Na.
OWM, DAR ES SALAAM.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista
Mhagama (Mb), ameeleza kuwa serikali inatambua juhudi za taasisi za dini hapa
nchini ikiwa ni pamoja na kudumisha amani na utulivu, hivyo itaendelea
kushirikiana na taasisi hizo katika kuunga juhudi za serkali za kujenga amani,
umoja, upendo na mshikamano na
hatimaye kuleta ustawi wa Taifa.
“Napenda kuwahakikishia
ushirikiano wa serikali katika kutekeleza majukumu yenu ya kiroho na ya huduma
za kiuchumi na kijamii kwa maendeleo ya watanzania. Pale mtakapoona mchango wa
serikali unahitajika msisite kuwasiliana nasi. Na iwapo mtaona kuna upungufu
wowote semeni kwa viongozi wa wilaya, mkoa na wa kitaifa. Sisi ni wasikivu.
Tuite tutawaitikia, tutatenda kwa lile ambalo lipo ndani ya uwezo wetu”
amesisitiza Mhe. Mhagama.
Akiongea kwa niaba ya Mheshimiwa
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,
katika Kongamano la maombi ya wanawake waombolezao, jijini Dar es salaam,
tarehe 25 Julai, 2019, Mhe. Waziri Mhagama amefafanua kuwa waratibu wa
Kongamano hilo wanapongezwa na viongozi wote serikalini, akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, kwakuwa linachagiza maendeleo katika Taifa
hili na ustawi wa watu wake.
“Viongozi wetu kwa pamoja ni
shupavu, wanaoaminiwa na kutumainiwa na wananchi hasa wanyonge. Viongozi
wanachukia na kupinga rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma kwa vitendo
na Rais anayejipambanua kwa kufanya maamuzi magumu ya kulinda rasilimali za
Taifa. Lakini haya yote yamewezekana kwa kuwa wamejikabidhi katika mikono ya
Mungu na nyie mmekuwa mkiwaombea” amesema Mhe. Mhagama.
Katika hatua nyingine, Mhe.
Mhagama amewataka Wanawawake waombolezao waendelee kumuombea Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ambazo anaendelea
kuzifanya tangu aliposhika hatamu ya uongozi, kwa kuthubutu kutenda na kuiletea nchi mafanikio makubwa.
“Kwa uchache kazi kubwa ambazo
amezitekeleza Mhe. Rais, ni pamoja na kutoa elimu ya msingi bila malipo ambapo
ameweza kuwagusa hata walewasiojiweza, kuongeza bajeti ya dawa, vifaa tiba na
vitendanishi na kujenga Hospitali na Vituo vya Afya vingi ili watanzania wengi wapate huduma za Afya
kwa karibu. Pia umeme kwa sasa umesambazwa vijijini kupitia mradi wa REA na
sasa mradi mkubwa wa uzalishaji umeme wa Maji (Rufiji) umeanzishwa” amesisitiza
Mhagama.
Awali
wakiongea katika Kongamano hilo,
waratibu wa Kongamano hilo, Mchungaji Deborah Malassy na Askofu Dkt. Godfrey
Malassy wamebainisha kuwa wameamua kuendesha Kongamano hilo kwa kuwa wanatambua
kuwa viongozi wa dini kama walivyo wa serikali wanao wajibu maalamu wa kulilea Taifa. Aidha wameongeza
kuwa ushirikiano ukiwa imara watafanikiwa kuendeleza amani, umoja na mshikamano
uliopo hapa nchini.
“Tutaendelea
kutekeleza wajibu pekee wa kujenga uhai wa Taifa letu na watu wake.
Tunampongeza Mhe.Rais wetu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa uongozi wake bora
uliokidhi kiu na kilio cha watanzania kwani tumeona jitihada anazofanya
pamoja na kutiwa moyo na kazi zake
anazozifanya na viongozi wote wa
serikali ya awamu ya tano. Kwa hamasa hii tunapata nguvu ya kuendelea na wajibu
huu mkubwa tuliopewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kuliombea Taifa letu”
amesema, Mchungaji Deborah.
Kongamano
hilo la kumi la Kihistoria hapa nchini liliohusisha Wanawake Waombolezao
Kitaifa kutoka mikoa yote Tanzania na Zanzibar, pamoja na viongozi wa Taasisi
mbalimbali, limebebwa na maudhui ya Mwaka
wa Maachilio kwa Wanawake wote. Kongamano hilo ni sehemu ya Maombi ya kila
mwisho wa mwaka wa tarehe 31 Disemba ya kuliombea Taifa hili yajulikanayo kama
MKESHA MKUBWA KITAIFA DUA MAALUM, ambayo yamekuwa yakifanyika katika viwanja
vya wazi katika mikoa mbalimbali ikiwemo Zanzibar kwa takribani kwa miaka 22
sasa.
MWISHO.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.