Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa na Kitengo cha Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu imechukua hatua ya kuwafikia watu wasioona kwa kuwaandalia vipeperushi vya Nukta Nundu vyenye elimu kuhusu hatua za kuchukua kukabiliana na madhara yanayoweza kusababishwa na mvua za El Niño zinazotarajiwa kunyesha kuanzia mwezi Oktoba 2026.
Hayo yamesemwa leo, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga, alipokutana na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) pamoja na Chama cha Wasioona Mkoa wa Dodoma na wanahabari kwa ajili ya kuhakiki ufasaha na usahihi wa maudhui ya kipeperushi hicho cha Nukta Nundu.
Mhe. Nderiananga amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha taarifa za tahadhari na maandalizi ya kukabiliana na El Niño zinawafikia wananchi wote kwa kuzingatia mahitaji yao.
Amesema, baada ya vipeperushi vya Nukta Nundu, Serikali itaendelea kuandaa taarifa kwa njia ya lugha ya alama na maandishi makubwa ili kuhakikisha makundi yote ya watu wenye ulemavu yanashirikishwa kikamilifu.
Aidha, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Naibu Waziri amewashukuru viongozi pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu kwa umma kuhusu hatua za kuchukua kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na El Niño.
Ameitaka mikoa yote 14 iliyotabiriwa kuathiriwa na El Niño pamoja na mikoa mingine nchini, kuhakikisha mipango na hatua za kukabiliana na athari hizo zinakuwa jumuishi kwa watu wenye ulemavu, ikiwemo kuwashirikisha viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu katika ngazi za mikoa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa SHIVYAWATA Mkoa wa Dodoma Bw. Omar Lubuva, amesema hatua ya Serikali kuandaa taarifa katika mfumo wa Nukta Nundu imeleta faraja kwa watu wasioona kutokana na changamoto wanazokutana nazo katika kupata taarifa zinazoandikwa kwa maandishi ya kawaida.
“Kwa njia hii, watu wasioona wataweza kuchukua tahadhari za kutosha, lakini pia watashiriki katika kuhakikisha jamii inachukua wajibu wa pamoja katika kuwaepusha Watanzania na madhara ya El Niño tunayotarajia,” amesema Bw. Lubuva.

EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.