Thursday, March 30, 2017

WAZIRI MKUU AWASHAWISHI WAWEKEZAJI KUTOKA MAURITIUS KUWEKEZA NCHINI

§  Awataka waje kujenga viwanda vya sukari, nguo na samaki

SERIKALI imepanga kuondoka katika uchumi wa chini na kufikia uchumi wa kati ifikapo  2025 ambapo katika kufikia azma hiyo imeweka juhudi kwenye uanzishwaji wa viwanda mbalimbali kuanzia vidogo hadi vikubwa.

Mpango wa kufikia uchumi wa kati unalenga kuiwezesha serikali kujitegemea na tayari hatua mbalimbali zimechukuliwa ili kuweza kufikia azma hiyo.

Dira ya Taifa ya Maendeleo, imeainisha malengo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujenge uchumi imara wenye uwezo wa kukabiliana na ushindani.

Katika kuhakikisha mkakati huo unafanikiwa  Serikali imeweka sera na mazingira mazuri kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi  kuwekeza kwenye viwanda.

 Hivi karibuni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikwenda nchini Mauritius kumwakilisha Rais Dk. John Magufuli kwenye uzinduzi wa  Jukwaa la Uchumi Barani Afrika (AEP).

Baada ya kumaliza uzinduzi huo Waziri Mkuu alipata fursa ya kutembelea viwanda mbalimbali nchini Mauritius na kuhamasisha wawekezaji waje nchini ili kuongeza uzalishaji utakaokuza uchumi na kuongeza pato la taifa.

KIWANDA CHA SUKARI CHA ALTEO

Akiwa kiwandani hapo Waziri Mkuu alipata maelezo ya uendeshaji wake kuanzia hatua ya utayarishaji wa mashamba ya miwa hadi uzalishaji wa sukari.

Waziri Mkuu alifurahishwa na teknolojia ya kisasa inayotumika kiwandani hapo hali iliyomfanya ashawishike kuwashawishi wawekezaji hao kuja nchini kupanua uwekezaji kwa kuongeza mashamba ya miwa na uzalishaji wa sukari.

Kiwanda cha sukari kinachomilikiwa na kampuni ya Alteo kina uwezo wa kukamua tani 400 za miwa kwa saa na kuzalisha tani 170,000 za sukari kwa mwaka.

Kampuni ya Alteo inamiliki kiwanda cha sukari cha TPC mkoani Kilimanjaro kwa ubia na Serikali ya Tanzania na  kinazalisha tani 110,000 kwa mwaka.

Aidha, Waziri Mkuu amefanya mazungumzo na uongozi wa kiwanda hicho na kuwashawishi waongeze maeneo ya uwekezaji nchini.

 “Tekonolojia wanayoitumia katika uendeshaji wa kiwanda chao ni nzuri hivyo tumewashawishi waje kuongeza maeneo ya uzalishaji wa sukari nchini ili tuweze kukidhi mahitaji,” amesema.

Waziri Mkuu amesema Tanzania kuna viwanda vitano vya sukari ambavyo ni Mtibwa, Mahonda (Zanzibar), TPC, Kilombero na Kagera ambavyo uzalisha tani 320,000 kwa mwaka wakati mahitaji ya ndani ya nchi kwa mwaka ni tani 420,000.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Khalid Salum Mohammed amesema Zanzibar kuna kiwanda kimoja cha sukari ambacho uzalishaji wake haukidhi mahitaji kutokana na uhaba wa malighafi.

 Dk. Khalid amewakaribisha kampuni ya Alteo kwenda Zanzibar kushirikiana na Serikali katika uwekezaji hususani kwenye viwanda vya sukari.

 Naye Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo Bw. Patrick de Labauve amesema wamekubali kuongeza maeneo ya uwekezaji wa mashamba ya miwa nchini.

 Pia ameomba Serikali iwapatie fursa ya uwekezaji katika sekta ya utalii mkoani Kilimanjaro kwani kuna vivutio vingi vya utalii ukiwemo mlima Kilimanjaro.

Akizungumzia kuhusu ajira amesema kiwanda cha TPC kimeajiri wafanyakazi 3,000 wakiwemo 1,900 wa kudumu wa ndani utakaotosheleza mahitaji na kupata ziada.

Kusimamia mfumo mzima wa usambazaji wa sukari nchini ikiwa ni pamoja na kuwadhibiti wafanyabishara wenye tabia ya kuhodhi soko la sukari kwa lengo la kusababisha upungufu usio halisi wa sukari (artificial shortage).

Kuendelea kuhamasisha na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa wazalishaji wa sukari wa ndani ya nchi.

KIWANDA CHA SAMAKI

Waziri Mkuu pia alitembelea kiwanda cha kusindika samaki aina ya jodari na kuwakaribisha viongozi wa kiwanda hicho kuja nchini kuangalia maeneo ya uwekezaji wa viwanda vya samaki.

Amesema Serikali imeweka sera nzuri za uwekezaji na pia ina maeneo mengi na mazuri kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vya samaki, ambayo ni bahari, mito na maziwa ambayo aina mbalimbali za samaki.

