Friday, July 19, 2019

WAZIRI MKUU AMSIMAMISHA KAZI MHANDISI WA MAJI SAME

*Azivunja Jumuiya za watumiaji maji Hedaru
*Aagiza Katibu wa Jumuiya moja akamatwe

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Same, Mussa Msangi kwa kosa la kumdanganya kuhusu mradi wa maji aliouzindua leo katika kata ya Hedaru.

Amechukua uamuzi huo leo jioni (Ijumaa, Julai 19, 2019) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa Hedaru mara baada ya kuzindua mradi wa maji wa Lengeni-Hedaru, wilayani Same.

Waziri Mkuu alibaini kuwepo kwa tatizo wananchi walipoanza kuzomea wakati zikitolewa salaam za utambulisho kwa viongozi alioambatana nao. Kabla hajahutubia, aliamua kumuita Mhandisi huyo aelezee ukweli wa madai ya wananchi kwamba maji yametoka leo kutokana na ujio wake.

"Eleza ni kwa nini nilipofungua maji, hayakuwa na presha ya kutosha na wewe umesema upatikanaji wa maji umefikia zaidi ya asilimia 80?"

Alipoulizwa kwa mwezi wanakusanya kiasi gani cha fedha kutokana na mauzo ya maji hayo, Mhandisi Msangi alijibu kwa mwaka uliopita walikusanya sh. milioni saba tu.

"Haiwezekani kama maji yanatoka, wenye KAMATI wapate shilingi milioni saba. Ni ama maji hayatoki au wanakusanya hela na wanazila."

Alipoambiwa aelezee utendaji wa mradi huo wa maji na kama alikuwa akiufuatilia, alishindwa kutoa maelezo kamili, akidai kuwa leo maji yanatoka kidogo kwa sababu kuna hali ya mawingu. "Mbona kule ndani ulisema zile betri zinasaidia kuvuta maji na kubalance upatikanaji wa maji wakati hakuna jua la kutosha?" alihoji Waziri Mkuu. 

Waziri Mkuu aliamua kumuita mwenyekiti wa Jumuiya ya watumiaji maji au Kiongozi mwingine yeyote aje atoe maelezo, lakini wote hawakuwepo kwenye mkutano huo. Ndipo akachukua uamuzi wa kuzivunja jumuiya hizo.

"Jumuiya zote za maji nazivunja kuanzia leo, na wahusika wote watafutwe na Jeshi la Polisi. Haiwezekani nipewe kazi ya kuzindua mradi ambao hauna maji," alisema Waziri Mkuu.

"Katibu Tawala wa Mkoa lete wakaguzi wa mahesabu kwenye huu mradi, pia leta Mhandisi mwingine asimamie huu mradi. Huyu arudishwe kwa Waziri wake," alisema.

Waziri Mkuu pia alimwagiza Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Awesu abaki Hedaru na afuatilie utendaji wa mradi huo kisha ampe taarifa.

Wakati akimaliza kutoa maagizo hayo, Katibu wa Jumuiya ya watumiaji maji Hedaru-Masasi (HEWAUA), Bw. Francis Kazen Kiondo aliletwa akiwa chini ya ulinzi wa polisi, lakini Waziri Mkuu alielekeza apelekwe kituoni akatoe maelezo.

Taarifa zilizothibitishwa zimebainisha kuwa Kata ya Hedaru inazo Jumuiya tatu za watumiaji maji ambao ni Hedaru-Masasi, Lung wana na Mradi wa Kati. Wakazi wa Hedaru wanakadiriwa kufikia 20,000.

Ilibainika kwamba wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Hedaru-Masasi, Bw. Clement Ngoka aliamua kujiuzulu nafasi hiyo kwa sababu ya upinzani aliokuwa akipata kwa viongozi wenzake ambao pia wanadaiwa kuwaunganishia maji baadhi ya watu hadi majumbani kwao na fedha zilizolipwa hazijulikani zilipoenda.

Awamu ya pili ya mradi wa maji alioenda kuuzindua Waziri Mkuu, inahusisha ujenzi wa chanzo cha maji katika korongo la mto Rangeni ambao ulikamilika Desemba 2018. Chanzo hicho cha mtiririko, kilitarajiwa kuzalisha lita 750,000 kwa siku ili kusaidia maji yanayozalishwa kwenye visima ambayo yana ujazo wa lita 7,500 kwa saa.

(mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.