Saturday, July 27, 2019

WAZIRI MKUU AAGIZA WALIMU WAWILI WAPELEKWE NANGANGA KESHOKUTWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Afisa Elimu wa Wilaya ya Ruangwa anayeshughulikia elimu ya msingi, Bw. Selemani Mrope atafute walimu wawili kutoka Ruangwa na kuwahamishia kata ya Nanganga mara moja.

"Lazima kuna walimu wamejazana pale Ruangwa mjini, leo tukitoka hapa nenda kaandike barua za uhamisho. Kesho Jumapili, wahusika wapewe barua zao na Jumatatu waje kuripoti hapa Nanganga," amesema Waziri Mkuu na kuamsha shangwe miongoni mwa wakazi wa Nanganga.

Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumamosi, Julai 27, 2019) wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Nanganga, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi alipopita kuwasalimia wakazi hao.

Waziri Mkuu ambaye amewasili Lindi leo kwa mapumziko mafupi, alipokea taarifa ya shule ya msingi Nanganga ambayo ilionesha kuwa shule hiyo yenye wanafunzi 237 ina walimu sita tu. Kati ya hao, wavulana ni 124 na wasichana ni 113.

“Shule hii ina madarasa nane likiwemo darasa la awali, masomo yanayofundishwa ni tisa, mkibaki na walimu hawa sita, mzigo unakuwa mkubwa kwa walimu hawa waliopo. Afisa Elimu tafuta wawili walimu waje hapa Jumatatu, na Mkurugenzi wa Halmashauri atakupa gari ya kuwahamishia hapa,” amesema. Shule ya msingi Nanganga, iliyoko kata ya Nanganga, iko umbali wa km. 59 kutoka Ruangwa mjini.

Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa Ruangwa, amewataka wakazi wa kata hiyo wafikirie kuanza ujenzi wa shule ya sekondari yao ya kata ili kuwapunguzia safari wanafunzi wa kijiji hicho ambao kwa sasa wanalazimika kwenda kusoma Nangumbu, iliyoko umbali wa km. 10.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, Serikali imetoa sh. milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne ambayo yakikamilika walimu watapata ofisi pia.

Amesisitiza kwamba fedha hizo zitumike kujenga madarasa manne ambapo walimu pia watapata ofisi moja. 

Pia amemwambia diwani wa kata ya Chinongwe, Bibi Maki Camillius kwamba katika bajeti ya mwaka huu, kata hiyo itapatiwa sh. milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba nne za walimu katika shule ya sekondari ya kata ya Chinongwe.

Mapema, akisoma taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bw. Amiri Musa Kambona alisema madarasa mawili na ofisi moja ya walimu vilibomoka mwaka 2014 kutokana na mvua na upepo mkali na kusababisha upungufu wa madarsa na ofisi.

Akielezea changamoto nyingnea za  shule hiyo, Mwalimu Kambona alisema shule ina upungufu wa nyumba moja ya walimu, darasa moja, matundu mawili ya vyoo vya walimu, ofisi moja ya walimu na kukosekana kwa chanzo cha maji safi na salama kwa matumizi ya wanafunzi na walimu. 


(mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.