 Waziri Mkuu amesema hayo wakati alipotembelea kiwanda cha samaki cha Mer des Mascareignes kilichoko  jijini Port Louis nchini Mauritius.

 “Tanzania kuna fursa nyingi za uwekezaji hasa kutokana na mazingira yake. Mnaweza kuja kuwekeza kwenye viwanda vya usindikaji wa samaki tuna bahari, mito na maziwa yenye samaki wa aina mbalimbali,” alisema.

Majaliwa alisema Serikali imedhamiria kuimarisha uchumi wake kupitia sekta ya viwanda ili kuongeza tija kwa Taifa na kwa wananchi kiujumla hivyo wanahitaji wawekezaji waliotayari kuja kuwekeza nchini.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohammed alisema Tanzania inahitaji wawekezaji watakaowekeza kwenye uvuvi wa kina kirefu na ujenzi wa viwanda vya samaki.

Dk. Khalid alisema lengo la uwekezaji huo ni kukuza uchumi wa Taifa pamoja kupanua soko la ajira na kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake.

Naye Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Bw. Patrick Hill alisema wamefurahia mualiko wa kuja Tanzania kwa ajili ya kuangalia fursa na uwekezaji na kwamba wako tayari kushirikiana na Serikali.

Alisema kampuni yao inajishughulisha na usindikaji wa samaki aina moja tu ya jodari na wananunua kutoka kwa makampuni makubwa ya uvuvi huku wateja wao wakubwa wakiwa ni bara la Ulaya.

 KIWANDA CHA NGUO

 Akiwa kwenye kiwanda cha nguo cha Compagnie Mauricienne De Textile Ltee kinachotengeneza nguo kwa kutumia teknolojia ya kisasa nchini Mauritius chenye uwezo wa kutengeneza tani milioni 40 hadi 50 kwa mwaka.

Waziri Mkuu aliwakaribisha wawekezaji hao kuja nchini kuwekeza katika viwanda vya kutengeneza nyuzi na nguo kwa kuwa kuna malighafi za kutosha kwa ajili ya uzalishaji huo.

“Tumefarijika na uwekezaji wenu na tumejionea namna ambavyo mnavyoendesha kiwanda chenu kuanzia utengenezaji wa nyuzi hadi nguo, hivyo tunahitaji viwanda kama hivi nchini Tanzania kwa sababu sisi tunazalisha pamba nyingi na yenye ubora unaokubalika kimataifa,” alisema.

Waziri Mkuu alisema madhumuni ya kuwakaribisha wawekezaji hao kuja Tanzania na kuwekeza katika  viwanda vya kutengeneza nyuzi yanalenga kuboresha kilimo cha pamba na kuwawezesha wakulima kupata tija.

 “Tunalima pamba nzuri na hawa hawalimi wananunua kutoka nje ya nchi yao, hivyo wakija kuwekeza Tanzania itawarahisishia kupata malighafi ya uhakika na kwa urahisi ”  alisema.
 Alisema viwanda hivyo vitasaidia maendeleo ya kilimo cha pamba kwa sababu vitatoa ajira kwa wananchi wengi hivyo kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini wa kipato.

Mbali na kuwakaribisha wawekezaji hao, Waziri Mkuu alitoa wito kwa wananchi wenye uwezo kuhakikisha wanajenga viwanda vya nyuzi kwenye mikoa yote inayozalisha pamba ili waweze kuiongezea thamani kabla ya kuiuza.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fedha wa kiwanda hicho David Too Sai Voon alisema wamefurahishwa na mualiko wa kuja Tanzania kwa ajili ya kuangalia maeneo ya uwekezaji wa viwanda vya nyuzi na nguo.


David alisema kiwanda chao kilianzishwa mwaka 1986 na kwa sasa kimeajiri wafanyakazi 18,000 ambapo mauzo yao kwa ni dola milioni 200. “Nguo tunazotengeza ni za kiwango cha kimataifa na tunauza katika maduka makubwa barani Ulaya,”
Read More

SERIKALI HAITAVUMILIA WAKANDARASI WAZEMBE - WAZIRI MKUU

*Amtaka Waziri wa Maji avunje mkataba ifikapo Mei 31
*Ni mkandarasi aliyenyang’anywa pasipoti na Rais Magufuli

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haitavumilia wakandarasi wasio na uwezo na ambao wanapewa kazi lakini wanashindwa kuzimaliza katika muda uliopangwa.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo, leo (Alhamisi, Machi 30, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa Halmamshauri ya Chalinze na wale wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (CHALIWASA) katika ofisi zao, karibu na daraja la mto Wami, wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.

Alikuwa ameenda kukagua mradi wa upanuzi wa mtambo wa maji Chalinze na ujenzi wa mfumo wa kusafirisha na kusambaza majisafi pamoja na matenki ya kuhifadhia maji ambao umechukua muda mrefu lakini haujakamilika. Awamu ya kwanza ilianza mwaka Septemba mosi 2001 na kukamilika Desemba mosi 2003.

