Wednesday, September 30, 2026

DKT. YONAZI ATEMBELEA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI UTURUKI

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Dkt. Jim Yonazi ameupongeza Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uturuki kwa kuendelea kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizo mbili katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya kidiplomasia, biashara, uwekezaji, na maendeleo ya kijamii.

Dkt. Yonazi ametoa pongezi hizo alipotembelea Ofisi za Ubalozi huo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mjini Ankara, Uturuki iliyolenga kuimarisha uwezo wa kitaasisi, kuongeza maarifa ya kiufundi na kukuza ushirikiano katika kupunguza vihatarishi vya maafa, kukabiliana na dharura na mifumo ya kurejesha hali kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kiteknolojia.

Dkt. Yonazi amesema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki unazidi kuimarika kwa kasi kubwa, ukiongozwa na diplomasia ya kiuchumi, miongozo ya kimkakati kama vile Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 ya Tanzania, pamoja na ziara za kitaifa za viongozi wakuu wa nchi hizo mbili.

Naye Kaimu Balozi Bi. Levina Maleo ambaye ni Mkuu wa Utawala wa ubalozi amempongeza na kumshukuru katibu Mkuu huyo kwa kutembelea ofisi za Ubalozi na kueleza kuwa wataendeleza mashirikiano yaliyopo kati ya nchi hizo mbili na kuendelea kutangaza fursa mbalimbali zilizopo nchini hasa za elimu, afya na kijamii.

Read More

Monday, September 28, 2026

SERIKALI YAFANYA KIKAO KAZI CHA KUKABILIANA NA MVUA ZA EL NINO -ZIARA KUFANYIKA NCHI NZIMA KUKAGUA UTAYARI WA KUKABILIANA NA ATHARI ZA MVUA HIZO


Serikali imeanza maandalizi ya kina ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua zinazotarajiwa kunyesha za EL Nino katika msimu wa Oktoba 2026, kwa kuendesha kikao kazi pamoja na ziara za ufuatiliaji katika mikoa yote nchini  nzima ili kutathmini utayari wa mamlaka za mikoa na wilaya.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha mifumo ya usimamizi na uratibu wa maafa inaendelea kufanya kazi kwa ufanisi, pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata taarifa na elimu sahihi kuhusu tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa kabla, wakati na baada ya mvua hizo.

Katika ziara hizo, Serikali itafuatilia utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa kwa Kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi za mikoa na wilaya, huku viongozi wa maeneo husika wakitakiwa kuimarisha maandalizi na mifumo ya mwitikio wa haraka endapo kutatokea mafuriko, uharibifu wa miundombinu au majanga mengine yanayohusiana na mvua.

 MIUNDOMBINU NA BARABARA

Miongoni mwa maeneo yatakayopatiwa kipaumbele ni ukaguzi wa miundombinu ya barabara, madaraja na mifereji ya maji, pamoja na kuhakikisha mifereji inasafishwa ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi na kupunguza uwezekano wa mafuriko katika maeneo ya makazi na biashara.

Aidha, utayari wa mitambo na vifaa vya dharura vinavyomilikiwa na TANROADS na TARURA utafuatiliwa ili kuhakikisha vinapatikana na vinaweza kutumika kwa wakati kurejesha mawasiliano endapo barabara au madaraja yataharibika.

 AFYA NA USALAMA WA MAJI

Katika sekta ya afya, Serikali itahakiki utayari wa vituo vya afya, ikiwemo upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na mahitaji muhimu ya kukabiliana na magonjwa yanayoweza kuongezeka wakati wa mvua na mafuriko.

Mamlaka husika pia zitatakiwa kuimarisha hatua za kuhakikisha usalama wa maji ya matumizi ya wananchi, pamoja na kutoa elimu kuhusu usafi wa mazingira na matumizi salama ya maji ili kupunguza hatari ya milipuko ya magonjwa yanayoweza kuhusishwa na uchafuzi wa maji.

MAENEO SALAMA NA ZANA ZA UOKOAJI

Serikali pia itafuatilia utambuzi na maandalizi ya maeneo salama kwa ajili ya kuwahifadhi wananchi ambao wanaweza kuathiriwa na mafuriko au majanga mengine yatayotokana na mvua hizo.

