Friday, September 15, 2017

WAZIRI MKUU AWAASA WATENDAJI WA TAASISI ZINAZOSIMAMIA MAZAO YA BIASHARA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa taasisi zilizopewa dhamana ya kusimamia mazao makuu matano ya biashara ambayo ni ya pamba, tumbaku, korosho, chai na kahawa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Amesema mazao hayo ni muhimu sana katika kuwezesha mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kufikia uchumi wa viwanda kwani ndiyo mhimili wa kutoa malighafi za kuendesha viwanda husika na yana mnyororo mpana wa uzalishaji ambao una fursa ya kutoa ajira nyingi.   

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Septemba 15, 2017) Bungeni mjini Dodoma alipowasilisha hotuba yake ya kuahirisha Mkutano wa Nane wa Bunge. Amesema Serikali imejipanga kuimarisha usimamizi katika uzalishaji na uuzaji wa mazao hayo.

Amesema Serikali itahakikisha kuwa kila taasisi iliyopewa dhamana ya kusimamia mazao hayo, inatekeleza majukumu yake ipasavyo sambamba na kuhakikisha kwamba Watendaji wake wanafanya kazi hiyo kwa uadilifu na ufanisi mkubwa.

Amesema jitihada hizo zinalenga kuwawezesha wakulima wengi hususan wa vijijini ambao ni takriban asilimia 75 ya Watanzania wote, kulima kilimo cha kisasa, chenye tija na cha kibiashara, hivyo kuondokana na umaskini wa kipato. 

“Vilevile, kuwawezesha wakulima kupata mbinu za kisasa za kuyafikia masoko ya uhakika ya mazao yao ili kupata bei nzuri ambayo itawakwamua kiuchumi. Mazao mengine ya kibiashara yatakayotiliwa mkazo ni katani, ufuta, alizeti, mbaazi na ngano.” 

Amesema kwa kipindi kirefu uzalishaji wa mazao hayo ulishuka kulitokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya baadhi ya viongozi wa vyama vya Ushirika kushindwa kutekeleza vyema wajibu wao, wizi, dhuluma kwa wakulima na pia ushiriki mdogo wa Maofisa Kilimo katika kusimamia kilimo cha kitaalam.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema jumla ya vijana 1,000,000 wamelengwa kupata urasimishaji  ujuzi kati ya mwaka 2017 na 2021 kupitia Mpango wa Kutathmini na Kurasimisha Ujuzi uliopatikana nje ya Mfumo Rasmi wa Mafunzo.

Amesea Serikali imeamua kuchukua hatua hiyo ili kuwawezesha vijana ambao ndiyo nguvu kazi wachangie kikamilifu katika kujenga uchumi wa Taifa. “Hadi sasa tayari vijana wengi wanaendelea kunufaika na mpango huu kutoka mikoa mbalimbali.”

Miongoni mwa faida za mpango huo ni pamoja na kuwasaidia mafundi waliojifunza kupitia sehemu za kazi kupata kazi zenye staha na kuwajengea uwezo wa kushiriki na kushindana kikamilifu katika soko la ajira. Pia kuinua tija mahali pa kazi na kusaidia waajiri/wenye makampuni kukidhi viwango katika eneo la rasilimali watu. 
Waziri Mkuu amesema mpango huu unafadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali na unatekelezwa kwa pamoja na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi ( VETA)
Read More

Thursday, September 14, 2017

AFRIKA IANDAE RASILIMALI WATU KUSIMAMIA SEKTA YA MADINI-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mataifa ya Afrika yanatakiwa yaandae maarifa, vitendea kazi na rasilimali watu watakaoweza kusimamia na kuendeleza ipasavyo sekta ya madini na kuleta tija kwa Taifa husika na wananchi kwa ujumla.

Amesema taarifa za kijiolojia zinaonesha kuwa Afrika ni Bara lenye utajiri mkubwa wa rasilimali madini huku sehemu kubwa ya madini hayo yakiwa bado hayajaanza au yako kwenye hatua mbalimbali za uendelezaji.

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Septemba 14, 2017) alipofungua mkutano wa 37 wa Baraza la Uongozi wa Kituo cha Madini na Jiosayansi cha Afrika (AMGC) uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kituo hicho mkoani Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema rasilimali za madini ilizopo Barani Afrika inaweza kuwa ni chanzo kikubwa cha kusukuma maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi nyingi iwapo itasimamiwa vizuri. 

