Na. OWM, KAGERA
Serikali kupitia uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu imezindua
zoezi la kupima utayari wa kukabili mlipuko
wa ugonjwa wa Ebola ili kupima utayari wa sekta na wadau mbalimbali,
ikiwemo jamii katika kukabili mlipuko wa
ugonjwa huo katika maeneo ya mipakani.
Akiongea
wakati wa kuzindua zoezi hilo la siku
tano jana, tarehe 30 Julai 2019, mjini
Bukoba, mkoani Kagera, Katibu Tawala wa
mkoa huo, Profesa Faustin Kamuzora aliwataka wananchi kuchukua tahadhari kwa
kujielimisha kuhusu ugonjwa wa Ebola na kusisitiza ni muhimu kuchukua tahadhari kwa kuwa hadi sasa hakuna
mgonjwa aliyegundulika kuwa na dalili za Ebola hapa nchini Tanzania.
“Tunapaswa
kufanya juhudi kubwa ili kama ambavyo hadi hivi sasa hakuna mgonjwa wa Ebola
nchini kwetu, basi tuendelee kuwa salama, kwa kuwa faida zake ni kubwa kuliko
kupambana na mlipuko,” alisema Prof. Kamuzora.
Aidha,
Profesa. Kamuzora aliongeza kuwa Uratibu wa sekta za Afya na sekta zingine katika kukabili na Ebola ni muhimu sana hususani kwenye kukabili na magonjwa ya mlipuko. Alifafanua
kuwa ugonjwa kama Ebola si suala la kiafya tu, ni suala la jamii na sekta zote
hivyo iwapo idara zote husika kama vile uhamiaji, afya, serikali za mitaa zikifanya
kazi zake vyema haitakuwa vigumu kuwagundua wenye dalili na kuchukua tahadhari
stahiki.
Awali akiongea wakati wa Uzinduzi wa zoezi hilo Mkurugenzi
Msaidizi (Utafiti na Mipango), Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri
Mkuu Bashiru Taratibu alisema juhudi zinapaswa kufanyika ili ugonjwa wa Ebola usiingie
nchini na kusababisha maafa ya ugonjwa wa mlipuko.
“Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya menejimenti ya maafa itaendelea
kufanya kadri inavyowezekana maafa ya ugonjwa wa mlipuko yasitokee, na ikishindikana
basi kupunguza athari zake. Ndio maana
malengo ya zoezi hili ni kupima utayari wa kukabili ugonjwa wa Ebola na
hatimaye tuweze kujenga utayari wetu,”
alisema, Taratibu.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa
zoezi hilo, Mratibu wa zoezi hilo kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faraja
Msemwa amefafanua kuwa watoa huduma za afya na sekta zingine watakuwa wakifanya
zoezi kwa namna ambavyo itakuwa iwapo mtu mwenye Ebola atapatikana mahali
fulani katika jamii.
“Watu watakaochukua nafasi ya ‘wagonjwa’’ wakati wa zoezi hili si
wagonjwa halisi wa Ebola, lakini shughuli zote zitakazofanyika wakati wa zoezi
la utayari zitaakisi mazingira halisi toka nchi ambazo zimewahi kukabiliwa na
mlipuko wa ugonjwa wa Ebola” alisisitiza Dkt. Msemwa.
Dkt.
Msemwa aliongeza kuwa pamoja na kuwa zoezi hilo kuwa litafanyika kwa mkoa wa Kagera na Kigoma, Aidha,
mikoa mingine ambayo Ipo hatarini kwa
mlipuko wa ugonjwa wa Ebola ni pamoja na Mbeya, Songwe, Katavi, Rukwa, Dar es
salaam, Mwanza na Dodoma.
Aidha, Dkt. Msemwa ali tishio la ugonjwa wa Ebola nchini Tanzania
linatokana na mlipuko wa ugonjwa huo kwenye jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC) tangu Agosti mwaka jana. Kwa
kuzingatia Mkoa wa Kagera unapaka na nchi ya Rwanda na Uganda
Kwa mujibu wa taarifa toka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto zinaeleleza kuwa tishio la ugonjwa wa Ebola nchini Tanzania
linatokana na mlipuko wa ugonjwa huo kwenye jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC) tangu Agosti mwaka jana ambapo hadi
kufikia Julai 23 mwaka huu jumla ya
wananchi wa DRC, 2612 walidhihirika kuambukizwa ugonjwa wa Ebola na kulikuwapo na vifo 1,756.
Zoezi hilo linaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ushirikiano na wadau wa
maendeleo. Mazoezi hayo yatafanyika kati
ya tarehe 30 Julai na tarehe 8 Agosti mwaka 2019 katika vituo vya kutolea
huduma za afya na maeneo ya mipaka mkoani Kagera na Kigoma.
MWISHO
Baadhi ya wawezeshaji wa zoezi la kupima utayari wa kukabili Ugonjwa wa Ebola mkoani Kagera, wakijadiliana namna ya kuendesha zoezi hilo ,tarehe 31 Julai, 2019. |
Baadhi ya wawezeshaji wa zoezi la kupima utayari wa kukabili Ugonjwa wa Ebola mkoani Kagera, wakijadiliana namna ya kuendesha zoezi hilo ,tarehe 31 Julai, 2019. |
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.