Amemuagiza Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge ahakikishe kuwa kazi ya ujenzi wa mradi huo inaimarika na kufikia asilimia 80 la sivyo, wakamilishe taratibu za kukatisha mkataba na kutafuta mkandarasi mwingine.

Agizo la Waziri Mkuu linafuatia taarifa aliyopewa kwamba mkandarasi wa mradi huo, Overseas Infrastructure Alliance (OIA) Pvt Ltd ya India alipaswa kumaliza kazi hiyo Februari 22, mwaka huu lakini hadi sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 23 tu.

“Nimeelezwa kwamba mmempatia nyongeza ya siku 100 ambayo inaisha tarehe 31 Mei 2017, kama kazi yake haitakuwa ya kuridhisha na kufikia walau asilimia 80, itabidi Mheshimiwa Waziri uendelee na taratibu zako za kukatisha mkataba, tuanze kutafuta mkandarasi mwingine,” amesema.

“Hii kampuni niliikuta Lindi kwenye mradi mwingine wa maji kama huu. Nilitoa maagizo ya kuharakisha ujenzi ukamilike lakini hawakufanya hivyo hadi Mheshimiwa Rais alipoenda na kuagiza mkandarasi anyang’anywe pasi yake ya kusafiria mpaka atakapomalizia kazi.”

“Kwa kifupi ni kwamba hii kampuni haina uwezo wa kufanya hizi kazi, na ndiyo maana hadi sasa wamekamilisha asilimia 23 tu ya mradi wakati walipaswa kuwa wamemaliza hivi sasa,” amesema Waziri Mkuu na kuongeza: “Mheshimiwa Waziri endelea na utaratibu wa kuwaondoa kisheria sababu hata tukiwaongezea muda bado hawatakamilisha kazi.”

“Nimesikitika sana kukuta mkandarasi hajafikia malengo. Mtu akipewa kazi anapaswa awe na uwezo wa kifedha wa kuifanya ile kazi ili hata Serikali ikichelewesha malipo yake, yeye aendelee na kazi,” ameongeza Waziri Mkuu.

Akizungumzia kuhusu ufanisi wa mradi huo, Waziri Mkuu amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa CHALIWASA, Eng. Christer Mchomba, ahakikishe kuwa wanapeleka maji hadi majumbani mwa wateja na kuweka mita ili wananchi waweze kulipa bili zao badala kuishia kutoa huduma hiyo kwenye vioski (viula).

“Kazi ya kupeleka maji majumbani ni yenu CHALIWASA na siyo ya Wizara. Pelekeni maji na mfunge mita ili watumiaji waweze kulipa bili zao. Pia toeni elimu kwa wananchi kupitia mikutano ya hadhara, waelezeni mipango yenu na wapi mlipofikia. Kazi yenu siyo kutandika mabomba tu, bali kutekeleza majukumu mliyopewa kwa niaba ya Serikali,” amesema.

Kuhusu mitambo inayotumika, Waziri Mkuu amesema mashine zilizopo ni za siku nyingi tangu 2003; hivyo amemuagiza Waziri Lwenge afuatilie upatikanaji wa mashine za kisasa kwani hilo suala ni kubwa na haliwezi kubebwa na CHALIWASA. “Bora mngeanza kuagiza mashine mpya hivi sasa, badala ya kusubiri zichakae kabisa, ndipo muanze kufikiria kuagiza.”

Mapema, akitoa taarifa ya mradi huo, Eng. Mchomba alisema awamu ya tatu ya ujenzi wa mradi huo ilisainiwa Mei 18, 2015 kati ya DAWASA na OIA yenye ubia na kampuni ya Pratibha Industries kutoka India kwa gharama ya dola za Marekani milioni 41.36 ambazo zilikuwa ni fedha za mkopo nafuu kutoka benki ya Exim ya India.

“Kazi zilizopangwa kufanyika ni upanuzi wa mtambo wa maji ili kuongeza uzalishaji wa maji kutoka mita za ujazo 500 hadi 900 kwa siku; ujenzi wa mfumo wa mabomba ya kusambaza maji wenye kilometa 1,022; ujenzi wa matenki makubwa 19 ya kuhifadhia maji; vituo tisa (9) vya kusukumia maji (booster stations) na vioski (viula) vya kuchotea maji 351.”

Alisema hadi sasa mkandarasi huyo amekwishalipwa dola za Marekani milioni 15.81 sawa na asilimia 38 na anaendelea na ulazaji mabomba ambapo hadi sasa amekwishalaza mabomba yenye urefu wa km.141 sawa na asilimia 12.4.

Alisema mradi huo umelenga kuvinufaisha vijiji 68 ambavyo 19 kati ya hivyo viko Kaskazini mwa mto Wami na 49 viko Kusini mwa mto huo.

