Sunday, July 28, 2019

WAZIRI MHAGAMA ATOA MAAGIZO KWA VIONGOZI WA SHAMBA LA KATANI LA HASSAN SISAL ESTATE

 Na; Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ametoa maagizo kwa viongozi wa Shamba la Katani la Hassan Sisal Estate kuhakikisha wanatatua migogoro na wafanyakazi pamoja na kusimamia haki zao ipasavyo.
Waziri Mhagama ametoa maagizo hayo wakati wa ziara yake Wilayani Same alipofanya ziara katika Shamba la Hassan Sisal Estate ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa kuhusu masuala ya kazi aliyoyatoa Julai 20, 2019 alipotembelea shamba hilo lililopo Mkoani Kilimanjaro, Wilaya ya Same.
Akizungumza na wafanyakazi pamoja na viongozi wa shamba hilo, alieleza kuwa waajiri wanatakiwa kutekeleza matakwa yote ya Sheria za ajira na mahusiano kazini kwa kuzingatia miongozo na kanuni ambayo inasimamia haki za msingi kwa wafanyakazi.  
“Tunataka kuona ninyi kama waajiri mnakuwa na vikao vyenye tija na wafanyakazi katika kuleta suluhu ya masuala mbalimbali ya kazi,” alisema Mhagama
Aliongeza kuwa Kampuni mbili zilizopo katika shamba hilo yaani Unique Consultancy na UPAMI kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wafanyakazi hao, ikiwemo kuwasilisha michango kwa wakati kwenye Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF). Pamoja na hayo alishauri pia kampuni hizo kuwaweka wazi wafanyakazi kuhusu mikataba yao.
“Malalamiko na Manung’uniko ya wafanyakazi ni mengi, mnatakiwa kukaa na kujadili pamoja namna bora ya kutatua matatizo yao yanayojitokeza hususani kwenye mikataba,” alisema Mhagama.
Katika hatua hiyo, Mhe. Mhagama alimuagiza Meneja wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA), kufanya kanguzi za mara kwa mara katika shamba hilo na kuangalia kama wafanyakazi wanakabidhiwa vifaa vya kujinginga na madhara kazini (Protective gears) kwa wakati, pamoja na kusimamia zoezi la upimaji afya kwa wafanyakazi  hao.
Pia, alitoa maelekezo kwa Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Kilimanjaro, kukabidhi kadi za uwanachama kwa wafanyakazi wa shamba hilo la Hassan Sisal Estate na kufuatilia uwasilishaji wa michango yao kutoka kwa waajiri wao.
Sambamba na hilo, Waziri Mhagama ametaka  Afisa Kazi Mfawidhi wa Mkoa wa Kilimanjaro kutembelea shamba hilo na maeneo mengine mbalimbali katika mkoa huo ili kuelimisha wafanyakazi sheria mbalimbali za kazi na ajira zitakazo wawezesha kutambua haki zao za msingi.
Aidha, Waziri Mhagama alitoa maelekezo juu ya uwepo wa vyama vya wafanyakazi kwenye mashamba yote ya katani yaliyopo nchini, vitakavyosadia kuongeza tija na ufanisi katika shughuli mbalimbali za utendaji kazi.
Pamoja na hayo, Mheshimiwa Mhagama aliwataka viongozi wa shamba hilo kuendelea kusimamia vizuri maslahi ya wafanyakazi wao ili waweze kutekeleza majukumu ya kila siku wanapokuwa katika maeneo yao ya kazi.
Naye, Meneja Mshauri wa Shamba hilo, Bw. Ndekirwa Nnyari aliahidi kufanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa ikiwemo kuwa na majadiliano ya mara kwa mara na wafanyakazi kwa itakayowapa munufaa ya pamoja.
Kwa upande wake, Meneja wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Victor Luvena amesema kuwa watatekeleza maagizo yaliyotolewa na Mheshimiwa Waziri kwa kuchukua hatua za kisheria kwa wale watakaoshindwa kutekeleza.
Pia mmoja wa Wafanyakazi wa Shamba hilo, Bi. Cheshi Juma alisema kuwa ujio wa Waziri na wataalamu alioambatana nao utasaidia kuondoa kero za wafanyakazi na kujenga mahusiano mazuri na waajiri wao.
“Tumehamasika sana kuona Serikali yetu ipo pamoja nasi katika kutetea maslahi ya wafanyakazi na kushughulikia kero tulizokuwa tukikabiliana nazo katika maeneo ya kazi,” alisema Cheshi

Meneja Mshauri wa Shamba la Katani la Hassan Sisal Estate, Bw. Ndekirwa Nnyari (Kushoto) akitoa maelezo kuhusu shamba hilo na masuala ya wafanyakazi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama alipofanya ziara katika shamba hilo Julai 27, 2019.
Baadhi ya wafanyakazi wa Shamba la Katani la Hassan Sisal Estate wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipofanya ziara katika shamba hilo kufuatia maagizo ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa kuhusu masuala ya kazi aliyoyatoa Julai 20, 2019 alifanyaziara Mkoani Kilimanjaro.
Sehemu ya Wataalamu walioambana na Mhe. Waziri na  wafanyakazi wa Shamba la Katani la Hassan Sisal Estate wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipofanya ziara katika shamba hilo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akiteta jambo na Afisa Kazi Mfawidhi kutoka Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Mwinyi Mkuu wakati wa ziara yake Wilayani Same katika Shamba la katani la Hassan Sisal Estate.
Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Large Mature akifafanua jambo kuhusu uwasilishaji wa michango ya wafanyakazi wa Shamba la katani la Hassan Sisal Estate.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akihakiki malipo ya wafanyakazi wa Shamba la katani la Hassan Sisal Estate alipokuwa akioneshwa na Meneja Mkuu wa Unique Consultance Bw. Edwin David (Kulia) . Afisa Kazi Mfawidhi kutoka Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Mwinyi Mkuu (katikati).
Mmoja wa Wafanyakazi wa Shamba la katani la Hassan Sisal Estate Bw. Salum Issa akimwelezea Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani), changamoto wanazokumbana nazo katika utendaji kazi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akisikiliza kero kutoka kwa mfanyakazi wa Shamba la katani la Hassan Sisal Estate, alipofanya ziara kwenye shamba hilo Julai 26, 2019 kwa lengo la kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa kuhusu masuala ya kazi aliyoyatoa Julai 20, 2019.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Rosemery Staki (kulia), alipofanya ziara Wilayani huo kwa lengo la kufuatia maagizo ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa kuhusu masuala ya kazi aliyoyatoa Julai 20, 2019.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama na Meneja Mshauri wa Shamba la Katani la Hassan Sisal Estate, Bw. Ndekirwa Nnyari (katikati) akiwatambulisha baadhi ya viongozi wa Shamba la katani la Hassan Sisal Estate.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.