Vilevile, utayari wa zana na vifaa vya uokoaji vitakavyotumika wakati wa dharura, ikiwemo vile vinavyosimamiwa na Jeshi la Zima Moto na Uokoaji, utakaguliwa ili kuhakikisha mwitikio wa uokoaji unafanyika kwa wakati.

USALAMA WA CHAKULA NA MIFUGO

Katika sekta ya kilimo na mifugo, mamlaka za maeneo zitatakiwa kuwahimiza wakulima kuchukua hatua stahiki kulingana na ushauri wa wataalamu, ikiwemo kuvuna mazao yaliyokomaa mapema pale inapofaa na kuhifadhi mazao katika maeneo salama.

Kwa upande wa mifugo, wananchi wanaofuga katika maeneo hatarishi, hususan mabondeni, wanahimizwa kuchukua hatua za mapema za kuhamisha mifugo kwenda maeneo salama ili kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mafuriko.

 ELIMU KWA UMMA

Serikali imeelekeza pia kuimarishwa kwa utoaji wa taarifa na elimu kwa umma kuhusu tahadhari za kuchukua kabla na wakati wa mvua, ikiwemo kuepuka kuvuka mito au maeneo yenye maji mengi, kutokujenga katika maeneo hatarishi na kufuata maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika.

 Hatua hizo ni sehemu ya maandalizi ya Serikali ya kuimarisha uwezo wa taifa wa kukabiliana na majanga na kupunguza madhara kwa maisha ya watu, mali na miundombinu endapo mvua kubwa au mafuriko yatatokea.

Serikali imewahimiza viongozi wa mikoa, wilaya, halmashauri na wananchi kwa ujumla kuendelea kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuchukua hatua za tahadhari kwa wakati.

Read More

TANZANIA YAENDELEA KUJIIMARISHA KATIKA USIMAMIZI WA MAAFA

SERIKALI ya Tanzania imesema inaendelea kujenga uwezo wa kukabiliana na maafa nchini kwa kutumia teknolojia za kisasa, ikiwamo satelaiti na akili unde (AI), ili kuimarisha tahadhari za mapema, mipango ya kujiandaa, kukabili na urejeshaji hali pindi maafa yanapotokea.

Kauli hiyo imetolewa, na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, wakati wa ziara yake ya kikazi mjini Ankara, Uturuki iliyolenga kuimarisha uwezo wa kitaasisi, kuongeza maarifa ya kiufundi na kukuza ushirikiano katika kupunguza vihatarishi vya maafa, kukabiliana na dharura na mifumo ya kurejesha hali kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kiteknolojia.

Dkt. Yonazi ametembelea na kujionea namna Taasisi ya Turksat inavyotekeleza majukumu yake ikiwemo ya huduma za satelaiti, mawasiliano na teknolojia za anga ambayo inamilikiwa na Mfuko wa Uwekezaji wa Serikali ya Uturuki. Turksat ndiyo mwendeshaji pekee wa satelaiti za mawasiliano nchini humo na hutoa huduma za data, interneti na mawasiliano kwa shughuli za kila siku za taasisi za umma na binafsi za ndani na nje ya nchi pamoja na maeneo ambayo miundombinu ya kawaida ni hafifu.

Katika kubadilishana uzoefu ameeleza kuwa, Tanzania inaendelea kuangalia namna ya kuongeza uwezo wa kutumia taarifa za satelaiti pamoja na teknolojia ya akili unde, hatua ambayo itasaidia kutoa taarifa za mapema kuhusu maeneo hatarishi na kuwezesha mamlaka kupanga namna bora ya kuzuia na kupunguza madhara ya majanga na kukabiliana na maafa.

Kwa mujibu wa Dkt. Yonazi, Ofisi ya Waziri Mkuu inalichukulia suala la kuzuia na kukabiliana na maafa kama jambo la kitaifa linalohitaji kujengewa uwezo wa kutosha katika maeneo yote ya nchi na si kuwa na uwezo wa kuokoa watu pekee wakati wa majanga, bali kuhakikisha usimamizi wa maafa unakuwa sehemu ya usalama wa nchi.

Akizungumzia matumizi ya teknolojia hiyo katika kukabiliana na mafuriko, Dkt. Yonazi alisema uwezo wa satelaiti unaweza kusaidia kutambua kina cha maji katika mito na maeneo yenye vihatarishi, pamoja na kutathmini ukubwa wa madhara yanayoweza kujitokeza.

