Friday, July 19, 2019

WAZIRI MKUU AMSIMAMISHA KAZI MHANDISI WA MAJI SAME

*Azivunja Jumuiya za watumiaji maji Hedaru
*Aagiza Katibu wa Jumuiya moja akamatwe

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Same, Mussa Msangi kwa kosa la kumdanganya kuhusu mradi wa maji aliouzindua leo katika kata ya Hedaru.

Amechukua uamuzi huo leo jioni (Ijumaa, Julai 19, 2019) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa Hedaru mara baada ya kuzindua mradi wa maji wa Lengeni-Hedaru, wilayani Same.

Waziri Mkuu alibaini kuwepo kwa tatizo wananchi walipoanza kuzomea wakati zikitolewa salaam za utambulisho kwa viongozi alioambatana nao. Kabla hajahutubia, aliamua kumuita Mhandisi huyo aelezee ukweli wa madai ya wananchi kwamba maji yametoka leo kutokana na ujio wake.

"Eleza ni kwa nini nilipofungua maji, hayakuwa na presha ya kutosha na wewe umesema upatikanaji wa maji umefikia zaidi ya asilimia 80?"

Alipoulizwa kwa mwezi wanakusanya kiasi gani cha fedha kutokana na mauzo ya maji hayo, Mhandisi Msangi alijibu kwa mwaka uliopita walikusanya sh. milioni saba tu.

"Haiwezekani kama maji yanatoka, wenye KAMATI wapate shilingi milioni saba. Ni ama maji hayatoki au wanakusanya hela na wanazila."

Alipoambiwa aelezee utendaji wa mradi huo wa maji na kama alikuwa akiufuatilia, alishindwa kutoa maelezo kamili, akidai kuwa leo maji yanatoka kidogo kwa sababu kuna hali ya mawingu. "Mbona kule ndani ulisema zile betri zinasaidia kuvuta maji na kubalance upatikanaji wa maji wakati hakuna jua la kutosha?" alihoji Waziri Mkuu. 

Waziri Mkuu aliamua kumuita mwenyekiti wa Jumuiya ya watumiaji maji au Kiongozi mwingine yeyote aje atoe maelezo, lakini wote hawakuwepo kwenye mkutano huo. Ndipo akachukua uamuzi wa kuzivunja jumuiya hizo.

"Jumuiya zote za maji nazivunja kuanzia leo, na wahusika wote watafutwe na Jeshi la Polisi. Haiwezekani nipewe kazi ya kuzindua mradi ambao hauna maji," alisema Waziri Mkuu.

"Katibu Tawala wa Mkoa lete wakaguzi wa mahesabu kwenye huu mradi, pia leta Mhandisi mwingine asimamie huu mradi. Huyu arudishwe kwa Waziri wake," alisema.

Waziri Mkuu pia alimwagiza Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Awesu abaki Hedaru na afuatilie utendaji wa mradi huo kisha ampe taarifa.

Wakati akimaliza kutoa maagizo hayo, Katibu wa Jumuiya ya watumiaji maji Hedaru-Masasi (HEWAUA), Bw. Francis Kazen Kiondo aliletwa akiwa chini ya ulinzi wa polisi, lakini Waziri Mkuu alielekeza apelekwe kituoni akatoe maelezo.

Taarifa zilizothibitishwa zimebainisha kuwa Kata ya Hedaru inazo Jumuiya tatu za watumiaji maji ambao ni Hedaru-Masasi, Lung wana na Mradi wa Kati. Wakazi wa Hedaru wanakadiriwa kufikia 20,000.

Ilibainika kwamba wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Hedaru-Masasi, Bw. Clement Ngoka aliamua kujiuzulu nafasi hiyo kwa sababu ya upinzani aliokuwa akipata kwa viongozi wenzake ambao pia wanadaiwa kuwaunganishia maji baadhi ya watu hadi majumbani kwao na fedha zilizolipwa hazijulikani zilipoenda.

Awamu ya pili ya mradi wa maji alioenda kuuzindua Waziri Mkuu, inahusisha ujenzi wa chanzo cha maji katika korongo la mto Rangeni ambao ulikamilika Desemba 2018. Chanzo hicho cha mtiririko, kilitarajiwa kuzalisha lita 750,000 kwa siku ili kusaidia maji yanayozalishwa kwenye visima ambayo yana ujazo wa lita 7,500 kwa saa.

(mwisho)
Read More

WAZIRI MKUU AAGIZA SAME SEKONDARI IPEWE GARI

*DED aahidi kuliwasilisha kesho kutwa jioni

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Bi. Anna-Clare Shija apeleke gari haraka katika shule ya sekondari ya wavulana ya bweni ya Same ili kumsaidia mwalimu mkuu endapo kutatokea dharura.

“Shule hii ina wanafunzi zaidi ya 800 lazima iwe na chombo cha usafiri kitakachotumika kwa dharura za kuwapeleka hospitali wanafunzi pale wanapougua. Sasa hivi mwanafuzi akiugua, Mwalimu Mkuu anafanyaje? Ni kama ameachiwa jukumu hili peke yake,” alisema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana (Ijumaa, Julai 19, 2019) wakati alipotembelea shule hiyo na kuzindua mradi wa ukarabati wa shule kongwe ya sekondari ya Same na kisha kuzungumza na wanafunzi, walimu na baadhi ya wazazi waliokuwepo.

Waziri Mkuu alimwita Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Bi. Shija na kumtaka atoe jibu hadharani kwamba ni lini atapeleka gari hilo shuleni hapo. Mkurugenzi huyo aliahidi kulipeleka gari hilo ifikapo Jumatatu jioni (Julai 22, 2019).

