Tuesday, July 2, 2019

RAIS KENYATTA AMTUMIA UJUMBE RAIS DKT. MAGUFULI

*Ni kuhusu kuchukizwa kwake na kauli ya Jaguar 
RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta amemtumia ujumbe maalumu Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli unaoelezea msimamo wa Serikali yake kuhusu kukerwa na matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Mbunge wa jimbo la Starehe, Charles  Njagua Kanyi maarufu kwa jina la Jaguar.

 Ujumbe huo wa maandishi umewasilishwa leo (Jumanne, Julai 02, 2019) na Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Dany Kazungu na kupokelewa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais Dkt. Magufuli, ofisini kwa Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar Es Salaam. 

Akipokea taarifa hiyo Waziri Mkuu amesema Watanzania wamefurahishwa na hatua mbalimbali zilizochukulia na Serikali ya Kenya dhidi ya mbunge huyo zinazodhihirisha kwamba matamshi hayo hayakuwa msimamo wa Serikali ya Kenya wala wananchi wake bali  ulikuwa ni msimamo  binafsi wa mbunge huyo.

Amesema siku zote Watanzania na Wakenya wamekuwa huru kuishi na kufanya kazi au biashara katika nchi za Afrika ya Mashariki na pale yalipotokea matatizo au kutokukubaliana serikali husika zilikaa mezani na kumaliza tofauti hizo.

"Uhusiano kati ya Kenya na Tanzania ni wa karibu mno na wa kidugu kwani kuna baadhi ya makabila yapo katika nchi mbili hizi kama vile Wamasai na Wakurya na  Wajaluo  hivyo ushirkiano katika masuala ya mbalimbali yakiwemo ya  kabiashara na ya kijamii haukwepeki."

Hivyo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa viongozi na wananchi wa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kujiepusha na kauli zenye viashiria vya  kujenga chuki, uhasama na migongano miongoni mwa wananchi kwani  kauli hizo zisipodhibitiwa mapema zinaweza kusabisha hofu na kutokuelewana miongoni mwao.

Waziri Mkuu  ametumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania kuendelea kuishi kwa amani na upendo na ndugu zao wa Kenya na wageni wote kutoka nchi za Afrika ya Mashariki na duniani kwa ujumla ambao wapo nchini wakifanya shughuli mbalimbali kwa mujibu wa sheria za nchi. 

“Mambo yetu yote katika nchi za Afrika ya Mashariki  hasa ya biashara na ya  kiuchumi kwa ujumla yataenda vizuri endapo  tutalinda na kudumisha amani, bila amani tutaogopana na tutashindwa kabisa  kushirikiana”, amesisitiza Mheshimiwa Majaliwa.

Waziri Mkuu  ameahidi kuwa Serikali ya Tanzania kamwe ahaitaruhusu wala kufumbia macho kauli au vitendo vyovyote vyenye viashiria vya uchochezi  dhidi ya nchi jirani  ili na kulinda na kuunga mkono juhudi mbalimbali za ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi zinazofanywa na viongozi  wakuu wa Mataifa ya Afrika.

Kwa upande wake Balozi Kazungu amemshukuru Waziri Mkuu kwa kauli yake aliyoitoa Bungeni jijini Dodoma iliyowataka Watanzania kuwa watulivu na wayachukulie matamshi ya Mbunge wa jimbo la Starehe nchini Kenya, Njagua kuwa ni msimamo wake binafsi na siyo  msimamo wa Wakenya na Serikali yao.

Balozi Njagua mesema Msimamo wa Rais Kenyatta siku zote umekuwa ni kuwapokea na kuwakubali ndugu zao  wote wanaotoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki walioamua kuishi au kufanya biashara nchini Kenya.

Mwanzoni mwa wiki iliyopita Mbunge wa jimbo la Starehe nchini Kenya Njagua alitoa matamshi ya kichochezi akiwataka raia wa kigeni kutoka Mataifa mbalimbali wanaofanya shughuli za kibiashara nchini Kenya wakiwemo Watanzania waondoke ndani ya muda wa saa 24.

 


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.