Aidha, amesema kuwa taarifa hizo zitasaidia kuwezesha Serikali kupanga mapema rasilimali zitakazohitajika katika kuzuia na kupunguza madhara pamoja na kuandaa rasilimali ikiwemo vifaa na timu kwenye maeneo yanayoweza kuathirika.

Akitoa maelezo kuhusu taasisi ya Turksat, Mkurugenzi wa huduma za satelaiti na mauzo Bw. Fuat Eroglu amesema taasisi hiyo ina sateliti sita angani na imeendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi yaliyogawanyika katika maeneo makuu matatu yanayohusu mawasiliano ya Satelaiti, huduma za mawimbi ya luninga na redio na data za interneti na Mifumo ya Teknolojia ya Habari kwa ajili ya Serikali Mtandao (e-Government).

Alisema pia taasisi hiyo inasambaza vifaa kwa ajili ya vituo vya huduma ya data za intaneti na mawimbi ya televisheni na redio kupitia satelaiti wakati wa maafa ili kuwezesha mawasiliano ya dharura pale ambapo minara ya simu na mkongo wa mawasiliano umeathirika.

“Kwa upande wa Mawasiliano ya Dharura na Kimkakati Turksat inatoa miundombinu salama ya mawasiliano kwa sekta za kimkakati kama vile usalama wa umma, jeshi, usafiri wa baharini, usafiri wa anga na mifumo ya mawasiliano wakati wa majanga ya asili au dharura,” alisema Eroglu.

 

Read More

SERIKALI YAWEKA MKAZO KULINDA HAKI ZA WATU WENYE UALBINO

SERIKALI imesema itaendelea kuweka kipaumbele katika kulinda haki, usalama na ustawi wa watu wenye ualbino, huku ikisisitiza umuhimu wa kuwapa fursa sawa za kushiriki katika maendeleo ya Taifa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Kitaifa la Uratibu na Utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Haki na Ustawi kwa Watu wenye Ualbino lilifanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema mpango huo umeandaliwa kwa lengo la kuweka mfumo jumuishi wa kulinda na kukuza haki na ustawi wa watu wenye ualbino, ikiwemo kuimarisha ulinzi na usalama, kuzuia ubaguzi, unyanyasaji na ukatili pamoja na kuhakikisha wanapata huduma na fursa sawa katika nyanja mbalimbali za maisha.

Mhe. Kabudi amesema Serikali pia imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha watu wenye ulemavu, wakiwemo wenye ualbino, wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa. Ametaja hatua hizo kuwa ni kutenga rasilimali kwa ajili ya upatikanaji wa mafuta kinga dhidi ya mionzi ya jua kwa watu wenye ualbino ili kuzuia madhara ya mionzi hiyo na saratani ya ngozi.

Hatua nyingine, amesema, ni kuimarisha huduma za afya na miundombinu inayozingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu, kuanzisha na kuimarisha vituo vya uchunguzi na matibabu ya saratani pamoja na kuendelea kupitia sera, sheria, kanuni na miongozo inayohusu watu wenye ulemavu.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi na usalama kwa watu wenye ulemavu, ikiwemo kupitia madawati ya jinsia na watoto ndani ya Jeshi la Polisi.

Mhe. Kabudi pia amesisitiza umuhimu wa kuwa na mfumo madhubuti wa kielektroniki wa taarifa za watu wenye ulemavu unaofika hadi ngazi za vijiji na mitaa ili kuwezesha Serikali kupanga na kutoa huduma kwa usahihi.

Amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira ya kuwawezesha watu wenye ulemavu kiuchumi kupitia fursa za mikopo yenye masharti nafuu zinazotolewa na Serikali na mamlaka za Serikali za mitaa.

Akizungumzia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Kabudi amesema lengo ni kujenga Taifa ambalo kila Mtanzania, bila ubaguzi, atakuwa na uwezo, ujuzi na fursa za kushiriki katika maendeleo na kufurahia maisha.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Africa Albinism Network, Bw. Martin Haule, alisema jukwaa hilo ni muhimu si kwa Tanzania pekee bali pia kwa Bara la Afrika, kutokana na changamoto zinazowakabili watu wenye ualbino katika nchi mbalimbali.