“Haya maelekezo ni kwa wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini wenye shule ambazo zina wanafunzi zaidi ya 700. Mnapaswa kuhakikisha kunakuwa na gari la shule ili ikitokea dharura, Mkuu wa Shule aweze kuingilia kati na kupata ufumbuzi.”

“Wakurugenzi mnatakiwa kutambua shule hizi ni zenu, kwa hiyo mnalo jukumu la kuzihudumia. Shule hii ya Same ina wanafunzi zaidi ya 800 na wanalala hapa hapa, ni lazima kuwe na gari la kuwahudumia hasa wakati wa dharura.”

Pia amemuagiza Mkurugenzi huyo atafute daktari na muuguzi mmoja na awapangie kwenye shule hiyo ili waweze kutoka huduma kwa wanafunzi na kuwapunguzia adha ya kwenda mjini kutafuta huduma hiyo.

Waziri Mkuu alifikia uamuzi huo baada ya kupokea changamoto zilizowasilishwa na kijana Omary Said wa kidato cha sita mchepuo wa PCB ambaye alisema shule hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji; uchakavu wa mabweni; ukosefu wa zahanati ya shule na uhaba wa walimu wa sayansi hasa wa masomo ya fizikia.


Mapema, akitoa taarifa ya ukarabati, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bw. Hoza Mgonja alisema ukarabati huo ambao umegharimu sh. milioni 919, ulifanikisha ukarabati wa majengo saba ya madarasa yenye vyumba 22; maabara tatu, vyoo viwili vyenye matundu tisa; jengo moja la walimu; maktaba yenye vyumba viwili na ofisi mbili; vyoo viwili vyenye matundu manne na miundombinu ya umeme na majitaka.

Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake mkoani Kilimanjaro kwa kutembelea wilaya ya Mwanga ambako atazungumza na watumishi na kisha ataenda kijiji cha Kirya, Nyumba ya Mungu kukagua mradi wa maji wa Same - Mwanga - Korogwe.

(mwisho)

Read More

NITAMTUMA WAZIRI MHAGAMA AJE MAKANYA – WAZIRI MKUU

*Ni katika mashamba ya mkonge, apokea kilio cha wafanyakazi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atamtuma Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Kazi, Ajira na wenye Ulemavu, Bi. Jenista Mhagama aende Makanya, wilayani Same, kwenye mashamba ya mkonge akatatue kero za wafanyakazi.

“Nitamleta Waziri wa Nchi anayesimamia masuala ya kazi, aje afuatilie kero za wafanyakazi hapa Makanya, manake watumishi wameweka malalamiko yao kwenye mabango na mimi nimeona wanaoendesha mitambo hawana gloves, wengine wamevaa kandambili badala ya mabuti, kofia za usalama nimeambiwa ziko 20 tu…” alisema Waziri Mkuu.

Ametoa ahadi hiyo jana (Ijumaa, Julai 19, 2019) wakati akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha kuchakata katani kilichopo kwenye shamba la mkonge la Hasani, kata ya Makanya, wilayani Same, Kilimanjaro, mara baada ya kukagua uzalishaji kwenye kiwanda hicho.

Alifikia uamuzi huo baada ya kusoma mabango yaliyokuwa yakitoa ujumbe juu ya hali mbaya kiwandani zikiwemo malipo ya sh. 3,800 kwa siku; mikataba mibovu ya kazi; wafanyakazi kutothaminiwa wanapougua na kutoridhika na mawakala wawili ambao ni UNIQUE na UPANI waliowekwa kusimamia uendeshaji wa shamba hilo. UNIQUE inasimamia wakata mkonge na UPANI inasimamia kazi ya upandaji na upanuzi wa mashamba.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alimweleza Meneja wa Mashamba ya METL likiwemo la Hasani, Bw. Ndekiwa Nyari kwamba uamuzi wa kuweka mawakala unawapunguzia wenye kampuni mzigo wa usimamizi kwenye mashamba lakini unaipa hasara kampuni yao.

“Kwa sasa unashughulika na watu watatu au wanne ambao ni mawakala wakati watu wote wanaokuzalishia wako hapa. Ni vema ungeajiri hao watu wanne, ukawasimamia kwa karibu na unaweza kuwapa motisha wakifanya vizuri au kuwafukuza wakiharibu. Lakini kwa sasa hawa mawakala huna mamlaka hayo, sababu ulishaweka mkataba nao,” alisema.

“Ni bora uwe na idara mbili za upandaji na uvunaji, kisha uweke wasimamizi watatu au wanne ambao watawajibika kwako moja kwa moja. Hii system uliyotumia ina walakini hasa kwenye maslahi ya wafanyakazi. Unawalipa fedha lakini haifiki yote kwa wafanyakazi,” alisema na kuamsha shangwe miongoni mwa wafanyakazi hao.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi wa Makanya wajipange na kutafuta maeneo ya ekari tatu hadi nne ili nao waanze kulima mkonge ambao alisema watakuwa wanauuza kwenye kiwanda hicho.

“Niwasihi wananchi wa hapa na vijiji jirani ingieni kwenye kilimo cha mkonge kwa sababu kina soko ndani na nje ya nchi. Tafuteni maeneo ya ekari tatu au nne anzisheni kilimo cha mkonge sasa. Zao hili lipo kwenye mazao ya nyongeza ya mkakati ambayo ni chikichi na mkonge.”

