyeji sherehe za Siku ya Uskauti ya Bara la Afrika.

Alisema lengo la chama hicho ni kuwalea watoto wa Kitanzania na kuwakuza kimaadili, kiakili, kielimu na kiroho. Alisema kaulimbiu ya mwaka huu ni “Kuwahamasisha Vijana Kuwa Raia Bora Wenye Kuwajibika na Kuhimiza Ustawi wa Amani, Utamaduni, Maadili na Maendeleo Endelevu  kwa ajili ya Dunia Bora Zaidi.”


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.