Alisema changamoto hizo ni pamoja na unyanyapaa, ubaguzi, ukosefu wa fursa sawa katika elimu na ajira, pamoja na changamoto za upatikanaji wa huduma za afya, ulinzi na haki.

Bw. Haule amesema uzoefu unaonyesha kuwa mabadiliko chanya yanawezekana pale watu wenye ualbino wanaposhirikishwa kikamilifu katika kupanga, kutekeleza na kufuatilia maamuzi yanayowahusu. 

Amepongeza Tanzania kwa kuendelea kuimarisha utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Watu wenye Ualbino kupitia nguzo zake za kinga, ulinzi, uwajibikaji na usawa pamoja na kutobagua.

Amesema anatarajia majadiliano ya siku nne ya jukwaa hilo yatazaa matokeo, majukumu yaliyo wazi, mifumo imara ya upatikanaji wa rasilimali na ramani ya utekelezaji itakayosaidia kulinda na kuendeleza haki za watu wenye ualbino hadi mwaka 2029 na kuendelea.

 “Mapambano ya watu wenye ualbino si suala la kundi moja pekee, ni suala la haki za binadamu, utu, usawa na maendeleo jumuishi kwa wote,” amesema.

Read More

Friday, September 25, 2026

SERIKALI YAJUMUISHA WENYE ULEMAVU KATIKA ELIMU YA KUKABILIANA NA EL NIÑO


Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa na Kitengo cha Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu imechukua hatua ya kuwafikia watu wasioona kwa kuwaandalia vipeperushi vya Nukta Nundu vyenye elimu kuhusu hatua za kuchukua kukabiliana na madhara yanayoweza kusababishwa na mvua za El Niño zinazotarajiwa kunyesha kuanzia mwezi Oktoba 2026.

 Hayo yamesemwa leo,  jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga, alipokutana na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) pamoja na Chama cha Wasioona Mkoa wa Dodoma na wanahabari kwa ajili ya kuhakiki ufasaha na usahihi wa maudhui ya kipeperushi hicho cha Nukta Nundu.

 Mhe. Nderiananga amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha taarifa za tahadhari na maandalizi ya kukabiliana na El Niño zinawafikia wananchi wote kwa kuzingatia mahitaji yao.

 Amesema, baada ya vipeperushi vya Nukta Nundu, Serikali itaendelea kuandaa taarifa kwa njia ya lugha ya alama na maandishi makubwa ili kuhakikisha makundi yote ya watu wenye ulemavu yanashirikishwa kikamilifu.

 Aidha, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Naibu Waziri amewashukuru viongozi pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu kwa umma kuhusu hatua za kuchukua kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na El Niño.

 Ameitaka mikoa yote 14 iliyotabiriwa kuathiriwa na El Niño pamoja na mikoa mingine nchini, kuhakikisha mipango na hatua za kukabiliana na athari hizo zinakuwa jumuishi kwa watu wenye ulemavu, ikiwemo kuwashirikisha viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu katika ngazi za mikoa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa SHIVYAWATA Mkoa wa Dodoma Bw. Omar Lubuva, amesema hatua ya Serikali kuandaa taarifa katika mfumo wa Nukta Nundu imeleta faraja kwa watu wasioona kutokana na changamoto wanazokutana nazo katika kupata taarifa zinazoandikwa kwa maandishi ya kawaida.

 “Kwa njia hii, watu wasioona wataweza kuchukua tahadhari za kutosha, lakini pia watashiriki katika kuhakikisha jamii inachukua wajibu wa pamoja katika kuwaepusha Watanzania na madhara ya El Niño tunayotarajia,” amesema Bw. Lubuva.

 

 

Read More

Tuesday, September 8, 2026

AFDP YAWA CHACHU YA MAENDELEO YA WANANCHI KIPUMBWI.

Wananchi wa Kata ya Kipumbwi Wilaya ya Pangani, Mkoa wa Tanga, wameeleza kunufaika na Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) inayotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD) chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu.

Hayo yameelezwa na wawakilishi wa wavuvi, wachakataji na wafanyabiasha wa mazao ya uvuvi kutoka Kata ya Kipumbwi wakati wa ziara kutathmini utekelezaji wa Programu hiyo katika mapitio ya utekelezaji wa kipindi cha kati (MTR) inayofanywa na Timu ya IFAD.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Katibu wa Umoja wa Wachakata Dagaa Kipumbwi (UWADAKI), Bw. Abdallah Mohamed, amesema AFDP imelenga kuboresha maisha ya wananchi kwa kuongeza kipato, kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi, kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi baada ya kuvunwa, kuimarisha matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi, kuimarisha lishe na masuala ya jinsia.