“Na uzuri wake unalima mara moja tu, halafu kila mwaka unakuwa unavuna tu. Viongozi wa Serikali ya Kijiji simamieni jambo hili,” alisisitiza.

Mazao mengine ya mkakati ambayo Serikali ya awamu ya tano ilianza kuyatilia mkazo ili kuimarisha uzalishaji wake, upatikanaji wa pembejeo na masoko ni pamba, chai, tumbaku, kahawa na korosho.

Mapema, akitoa taarifa juu ya uzalishaji kwenye kiwanda hicho, Bw. Nyari alisema shamba lote lina ukubwa wa ekari 2,453 na kwamba uzalishaji umekuwa ukiongezeka kidogo kidogo ambapo mwaka 2014 walizalisha tani za mkonge 713 na hadi kufikia mwka 2018 walifikisha tani 890 za mkonge. “Mwaka huu tunatarajia kufikisha tani 1,080 kwa sababu eneo lililopandwa mkonge limeongezeka,” alisema.

Alisema moja ya changamoto inayowasumbua ni tabia ya wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba yenye mkonge mchanga hali ambayo alisema inaua miche hiyo michanga.

Aliitaja changamoto nyigine kuwa ni ukosefu wa maji ya uhakika, hali ambayo inawafanya washindwe kuzalisha singa za katani ambazo ni safi.

Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake mkoani Kilimanjaro kwa kutembelea wilaya ya Mwanga ambako atazungumza na watumishi na kisha ataenda kijiji cha Kirya, Nyumba ya Mungu kukagua mradi wa maji wa Same - Mwanga - Korogwe.

(mwisho)
Read More

Thursday, July 18, 2019

WAZIRI MKUU: WEZI WA NONDO TANI 5 WASAKWE MARA MOJA

*Ni za ujenzi wa kituo cha kimataifa cha mabasi cha Moshi
*RPC athibitisha watu watano wamekamatwa kufuatia agizo hilo

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah awasake na kuwatia mbaroni watu waliohusika na wizi wa tani tano za nondo na kisha wakatoroka.

Alitoa agizo hilo jana jioni, (Alhamisi, Julai 18, 2019) wakati akizungumza na wafanyakazi na wananchi mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa stendi ya mabasi ya kimataifa ya Moshi, katika kata ya Ngangamfumuni, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Kilimanjaro kwa ziara ya kikazi za siku nne, alisema mradi huo ni maalum kwani uko miongoni mwa miradi ambayo Serikali imekuwa ikiweka utaratibu wa kupelekea fedha kwenye miradi iliyotengwa na Halmashauri.

“Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 9 za kuanzia mradi huu lakini inasikitisha kuona kwamba wanaMoshi mnahujumu kwa kuiba vifaa vya ujenzi. Ninazo taaarifa kuwa hapa zimeibiwa tani tano za nondo na zimeshakamatwa.”

“Ni aibu, ni aibu kwa wana-Moshi. Ninyi wenyewe mnauhujumu huu mradi. Manispaa iweke utaratibu wa ulinzi ili vifaa vingine visipotee zaidi. Mkuu wa Wilaya chukua hatua ya kuwafuatilia wote waliohusika,” alisema.

Kupitia maswali aliyouliza, Waziri Mkuu alibaini kuwa walinzi wawili waliokuwepo siku ya tukio walitoroka ndipo akaamua kumwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa, awasake na kuhakikisha wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Ujenzi wa stendi hiyo kubwa unafanywa na mkandarasi mkuu ambayo ni kampuni ya CRJE ya China akishirikiana na wakandarasi wasaidizi watano na unatarajiwa kukamilika Januari 2021. Hadi kukamilika, ujenzi huo unatarajiwa kugharimu sh. bilioni 28.8.

Ikikamilika, stendi hiyo ambayo itakuwa na ofisi, maduka, migahawa na hoteli, itakuwa na uwezo wa kuhudumia mabasi 300 kwa siku ambayo yataingia na kutoka. Kati ya hayo, mabasi 72 yanaweza kuegeshwa kwa wakati mmoja. Pia kutakuwa na maegesho ya ya magari binafsi 218, teksi 34 na bajaji na bodaboda 20.

Wakati huohuo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah amethibitisha kukamatwa kwa watu watano ambao wanatuhumiwa kuhusika na wizi wa tani tano za nondo katika eneo la ujenzi wa stendi hiyo lililopo Ngangamfumuni.

“Hawa watu tumewakamata jana jioni, na kati ya walinzi waliotoroka, tumemkamata mmoja wao tayari akiwemo mkazi wa Rau, Daudi Audifasi mwenye miaka 48 ambaye anadaiwa kutoboa ukuta wa uzio kwa chini, na kukutwa na nondo nyumbani kwake ambako ni mita 10 kutoka eneo la tukio.”

Amesema tukio hilo, lilitokea Julai 6, mwaka huu majira ya saa 2 asubuhi ambapo walinzi wa eneo hilo ambao ni Maxshield company walitoroka baada ya tukio hilo. Kamanda Issah alithibitisha kwamba nondo hizo zimekamatwa na ziko polisi.

(mwisho)
Read More

Wednesday, July 17, 2019

WAZIRI MKUU AITAKA TCU IVISAIDIE VYUO VIKUU BINAFSI

*Asisitiza kwamba hakuna mbadala wa elimu bora

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) itafute mbinu bora zaidi na kuvijengea uwezo vyuo vikuu binafsi ili visaidie kuongeza udahili.

