Thursday, February 9, 2017

CAG KUCHUNGUZA MAPATO YA SHIRIKA LA NDEGE TANZANIA-MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atamuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuchunguza ukusanyaji wa mapato ya Shirika la Ndege la Tanzania(ATCL).

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamis, Februari 9, 2017) alipotembelea Makao Makuu ya shirika hilo Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujionea mwenendo wa uendeshaji wake.

“Nitamuagiza CAG  aje aangalie mwenendo wa ukusanyaji wa mapato ya shirika hili kuanzia mwaka jana lilipoanza kufanya kazi hadi sasa,” amesema.

Waziri Mkuu amesema Serikali haiko tayari kuona shirika hilo linakufa tena, hivyo amewataka viongozi wake wahakikishe linaendeshwa kwa mafanikio kwa manufaa ya Taifa.

Pia amewataka waache kukusanya mapato kwa kutumia  risiti za kuandika kwa mkono na badala yake waanze kutumia mfumo wa kieletroniki ili kuzuia upotevu wa mapato hayo.

“Vitu vingi vinavyoenda manual ni rahisi kufa. Serikali tumeagiza malipo yote yafanyike kielektroniki na kote tunakotumia mfumo huu tumepata mafanikio,”amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemtaka Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Bi. Witness Mbaga ajiridhishe na fedha zinazokusanywa katika eneo la mizigo kama ziko sahihi, lengo ni kudhibiti upotevu wa mapato.

Hata hivyo Waziri Mkuu amewataka viongozi wa shirika hilo kuhakikisha wanazingaria ratiba ya njia na muda wa safari ili wasipoteze wateja.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.