Amesema kupitia Programu hiyo, makundi mbalimbali yamenufaika, yakiwemo Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU), Vyama vya Wavuvi, wachakataji na wafanyabiashara wadogo wa mazao ya uvuvi.

Ameongeza kuwa, Programu hiyo imewezesha ujenzi wa miundombinu mbalimbali inayolenga kuboresha shughuli za uvuvi na biashara ya mazao ya uvuvi, ikiwemo ujenzi wa soko la samaki la kimataifa, vichanja vya kukaushia dagaa, mtambo wa kuzalisha barafu na chumba cha ubaridi.

Miundombinu hiyo inatarajiwa kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi baada ya kuvunwa, kuboresha mazingira ya biashara, kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi na kuongeza upatikanaji wa masoko, kuongeza usalama wa chakula na lishe na fursa za ajira.

Aidha, Bw. Mohamed amesema AFDP imewamepatiwa mafunzo mbalimbali, ikiwemo mafunzo ya elimu ya fedha na ujasiriamali yaliyolenga kuwezesha wavuvi, wachakataji na wafanyabiashara wadogo wa mazao ya uvuvi kuanzisha na kuendesha biashara zenye mafanikio, usimamizi bora wa fedha hususan mapato na matumizi. 

Mafunzo ya lishe yaliyolenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa lishe bora, hususan kwa watoto na makundi mbalimbali kulingana na umri, pamoja na uhusiano uliopo kati ya lishe bora, afya na uwezo wa kufanya kazi. 

Pia, mafunzo ya jinsia yamelenga kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika shughuli za kiuchumi, maamuzi ya familia na vikundi, pamoja na kuwezesha usawa wa fursa katika uzalishaji, biashara na matumizi ya mapato.

Vilevile, AFDP inalenga kuchochea uvuvi endelevu unaozingatia mabadiliko ya tabia ya nchi na kuongeza upatikanaji wa samaki, hatua inayotarajiwa kuongeza kipato kwa wananchi katika ngazi ya jamii na Wilaya ya Pangani kwa ujumla. 

 Katika ziara hiyo, wataalamu waliendelea kuhamasisha ushirikishwaji wa makundi yote katika jamii kwa usawa, kuimarisha ushirikiano baina ya wadau wa mazao ya uvuvi na kuweka mifumo na mipango madhubuti itakayosaidia katika uendeshaji endelevu wa soko hilo la kimataifa la samaki, ili liweze kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Kipumbwi, Pangani na Taifa kwa ujumla.

 

Read More

Sunday, September 6, 2026

RAIS DKT. SAMIA KUZINDUA MIRADI KATIKA MJI WA SERIKALI MTUMBA, DODOMA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua majengo ya Ofisi za Wizara, Taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami zenye urefu wa kilomita 57.1 katika Mji wa Serikali Mtumba,Jijini Dodoma.

Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika jumanne Septemba  nane mwaka huu  katika Uwanja wa Mashujaa uliopo ndani ya Mji wa Serikali Mtumba.

Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma leo  na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Mhe.Profesa Palamagamba Kabudi, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya hafla hiyo.

Alisema uzinduzi huo utahusisha maeneo matatu makuu ambayo ni majengo ya Ofisi za Wizara 26, Taasisi 11 za Serikali na barabara za lami zenye urefu wa kilomita 57.1.

Profesa Kabudi alisema kukamilika kwa majengo hayo, kutawezesha watumishi 18,510 kutumia ofisi za Mji wa Serikali, Mtumba.

“Ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba ulianza kutekelezwa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza ilihusisha ujenzi wa majengo 23 ya Ofisi za muda.ujenzi wa majengo hayo ulianza Novemba 28 mwaka  2018 na kukamilika Machi 22 mwaka 2019, hatua iliyowezesha baadhi ya watumishi wa Wizara na taasisi kuanza kuhamia.

Aliongeza kuwa :” Awamu ya pili ya ujenzi ilianza Oktoba, 2021, ikiwa inalenga kujenga majengo ya kudumu kwa ajili ya watumishi wote wa Wizara na Taasisi zilizopangwa kuhamia Mtumba.Pia ilihusisha ujenzi wa miundombinu na huduma mbalimbali za kijamii, ikiwemo barabara za lami.

