*DED aahidi
kuliwasilisha kesho kutwa jioni
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Same, Bi. Anna-Clare Shija apeleke gari haraka katika
shule ya sekondari ya wavulana ya bweni ya Same ili kumsaidia mwalimu mkuu
endapo kutatokea dharura.
“Shule hii ina wanafunzi zaidi ya 800 lazima iwe na
chombo cha usafiri kitakachotumika kwa dharura za kuwapeleka hospitali
wanafunzi pale wanapougua. Sasa hivi mwanafuzi akiugua, Mwalimu Mkuu
anafanyaje? Ni kama ameachiwa jukumu hili peke yake,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana (Ijumaa, Julai
19, 2019) wakati alipotembelea shule hiyo na kuzindua mradi wa ukarabati wa
shule kongwe ya sekondari ya Same na kisha kuzungumza na wanafunzi, walimu na
baadhi ya wazazi waliokuwepo.
Waziri Mkuu alimwita Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Bi.
Shija na kumtaka atoe jibu hadharani kwamba ni lini atapeleka gari hilo shuleni
hapo. Mkurugenzi huyo aliahidi kulipeleka gari hilo ifikapo Jumatatu jioni
(Julai 22, 2019).
“Haya maelekezo ni kwa wakurugenzi wa Halmashauri
zote nchini wenye shule ambazo zina wanafunzi zaidi ya 700. Mnapaswa
kuhakikisha kunakuwa na gari la shule ili ikitokea dharura, Mkuu wa Shule aweze
kuingilia kati na kupata ufumbuzi.”
“Wakurugenzi mnatakiwa kutambua shule hizi ni zenu, kwa
hiyo mnalo jukumu la kuzihudumia. Shule hii ya Same ina wanafunzi zaidi ya 800
na wanalala hapa hapa, ni lazima kuwe na gari la kuwahudumia hasa wakati wa
dharura.”
Pia amemuagiza Mkurugenzi huyo atafute daktari na
muuguzi mmoja na awapangie kwenye shule hiyo ili waweze kutoka huduma kwa
wanafunzi na kuwapunguzia adha ya kwenda mjini kutafuta huduma hiyo.
Waziri Mkuu alifikia uamuzi huo baada ya kupokea changamoto
zilizowasilishwa na kijana Omary Said wa kidato cha sita mchepuo wa PCB ambaye
alisema shule hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji; uchakavu wa mabweni;
ukosefu wa zahanati ya shule na uhaba wa walimu wa sayansi hasa wa masomo ya
fizikia.
Mapema, akitoa
taarifa ya ukarabati, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bw. Hoza Mgonja alisema
ukarabati huo ambao umegharimu sh. milioni 919, ulifanikisha ukarabati wa
majengo saba ya madarasa yenye vyumba 22; maabara tatu, vyoo viwili vyenye
matundu tisa; jengo moja la walimu; maktaba yenye vyumba viwili na ofisi mbili;
vyoo viwili vyenye matundu manne na miundombinu ya umeme na majitaka.
Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake mkoani
Kilimanjaro kwa kutembelea wilaya ya Mwanga ambako atazungumza na watumishi na
kisha ataenda kijiji cha Kirya, Nyumba ya Mungu kukagua mradi wa maji wa Same -
Mwanga - Korogwe.
(mwisho)
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.