“Tume itafute mbinu bora zaidi ikiwa ni pamoja na kuvijengea uwezo vyuo vikuu binafsi ili visaidie kuongeza udahili. Ni wakati muafaka kwa Tume kujipambanua kwenye uwezeshaji na ushauri ili kuondoa taswira hasi miongoni mwa jamii kwamba kazi kubwa ya TCU ni kuvifungia vyuo vikuu badala ya kuvisaidia kutatua changamoto zinazovikabili,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo, (Jumatano, Julai 17, 2019) wakati akifungua maonesho ya 14 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam. Maonesho hayo yatafungwa Julai 20, mwaka huu.

Amesema Serikali inatambua kwamba vyuo vikuu binafsi ni washirika muhimu wa maendeleo ya sekta ndogo ya elimu ya juu nchini. “Naomba nieleweke vizuri kwamba hakuna mbadala wa elimu bora bali nasisitiza Tume ivisaidie vyuo vikuu kufikia viwango vinavyotakiwa na siyo kuwapunguzia viwango vya matakwa ya usajili,” amesema.

Akitoa ufafanuzi kuhusu idadi ndogo ya wahitimu wa elimu ya juu, Waziri Mkuu amesema takwimu za kimataifa za ushiriki wa elimu ya juu zinaonesha kwamba kufikia mwaka 2017 ni asilimia moja hadi tatu tu ya Watanzania kwa kila Watanzania 100 wenye umri chini ya miaka 25 wanapata elimu ya Chuo Kikuu.

“Idadi hii ni ndogo zaidi ya majirani zetu wa Kenya wenye asilimia nne, Zambia asilimia nne na Namibia asilimia 14. Bado tunayo kazi kubwa sana ya kufanya. Natoa maelekezo kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iongeze jitihada na mikakati ya kuboresha uwiano huu ambao upo chini ikilinganishwa na majirani zetu,” alisisitiza.

Amesema ili kuongeza idadi ya Watanzania wanaopata nafasi ya elimu ya juu, ni lazima tupange mikakati yetu kama nchi kwa kushirikiana na sekta binafsi, ambao ni wadau wakubwa katika elimu ya juu. “Taarifa nilizonazo ni kwamba, kati ya wahitimu wote wa vyuo vikuu kwa mwaka, asilimia 25 wanatoka katika vyuo vikuu binafsi. Mchango huu si mdogo, na ningetamani uongezeke zaidi,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewapa changamoto wakuu wa vyuo vikuu nchini wabadilishe mtazamo wao juu ya upimaji wa ufanisi wa wahitimu na badala yake upimaji wao ujielekeze kwenye kutoa suluhisho na kubadilisha maisha ya Watanzania badala ya kutumia machapisho ya kitaaluma.

“Kipimo cha ufanisi katika taaluma ilikuwa ni machapisho ya kitaaluma, ambapo mengi ya hayo, jamii pana haifaidiki nayo. Sasa ni wakati mwafaka kutafakari iwapo kipimo hicho kinatosheleza. Kwa vyuo vikuu ambavyo mmehudhuria hapa leo, naomba niwape mtazamo tofauti. Kipimo cha ufanisi wa wanataaluma wa Tanzania, kuanzia sasa kinafaa kiwe ni kiasi gani taaluma yao inawafikia na kubadilisha maisha ya wananchi, na kiwango cha bidhaa na hatimiliki (patents) zilizozalishwa na kusajiliwa na wasomi wetu waliopo vyuo vikuu.”

Amesema matarajio ya Serikali ni kuona kwamba tafiti na vipimo vya ufanisi kwenye vyuo vikuu viwe ni kiasi gani vyuo hivyo vinatoa bidhaa mbalimbali za kuleta ajira pamoja na kukabiliana na matatizo ya kijamii. “Ningefurahi iwapo kuanzia sasa kipimo cha ufanisi wa vyuo vikuu vyetu iwe katika kupima jitihada za vyuo vyetu kuisaidia Serikali katika azma yake ya kufikia kwenye uchumi wa kati,” amesema. 

“Huu ni wakati muafaka kuanza kupima ufanisi wa wakuu wa vyuo kwa kuangalia kiasi gani mazao ya Chuo Kikuu hicho yamewafikia wananchi na pia katika utekelezaji wa mikakati ya maendeleo ya Serikali, hasa mapinduzi ya viwanda,” amesisitiza.

Mapema, akielezea kuhusu maonesho hayo, Mwenyekiti wa TCU, Prof. Jacob Mtabaji aliwataka wahitimu wa kidato cha sita wanaoomba kujiunga na vyuo vikuu, wasome kwa umakini mwongozo uliowekwa kwenye tovuti na wasikubali kupitia mawakala wanaodai kuwa wanaweza kufanya usajili kwa niaba yao. Pia aliwataka wazingatie kalenda ya udahili.

Akielezea changamoto za elimu ya juu nchini, Prof. Mtabaji alisema kuna uhaba wa wahadhiri wenye sifa stahiki katika vyuo vikuu vingi na akawaomba wakuu wa vyuo hivyo wawasomeshe wahadhiri katika ngazi mbalimbali ili wakirudi wajiunge na vyuo husika.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TCU, Prof. Charles Kihampa alisema taasisi 81 za elimu ya juu zimeshiriki maonesho hayo ambapo taasisi 15 ni za nje ya nchi na taasisi 66 ni za hapa nchini.