Ametolea mfano Tanzania ambayo licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa madini ya dhahabu, almasi, chuma, madini ya vito kama tanzanite lakini mchango wa sekta ya madini ni asilimia 4.8 ya pato ghafi la Taifa.

“Changamoto kuu kwa sasa ni kwa jinsi gani tunaweza kuwa na sekta ya madini inayotoa mchango stahiki katika nchi husika pamoja na kusimamia sekta hii kwa kuwafanya wananchi wetu hususan katika maeneo yenye rasilimali wakanufaika na kuona fahari badala ya kuacha mashimo, umasikini na mateso kwa wananchi.”

Amesema lengo la kuanzishwa kwa kituo hicho ambacho leo kimetimiza miaka 40 ni kuhakikisha sekta ya madini inawajibika kuleta maendeleo ya kijamii na uchumi pia ikijali masuala ya mazingira, hivyo ni vema kikatumika kama ilivyokusudiwa.

Waziri Mkuu amesema kituo hicho kikitumika vema kwa mujibu wa kusudia la uanzishwaji wake kinaweza kuleta tija kubwa kwenye sekta ya uchumbaji wa madini, uongezaji wa thamani na usimamizi wa sekta.

Amesema kituo hicho ni moja kati ya taasisi chache duniani yenye teknolojia za kisasa ambazo zinaweza kusaidia kufanya uchambuzi wa miamba na madini yaliyimo. “Pia ni sehemu ambayo unaweza kupata huduma za ushauri na kusaidia teknolojia utakayoweza kutumia ili kufanya uzalishaji wa madini mbalimbali.”

Hivyo amewakumbusha wajumbe na wanachama wa AMGC kuwa kituo hicho hawajakitumia ipasavyo ni vema kikatumika ili kupata tija kwenye uendelezaji na usimamizi wa madini, ambapo ameiagiza Bodi iandae mpango utakaoziwezesha nchi wasnachama kukitumia.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani amesema kwa sasa kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ya kwanza ni kwa wanachama kutolipa ada kwa wakati.

Dkt. Kalemani ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Kituo cha AMGC amesema changamoto ya pili ni wanachama wa kituo hicho kutokitafutia wateja na masoko. Pia miundombinu mingi ya kutuo ni chakavu.

Akizungumzia changamoto hizo Waziri Mkuu ameziagiza nchi zote zinazodaiwa ada ikiwemo Tanzania zilipe ada stahiki kwa wakati na kuweka mkakati wa kukitangaza kituo hicho ili kukiwezesha kupata wateja kwa ajili ya kutumia huduma zitolewazo.

Read More

Wednesday, September 13, 2017

MATUKIO BUNGENI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akimsikiliza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa mkutano wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma.
Naibu waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Mhe. Antony Mavunde akisalimiana na baadhi ya walimu wa Shule ya Sekondari ya Jamhuri walipotembelea Bungeni Septemba, 2017 Mjini Dodoma.


Naibu waziri Ofisi ya Waziri Mkuu(Kazi, Ajira na Vijana), Mhe. Antony Mavunde (wa tatu kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya walimu wa Shule ya Sekondari ya Jamhuri waliotembelea  Bungeni Septemba, 2017 Mjini Dodoma.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Mhe. Antony Mavunde akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Jamhuri waliotembelea  Bungeni  tarehe 13 Septemba, 2017 Mjini Dodoma.

Read More

MHAGAMA AKUTANA NA UONGOZI WA VYAMA VYA WATU WENYE ULEMAVU.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (wa pili kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu walipomtembelea Ofisini kwake Bungeni Dodoma 13 Septemba, 2017.

Read More

TANZANIA IPO SALAMA NA IMARA -MAJALIWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na Balozi wa Iran. Mousa Farhang nakufanya  mazungumzo ya kikazi leo Septemba 13/2017.Ofisini kwake Magogoni Dar es salaam.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiongea  na Balozi wa Iran. Mousa Farhang  leo Septemba 13/2017.Ofisini kwake Magogoni Dar es salaam.

Read More

TANZANIA IPO SALAMA NA IMARA -MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania ipo salama na imara na kwamba mtu yeyote atakayejaribu kutaka kuvuruga amani atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Septemba 13, 2017) alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Iran nchini Tanzania, Bw. Mousa Farhang jijini Dar es Salaam.

“Hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote kutoka popote atakayejaribu kuvuruga amani yetu. Nawaomba wananchi muwe makini na muendelee kuidumisha amani yetu.”

