Tuesday, February 7, 2017

WAZIRI MKUU AWATAKA MABALOZI KUTAFUTA WAWEKEZAJI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka mabalozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali kuhakikisha wanatumia uwakilishi wao kutafuta wawekezaji watakaokuja kuwekeza katika sekta ya viwanda nchini.

Amesema  mkakati wa Serikali ni kuimarisha uchumi  hadi wa kati kupitia sekta ya viwanda, hivyo jukumu la mabalozi hao ni kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Februari 7, 2017) alipokutana na mabalozi wa wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi za Uturuki, Brazil, China, Italy, Ufaransa, Jamuhuri ya Kidemkrasi ya Congo (DRC) na Uswisi.

Mabalozi hao ni Balozi Dk. Emmanuel Nchini (Brazil), Balozi Elizabeth Kiondo (Uturuki), Balozi George Madafa (Italy), Balozi James Msekela (Uswisi),Balozi Samuel Shelukindo (Ufaransa), Balozi Paul Mella (DRC), Balozi Mbelwa Kairuki (China).

“Serikali inahitaji watu wa kuja kuwekeza katika viwanda ili kuongeza thamani ya mazao kabla ya kuyauza nje ya nchi, hivyo jukumu lenu ni kuhakikisha tunapata wawekezaji wenye sifa,” amesema.

Pia Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao kutumia uwakilishi wao katika nchi hizo kwa kuhakikisha wanatangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili kuongeza idadi ya watalii wanaokuja Tanzania.

“Tulinde bidhaa za ndani ya nchi yetu mfano madini ya tanzanite ambayo yanazalishwa Tanzania pekee lakini leo zinazalisifiwa nchi nyingine kwa uzalishaji huo zikiwemo India na China, hivyo jukumu lenu ni kuhakikisha mnatangaza madini yetu ipasavyo,” amesema.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao kulinda maslahi ya Taifa katika nchi hizo ikiwa ni pamoja na kuimarisha uhusiano uliopo kati ya Tanzania na mataifa hayo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao kuhakikisha wanawatambua Watanzania wanaoishi katika mataifa hayo na kushirikiana nao katika kutafuta wawekezaji wa kuja kuwekeza nchini.


Kwa upande wake Balozi Mella ambaye alizungumza kwa niaba ya mabozi wenzake alimuhakikishia Waziri Mkuu kwamba watakwenda kutekeleza wajibu wao ipasavyo.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.