Sunday, July 28, 2019

WAZIRI MKUU APOKEA MSAADA WA VIFAA TIBA VYENYE THAMANI YA SH. MILIONI 250


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea msaada wa vifaa tiba wenye thamani ya sh. milioni 250 vilivyotolewa na Shirika la Helping Hand for Relief and Development (HHRD) kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa.

Baadhi ya vifaa hivyo ni vitanda vya kujifungulia, vitanda na magodoro ya wagonjwa, mashine za matibabu, viti vya wagonjwa (wheelchairs), vifaa vya maabara, mashine ya oksijeni, meza za kufanyia upasuaji, mablanketi, mafriji na samani za ofisini.

Akipokea msaada huo leo mchana (Jumapili, Julai 28, 2019) kwenye zahanati ya Nandagala, wilayani Ruangwa mkoani Lindi, Waziri Mkuu amewashukuru viongozi wa shirika hilo kwa kuchangia vifaa vingi ambavyo amesema vitasambazwa katika wilaya nzima ya Ruangwa.

“Tunawashukuru wadau wetu wa HHRD ambao wanashirikiana na taasisi ya Jamii Bora. Vifaa hivi ni kwa niaba ya wilaya nzima. Nitamkabidhi Mkuu wa Wilaya ili aone ni wapi pana uhitaji zaidi, naye atavisambaza,” amesema.

Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Nandagala mara baada ya kupokea vifaa hivyo, Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruangwa, amesema ujenzi wa vituo vya afya kwenye kata za Mandawa, Nkowe na Mbekenyera umesaidia kuwafanya wananchi wa kata hizo wapate huduma muhimu za matibabu wakiwa huko huko.

“Kwenye bajeti ya mwaka huu, tunatarajia kupata sh. milioni 400 ambazo zitapelekwa Luchengelwa ili wapate kituo cha afya na huduma nyingine zote ziishie huko huko. Nimefurahi kumsikia Mkuu wa Wilaya akisema kuwa wataipigia debe zahanati ya Nandagala ili ipandishwe hadhi na kuwa kituo cha afya.”

Pia alilipongeza Shirika la HHRD kwa kuamua kuwahudumia watoto yatima, wajane na kuamua kutoa huduma za maji kwa kuchimba visima. “Ninawapongeza pia kwa kuamua kuwafundisha vijana wanaohitimu vyuo vikuu na kuwapa elimu ya ujasiriamali vijana wetu, kwa kuwaandaa wawe wabunifu na wajiajiri. Asanteni sana kwa kuwaondolea dhana ya ajira kwamba ni lazima washike kalamu na wakae ofisini,” alisema.

Mapema, akitoa taarifa ya msaada huo, Mwenyekiti wa Bodi ya HHRD, Bw. Yassir Salim Awadh alisema wana mradi wa utoaji vifaa tiba, chakula, nguo na sabuni unaolenga kuziwezesha hospitali za wilaya, mkoa na rufaa za Serikali, familia maskini na magereza ambao ulianza tangu mwaka 2014.

“Kupitia mradi huu, kati ya mwaka 2014 na 2018 tumeweza kugawa makontena 62 kwa nchi nzima. Mwaka huu 2019, tumepanga kuleta makontena 20 ambapo saba tayari yameshatumwa, matatu yameshafika na kugawiwa Zanzibar, manne yako njiani na yanatarajiwa kufika Oktoba, 2019.”

Alisema thamani ya vifaa kwa makontena yote pamoja na yale yanayotarajiwa kufika mwaka huu ni sh. bilioni 23.75. “Kupitia mradi huu tumeweza kutoa vifaa tiba vya aina mbalimbali katika hospitali za Kivunge, Makunduchi, Mnazi Mmoja, Wete, Abdallah Mzee (zote za Zanzibar). Nyingine ni Temeke, Kisarawe, Muhimbili, Mwananyamala, Bagamoyo na leo ni katika wilaya ya Ruangwa,” alisema.

Pia alisema shirika hilo lenye makao yake makuu Marekani na linajishughulisha na utatuzi wa changamoto za kijamii kweye sekta za afya, elimu, mayatima na matukio ya dharura, limeweza kuhudumia watoto yatima waishio majumbani 250 kutoka shule tisa za wilayani Kisarawe kwa kuwapatia vifaa vya shule, upimaji wa afya, mafunzo ya kujitegemea, michezo na safari za kimasomo.

“Shirika pia linajihusisha na uchimbaji visima vifupi. Hadi mwaka huu tumechimba visima zaidi ya 100 katika wilaya za Mkuranga, Kilwa, Kigambini, Ilala, Temeke, Morogoro, Kilosa, na wilaya zote za Unguja.”

Bw. Awadh alisema huduma nyingine wanayotoa ni upasuaji wa mtoto wa jicho ambapo katika kipindi cha miaka mitatu wameweza kufanya operesheni 525 kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo Kilwa, Kibaha, Mkuranga, Kisarawe, Unguja na Pemba. “Mwaka huu, tunatarajia kufanya operesheni nyingine 75 mkoani Dar es Salaam,” alisema.

Naye Mkazi wa Nandagala ‘A’, Bi. Atiya Chilatu aliishukuru taasisi ya HHRD kwa kuwapatia vifaa tiba kwenye zahanati yao. “Hii maana yake tutapata huduma zote hapahapa, hatuna haja ya kwenda wilayani,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Bw. Hashim Mgandilwa alisema msaada wa vifaa hivyo utaharakisha ujenzi wa zahanati ya Nandagala. “Msaada huu utaharakisha safari ya kupandisha hadhi zahanati ya Nandagala ifikie kuwa kituo cha afya,” alisema.

Alisema wilaya hiyo imepokea sh. bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya na kukiri kuwa wamepokea fedha nyingine za uboreshaji wa vituo vya afya katika kata za Mkowe, Mbekenyera na Mandawa. “Hadhi ya vituo hivi kwa sasa imebadilika,” alisema.

(mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.