Profesa Kabudi alisema mbali na barabara hizo, miundombinu ya kudumu ya mawasiliano pamoja na Uwanja wa Mashujaa imekamilika na itakuwa sehemu ya miundombinu itakayotumika katika shughuli za Serikali.

Hata hivyo, alisema baadhi ya miradi bado iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya umeme inayopita chini ya ardhi yenye urefu wa kilomita 42.

“Kazi ya ujenzi wa miundombinu ya maji safi na uondoshaji wa maji taka, TEHAMA, ufungaji wa mifumo ya usalama ya CCTV Camera, ujenzi wa kituo cha zimamoto pamoja na utekelezaji wa mpango wa upandaji miti na ustawishaji wa Mji wa Serikali nazo zinafanyika, "alisema.

Alisema Rais Dkt.Samia ameendelea kuweka msisitizo katika kuboresha mazingira hayo, ikiwa ni pamoja na kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa samani za Wizara na taasisi 26 zinazohamia katika majengo hayo.

Profesa Kabudi alisema hatua hizo zinaendelea kuifanya Mji wa Serikali Mtumba kuwa miongoni mwa alama muhimu za utekelezaji wa dhana ya Dodoma kuwa kitovu cha shughuli za Serikali.

Alisema uwekezaji huo pia unatarajiwa kuongeza fursa za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Dodoma na Tanzania kwa ujumla.

Read More

Wednesday, September 2, 2026

SERIKALI YATOA MAELEKEZO 13 KUKABILIANA NA EL-NINO

 


SERIKALI imetoa maelekezo 13 kwa umma, kamati za usimamizi wa maafa, Wizara, Taasisi, Mikoa, Halmashauri na sekta mbalimbali nchini, kwa ajili ya kujiandaa na kukabiliana na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua za El-Nino.

Imeelekeza maeneo yote hatarishi yatambuliwe mapema, tathmini za vihatarishi zifanyike na hatua stahiki zichukuliwe, ikiwemo kuwahamasisha wananchi kuondoka katika maeneo hatarishi na kwenda maeneo salama.

Maelekezo hayo yametolewa hii leo  na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El-Nino.

Profesa Kabudi amesema Serikali imeelekeza kuhakikisha mvua hizo zinatumika kikamilifu kwa shughuli za uzalishaji, ikiwemo kilimo, ufugaji, uvunaji wa maji na uvuvi.

Aidha, amesisitiza wananchi wanapaswa kuelimishwa na kuhimizwa kuchukua hatua za kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo, ikiwemo kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo salama, kuweka akiba ya chakula, kutumia mbinu bora za kilimo na kuchagua mazao pamoja na mbegu bora kwa msimu wa Vuli.

“Kuandaa rasilimali kwa ajili ya kuzuia au kupunguza madhara, kujiandaa na kukabiliana na maafa yatakayotokea na kushirikisha wadau wote wa maafa, wakiwemo wananchi, taasisi na sekta binafsi katika maeneo yao,” amesema.

Ameongeza kuwa: “Serikali imeagiza kuandaliwa na kutekelezwa kwa mipango ya kuzuia milipuko ya magonjwa kwa binadamu, wanyama na mimea.”

Profesa Kabudi amesema Wizara, Taasisi, Mikoa na wadau wengine wanaohusika na miundombinu wanapaswa kufanya ukaguzi wa miundombinu muhimu na kuhakikisha inaimarishwa na kusafishwa, ikiwemo madaraja, makaravati na mitaro.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu kabla, wakati na baada ya maafa kutokea, zikiwemo huduma za usafirishaji, maji na umeme.

Serikali pia imeagiza kuimarishwa kwa usimamizi wa mazingira, ikiwemo udhibiti wa taka ngumu, usafishaji na uimarishaji wa njia za maji, kingo za mito na mabwawa.

Aidha, imeelekeza kuhakikisha vifaa vya uokoaji, huduma za dharura na mifumo ya mawasiliano vinapatikana na kuwa katika hali ya utayari wakati wote.

Katika hatua nyingine, Serikali imeagiza kubainisha na kutenga maeneo salama yatakayotumika kwa ajili ya makazi ya dharura pindi maafa yatakapotokea.

