Na.
OWM, DODOMA.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, amelitaka
Baraza la Vyama vya siasa nchini kuendelea kutekeleza majukumu yake ipasavyo
kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu juu ya masuala
yenye maslahi kwa Taifa kuhusiana na vyama vya siasa pamoja na hali ya kisiasa nchini ili
kuimarisha ustawi wa siasa na vyama vya siasa nchini.
Mhe. Waziri Mhagama ameyasema hayo wakati
akifungua kikao cha siku mbili cha Baraza hilo kilichoanza jana na kinafungwa
leo, tarehe 24, Julai 2019, mjini Dodoma katika ukumbi wa Pius Msekwa, ambapo Mhe.
Mhagama amesisitiza vyama hivyo kuendelea kushirikiana na kudumisha upendo na
umoja wa kitaifakatika katika kutekeleza majukumu yao ya kisiasa ili kuweza
kuijenga Tanzania yenye umoja.
“Endeleeni kutumia fursa za vikao vya
Baraza kutatua matatizo yenu na niwashauri muunde kamati za Baraza na kutumia kamati hizo
katika kutatua matatizo yenu, lakini pia tekelezeni majukumu yenu kwa
kuzingatia sheria, kanuni na taratibu tulizonazo hapa nchini ili vyama viweze
kuisaidia nchi na watanzania kuyafikia malengo yao kwa kuwajenga watanzania
kuwa wamoja badala ya kuwagawanya” amesema Mhagama
Mhe. Waziri Mhagama amefafanua kuwa
katika vikao vyao na serikali Baraza hilo walikuwa na matakwa yao ambayo
walitaka serikali iyatekeleze kupitia ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa
nchini ambapo tayari serikali imeyatekeleza ikiwemo kuanzisha ofisi ya Naibu
msajili wa vyama vya siasa Zanzibar.
“Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais, Mhe. Dkt John Pombe Magufuli, kupitia
ofisi ya Waziri Mkuu, katika bajeti yake, ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
siasa, tayari imetenga bajeti ya kuiendesha Ofisi ya Naibu Msajili wa vyama vya
siasa Zanzibar, lakini pia sisi serikalini tumeshakubaliana kuwashirikisha
viongozi wa Baraza la vyama vya siasa katika matukio ya shughuli za maendeleo
ya serikali ili viongozi nyie muweze kuelewa vyema mabadiliko ya utekelezaji
yanayofanywa na serikali ya awamu ya tano” Amesisitiza Mhe. Mhagama.
Aidha, Mhe. Mhagama ameeleza kuwa
Wajumbe wa Baraza hilo watakuwa wakijengewa uwezo katika masuala ya siasa ili
kuweza kuendelea kujenga msingi imara na ustawi wa demokrasia nchini.
Awali, akiongea katika kikao hicho,
Mwenyekiti wa Baraza hilo, John Shibuda, ameeleza kuwa wanashukuru kwa
ushirikiano ambao wamekuwa wakiupata kutoka serikalini kupitia Ofisi ya Msajili
wa Vyama vya siasa ambapo ameomba kuendelea kushirikishwa ipasavyo ili waweze
kuelewa vyema utekelezaji wa shughuli za maendeleo za serikali ya awam ya tano.
“Baraza tunamshukuru sana Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Mhagama kwa ushirikianao ambao amekuwa
akitupatia Baraza kimsingi hivi leo tunajivunia miaka miwili ya utendaji wa
Baraza letu lakini msingi wa mafanikio hayo ni Waziri huyu amekuwa ufungua ambao atufungulia milango kila jambo
tunalotaka kulitekeleza kwa wakati ” amesema Shibuda.
Kikao hicho kimehudhuriwa na
Msajili wa vyama vya siasa nchini, Mhe. Jaji Francis Mutungi, Naibu Msajili wa Vyama vya siasa, Mhe. Mohammed
Ally Ahmed, pamoja na wajumbe wa Baraza hilo ambao ni vyama vyenye usajili wa
kudumu. Baraza la Vyama vya Siasa limeanzishwa chini ya kifungu cha 21B cha
Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258 ikiwa ni jukwaa la viongozi wa kitaifa wa
vyama vya siasa kukutana mara kwa mara kujadiliana masuala yanayohusu
demokrasia ya vyama vingi na siasa hapa nchini kwetu. Baraza
hilo limeundwa ndani ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambapo, Wajumbe wa
Baraza hilo hujumuisha viongozi wa kitaifa wawili wa kila chama cha siasa
chenye usajili wa kudumu. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa ndio yenye jukumu
la kisheria ya kuratibu shughuli za Baraza la Vyama vya Siasa.
Majukumu ya Baraza hilo ni
pamoja na kumshauri Msajili wa vyama vya siasa juu ya masuala yenye maslahi kwa
Taifa kuhusiana na vyama vya siasa au kuhusiana na hali ya kisiasa nchini Siasa na sheria zingine zinazohusu masuala.
MWISHO
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.