Amesema kwa sasa Serikali ipo katika mapambano dhidi ya vitendo vya ufisadi, rushwa, biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja na wahujumu uchumi.

Waziri Mkuu amesema licha ya Tanzania kuwa ni nchi ya amani na yenye utulivu wa kisiasa, wameendelea kuwahamasisha wananchi wake kudumisha mshikamano.

Amesema mbali ya kuimarisha amani nchini, pia Serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji jambo ambalo litawawezesha watakaokuja kuwekeza nchini kupata tija.

Hivyo ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini Iran ili waje kuwekeza kwenye viwanda mbalimbali vikiwemo  vya kuchakata mazao ya  kilimo.

Pia amewakaribisha raia wa Iran kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyoko nchini Tanzania kama mlima wa Kilimanjaro, fukwe, mali kale na mbuga za wanyama.

Kwa upande wake, Balozi Farhang  ameipongeza Serikali kwa kuwa na dhamira ya dhati ya kuimarisha uchumi na kupambana na dawa za kulevya na ufisadi.

Balozi huyo amesema Serikali ya Irani ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi pamoja na vitendo vingine vya kihalifu.

Balozi Farhang ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali ya Tanzania ifungue Ofisi ya Ubalozi nchini Iran ili kuimarisha uhusiano huo, ambapo Waziri Mkuu amekubali.

Pia Bw. Farhang amesema aliwahi kutembelea mbuga za wanyama za Serengeti na Ngorongoro na kusema kwamba ni maeneo mazuri ambayo hajawahi kuyaona tangu azaliwe.

Read More

Tuesday, September 12, 2017

WAZIRI MKUU AKUTANA NA MKURUGENZI WA KAMPUNI YA NAMERA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (R)amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Namera Group of Industries Bw. Hamza Rafiq Pardesi (c) ambaye ameahidi kununua pamba yote itakayozalishwa nchini kuanzia msimu ujao.(L) Ni Meneja wa Namera Bwana Muhammad Waseem. Waziri Mkuu amekutana nao leo Septemba 12/ 2017 Ofisini kwake Dar es salaam

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Namera Group of Industries Bw. Hamza Rafiq Pardesi (L)ameahidi kununua pamba yote itakayozalishwa nchini kuanzia msimu ujao. Waziri Mkuu amekutana naye leo Septemba 12/ 2017 Ofisini kwake Dar es salaam.

Read More

WAZIRI MKUU AKUTANA NA MKURUGENZI WA KAMPUNI YA NAMERA



*Aahidi kununua pamba yote itakayozalishwa nchini

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Namera Group of Industries Bw. Hamza Rafiq Pardesi ambaye ameahidi kununua pamba yote itakayozalishwa nchini kuanzia msimu ujao.

Amekutana na Bw. Pardesi leo (Jumanne, Septemba 12, 2017)  kwenye makazi ya Waziri Mkuu Oysterbay jijini Dar es Salaam na amesema kwamba tayari Serikali imeanza kuwahamasiha wakulima kuongeza uzalishaji kwa kuwa kuna soko la uhakika.

Waziri Mkuu amempongeza Bw. Pardesi kwa kuiunga mkono Serikali katika mpango wake wa kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda. Kampuni ya Namera Group of Industries inamiliki kiwanda cha nguo cha NIDA na cha Namera vya jijini Dar es Salaam.Kampuni inatarajia kufungua kiwanda kingine cha nguo wilayani Kahama.

Pia Waziri Mkuu amesema katika kuhakikisha zao la pamba linapewa kipaumbe alikutana na wakuu wa mikoa yote inayolima pamba Ijumaa, Septemba 8, 2017 na aliwaagiza wasimamie zao hilo kwa karibu ili kuinua uzalishaji wake na kuwaongezea kipato wananchi hususan wakulima wa zao la pamba.