Kwa upande wa sekta ya utalii, Serikali imeagiza kufanyika kwa ukaguzi na ukarabati wa miundombinu iliyopo katika maeneo ya Hifadhi za Taifa na Hifadhi za Jamii ili kuhakikisha shughuli za utalii zinaendelea wakati wote.

“Wizara, Taasisi, Mikoa na Halmashauri zote zimeagizwa kufuatilia na kuzingatia maelekezo ya kitaalamu pamoja na taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ili hatua stahiki za kujiandaa na kukabiliana na madhara ya El-Nino zichukuliwe kwa wakati.”

KUHUSU BILIONI 730

Akizungumzia taarifa iliyosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu makadirio ya matumizi ya Sh. bilioni 730 katika kujiandaa na kukabiliana na El-Niño, Profesa Kabudi amesema taarifa hiyo haikutoa ufafanuzi wa kina kuhusu shughuli zilizoainishwa katika mpango huo.

Amesema Sh. bilioni 730 ni makadirio ya fedha zinazohitajika kutekeleza Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El-Niño kabla, wakati na baada ya El-Nino kutokea.

“Kwa mujibu wa Mpango, makadirio ya fedha zinazohitajika kutumika katika kutekeleza Mpango huo ni Sh. bilioni 730,” amesema.

Hata hivyo, amesema fedha zilizotengwa katika bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli hizo katika sekta zote ni Sh. bilioni 10

Read More

Sunday, August 30, 2026

WAZIRI KABUDI AMUWAKILISHA RAIS SAMIA MKUTANO WA UA ANGOLA


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Prof. Palamagamba Kabudi, amesisitiza haja ya nchi za Afrika kuendelea kuitumia kikamilifu mifumo ya kikanda na kibara ya ulinzi na amani ili kuimarisha juhudi za kutatua migogoro na kudumisha utulivu Barani Afrika. 

Prof. Kabudi ameyasema hayo leo Jijini Luanda, Angola, alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano Maalumu wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (UA) unaojadili mifumo ya kuzuia na kutatua migogoro barani humo.

 

Akihutubia mkutano huo kwa niaba ya Mkuu wa Nchi, Waziri Kabudi ameeleza kuwa ufanisi wa utatuzi wa migogoro unategemea kuheshimiwa na kutekelezwa kwa sheria, taratibu na mikataba iliyowekwa na nchi wanachama kupitia vyombo vya kikanda.

 

“Tunahitaji kuendelea kuweka msisitizo kupitia maamuzi yetu ya pamoja ili kuzuia migogoro na kuhakikisha tunapata matokeo chanya na ya kudumu. Tanzania inaunga mkono kikamilifu na inakubaliana na jitihada zote zinazolenga kuimarisha ulinzi, amani na usalama Barani Afrika,” amesema Prof. Kabudi.

 

Tanzania imekuwa mshirika mkuu katika juhudi za diplomasia ya amani na usuluhishi wa migogoro barani Afrika, msimamo unaoendelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.



 

 

Read More

Friday, August 28, 2026

MKATABA WA UJENZI WA MELI TATU ZA UVUVI WA BAHARI KUU WASAINIWA


Serikali kupitia Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) imesaini mkataba wa ujenzi wa meli tatu za uvuvi wa bahari kuu na Kampuni ya Rongcheng Xinyang Ship Industry Limited ya China, ikiwa ni hatua ya kuimarisha na kuongeza tija katika sekta ya uvuvi nchini.

Mkataba huo umesainiwa, Jijini Dar es Salaam kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) inayofadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) ambapo Shirika la Uvuvi Tanzania - TAFICO  kuwa na meli mbili Kwa upande wa Tanzania bara na Shirika la Uvuvi Zanzibar -ZAFICO kuwa na meli moja.

Akizungumza wakati wa kushuhudia utiaji saini wa mkataba huo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Bashiru Kakurwa, amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025 pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwa lengo la kuleta mapinduzi katika sekta ya uvuvi.

Dkt. Kakurwa ameishukuru IFAD kwa ufadhili wa ujenzi wa meli hizo kupitia AFDP, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kufungua fursa zaidi za uvuvi wa bahari kuu na kukuza uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, amesema Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwa Mratibu Mkuu wa AFDP, inatambua utiaji saini wa mkataba huo kuwa hatua muhimu katika utekelezaji wa programu hiyo.

