Friday, July 5, 2019

VIONGOZI WA DINI IMARISHENI MALEZI KWA VIJANA-MAJALIWA

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema viongozi wa dini waendelee kuimarisha malezi na mafundisho ya kiroho kwa vijana na kuepusha mmomonyoko wa maadili ili Taifa liendelee kung’ara, kuheshimika na kusifika duniani kwa utulivu, amani na umoja. 

Amesema Serikali inatambua mchango wa madhehebu ya dini ikiwemo CCT katika kutengeneza mustakabali mwema na ustawi wa familia kupitia mahubiri ya injili na malezi ya kiroho kwa waamini. “Mtakubaliana nami kuwa siku zote Taifa imara msingi wake hujengwa na familia imara.” 

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Julai 5, 2019) wakati alipomwakilisha Rais Dkt. John Magufuli kwenye Mkutano wa Halmashauri Kuu ya 53 ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) ulioambatana na harambee ya kukusanya fedha kwa ajili ya ujenzi wa kitegauchumi cha jumuiya hiyo. Mkutano huo umefanyika jijini Dodoma.

Amesema Serikali inatambua mchango wa malezi ya kiroho katika ustawi wa wananchi na Taifa kwa ujumla na mafundisho yake kwani yamesaidia kujenga watumishi wa umma ambao wamelelewa katika misingi bora ya kumcha Mwenyezi Mungu.    

Waziri Mkuu amesema Serikali inaamini kwamba watumishi wa namna hiyo watachapa kazi kwa bidii, uadilifu, uaminifu na kupiga vita vitendo vyote vya rushwa na ubadhilifu wa mali za umma. Serikali itaendelea kushirikiana na Taasisi za kidini kwa ajili ya ustawi wa Taifa na watu wake.

Akizungumzia kuhusu harambee hiyo ambayo jumla ya sh. milioni 357.35 zilipatikana, Waziri Mkuu amesema ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa CCT wa miaka mitano (2017 – 2022) wenye lengo la kuiwezesha CCT kujitegemea kwa kuwa na vitega uchumi vyake ambavyo vitawawezesha kujiendesha kwa asilimia 80.

Waziri Mkuu ameipongeza CCT kwa kuanza kuchukua hatua za kujenga uwezo wa ndani wa kujitegemea kiuchumi kwani zinahitajika nguvu za pamoja katika kuhakikisha wanawahudumia Watanzania na kuwaletea maendeleo. 

“Kujizatiti kwa CCT katika kufikia malengo yake ya kujitegemea kiuchumi ni muhimu katika kutimiza kusudio na agizo la Mungu la kuwahudumia wahitaji ambao ni Watanzania lakini pia mtakuwa mnajaliza juhudi za Serikali katika wajibu wake wa kuwahudumia wananchi.”

Waziri Mkuu amesema kwa msingi huo, Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za CCT na madhehebu mengine ya dini katika kuwahudumia Watanzania kupitia sekta za elimu, maji, afya na shughuli za ujasiriamali.

Amesema suala la kujitegemea ndiyo msingi wa uongozi wa Rais Dkt. Magufuli wa kujenga uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025 na katika kufanikisha hilo, Serikali imeendelea kupunguza kiwango cha utegemezi.

Amesema kiwango cha utegemezi kutoka kwa Washirika wa Maendeleo katika bajeti kimepungua kutoka asilimia 12.5 mwaka 2017/2018 hadi asilimia nane 2019/2020. “Kuimarika huko kwa bajeti yetu kunakwenda sambamba na kuimarika kwa huduma za kijamii kama vile elimu, maji na kupungua kwa umaskini wa mahitaji muhimu.”

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCT, Mchungaji Canon Moses Matonya, amesema jumuiya hiyo imeanzisha mkakati wa kuwa na vitegauchumu vyake kwa lengo kuondokana na utegemezi wa fedha za ufadhili ambazo zimekuwa zikipungua mwaka hadi mwaka.

(mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.