Akizungumzia utendaji kazi wa mkandarasi huyo, Eng. Mchomba alisema Serikali imechukua hatua za kimkataba dhidi yake kwa kumtoza gharama ya kuchelewa kumaliza mradi (liquidated damages) kuanzia Februari 23, 2017.

“Pia mkandarasi amepewa notisi ya siku 100 ya kumtaka aongeze kasi ya kazi, vinginevyo tutasitisha mkataba ifikapo terehe 31 Mei, 2017 kulingana na kipengele namba 8.7 cha mkataba,” alisema.

Read More

Tuesday, March 28, 2017

KIKAO CHA BARAZA LA WAFANYAKAZI OFISI YA WAZIRI MKUU-DODOMA

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Dkt. Hamisi Mwinyimvua akiimba wimbo wa uzalendo wakati wa ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi wa ofisi yake Dodoma Machi 28, 2017.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya Waziri Mkuu wakiimba wimbo wa uzalendo wakati wa mkutano wao wa mwaka katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi hiyo Dodoma.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Dkt. Hamisi Mwinyimvua (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya Waziri Mkuu mara baada ya ufunguzi wa mkutano huo katika ukumbi wa ofisi hiyo Dodoma.
Mkurugenzi wa Sera na Mipango Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Packshard Mkongwa akiwasilisha hoja za bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi uliofanyika Dodoma Machi 28, 2017.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Dkt. Hamisi Mwinyimvua akiwasilisha hotuba yake wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi yake ukumbi wa mikutano Dodoma Machi 28, 2017.


Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Flora Bilauri akitoa neno la utangulizi wakati mkutano wao wa mwaka uliofanyika Ukumbi wa mikutano wa Ofisi hiyo Dodoma Machi 28, 2017.

Read More

MFUMO MPYA WA KIELEKTRONIKI WAZINDULIWA DODOMA

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Agustino Tendwa akiratibu shughuli ya uzinduzi wa mfumo wa Kielektroniki wa Kufuatilia Utekelezaji wa Ahadi, Ilani ya Chama Tawala na Maagizo ya Viongozi Wakuu uliofanyika Ofisi ya Waziri Mkuu Bungeni Machi 28, 2017.

Mchumi Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Novatus Tesha akionesha namna mfumo wa Kielektroniki wa Ufatiliaji wa Taarifa za Serikali unavyofanya kazi kwa wajumbe wa mkutano huo (hawapo pichani) Dodoma. 

Mchumi Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Novatus Tesha akionesha namna mfumo wa Kielektroniki wa Ufatiliaji wa Taarifa za Serikali unavyofanya kazi kwa wajumbe wa mkutano wa uzinduzi wa mfumo huo Machi 28, 2017 Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akieleza umuhimu wa mfumo mpya wa Kielektroniki wa Kufuatilia Utekelezaji wa Ahadi, Ilani ya Chama Tawala na Maagizo ya Viongozi Wakuu wakati wa uzinduzi wa mfumo huo Machi 28, 2017 katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Bungeni Dodoma na kulia kwake waliokaa ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Mhe. Antony Mavunde.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Dkt. Hamisi Mwinyimvua akiwasilisha hotuba yake wakati wa uzinduzi wa mfumo wa Kielektroniki wa Kufuatilia Utekelezaji wa Ahadi, Ilani ya Chama Tawala na Maagizo ya Viongozi Wakuu Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Bungeni Dodoma.



Read More

WAZIRI MHAGAMA AZINDUA MFUMO MPYA WA KIELEKTRONIKI


 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama amezindua mfumo mpya wa Kielektroniki wa Kufuatilia Utekelezaji wa Ahadi, Ilani ya Chama Tawala na Maagizo ya Viongozi Wakuu ulianzishwa kwa lengo la kusaidia upatikanaji na utoaji wa taarifa za utekelezaji kupitia mfumo wa kisasa (kidigitali).

Akizindua mfumo huo wakati wa mkutano na waandishi wa habari Machi 28, 2017 Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Bungeni, Waziri alieleza umuhimu wa mfumo huo kuwa  umejikita katika kusaidia Viongozi Wakuu kupata Taarifa za utekelezaji wa Maagizo yao na yale yaliyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala.

“Mfumo huu utasaidia sana katika kufuatilia shughuli za Serikali ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa maagizo yote na ahadi zilizotolewa ili kuona utekelezaji wake kwa urahisi tofauti na ilivyokuwa awali” Alisema Mhe.Waziri.

Aidha mfumo utasaidia pia Ofisi ya Waziri Mkuu kuongeza ufanisi wa uratibu na ufuatiliaji wa shughuli za kila siku za Serikali kwakuwa taarifa zote zitapatikana kwa wakati na takwimu za uhakika.

Alibainisha kuwa, kuanzishwa kwa mfumo ni moja ya sehemu ya kuondoa changamoto kadhaa ikiwa ni kuongeza ufanisi maeneo yetu ya kazi “kuanzishwa kwa mfumo huo kutatua changamoto za uchelewashwaji wa taarifa, na kutowajibika kwa ujumla na kuleta ufanisi kazini”.Alisisitiza waziri.