Akitoa shukrani, Mwenyekiti wa Kamati ya Watendaji Wakuu wa Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki (CVCPT), Prof. Raphael Chibunda alisema anaishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa uboreshwaji uliofanywa kwenye upatikanaji na upelekwaji kwa wakati wa fedha kutoka Bodi ya Mikopo. “Zamani, sauala hili hiloi likuwa ni chanzo cha migomo mingi vyuoni lakini kwa sasa limekwisha,” alisema.

Pia aliishukuru Serikali kwa kukubali kurudisha jukumu la udahili wa wanafunzi katika Seneti za Vyuo Vikuu kwani hapo nyuma lilikuwa sehemu ya mgogoro baina ya TCU na vyuo vikuu.

(mwisho)
Read More

NYANGAO SEKONDARI YAUBEBA MKOA WA LINDI

*Mwanafunzi wake aibuka nafasi ya saba Kitaifa masomo ya lugha na sanaa
*Yaupandisha mkoa kutoka nafasi ya pili hadi nafasi ya kwanza Kitaifa
*Mkuu wa Mkoa wa Lindi atuma salamu kwa mikoa mingine ijipange
WAHENGA walisema ‘penye nia pana njia’ usemi huu umejidhirisha katika matokeo ya kidato cha sita kwa mwaka huu wa 2019, baada ya shule zote Mkoani Lindi zikiongozwa na shule ya Sekondari ya Nyangao kufanya vizuri katika matokeo hayo na kuufanya mkoa kushika nafasi ya kwanza katika mpangilio wa ubora wa ufaulu nchini.
Ni ukweli usiopingika kwamba hakuna aliyetarajia kuona mkoa wa Lindi ukiibuka kidedea kwani kwa miaka mingi mikoa ya kusini ukiwemo Lindi ilisifika kwa kuwa nyuma kielimu kutokana na matokeo yasiyoridhisha yaliyokuwa yanapatikana.
Matokeo duni kielemu yalichangia kudorora kwa maendeleo ya mikoa hiyo kwa kiasi kikubwa. 
Jitihada mbalimbali zilizofanyika kwa ushirikiano wa Serikali, wazazi na wadau wa maendeleo kuhakikisha mikoa hiyo inaondoka katika kundi la kuongozwa zimezaa matunda kufuatia matokeo mazuri.
Hamasa kubwa inajengwa kwa wazazi na walezi kutambua umuhimu wa elimu kwa watoto wao kwa ajili ya faida yao na Taifa kwa ujumla. Kampeni kuhusu kipaumbele cha elimu ndio ukombozi katika kupambana na umaskini imeleta matokeo chanya mkoani Lindi. 

Mara baada ya uhuru Hayati Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere alihakikisha kuwa, Watanganyika wanakuwa na elimu ili waweze kujikomboa kutoka utumwa wa wakoloni na kujiongoza katika kujieletea maendeleo kwenye maisha yao. 

Akizungumzia kuhusu matokeo hayo Mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi alisema kuwepo kwa dhamira ya dhati iliyooneshwa na viongozi wa Serikali katika ngazi mbalimbali, wanasiasa na wananchi wa mkoa wa Lindi ili kuboresha na kuinua kiwango cha ufaulu imeanza kuonekana, ambapo kwa sasa mkoa unaongoza matokeo kidato cha sita na kufaulisha wanafunzi wote.

Alisema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwezesha mkoa huo kufanya vizuri katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo ikiwe kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu. Hali hiyo imetokana na mikakati mbalimbali iliyofanywa kati ya walimu, wanafunzi na Serikali.

Alisema hatua ya kwanza waliyoichukua ni kutafuta sababu za mkoa kutofanya vizuri kielimu, baada ya kuzibaini waliweka mikakati ya kutatua changamoto hizo kwa kusimamia mahudhurio ya wanafunzi kwa sababu kulikuwa na utoro  pia ukaguzi kwa walimu pamoja kuandaa majaribio ya mara kwa mara.

“Pia tulikuwa tunafanya mikutano ya kujadili na kuweka mikakati ya kuinua kiwango cha elimu katika mkoa wa Lindi kwa ushirikiano baina ya Serikali na wadau wa masuala ya elimu. Tulikubaliana kufanya ziara za mara kwa mara mashuleni pamoja na kuanzisha vituo kwa ajili ya wanafunzi wanaojiandaa na mitihani.”

Kiongozi huyo aliongeza kuwa hakuna mkoa uliondikiwa kuwa wa mwisho, waliamua kufanya jitihada mbalimbali ili kuuwezesha mkoa wao kusonga mbele kimaendeleo na wameanza kuyaona mafanikio, hivyo mikoa mingine inayodhani kuwa itakuwa ya kwanza kila wakati ijipange. 

Alisema kuwa katika mkoa wao kulikuwa na shule ya Sekondari ya Nyangao ambayo ilikuwa imeshapotea katika ramani, lakini kutokana na jitihada mbalimbali zilizofanywa na wadau wa elimu shule hiyo imeibuka na kuwa ya kwanza Kitaifa. “Hili ni jambo la faraja.”

“Niwapongeze walimu wote na wanafunzi kwani shule zote tisa za sekondari za kidato cha tano na sita mkoani hapa zimefanya vizuri katika matokeo ya kidato cha sita na kuufanya mkoa kuongoza mikoa yote. katika shule hizo nane ni za Serikali na moja inamilikiwa na mtu binafsi.”

Shule zilizofanya vizuri
Shule ya Sekondari ya Nyangao iliyopo Halmashauri ya wilaya ya Lindi imeshika nafasi ya kwanza Kitaifa kati ya shule 134 zenye wanafunzi chini ya 40, ambapo kati ya wanafunzi 25 waliofanya mtihani wa kumaliza kidato cha sita wanafunzi 22 walipata daraja la kwanza huku watatu waliosalia walipata daraja la pili.