Amesema Serikali imeamua kufufua mazao makuu matano ya biashara ambayo ni pamba, chai, kahawa, korosho na tumbaku ili kuwawezesha wakulima kupata tija na kuondokana na umasikini wa kipato, hivyo kukuza uchumi wa Taifa.
Waziri Mkuu amesema Serikali imeamua kusimamia kilimo cha pamba kuanzia maandalizi ya shamba, kupanda, matumizi ya pembejeo na dawa, kuvuna na kutafuta masoko, hivyo ahadi yao ya kununua pamba yote ni faraja kwa wakulima.
“Nimefurahishwa na uamuzi wenu wa kutaka kununua pamba yote itakayozalishwa nchini kuanzia msimu ujao kwani kwetu sisi ni faraja kwa sababu wakulima walipunguza uzalishaji baada ya kukosa soko la uhakika.”
Kwa upande wake Bw. Pardesi amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba kampuni yao inauwezo wa kununua pamba yote inayozalishwa nchini na kuichakata katika viwanda vyao na kutengeneza nguo zitakazouzwa nchini kwa bei nafuu.
Amesema kwa sasa wameajiri mafundi katika viwanda vyao ambao watakuwa wa nashona nguo na kuziuza nchini kwa gharama nafuu ili kuwawezesha wananchi wa hali ya chini kumudu kununua na kuondokana matumizi ya nguo za mitumba.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu sisi Namera tuko tayari kununua pamba yote inayozalishwa nchini kwani viwanda vyetu vinafanya kazi ya kuchambua pamba, kutengeneza nyuzi na majora kisha tunashona nguo na kuziuza. Hapa Kazi Tu maana bila ya kufanya kazi huwezi kuheshimika.”
Hata hivyo Mkurugenzi huyo amesema kitendo cha kununua pamba inayolimwa nchini na kuchakata katika viwanda vyao kwa lengo la kutengeneza nguo za aina mbalimbali wataiwezesha Serikali kuokoa fedha nyingi za kigeni zilizokuwa zinatumika kuagiza nguo nje ya nchi.
Read More

Wednesday, September 6, 2017

WAZIRI MKUU APOKEA RIPOTI ZA UCHUNGUZI WA BIASHARA YA ALMASI NA TANZANITE

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea ripoti mbili za kamati ya Maalumu ya Bunge ya kuchunguza biashara ya madini ya almasi na tanzanite na kuahidi kuiwasilisha kwa Rais Dkt. John Magufuli kesho asubuhi.

Pia amesema Serikali haina mchezo katika usimamizi wa rasilimali za Taifa, hivyo amewataka viongozi  na watendaji wote waliokabidhiwa dhamana ya kusimamia sekta ya madini hakikisha wanatimiza vyema wajibu wao.

Waziri Mkuu amepokea ripoti hizo leo (Jumatano, Septemba 6, 2017) kutoka kwa Spika wa Bunge, Bw. Job Ndugai ambaye alikabidhiwa ripoti hizo  na Wenyeviti wa kamati Bw. Mussa Zungu (Almasi) na Bw. Dotto Biteko (Tanzanite).

“Kesho saa 4.30 asubihi nitaziwasilisha ripoti hizi kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli. Hakuna ucheleweshaji katika jambo hili na Mheshimiwa Spika (Job Ndugai) kesho twende tukakabidhi wote.”

Waziri Mkuu amesema kamati hizo zimefanya kazi nzuri na kwamba Serikali inaimani  na ripoti hizo na ushauri uliotolewa utawezesha Taifa kunufaika na rasilimali zake, hivyo mapendekezo na hoja zote zilizoibuliwa zitafanyiwa kazi katika kipindi kifupi.

Amesema taarifa hiyo zimewasilishwa katika kipindi muafaka na zimeonyesha  dhamira ya dhati ya Bunge, kuunga  mkono juhudi za Rais Dkt. Magufuli  na Serikali yote kwa ujumla katika kulinda rasilimali za Taifa.

“Watanzania ni mashahidi kwamba Mwenyezi Mungu ameijalia Tanzania utajiri wa rasilimali za kila aina.  Tunayo ardhi yenye rutuba, madini ya aina mbalimbali na mengine hayapatikani katika nchi nyingine isipokuwa Tanzania tu kama vile Tanzanite.”

Amesema ni  lazima rasilimali hizo zisimamiwe na kutunzwa vizuri ili ziwezeshe kuboresha hali na maisha ya Watanzania wote na kila mwananchi ana jukumu la kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuleta mageuzi katika Sekta ya madini nchini.

Waziri Mkuu amesema suala la kusimamia rasirimali za nchi ni la Watanzania wote kama ilivyoainishwa kwenye ibara ya 27 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo aliinukuu Ibara hiyo kama ifuatavyo:

“27 (1) kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na Wananchi na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine.

“(2) Watu wote watatakiwa na Sheria kutunza vizuri mali ya Mamlaka ya nchi na pamoja vita aina zote za uharibifu na ubadhilifu na kuendesha uchumi wa Taifa na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao.”