Aidha kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. Hamisi Mwinyimvua alibainisha kuwa mfumo umepitia hatua zote muhimu ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha Mawaziri wote, Makatibu Wakuu wote, Wasaidizi wa Mhe. Rais John Pombe Magufuli na Watendaji  wa Serikali.

Kwa kumalizia Waziri alipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao kwa kuona umuhimu wa kuwepo kwa mfumo huu na kutoa rai kwa Watendaji wote wa Serikali kuutendea haki kwa kufanya kazi bila uzembe wowote. “rai yangu kwa Watumishi wa Umma wote Nchini kuwajibika kwa kufanya kazi kwani kupitia Mfumo huu, mzembe atajulikana na mchapa kazi atajulikana. Na ikumbukwe tu, wazembe na wavivu hawana nafasi katika Serikali ya Awamu ya Tano”.



Read More

Monday, March 27, 2017

WAZIRI MKUU ATEMBELEA MGODI WA BUZWAGI NA KUCHUKUA SAMPULI ZA MCHANGA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefanya ziara kwenye mgodi wa dhahabu wa Buzwagi uliopo wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga na kuchukua sampuli za mchanga katika makontena mbalimbali kwa lengo la kwenda kuyapima kwa wataalamu wa madini ili kubaini kiasi cha dhahabu kilichomo.

Amesema wanataka kuona mchanga unaosafirishwa na mwekezaji huyo unakiasi gani cha dhahabu, pia Serikali inataka kufahamu kama kodi inayolipwa ni sahihi.” Hata hivyo tayari Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli alishatoa tangazo la kuzuia usafirishaji wa michanga kwenda nje ya nchi,”.

Waziri Mkuu alitembelea mgodi huo jana jioni (Jumatatu, Machi 27, 2017) na kuchukua sampuli za mchanga kwa lengo la kuondoa mashaka juu ya kinachosafirishwa. Sampuli hizo amezichukuwa kwenye makontena yaliyofungwa kwa ajili ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

“Tumeamua kuchukua sampuli za mchanga ambao mwekezaj anasema wanaupeleka nje ya nchi kwa ajili ya kwenda kutenganisha madini ya dhahabu na shaba. Hata hivyo nimemuhoji kwa nini mitambo hiyo isiletwe nchini ili kila kitu kifanyike hapahapa,”

Waziri Mkuu amesema sera ya uwekezaji inasema mtambo huo unatakiwa uwepo nchini ili kila hatua ya uchenjuaji ifanyike hapa hapa, hivyo tunataka kujiridhisha na mwenendo wa mwekezaji na mapato tunayoyapata kama yanastahili.

Aliongeza kwamba “Hili lipo miongoni mwa masharti ya uwekezaji kwenye sekta ya madini nchini kwamba mitambo hiyo ije kujengwa hapa nchini na itaongeza fursa ya ajira na kukuza sekta nyingine ikiwemo ya kilimo,”.

Wakati huohuo Waziri Mkuu amewataka Watanzania kuwa nasubira wakati Serikali ikiendelea na zoezi la kuchunguza athari zitokanazo na kusafirisha mchanga wa madini nje ya nchi. Pia  amewatoa wasiwasi wafanyakazi katika migodi na wamiliki kutowapunguza na badala yake waache waendelee na majukumu yao.

Kwa upande wake Meneja Uendelezaji wa mgodi huo Bw. George Mkanza alisema mgodi huo ulionzishwa mwaka 2009 umeajiri watumishi 720 pamoja na vibarua 500.

Alisema kwa siku wanachenjua makontena matatu hadi sita ambapo katika kila kontena moja wanapata kilo tatu za madini ya dhahabu na tani nne za madini ya shaba.

Bw. Mkanza alisema wanazalisha asilimia 50 ya madini ya dhahabu na asilimia 50 ya dhahabu iko kwenye mchanga na inakuwa imechanganyika na madini ya shaba ambayo ndiyo unaosafirishwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kutenganishwa.

“Hapa Buzwagi tuna makontena 179, makontena mengine 152 yako Dar es Salaam kwenye bandari kavu ya Nazam na 21 yako bandarini. Kila siku tunapoendelea kuzalisha tunakuwa na makontena manne hadi sita. Ndugu zetu wa Bulyanhulu nao wanamakontena 108 yako mgodini na 104 yako Nazam Cargo Dar es Salaam,” alisema.