Mwanafunzi wa shule hiyo ya sekondari ya Nyangao, Karimu Kassimu Muhibu (HKL) ameibuka katika namba saba kati ya wanafunzi kumi bora waliofanya vizuri Kitaifa katika masomo ya lugha na sanaa. 


Mbali na shule ya Sekondari ya Nyangao kupata matokeo hayo, shule zingine za sekondari za mkoa wa Lindi zilizopata matokeo mazuri ni shule ya kutwa ya Nachingwea iliyokuwa na watahiniwa 64 kati yake 49 walipata daraja la kwanza na waliosalia 15 walipata daraja la pili.

Shule ya sekondari ya kutwa ya Liwale kati ya wafunzi 186 waliofanya mtihani wanafunzi 43 walipata daraja la kwanza, 121 walipata daraja la pili na wanafunzi 22 walipata daraja la tatu.

Shule ya sekondari ya Mbekenyera iliyoko wilayani Ruangwa ambayo kati ya wanafunzi 98 waliofanya mtihani huo, wanafunzi 37 walipata daraja la kwanza, 56 walipata daraja la pili huku wengine watano waliosalia walipata daraja la tatu.

Shule ya sekondari ya Kilwa ambayo ilikuwa na jumla ya wanafunzi 103 walioifanya mtihani huo, wanafunzi sita walipata daraja la kwanza, 76 walipata daraja la pili huku weingine 21 wakipata daraja la tatu.

Ni dhahiri kwamba matokeo hayo ni ishara nzuri inayoashiria kuwepo kwa mwamko wa kutosha na kukubali mabadiliko makubwa ya kielimu miongoni mwa wananchi wa mkoa wa Lindi 

Inatarajiwa kuwa hatua hizo zitachangia kuongezeka kwa wasomi katika jamii za wakazi wa mkoa huo, ambao kwa vyovyote vile wanafunzi hawa watakuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha umuhimu wa elimu kwa wenzao ambao bado wanasoma katika ngazi mbalimbali zikiwemo shule za msingi.

Wanafunzi waliofanya vizuri katika matokeo ya kidato cha sita wanatarajiwa hapo baadae kusaidia mkoa wa Lindi na nchi kwa ujumla katika kupambana na changamoto mbalimbali zikiwemo za upungufu wa walimu, madaktari, wauguzi na watumishi wengi kwa kuwa baada ya kumaliza masomo yao watajiunga na vyuo kusomea taaluma mbalimbali.



Read More

BENKI YA DUNIA NA TANZANIA WAWEKA HISTORIA MENEJIMENTI YA MAAFA AFRIKA


Na. OWM, ARUSHA

Kwa mara ya kwanza Barani Afrika na kwa mara ya kwanza katika utendaji wake Benki ya Dunia, kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania kupitia  Ofisi ya Waziri  Mkuu,  Idara ya Menejimenti ya Maafa, wamefanya zoezi la mezani la  Kupima uwezo utekelezaji  wa Mpango wa  Kujiandaa na kukabili Maafa kwa kutumia maafa ambayo yamepata kutokea kweli hapa nchini, ambapo zoezi hilo limetumia maafa ya   mafuriko mkoani Morogoro, wilayani  Kilosa kwa mwaka 2014 na mwaka 2016. Mazoezi mengine ya mezani ya kujiandaa na kukabli maafa hutumia matukio ya maafa ya kinadharia na hufanyika kabla ya maafa kutokea.

Mtaalam Mwandamizi wa menejimenti ya Maafa, kutoka Benki ya Dunia, Elad Shenfeld, amebainisha mambo matano ambayo yameifanya Benki hiyo kuichagua Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika  kufanya zoezi hilo, kuwa ni Uwajibikaji na uwazi katika kuratibu shughuli za menejimenti ya  maafa unaofanywa na  serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Menejimenti ya Maafa,  uwepo wa Sheria ya Maafa, ambayo ni  Sheria  ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2015, Mpango wa Taifa wa kujiandaa na Kukabili maafa wa mwaka 2012, Uwezo, Weledi na Uwajibikaji wa watumishi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa katika menejimenti ya maafa  pamoja na Ushirikiano mzuri wa serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia Tanzania na Kanda ya Afrika katika masuala ya menejimenti ya maafa nchini.

Akiongea mara baada ya kufunga zoezi hilo mjini Arusha, tarehe 16, Julai, 2019, Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe amebainisha kuwa nchi nyingi barani Afrika ikiwemo Tanzania zimekuwa zikifanya  mazoezi ya kujiandaa na kukabili maafa kwa kutumia nadharia za maafa yanoyoweza kutokea, lakini zoezi hilo  ni tofauti kwani limejikita kwa maafa ambayo yamewahi kutokea kweli  hapa nchini.

“Zoezi hili  ambalo limeangalia maafa ya mafuriko yaliyotokea, Kilosa kwa mwaka 2014 na 2016,  litatusaidia kuimarisha mifumo yetu serikalini ya kujiandaa na kukabili maafa ya mafuriko na majanga mengine kwani tumejua ni wapi hatukufanya vizuri na namna gani ya kuboresha mifumo yetu,  lakini pia zoezi hili litawajengea uwezo waratibu wa maafa serikalini na wataalam kutoka katika mashirika yasiyokuwa ya serikali katika kushirikiana na serikali katika kujiandaa na kukabili maafa yatapotokea” Alisema Matamwe.