Kamati hizo zilipewa jukumu la kutathmini mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya Tanzanite na Almasi Nchini, ambazo zimeishauri Serikali kuhusiana na mfumo bora wa uendeshaji na udhibiti wa biashara ya Tanzanite na Almasi  nchini.  
Read More

MAJALIWA AKABIDHIWA NA SPIKA WA BUNGE TAARIFA TA KAMATI YA KUCHUNGUZA BIASHARA YA TANZANITE NA ALMASI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea kutoka kwa Spika wa  Bunge, Job Ndugai Taarifa ya Kamati Maalum ya Bunge ya Kuchunguza Biashara ya Tanzanite na Almasi kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Septemba 6, 2017.  Katikati ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati Maalum iliyoundwa na Spika wa Bunge Job Ndugai kuchunguza Biashara ya Tanzaniate wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza  baada ya kukabidhiwa na Spika wa Bunge Job Nduga  Taarifa hiyo kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Septemba 6, 2017.

Baadhi ya Wabunge walioshiriki katika hafla ya kupokea Taarifa ya Kamati Maalum ya Bunge ya Kuichunguza Biashara ya Tanzanite na Almasi kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Septemba 6, 2017.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Spika wa Buge, Job Ndugai baada ya kukabidhiwa na Spika Taarifa ya Kamati Maalum ya Bunge ya Kuichunguza Biashara ya Tanzanite na Almasi kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Septemba 6, 2017.

Spika wa Buge Job Ndugai akizungumza baada ya kupokea Taarifa ya Kamati Maalum ya Bunge ya Kuchunguza Biashara ya Tanzanite na Almasi kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Septemba 6, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea kutoka kwa Spika wa  Bunge, Job Ndugai Taarifa ya Kamati Maalum ya Bunge ya Kuchunguza Biashara ya Tanzanite na Almasi kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Septemba 6, 2017.  Katikati ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza baada ya  kupokea Taarifa ya Kamati Maalum ya Bunge ya Kuchunguza Biashara ya Tanzanite na Almasi kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Septemba 6, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza baada ya  kupokea Taarifa ya Kamati Maalum ya Bunge ya Kuchunguza Biashara ya Tanzanite na Almasi kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Septemba 6, 2017.
 Waziri Mkuu, Kassim  Majaliwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai (kushoto kwake) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati  Maalum iliyoundwa na Spika ya  Kuchunguza Biashara ya Tanzanite baada ya Spika kupokea Tarifa hiyo na kumkabidhi Waziri Mkuu kwenye Viwanja vya Bunge mjini Dodoma Septemba 6, 2017. Aliyekaa kushoto ni Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson na aliyeka kulia ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Job Ndugai.

Waziri Mkuu, Kassim  Majaliwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai (kushoto kwake) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati  Malum iliyoundwa na Spika   Kuchunguza biashara ya  Almasi baada ya Spika kupokea Taarifa hiyo na kumkabidhi Waziri Mkuu kwenye Viwanja vya Bunge mjini Dodoma Septembea 6, 2017. Aliyekaa kushoto ni Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson na aliyeka kulia ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Job Ndugai.

Read More

MAJALIWA AZINDUA MPANGO MKAKATI JUMUISHI WA KITAIFA WA LISHE

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi walioshiriki katia Uzinduzi wa Mpango Mkakati Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe uliofanywa na Waziri Mkuu,  kwenye ukumbi wa Hazina mjini Dodoma Septemba 6, 2017.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza kabla ya kuzindua  Mpango Mkakati Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe kwenye ukumbi wa Hazina mjini Dodoma Septemba 6, 2017.

Baadhi ya Washiriki wa Uzinduzi wa Mpango Mkakati Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozindua Mpango huo kwenye ukumbi wa Hazina mjini Dodoma Septemba 6, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akimkabidhi Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Phillip Mpango  nakala ya Mpango Mkakati Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe  baada ya Waziri Mkuu kuuzindua kwenye ukumbi wa hazina mjini Dodoma Septemba  6, 2017.  Kulia kwake ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu  na kushoto  ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Anthony Mavunde. Watatu kulia ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Selemani Jaffo, wapili kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa UNICEF nchini, Minaz Zaman na kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa USAID nchini, Andy Karas.