Amesema ujenzi wa meli hizo ni hatua itakayochangia ukuzaji wa uchumi kupitia uvuvi wa bahari kuu, pamoja na kuongeza uwezo wa Tanzania kutumia kikamilifu rasilimali zake za bahari.

Naye Mratibu wa AFDP kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Salum Mwinjaka, amesema utiaji saini wa mkataba huo ni hatua muhimu katika kuhakikisha malengo ya programu yanafikiwa kwa wakati na utekelezaji wake unakuwa na mafanikio.

Amesema Serikali inalenga kuhakikisha walengwa wa programu pamoja na Taifa kwa ujumla wananufaika na fursa zinazotokana na utekelezaji wa AFDP.

AFDP inalenga kukuza uzalishaji endelevu wa kibiashara unaozingatia mazingira, hususan katika uzalishaji wa mbegu za mazao ya kilimo kama mahindi, alizeti, maharagwe na jamii ya mikunde, pamoja na uvuvi na ufugaji wa viumbe maji.

Programu hiyo pia inalenga kuwawezesha wanawake na kuongeza ushiriki wa vijana katika shughuli za uzalishaji.

AFDP inaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) na kutekelezwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar kupitia taasisi mbalimbali, ikiwemo TAFICO, ZAFICO, Wakala wa Mbegu (ASA), TARI na TOSCI.

Hatua hiyo ya kusaini mkataba wa ujenzi wa meli tatu inatarajiwa kuongeza uwezo wa Tanzania katika uvuvi wa bahari kuu, kuchochea uwekezaji, kuongeza ajira na mapato, na hatimaye kuimarisha mchango wa sekta ya uvuvi katika uchumi wa Taifa.

Read More

Tuesday, August 18, 2026

DKT. YONAZI AWAKUMBUSHA VIJANA KULINDA AFYA ZAO KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA UKIMWI


 Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dkt. Jim Yonazi, Amewaasa vijana kulinda afya zao na kuepuka tabia hatarishi ili kupunguza maambukizi mapya ya VVU, kwa kuzingatia kuwa ni kundi linaloongoza kuwa hatarini zaidi nchini Tanzania.

Dkt. Yonazi ameyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Afua za UKIMWI Wilaya ya Uvinza Mkoa wa Kigoma alipoambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Dkt. Adam Mrisho, timu ya wataalam kutoka Ofisi yake, Wizara ya Afya, TAMISEMI na Ofisi ya Mkoa huo.

Aidha amepata wasaa kutembelea Kituo cha Maarifa Kata ya Kazuramimba mkoani humo kinachotoa huduma za masuala ya VVU na UKIMWI, na kukutana na vijana wanaotekeleza afua za UKIMWI kupitia vikundi vya uzalishaji mali kwa lengo la kujiinua kiuchumi na kujiletea maendeleo yao.

Akiwa katika kituo hicho, Dkt. Yonazi amepokea taarifa kutoka kwa mwenyekiti wa kikundi, Billy Sekibaha, kuhusu shughuli zinazofanywa na kikundi hicho ikiwemo za biashara ndogondogo za kuuza dagaa pamoja na shunguli za ushonaji wa nguo kwa lengo la kujikwamua kiuchumi na kuondokana na dhana ya utegemezi.

Amesisitiza kuwa, kundi la vijana linategemewa na Taifa katika shughuli za uzalishaji mali na kujiletea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla hivyo ni vyema vijana wakaendelea kujilinda na kulinda wengine kwa kutambua hali zao na endapo wakagundulika kuwa na maambukizi ya VVU inashauriwa kuanza kutumia dawa mapema.

"Mnafanya kazi nzuri sana, endeleeni kuchangamkia uwepo wa mitandao ya kijamii kutangaza bidhaa zenu ili kuwafikia wateja wengi zaidi na kujitangaza kitaifa na kimataifa," alisisitiza Dkt. Yonazi

Kwa upande wake Mtendaji  wa TACAIDS, Dkt. Adam Mrisho amewapongeza vijana hao kwa kazi nzuri wanazofanya na kusisitiza kuwa Tume itaendelea kuwawezesha vijana kiuchumi na kuwajengea uwezo ili kuendeleza mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya VVU na kufikia lengo la kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030.

 

Read More