*Apokea treni ya
kwanza yenye tani 800 za saruji
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea treni ya kwanza
ya mizigo kutoka Tanga ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa reli ya kutoka Tanga hadi
Moshi.
Waziri Mkuu amepokea treni hiyo leo (Jumamosi, Julai
20, 2019) ambayo iliwasili saa 4:30 asubuhi kwenye stesheni ya Moshi na kukata
utepe wa uzinduzi saa 4:32, kisha akapanda kwenye treni hiyo saa 4:33.
Akizungumza na mamia ya wakazi wa mji wa Moshi na
wengine kutoka mkoa jirani wa Tanga, Waziri Mkuu amesema amefurahi kupokea
treni hiyo yenye mabehewa 20 yaliyokuwa na mzigo wa tani 800 za saruji kutoka
kampuni ya Saruji ya Tanga.
Amesema kukamilika kwa kipande cha reli ya Tanga - Moshi
na kuanza kutoa huduma leo hii, ni mwendelezo wa utekelezaji wa dhamira ya
Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji inafaidika
na fursa ya kijiografia iliyopo nchini kwa kutoa huduma za usafiri na uchukuzi
wa reli kwa uhakika, usalama na kwa gharama nafuu.
“Wataalamu wa masuala ya usafirishaji duniani wanaeleza
kuwa matumizi ya reli kwa ajili ya usafirishaji wa shehena, hupunguza gharama za
bidhaa kwa asilimia kati ya 30 na 40. Vilevile, matumizi ya reli huwa ni
kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi kutokana na ukweli kwamba, kupitia usafiri
wa reli unaweza kusafirisha mizigo mingi kwa haraka na kwa wakati mmoja kwenda
kwa mlaji,” amesema.
Amesema kama ilivyo kwa mradi wa SGR, njia ya reli ya Tanga - Moshi yenye
urefu wa km. 353, ukarabati wake unagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na umetekelezwa na wataalamu wazawa.
“Kwa msingi huo, naagiza viongozi na watendaji wa mikoa na maeneo ambayo
yanapitiwa na reli hii, kwa kushirikiana na Shirika la Reli Tanzania, waanze
mara moja kampeni ya kutoa elimu kwa umma kuhusu usalama lakini pia
kuwakumbusha wananchi kuwa walinzi wa miundombinu hii muhimu ya reli,” amesema.
Akitoa salamu kwa
niaba ya makatibu wakuu wa vyama 19 vya siasa nchini, Katibu Mkuu wa ADC, Bw.
Hassan Doyo alisema kufufuliwa kwa treni hiyo ya mizigo kutawasaidia wachimbaji
wa madini walioko Makanya, Same ambao walikuwa wakipata taabu ya kukodisha
malori na kusafirisha bidhaa zao hadi kiwanda cha saruji cha Tanga.
Alisema reli hiyo itawanufaisha pia wachimbaji wa
Kabuku, wilayani Handeni. "Wachimbaji wa madini ya chuma walioko
Kabuku, walikuwa wanapata shida ya kusafirisha mizigo yao kwa barabara hadi
Mtwara, gharama ziko juu mno. Lakini sasa watapata ufumbuzi baada ya reli
hii kufufuliwa," alisema.
Mapema, akitoa
taarifa kuhusu mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC),
Bw. Masanja Kadogosa alisema makadirio ya gharama za kufufua reli hiyo kutoka
Korogwe hadi Arusha yalikuwa sh. bilioni 14 lakini mpaka sasa wametumia sh.
bilioni 5.7.
Alisema ujenzi huo ulifanywa na wafanyakazi wazawa
525 kutoka TRC wakiwemo vibarua 466, wahandisi 12 na mafundi wa reli na nyanja
nyingine 47. "Hawa watapata ajira ya kudumu na ndiyo wataisimamia hii
reli," alisema.
Alisema reli ya mizigo ilikuwa haifanyi kazi kwa
miaka 12 iliyopita na huduma ya kusafirisha abiria ilisitishwa tangu mwaka
1994.
Hafla huyo ilihudhuriwa na Naibu Mawaziri wa
Uchukuzi, TAMISEMI, Wabunge, watendaji wa Serikali, wawakilishi wa vyama vya
siasa na wananchi mbalimbali.
(mwisho)
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.