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Mkurugenzi Mkazi wa UNICEF nchini nakala ya Mpango Mkakati Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe baada ya kuzindua Mpango huo kwenye ukumbi wa Hazina Mjini Dodoma Septemba 6, 2017. Kulia ni Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango na kushoto ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Phillip Mpango(kushoto kwake) na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (kulia kwake) wakionyesha vitabu vya Mpango Mkakati Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe baada ya Waziri Mkuu kuuzindua kwenye ukumbi wa hazina mjini Dodoma Septemba 6, 2017. Kushoto ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Anthony Mavunde, watatu kulia ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Selemani Jaffo, wapili kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa UNICEF nchini, Minaz Zaman na kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa USAID nchini, Andy Karas.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi walioshiriki katia Uzinduzi wa Mpango Mkakati Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe uliofanywa na Waziri Mkuu,  kwenye ukumbi wa Hazina mjini Dodoma Septemba 6, 2017.

Read More

Tuesday, September 5, 2017

FANYENI TATHMINI YA ZAO LA KOROSHO – WAZIRI MKUU


*Apiga marufuku biashara ya kangomba, makato ya unyaufu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na Bodi ya Korosho Tanzania zifanye tathimini ya maandalizi ya msimu ujao kwa wakati na zimpatie taarifa mara moja.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana usiku (Jumanne, Septemba 5, 2017) wakati akizungumza na wadau wa zao la korosho kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake mjini Dodoma kujadili mwenendo wa zao la korosho na ununuzi wa pembejeo.

“Lipo tatizo la tathmini ya maandalizi ya msimu kutofanyika kwa wakati na kusababisha matatizo kutotatuliwa kwa wakati. Bodi na Wizara zitoe tathimini ya maandalizi ya msimu ujao kuhusu vyama vya ushirika vilivyojipanga, upatikanaji wa vifaa kama magunia na nyuzi, maghala, masoko, mizani, minada, malipo na mfumo wake,” alisema.

Waziri Mkuu pia alizitaka Wizara ya Kilimo pamoja na Bodi ya Korosho zitoe tathimini ya maandalizi ya msimu ujao katika maeneo ya mashamba, miche, pembejeo na viatilifu. 

Alisema tangu Serikali iamue kusimamia mazao makuu matano ya pamba, chai, kahawa, korosho na tumbaku hajapata muda wa kukaa na kuongea na wadau wote. “Serikali imeamua kufuatilia usimamizi wa mashamba; kusimamia upatikanaji wa mbegu, miche na pembejeo; kufuatilia uvunaji na mfumo wa masoko ya korosho na pia kufuatilia mfumo wa ushirika katika baadhi ya mazao,” alisema.

Alisema hivi sasa zao la korosho linalimwa katika wilaya 50 kwenye mikoa 11 ya Dodoma, Iringa, Lindi, Mbeya, Morogoro na Mtwara. Mingine ni Njombe, Pwani, Ruvuma, Singida na Tanga. 

“Katika msimu wa mwaka 2016/2017 zao la korosho lilikuwa ni moja kati ya mazao ya kibiashara yenye tija na faida nyingi kwa kuliingizia Taifa fedha za kigeni kiasi cha dola za Marekani milioni 346.6,” alisema na kuongeza kuwa katika msimu wa mwaka 2017/2018 watendaji hawana budi kujipanga vizuri ili zao la hilo liendelee kuliingizia Taifa dola nyingi zaidi kwa kuwa Serikali imetoa viatilifu bure.  

“Ninasisitiza eneo hili kwa sababu tumebaini kuwa korosho inachangia zaidi ya asilimia 50 ya mapato kwenye Halmashauri zinazolima kwa wingi zao hilo. Kwa kuwa zao hili ni la kimkakati, naitaka Wizara inipatie taarifa sahihi na kwa wakati,” alisisitiza.

Alisema Agosti mwaka huu, alipofanya ziara mkoani Tabora, alielezwa kwamba wilaya ya Uyui na Tabora Manispaa zimeanza kulima zao hili kama zao mbadala ili kuinua uchumi wa wananchi wake. “Tabora itakuwa mkoa wa 12, kwa hiyo Wizara ya Kilimo itembelee maeneo haya na kuona inawezaje kuwasaidia, ikaangalie uzalishaji ukoje kwani mti unaweza kukubali kuota pale Tabora lakini usizae kwa wingi kama ilivyo kwa mikoa mingine,” aliongeza.