Aidha, washiriki wa zoezi hilo waliweza kutoa uzoefu wao katika kujiandaa na kukabili maafa ya mafuriko ambayo yalitokea wilayani Kilosa  kwa mwaka 2014 na 2016. Washiriki hao kwa nyakati tofauti walibainisha kuwa wamejifunza kutoka mafuriko ya Kilosa kuwa ipo haja ya kila Serikali za mitaa na Taasisi za serikali pamoja na wadau wa menejimenti ya maafa kutenga bajeti kwa ajili ya masuala ya usimamizi wa shughuli za maafa.

Zoezi hilo lililofanyika kwa muda wa siku mbili tarehe 15 hadi 16, Julai, 2019,  liliwashirikisha wataalam wa usimamizi wa shughuli za maafa kutoka serikalini na mashirika yasiyo kuwa ya kiserikali, limeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Menejimenti ya Maafa,  kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.
MWISHO.

Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali  Jimmy Matamwe (mwenye tai nyekundu), kushoto ni kwake Mkurugenzi Msaidizi wa Ofisi hiyo (Utafiti na Mipango), Bashiru Taratibu, kushoto kwake ni Wawezeshaji  kutoka Benki ya Dunia, Elad Shenfeld, Adam Mc Allister na HugoWesley, wakati  wa zoezi la mezani la kupima uwezo wa utekelezaji  wa Mpango wa  Kujiandaa na Kukabili Maafa nchini, kwa  taasisi za serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayohusika katika menejimenti za maafa , mjini Arusha tarehe 16 Julai, 2019.
Mkurugenzi, Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe akiongea na wataalam kutoka taasisi za serikali na mashirika yasiyo kuwa ya kiserikali yanayohusika katika menejimenti za maafa wakati wa zoezi la mezani la kupima uwezo  wa Utekelezaji wa Mipango ya  menejimenti ya maafa nchini, mjini Arusha, tarehe 16 Julai, 2019.
Mkurugenzi  Msaidizi  (Utafiti na Mipango), Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu Bashiru Taratibu akisisitiza jambo kwa wataalam kutoka taasisi za serikali na mashirika yasiyo kuwa ya kiserikali yanayohusika katika menejimenti za maafa wakati wa  zoezi la mezani la kupima uwezo wa wa Utekelezaji wa Mipango ya  , tarehe 16 Julai, 2019.
Mtaalam wa Shughuli za Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Menejimenti ya Maafa, Charles Msangi akieleza jinsi ofisi hiyo inavyoratibu shughuli za maafa wakati wa  zoezi la mezani la kupima uwezo wa Utekelezaji wa Mpango wa Kujiandaa na Kukabili Maafa nchini, kwa taasisi za serikali na mashirika yasiyo kuwa ya kiserikali yanayohusika katika menejimenti za maafa wakati wa  mjini Arusha, Julai 16, 2019.
Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Polisi kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi nchini, Balele Edward, akiandika katika moja ya nyenzo za kujifunzia wakati wa zoezi la mezani la kupima uwezo wa Utekelezaji wa Mpango wa Kujiandaa na Kukabili Maafa nchini kwa taasisi za serikali na mashirika yasiyo kuwa ya kiserikali yanayohusika katika menejimenti za maafa, mjini Arusha Julai 16, 2019, zoezi hilo limeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.
Baadhi ya washiriki kutoka taasisi za serikali na mashirika yasiyo kuwa ya kiserikali yanayohusika katika menejimenti ya maafa wakijadiliana wakati wa zoezi la mezani la kupima uwezo wa utekelezaji wa  Mpango wa Kujiandaa na Kukabili Maafa nchini, mjini Arusha Julai 16, 2019, zoezi hilo limeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Ufadhili wa Benki ya Dunia
Baadhi ya washiriki kutoka taasisi za serikali na mashirika yasiyo kuwa ya kiserikali yanayohusika katika menejimenti ya maafa wakijadiliana wakati wa zoezi la mezani la kupima uwezo wa utekelezaji wa  Mpango wa Kujiandaa na Kukabili Maafa nchini, mjini Arusha Julai 16, 2019, zoezi hilo limeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Ufadhili wa Benki ya Dunia
Mwezeshaji kutoka Benki ya Dunia Adam Mc Allister akisisitiza umuhimu wa Mipango ya Menejimenti ya Maafa kwa   taasisi za serikali na mashirika yasiyo kuwa ya kiserikali yanayohusika katika menejimenti za maafa wakati wa  zoezi la mezani la kupima Utekelezaji wa Mpango wa Kujiandaa na Kukabili Maafa nchini, mjini Arusha, Julai 16, 2019, zoezi hilo limeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Ufadhili wa Benki ya Dunia.
Baadhi ya washiriki kutoka taasisi za serikali na mashirika yasiyo kuwa ya kiserikali yanayohusika katika menejimenti ya maafa wakijadiliana wakati wa zoezi la mezani la kupima uwezo wa utekelezaji wa  Mpango wa Kujiandaa na Kukabili Maafa nchini, mjini Arusha Julai 16, 2019, zoezi hilo limeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Ufadhili wa Benki ya Dunia.

Read More

Monday, July 15, 2019

SERIKALI YAWATOA HOFU WAKULIMA WA PAMBA


*Waziri Mkuu asema hadi Julai 30 wakulima wote watakuwa wamelipwa

Na Mwandishi Wetu

ZAO la pamba ni miongoni mwa mazao makuu ya biashara hapa nchini yakiwemo ya korosho, chai, tumbaku, katani na chikichi ambayo yamekuwa yakitegemewa katika kuinua uchumi wa wakulima na Taifa kwa ujumla.

