*Ataka waandike barua ya kuomba radhi kwa Rais Magufuli
*Aagiza Waziri wa Biashara aje na timu yake
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema haridhiki na hali aliyoikuta kwenye kiwanda cha kutengeneza mbolea cha Minjingu baada ya kubaini kuwa wanatumia mifuko yenye lebo ya Kenya wakati mbolea hiyo inazalishwa hapa nchini.
Kutokana na hilo, Waziri Mkuu amewataka wamiliki wa kiwanda hicho waandike barua kwa Mheshimiwa Rais Dk. John Pombe Magufuli kabla hajamaliza ziara yake Jumatano, Februari 22, 2017 apate nakala ya barua hiyo.
Ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Februari 19, 2017) baada ya kutembelea kiwanda hicho kilichopo wilaya Babati akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake mkoani Manyara. Waziri Mkuu amerejea Babati leo akitokea Dar es Salaam ambako alikuwa na ratiba za kitaifa.
“Nilikuja kukagua kiwanda baada ya kupokea malalamiko kuwa mbolea hii haikubaliki huko vijijini. Watafiti wameonyesha kuwa ikitumika inasaidia kutoa mazao mengi. Lakini wakati niko kiwandani nimekerwa kukuta mifuko ya kupakia mbolea hii ina anuani ya Nairobi, Kenya wakati mali ghafi inatoka Tanzania,” amesema.
“Ni kwa nini mifuko hii ina anuani ya Kenya? Hapa tulipaswa tuone anuani ya Babati! Je mlipata kibali kutoka serikalini? Tena kuna lebo ya TBS. Kwa nini Tanzania haionekani? Kwani malighafi iko Kenya? Haiwezekani, ni lazima uandike barua na uombe radhi kwa Mheshimiwa Rais Magufuli. Yeye anahimiza ujenzi wa viwanda ndani ya nchi, halafu ninyi mnafanya hivyo?”
Akiwa ndani ya kiwanda hicho, Waziri Mkuu alikuta baadhi ya mifuko ya mbolea ikiwa imeandikwa: ‘County Government of Bungoma’, ina nembo ya Serikali ya Kenya, na anuani ikionesha kuwa mbolea hiyo imetengenezwa na kiwanda cha mbolea cha Minjingu lakini anuani inasomeka P. O Box 2941 – 00200 Nairobi, Kenbro Industrial Park, Mombasa Road; namba ya simu +254-20-6000-970 lakini mifuko hiyo pia ina muhuri wa TBS.
Baadhi ya mifuko ilikuwa ikipakiwa ndani ya lori tayari kwa kusafirishwa kwenda kwa wateja.
Pia amesema atamwagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage aje hapa na wanasheria wake na wataalamu kutoka Tume ya Ushindani wa Kibiashara (FCC) ili waje kuangalia hatua gani zinapaswa kuchukuliwa.
“Kwa staili hii hii tumeona watu wakinunua kahawa yetu na kwenda kuipakia upya huku wakiweka lebo za kwao. Leo hii hata Tanzanite pia inasemwa imetengenzwa India. Hatuwezi kukubali hali hii iendelee,” amesisitiza.
“Tukiruhusu hali hii, watu watajuaje kuwa mbolea hii ambayo ni first class duniani kuwa inapatikana Tanzania? Kiwanda chetu, ardhi yetu, suala la kutangaza nchi yetu kwa kutumia bidhaa zetu litafanikiwa kwa njia hii kweli?”
“Nataka wakati namaliza ziara nipate taarifa ya hili jambo pamoja na nakala ya barua ambayo imetumwa kwa Mheshimiwa Rais,” amesisitiza.
Akitoa maelezo kuhusu hali hiyo, Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Bw. Tosky Hans alimweleza Waziri Mkuu kwamba wametumia lebo hiyo kutokana na makubaliano na wanunuzi jibu ambalo Waziri Mkuu hakulikubali na kusisitiza kuwa anapaswa aombe radhi.
Waziri Mkuu kesho anaendelea na ziara yake wilayani Mbulu ambako atatembelea hospitali ya Haydom, kuzungumza na watumishi wa wilaya hiyo na kuzindua shule ya sekondari Singland.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.