“Viongozi wa juu Serikalini hadi kwa mtendaji wa kijiji ni lazima tusimamie zao la korosho, kila mtendaji ashirikiane na taasisi ambata, wizara mama iimarishe vyuo vya kilimo na utafiti. Kila mtendaji ni lazima ajue na wakulima wangapi, je kila mkulima ana ekari ngapi na kila ekari ina miche mingapi,” aliongeza.

Ili kurekebisha dosari zilizojitokeza katika msimu uliopita na kuboresha utendaji katika msimu ujao, Waziri Mkuu alisema Wizara na Bodi zinapaswa kufanya tathmini ya uhakika kwa kushirikiana na ofisi za mikoa. 

“Tumepata matatizo ya msimu kutoanza kwa wakati kwa sababu ya kukosekana kwa tathmini za nyuma, hatuna pa kuanzia kufanya marekebisho kwa sababu hatuna uzoefu wa yaliyojiri kwenye msimu uliotangulia. Siyo Bodi, Wizara wala Ofisi ya Mrajisi ambayo imekwishafanya tathmini. Kazi zote zimeacha kwa Wakuu wa Mikoa kupitia Sekretarieti za Mikoa.”

Akielezea kuhusu mwenendo wa biashara ya zao hilo, Waziri Mkuu alisema ili wakulima waweze kuwanufaika zaidi, Serikali imeendelea kuimarisha mfumo wa malipo wa stakabadhi ghalani na kupambana na watu wasio waaminifu wanaotumia kangomba. Kangomba ni kopo linalotumiwa na wanunuzi binafsi ambalo ujazo wake haufikii hata kilo moja, lakini wao wanalitumia kama kipimo cha kilo moja kununulia korosho kwa wakulima.

“Kuanzia sasa, biashara ya kangomba ni marufuku, kangomba ni wizi na yeyote atakayekamatwa, achukuliwe hatua za kisheria. Kila mkoa uweke mkakati makini wa kudhibiti biashara ya kangomba,” aliagiza.

“Hatutaki kusikia biashara ya kangomba. Viongozi wa Serikali msiwatumie vijana kwa kuwapa mitaji ili wafanye biashara hii. Mkizikamata korosho za kangomba, piga mnada na fedha ziende kwenye chama cha ushirika cha pale zilipokamatwa,” alisema.

Kuhusu makato ya unyaufu (shrinkage), Waziri Mkuu alisema kuanzia sasa, vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) na Chama Kikuu haviruhusiwi kutoza hela ya unyaufu kwa wakulima.

“Sheria ya unyaufu inasema utauza korosho kwa asilimia 0.5 ya bei halisi ya korosho iliyokaa kwa zaidi ya miezi sita. Sasa hapa kwetu msimu wa kuuza ni Oktoba hadi Desemba, unyaufu hapo unatoka wapi? Hili haliwahusu wakulima wetu kabisa,” alisema.

Alisema suala la unyaufu litawahusu wanunuzi ambao watakuwa wamenunua korosho na kuzihifadhi kwenye maghala kwa muda mrefu.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Nchi OR- TAMISEMI, Bw. George Simbachawene; Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage; Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha; Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dkt. Tito Haule; Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho, Mama Anna Abdallah; Warajis Wasaidizi wa Mikoa; Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho, Mkurugenzi wa Maghala na Mizani, Wajumbe wa Bodi ya Korosho, Wenyeviti wa Vyama Vikuu vya Ushirika na Vyama vya Msingi, na Mameneja wa Vyama Vikuu.
Read More

WAZIRI MKUU AONYA WATAKAOKWAMISHA SHUGHULI ZA SERIKALI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua mifumo miwili ya kielektroniki itakayosaidia kuandaa bajeti kwenye ngazi ya Serikali za Mitaa na ameonya kwamba mifumo hiyo isitumike kukwamisha shughuli au utaratibu wa kazi za Serikali .

Mifuyo iliyozinduliwa ni Kupanga Mipango, Kuandaa Bajeti na Kutolea taarifa za hatua za Utekelezaji wa Bajeti (Planning, Budgeting and Reporting System- PlanRep) pamoja na mfumo wa Kufanya Malipo na Kutoa Taarifa za fedha ambazo zimetumwa kwenye Vituo vya Kutoa Huduma (Facility Financial Accounting and Reporting System-FFARS).

Akizindua mifumo hiyo leo (Jumanne, Septemba 5, 2017) mjini Dodoma, Waziri Mkuu  amesema lengo la mifumo hiyo mipya ni kuongeza uwajibikaji na ufanisi na kamwe isiwe kikwazo katika utoaji wa huduma kwa jamii.
                              