Read More

WAZIRI MKUU AFANYA ZIARA KATIKA MGODI WA BUZWAGI

Mtaalam wa madini akiweka sampuli ya mchanga katika mfuko kutoka katika baadhi ya makontena na kumkabidhi Waziri Mkuu Kassim Majaliwa nakuondoka nao kwa ajili ya kuupeleka katika maabara ya serikali inayoshughulika na upimaji wa madini. Waziri Mkuu alifanya ziara katika mgodi wa Buzwagi 27 March, 2017 kwa lengo ya kujionea aina ya mchanga unaosafirishwa nje ya nchi na baadhi ya Migodi inayochimba Dhahabu hapa Nchini. 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga  Josephine  Matiro katika uwanja wa ndege wa mgodi wa  Buzwagi 27 March,2017 katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga  Zainabu  Telaki viongozi hao walifika kumpokea Waziri Mkuu alipofika kuangalia shughuli za mgodi wa Buzwagi uliopo wilaya Kahama mkoa wa Shinyanga 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga  Josephine  Matiro katika uwanja wa ndege wa mgodi wa  Buzwagi 27March2017, Katikati ni Mkuu wa mkoa wa Shinyanga  Zainabu  Telaki. Viongozi hao walifika kumpokea Waziri Mkuu alipofika kuangalia shughuli za Mgodi wa Buzwagi uliopo wilaya Kahama Mkoa wa Shinyanga. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  afanya ziara  katika Mgodi wa Buzwagi  27 March 2017 kwa ajili ya kuangalia  Mchanga  uliowekwa katika  Makontena  kwa ajili yakusafirishwa nje ya nchi katikati ni Mkuu wa  Mkoa wa Shinyanga  Zainabu Telaki, na kushoto ni Meneja  Mkuu wa  Mgodi wa Buzwagi Bwana  Stewart Hamilton Picha na PMO.



Read More

WAZIRI MKUU APOKEA TAARIFA YA KIFO CHA FARU JOHN

*Ni ya uchunguzi uliofanywa na Mkemia Mkuu wa Serikali

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea taarifa rasmi ya uchunguzi wa kifo cha Faru John kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele ambaye alikuwa akiongoza tume maalum iliyoundwa na Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amepokea taarifa hiyo, leo (Jumatatu, Machi 27, 2017) kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.

Akisoma taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Prof. Manyele amesema tume yake ilifanya uchunguzi wa kifo cha Faru John kwa kupima vinasaba vya sampuli mbalimbali vikiwemo mzoga, fuvu, mifupa, pembe, damu, ngozi na kinyesi kilichokaushwa ambapo ilibainika kuwa vyote ni vya mnyama mmoja, aina ya faru mweusi ambaye ni dume.

Prof. Manyele amesema matokeo hayo yamethibitisha kuwa faru John alikufa katika hifadhi ya Sasakwa Grumeti kwa kukosa matunzo na uangalizi wa karibu.

“Maabara iliyotumika ni ya Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini chini ya usimamizi wa timu ya wataalamu kutoka Tanzania, wachunguzi wa Serikali, chini ya Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Sababu za kifo chake zilichangiwa na kukosa matunzo na uangalizi wa karibu, kukosa matibabu alipoumwa, mazoea yanayotokana na kutofuata taratibu zilizowekwa kisheria na mapungufu ya kiuongozu kwa Wizara husika, hifadhi na taasisi zake,” amesema.

Prof. Manyele amesema mapungufu waliyoyabaini kutokana na uchunguzi huo ni kutokuwepo kwa kibali rasmi cha kumhamisha Faru John; kukosekana kwa mkataba wa kupokelewa kwa Faru John hifadhi ya Sasakwa Grumeti na kutofuatiliwa kwa afya na maendeleo ya Faru John baada ya kuhamishwa.  

Mengine ni uchukuaji holela wa sampuli za wanyama pori kwa lengo la utafiti na kuzisafirisha nje ya nchi; migongano ya kimaslahi kati ya watumishi waliolenga kusimamia taratibu na wale wenye kusimamia maslahi binafsi na uwepo wa taasisi nyingi zenye mamlaka sawa juu ya masuala ya uhifadhi wa wanyamapori.

Pamoja na kwamba mawasiliano yanaonyesha zoezi hilo liliridhiwa na Wizara, hapakuwepo na kibali rasmi kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori cha kuruhusu kumhamisha Faru John kutoka NCAA kwenda Grumeti,” amesema Prof. Manyele katika ripoti yake.  

Akizungumzia kuhusu uchukuaji holela wa sampuli za wanyama pori kwa lengo la utafiti na kuzisafirisha nje ya nchi, Prof. Manyele amesema kumbukumbu za watafiti na aina ya sampuli wanazochukua haziwekwi vizuri  na kwamba tume inashauri TAWIRI na TANAPA wapewe msisitizo juu ya umuhimu wa kuzingatia majukumu yao.

Amesema kuna umuhimu wa kudhibiti watafiti na tafiti ili kulinda taarifa muhimu za vinasaba vya wanyamapori (Genetic information) dhidi ya mataifa mengine. “TUME inashauri maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ianzishe kitengo cha Sayansi Jinai na Uchunguzi wa Vinasaba vya Wanyamapori (DNA Forensic Wildlife Laboratory) ili Serikali na vyombo vyake iweze kufanya maamuzi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata ushahidi wa kimahakama katika kesi za jinai zinazohusu wanyamapori (Expert Witness).

