Tuesday, July 9, 2019

SERIKALI YAKARIBISHA WAWEKEZAJI WA VIWANDA VYA NGOZI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara mbalimbali kutoka Misri ikiwemo kampuni ya Cairo for Investment and Development inayoshughulika na usimamizi wa kiwanda cha ngozi waje kuwekeza nchini Tanzania.

Ametoa kauli hiyo jana (Jumanne, Julai 9, 2019) alipotembelea kiwanda kikubwa cha ngozi cha Robbiki kilichoko katika mkoa wa Sharkianchini Misri, ambapo alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji hao waje wawekeze nchini kwani kuna malighafi za kutosha.

Waziri Mkuu ambaje jana alikuwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi nchini Misri alisema Tanzania inamifugo mingi hivyo inahitaji wawekezaji watakaojenga viwanda vya kuchakata bidhaa mbalimbali zitokanazo na mifugo hiyo ikiwemo ngozi.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imeboresha mazingira ya biashara na ya uwekezaji pamoja na kusimamia uwajibikaji kwa watumishi wa umma, hivyo Tanzania ni mahali bora na salama kwa wawekezaji na wafanyabiashara.

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Kampuni ya Cairo for Investment and Development ya nchini Misri, ambayo inasimamia kiwanda cha ngozi cha Robbiki, Yasser Mohamed Ahmed Al Maghraby alisema kiwanda hicho kinauhitaji mkubwa wa ngozi kutoka Tanzania.

Awali, Waziri Mkuu alitembelea mradi mkubwa wa mabwawa ya kufugia samaki, mradi wa upanuzi wa awamu ya pili ya mfereji wa suez canal, ambapo aliipongeza Serikali ya Misri kwa ujenzi wa mradi huo mkubwa kwa kutumia fedha za ndani (Dola bilioni 8.2).

(mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.