“Napenda kutumia fursa hii kuwafahamisha Viongozi na Watendaji pamoja na Wananchi wote kwamba, lengo la matumizi ya mifumo ya TEHAMA ni kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi wa shughuli za Serikali na isitumike kukwamisha shughuli au utaratibu wa kazi za Serikali.”

Amesema ni muhimu mifumo hiyo itumike kwa ufasaha ili kuleta tija inayotarajiwa na kila muhusika kwa ahakikishe anailinda, anaitunza na kuitumia mifumo hiyo ili iweze kudumu na kuwa endelevu kwa manufaa ya Taifa.

Pia Waziri Mkuu amewataka viongozi wa mikoa na halmashauri na Vituo vya kutoa huduma za Elimu na Afya kutoa taarifa ya mapato na matumizi kwa mamlaka zinazohusika kwa wakati.
                    
Amesema ngazi zote za Mamlaka za Serikali za Mitaa zitoe taarifa za mapato na matumizi kwa Wananchi wanaowahudumia kupitia mikutano, mbao za matangazo, tovuti, vyombo vya habari na njia nyinginezo.

Waziri Mkuu amesema kwa sasa Serikali haitarajii kuona kituo chochote cha kutoa huduma za Elimu na Afya kilichopo chini ya Halmashauri kinakuwa na matumizi yasiyozingatia taratibu na kanuni za fedha za umma.

“Hatutarajii kuona viongozi wa mikoa na halmashauri wakibadilisha matumizi ya fedha bila kuwasiliana na Mamlaka husika. Matumizi ya fedha yafanyike kutegemea chanzo cha fedha kilichopokelewa kwa wakati na kwa mujibu wa bajeti iliyotengwa kwa mwaka husika.”

Amesema mifumo hiyo imeshirikisha Wizara za Kisekta na Taasisi za Serikali      ikiwemo Wakala wa Serikali Mtandao (e-Government Agency-eGA) kuanzia hatua za awali za ukusanyaji wa mahitaji hadi utengenezaji wa mifumo na ndiyo itakayotumika katika Halmashauri na Vituo vya kutolea Huduma za Jamii.

Waziri Mkuu amesema iwapo kuna mdau anataka kushirikiana na Serikali anapaswa kutumia na kuboresha mifumo hiyo na siyo kuleta mifumo mingine kwa sababu uwingi wa mifumo huondoa ufanisi na uwajibikaji.

“Serikali ina matarajio makubwa na mifumo hii, na nitapenda Ofisi ya Rais - TAMISEMI na Ofisi yangu zipate taarifa zote za mipango, bajeti pamoja na taarifa za fedha zinazopelekwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa wakati na zikiwa katika ubora wa hali ya juu.”

Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Marekani Nchini Tanzania Bi. Inmi Patterson amesema mifumo hiyo iliyozinduliwa leo itaisaidia Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na uboreshaji wa huduma za jamii.

Amesema Serikali ya Marekani inaungana na Serikali ya Tanzania katika vita dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi kwa sababu vinakwamisha utoaji wa huduma mbalimbali za maendeleo kwa jamii.

“Ufisadi ni ugonjwa hatari na unaua kama magonjwa mengine yanavyoua. Ufisadi unazuia maendeleo ya jamii katika nchi husika pamoja na kukwamisha ukuaji wa uchumi na pia unaua ushindani na ndoto za vijana.”

Amesema anatambua namna ambavyo Rais Dkt. John Magufuli na wasaidizi wake wanavyopambana na vitendo vya rushwa na ufisadi ili kuhakikisha fedha zote za maendeleo zinazotolewa zinatumika vizuri.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi Bw. George Simbachawene amesema mifumo hiyo itaziwezesha Halmashauri kupunguza gharama kubwa katika kukamilisha zoezi zima la uandaaji wa Mipango na Bajeti kwani zilikuwa zikitumia muda mrefu na gharama kubwa kwenye kuandaa na kuwasilisha Bajeti.

Hesabu za mwaka 2017/2018 zilizotolewa zinaonyesha kuwa gharama za mchakato wa maandalizi ya Mipango ya Bajeti ya mwaka kwa Halmashauri 185 ni takriban sh. Bilioni 8.32 za kulipia usafiri (Mafuta), posho ya kujikimu, shajala na gharama za kudurufu Vitabu.

Read More