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kusomewa ripoti huyo, Waziri Mkuu aliishukuru timu ya uchunguzi iliyokuwa chini ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kazi iliyoifanya ikiwemo kuainisha udhaifu uliokuwemo ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake.

“Ofisi yangu itaipitia taarifa hii ambayo ni kubwa kiasi na kuifanyia kazi. Matokeo ya kazi hiyo, tutayatoa hivi karibuni ili kuonyesha Serikali imeamua kufanya nini juu ya mapendekezo yaliyotolewa.”

Alimtaka Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Bw. Robert Mande, afuatilie mapendekezo yaliyoainishwa na tume hiyo na wayafanyie kazi mapema iwezekanavyo.

Waziri Mkuu aliiunda tume hiyo Desemba 10, mwaka jana baada ya kupokea pembe mbili za faru John na taarifa yenye nyaraka zilizotumika kumhamisha faru huyo. Hatua hiyo ilifuatia agizo alolitoa Desemba 6, 2016, akiwa ziarani mkoani Arusha, ambapo alitoa siku mbili na kuutaka uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), umletee nyaraka zote zilizotumika kumhamisha faru John kutoka kwenye hifadhi hiyo.


Alitoa agizo hilo alipotembelea ofisi za makao makuu ya NCAA zilizoko wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha na kuzungumza na watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafugaji ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.
Read More

MAJALIWA APOKEA TAARIFA YA TUME YA FARU JOHN

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Mkemia Mkuu wa Serikali , Profesa Samwel Manyele wakati  alipowasilisha taarifa ya tume ya uchunguzi wa suala Faru John baada ya kukabidhi taarifa hiyo , Ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam Machi27, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya kukabidhiwa taarifa ya tume ya kuchunguza suala la Faru John na Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele, Ofisini kwake jijini Dar es salam Machi 27, 2017.



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea  kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele  taarifa ya Tume aliyoiunda ya kuchunguza suala la Faru John, ofisini kwake jijjini Dar es salaam Machi 27, 2017.

Read More

Friday, March 24, 2017

MAJALIWA: TANZANIA INAUTASHI WA DHATI KUBORESHA MAZINGIRA YA UWEKEZANI NA BIASHARA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli inautashi wa dhati wa kuboresha mazingira ya uwekezani na biashara nchini kwa kuondoa rushwa na urasimu katika sekta ya umma, hivyo amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Mauritius kuja nchini.

Amesema Tanzania imefanya mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa kubadili mifumo yake ya kisheria, kitaasisi na kifedha ili kuhakikisha wawekezaji wanahudumiwa ipasavyo na kupewa umuhimu wanaostahili kwani ni wadau muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Waziri Mkuu amesema hayo jana (Alhamisi, Machi 23,2017) wakati akifungua  kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Mauritius lilifanyika katika Hotel ya Labourdonnaise mjini  Port Louis nchini Mauritius. Kongamano hilo  liliandaliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Alisema Tanzania ina uchumi imara unaofuata misingi ya soko huria, ambapo mwekezaji ana uhuru wa kufanya biashara bila ya kuingiliwa na Serikali, hivyo sekta binafsi imepewa kipaumbele katika shughuli za kiuchumi na kibiashara nchini.

“Kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli nawakaribisha  kwa mikono miwili kuja na kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali zikiwemo za viwanda na utalii na kutembelea vivutio vya utalii na kupata burudani ya aina yake na kwa wafanyabiashara Tanzania ni mahali pazuri kwa kuwekeza,” alisema.

Alisema TIC na Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar kwa pamoja vimeweka taratibu ambazo zinamwezesha mwekezaji kupata mahitaji yake muhimu ya kuwekeza katika kituo kimoja (One stop Centre).

Alibainisha baadhi ya mahitaji hayo kuwa ni huduma za kusajili kampuni, kodi, uhamiaji, leseni za biashara, ardhi pamoja na masuala mbalimbali yanayohusu uwekezaji. Hali ambayo inachangia Tanzania kupata wawekezaji wengi kutoka ndani na nje.

Waziri Mkuu alisema wawekezaji wanaokuja kuwekeza Tanzania wanatoka katika mataifa mbalimbali kama Marekani, Canada, Afrika Kusini, Kenya, Autsralia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na hivi karibuni wanatarajia wawekezaji kutoka nchini Mauritius.

“Ujio wa wawekezaji hawa haukuwa wa bahati bali ni kutokana na mazingira mazuri yaliyowekwa na Serikali pamoja na  suala zima la soko kubwa la bidhaa zao na huduma. Soko hili linalozidi watu milioni 300 katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika linatoa uhakika wa soko kubwa kwa mwekezaji yeyote anayekuja Tanzania kuwekeza,”.

“Kuwekeza nchini Tanzania kunampa fursa mwekezaji kupata fursa maalumu kupitia Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) na ile ya Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na soko la nchi ambazo hazipakani na bahari. Nchi ambazo Tanzania ina mahusiano nazo mazuri ya kibiashara ni Rwanda, Burundi, Uganda, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Zambia.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa katika kuheshimu wawekezaji Tanzania  imesaini mikataba mbalimbali inayolenga kuwalinda popote walipo kama Multilateral Investment Guarantee Agency (MIGA) na Africa Trade Insurance Agency.