Hivi karibuni kumetokea hali ya sintofahamu kuhusiana na suala ununuzi wa zao hilo baada ya kutangazwa kwa bei elekezi ambayo ni sh. 1,200 kwa kilo moja katika mikoa yote inayozalisha zao hilo.

Bei elekezi ya pamba kwa msimu huu ilitangazwa Aprili 30, 2019 mkoani Shinyanga na kwamba bei hiyo ilitakiwa ianze kutumika kuanzia Mei 2, 2019. Hata hivyo ununuzi wa zao hilo ulianza kwa suasua jambo ambalo Serikali haikuridhishwa nalo.

Jumapili ya Julai 14, mwaka huu ndipo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliamua kuitisha kikao kilichojumuisha wakuu wa mikoa 11 inayolima pamba, wanunuzi wa zao hilo, taasisi mbalimbali za kifedha pamoja na Gavana wa Benki Kuu.

Kikao hicho kilichoitishwa na Waziri Mkuu na kufanyika katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi kilikuwa na lengo la kutafakari mwenendo wa zao la pamba ambalo ununuzi wake unaendelea lakini kwa kasi ndogo.

Waziri Mkuu baada ya kusikiliza changamoto za wanunuzi ambao wengi wao waliomba Serikali iwadhamini katika taasisi mbalimbali za fedha walizoomba mikopo kwa ajili ya kununua zao hilo kwa kuwa ilikuwa imekwama. Serikali iliwakubalia.

“Sasa tumefikia muafaka wa jambo hili kibali kitatoka na wote watakaopata dhamana ya mikopo hakikisheni fedha hizo zinaenda kutumia kwa ajili ya ununuzi wa pamba kama ilivyokusudiwa na si vininevyo.”

Hivyo, Waziri Mkuu aliwaagiza wakuu wa mikoa na wilaya katika maeneo yote yanayolima pamba wawasimamie ipasavyo wanunuzi wote ili kuhakikisha fedha zitakazopatikana zinakwenda kutumika kwa ajili ya kununulia pamba.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wanunuzi Binafsi wa Pamba (TCA), Bw. Christopher Gachuma aliishukuru Serikali kwa kukubali kuwadhamini pamoja na Waziri Mkuu kwa maelekezo aliyoyatoa kuhusu suala la ununuzi wa zao hilo.

Waziri Mkuu, baada ya kufanya kikao na wadau wa pamba wakiwemo na wanunuzi ambao walikubali kwenda kununua pamba iliyoko kwa wakulima, Julai 15, 2019 alifanya ziara katika wilaya ya Igunga kwa lengo la kukagua mwenendo wa ununuzi wa zao la pamba.

Akiwa katika ziara hiyo, Waziri Mkuu alianza kwa kukagua ghala la ununuzi wa pamba la AMCOS ya Mbutu na kisha alikwenda katika kijiji cha Mwabakina na kukagua ghala la kununulia pamba la Mwabakima.

Baada ya kukagua maghala hayo Waziri Mkuu alizungumza na wananchi wa maeneo hayo ambao wengi wao ni wakulima wa pamba ambapo aliwahakikishia kwamba hadi kufikia tarehe 30 mwezi Julai mwaka huu pamba yote iliyoko katika mikoa mbalimbali nchini itakuwa imeshanunuliwa na wakulima wote kulipwa fedha zao.
  
Alisema Serikali imeamua kuingilia kati suala la ununuzi wa zao la pamba kutokana na kusuasua kwa soko lake kwa kutoa dhamana ili kuwawezesha wanunuzi kukopeshwa fedha na benki mbalimbali kwa ajili ya kununulia pamba kutoka kwa wakulima.
  
“Tunatambua adha mliyoipata tangu kuanza kwa msimu wa mwaka huu na hayo ni mapito tu. Nawasihi muwe na amani kwani Serikali yenu inafuatilia suala hili na Rais Dkt. John Magufuli anataka kuona pamba yote inatoka kwa wakulima ili kuwawezesha kupata tija.”

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwasihi wakulima wa zao hilo la pamba na wakulima wa mazao mengine nchini wahakikishe mara baada ya kuuza mazao yao wanatenga kiasi cha fedha kwa ajili ya kununulia pembejeo watakazozitumia katika msimu ujao.

Wananchi kwa upande wao waliishukuru Serikali kwa hatua yake ya kuingilia kati suala la ununuzi wa zao la pamba pamoja na malipo kwa wakulima ambao tayari pamba yao walishaipeleka katika AMCOS zao.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga alisema Serikali itahakikisha inaendelea kutafuta masoko ya mazao hayo ndani na nje ya nchi ili kuwawezesha wakulima kuwa na uhakika wa masoko kwa mazao yao na hivyo kujiongezea tija.

Pia, Waziri huyo alisema mbali na kutafuta masoko, Serikali imedhamiria kufufua viwanda mbalimbali vya nguo hapa nchini ili kuwawezesha wakulima wa zao la pamba kuwa na soko la uhakika. “Kuhusu suala la maghala tunatambua tatizo hilo na tutahakikisha tunayaboresha ili pamba iweze kuhifadhiwa katika mazingira bora”.

Akizungumzia kuhusu changamoto ya viuatilifu, Waziri Hasunga alisema Serikali itahakikisha vinapatikana kwa kuzingatia eneo husika ili kuweza kudhibiti wadudu waharibufu.

(MWISHO)
Read More