Alisema Tanzania mbali ya hali ya amani na utulivu wa kisiasa, pia imebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali asilia ambazo zinatoa fursa nzuri kwa mwekezaji. “Hii ni pamoja na ardhi yenye rutuba nzuri kwa kilimo, madini ya kila aina kuanzia dhahabu, almasi, makaa ya mawe, tanzanites, chuma na gesi asilia,”.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na Waziri Mkuu wa Mauritius Mheshimiwa Pravind Kumar Jugnauth, Prime Minister of the Republic of Mauritius; Waziri wa Mambo ya Nje wa Mauritius Bw. Seetanah Lutchmeenaaraidoo, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohammed, Balozi wa Heshma wa Tanzania nchini Mauriutius Bw. Cliford Tandali.


Wengine ni Mwenyekiti wa ‪Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Godfrey Simbeye,, Executive Director of Tanzania Investiment Centre; ‪Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Bw. Clifford Tandar pamoja na Maofisa wa Serikali ya Tanzania na Mauritus
Read More

Thursday, March 23, 2017

MAJALIWA AFUNGUA MKUTANO WA UWEKEZAJI NCHINI- PORT LOUIS MAURITIUS

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Waziri Mkuu wa Mauritius, Bw. Pravind Kumar Jugnauth katika mkutano wa Uwekezaji na Biashara kati ya Tanzania na Mauritius kabla ya kufungua mkutano huo mjini Port Louis, Machi 23, 2017.
 Waziri Mkuu wa Mauritius, Bw. Pravind  Kumar Jugnauth akizungumza katika mkutano wa Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Mauritius mjini Port Louis Machi 23, 2017.
 Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Biashara na Uwekezaji  kati ya Tanzania na Mauritius wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua  mkutano huo mjini Port  Louis  Machi 23, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akifungua mkutano wa Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Mauritius mjini Port Louis nchini Mauritius , Machi 23, 2017. 
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Biashara na Uwekezaji  kati ya Tanzania na Mauritius wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua  mkutano huo mjini Port  Louis  Machi 23, 2017.



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na Waziri Mkuu wa Mauritius, Bw. Pravind Kumar Jugnauth baada ya kufungua mkutano wa Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Mauritius mjini Port Louis Machi 23, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na Waziri Mkuu wa Mauritius, Bw. Pravind Kumar Jugnauth baada ya kufungua mkutano wa Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Mauritius mjini Port Louis Machi 23, 2017.




Read More

Wednesday, March 22, 2017

WAZIRI MKUU AHAMASISHA WAWEKEZAJI KUJA NCHINI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea kiwanda cha kusindika samaki aina ya jodari na kuwakaribisha viongozi wa kiwanda hicho kuja nchini kuangalia maeneo ya uwekezaji wa viwanda vya samaki.

Amesema Serikali imeweka sera nzuri za uwekezaji na pia ina maeneo mengi na mazuri kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vya samaki, ambayo ni bahari, mito na maziwa ambayo aina mbalimbali za samaki.

Waziri Mkuu amesema hayo jana jioni (Jumanne, Machi 21,2017) wakati alipotembelea kiwanda cha samaki cha Mer des Mascareignes kilichoko  jijini Port Louis nchini Mauritius.

“Tanzania kuna fursa nyingi za uwekezaji hasa kutokana na mazingira yake. Mnaweza kuja kuwekeza kwenye viwanda vya usindikaji wa samaki tuna bahari, mito na maziwa yenye samaki wa aina mbalimbali,” alisema.

Waziri Mkuu alisema Serikali imedhamiria kuimarisha uchumi wake kupitia sekta ya viwanda ili kuongezatija kwa Taifa na kwa wananchi kiujumla hivyo wanahitaji wawekezaji waliotayari kuja kuwekeza nchini.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohammed alisemaTanzania inahitaji wawekezaji watakaowekeza kwenye uvuvi wa kina kirefu na ujenzi wa viwanda vya samaki.

Dkt. Khalid alisema lengo la uwekezaji huo ni kukuza uchumi wa Taifa pamoja kupanua soko la ajira na kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake.

Naye Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Bw. Patrick Hill alisema wamefurahi na mualiko wa kuja Tanzania kwa ajili ya kuangalia fursa na uwekezaji na kwamba wako tayari kushirikiana na Serikali.

Alisema kampuni yao inajishughulisha na usindikaji wa samaki aina moja tu ya jodari na wananunua kutoka kwa makampuni makubwa ya uvuvi huku wateja wao wakubwa wakiwa ni bara la Ulaya.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alitembelea kiwanda kingine cha  Chantier Naval Del`Ocean Indien Limited (CNOI) ambacho kinatengeneza na kukarabati meli , boti na pantoni na kujionea uwezo mkubwa walionao, ambapo Watanzania wanaweza kuja kujifunza.
Read More