Wednesday, October 31, 2018

TRAFIKI WAOMBA RUSHWA WASHTAKIWA KWA WAZIRI MKUU


*Waziri Mkuu akabidhi majina hayo kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga kwa hatua

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigela orodha ya matrafiki wanaodaiwa kuwaomba rushwa madereva wa noah wilayani Lushoto.

Majina ya trafiki hao wanadaiwa kuomba rushwa kwa madereva wa noah wanaofanya kazi ya kusafirisha abiria ndani ya wilaya hiyo yaliwasilishwa kwa Waziri Mkuu kupitia mabango.

Waziri Mkuu alimkabidhi majina hayo jana jioni (Jumatano, Oktoba 31, 2018) baada ya kumaliza kuhutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Sabasaba, Lushoto mjini.

Baada ya kumkabidhi majina hayo alimuagiza afanye uchunguzi wa tuhuma za rushwa zinazowakabili askari hao na kisha awasilishe taarifa kwake leo Alhamisi Novemba 1, 2018.

Mbali ya wananchi kuwasilisha malalamiko hayo, Pia mbunge wa Lushoto, Shaaban Shekilindi alimuomba Waziri Mkuu awasaidie kutatua kero hiyo inayowakabili wananchi.

Awali, Waziri Mkuu alizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Lushoto katika ukumbi wa chuo cha Mahakama Lushoto ambapo aliwasisitiza wafanye kazi kwa bidii.

Alisema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli haina msamaha na mtumishi wa umma asiyetaka kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia weledi.

Alisema watumishi wa umma wanatakiwa kufanya kazi kwa kufuata maadili ya utumishi ili waweze kutimiza lengo la Serikali la kuwahudumia wananchi kwa kutumia taaluma zao.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi mkoani Tanga alisema Serikali haina msamaha na mtumishi asietaka kubadilika na kufanya kazi.

Pia, Waziri Mkuu aliwataka watumishi wa umma wahakikishe fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo zinatumika kama ilivyokusudiwa.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwataka Wakuu wa Idara kutumia kitabu cha ilani ya uchaguzi cha CCM cha mwaka 2015/2020 kwa sababu kina maelekezo wanayopaswa kuyatekeleza.

“Kitabu kile kina maelezo ya msingi yaliyotolewa na Rais. Dkt. Magufuli ambayo yanatakiwa yapewe kipaumbele cha utekelezwaji, wakuu wa Idara ni muhimu musome na kutekeleza.”

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwataka wakuu wa wilaya wahakikishe wanasimamia utekelezwaji wa maelekezo yote yaliyoainishwa kwenye kitabu cha Ilani katika maeneo yao.

Kuhusu changamoto ya upungufu wa watumishi wa kada mbalimbali nchini, Waziri Mkuu alisema Serikali inatambua na kwamba suala hilo linaendelea kufanyiwa kazi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Sabasaba na kuwapongeza wakazi hao kwa kutunza misitu.

Alisema maeneo mengi nchini wananchi wamekata miti na kusababisha kukauka kwa vyanzo vya maji, ambapo ni tofauti na wilaya ya Lushoto ambayo bado ina misitu minene.

Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu aliwaagiza watendaji wote wa vijiji na kata waainishe sehemu  zote zenye misitu na vyanzo vya maji katika maeneo yao na wahakikishe wanayalinda.

Alisema mtu yeyote atakayebainika kuharibu mazingira hayo iwe kwa kuchoma au kukata miti achukulie hatua kali. “Ni marufuku mtu yeyote kukata miti bila kibali cha Serikali.”

Nae, Mbunge wa Lushoto Shekilindi alimuomba Waziri Mkuu awasaidie katika kuwatatulia changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa katika jimbo hilo ikiwemo ya afya.

Mbunge alisema kwa sasa hospitali ya wilaya hiyo inakabiliwa na ukosefu wa mashine ya x
rey, hivyo kusababisha wananchi kusafiri hadi Korogwe au Tanga kufuata huduama hiyo.

Waziri Mkuu alisema tayari ameshamuagiza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu kupeleka mashine ya x-rey katika hospitali hiyo.


 (mwisho)

Read More

SERIKALI IMEDHAMIRIA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA-MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuboresha huduma za afya kwenye maeneo mbalimbali nchini yakiwemo ya halmashauri ya wilaya ya Lushoto.

Amesema lengo ni kuhakikisha kila kata inakuwa na kituo cha afya chenye uwezo wa kutoa huduma mbalimbali muhimu zikiwemo za maabara, upasuaji na mama na mtoto.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Oktoba 31, 2018) wakati akizungumza na wakananchi katika kata ya Malindi, baada ya kutembelea jengo la soko mbogamboga la Malindi.

Waziri Mkuu amesema Serikali imejipanga vizuri katika sekta ya afya baada ya bajeti ya kununulia dawa kuongezeka kutoka sh. bilioni 31 kwa mwaka na kufikia bilioni 269.

“Hatutaki tena kusikia mgonjwa anaenda hospitali na kukosa dawa biashara hiyo tumeimaliza, Rais Dkt. John Magufuli ametoa fedha nyingi kwa ajili ya ununuzi wa dawa.”

Amesema katika wilaya ya Lushoto Serikali imetenga sh. bilioni 1.4 kwa ajili ujenzi na ukarabati wa majengo ya vituo vya afya vya kata za Kangagai. Mnazi na Mlola.

“Halmashauri wekeni mpango thabiti wa kujenga wodi mbili kati yake moja ya wanaume na nyingine ya wanawake, lengo la Serikali ni kuboresha huduma za afya kwa wananchi.”

Aizungumzia kuhusu mradi wa ujenzi wa soko, Waziri Mkuu amesema mradi huo ni sehemu ya huduma zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kuboresha huduma za jamii nchini.

Waziri Mkuu ametaja huduma nyingine zinazotolewa na Serikali kwa wananchi ni za afya, elimu, maji, uchumi na ujenzi na uboreshwaji miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara.

Hivyo, amewataka wananchi watumie vizuri soko hilo  ambalo linatoa fursa kwao kufanya biashara katika eneo zuri na kuwawezesha kuuza bidhaa zao zikiwa katika ubora.

Pia amewashauri wakulima hao wajiunge katika vikundi na kuanzisha ushirika wao ili waweze kusaidiwa na Serikali katika kupata mikopo kwa ajili ya kuzalisha kwa ubora zaidi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Lushoto, Bibi Ikupa Mwasyoge amesema kukamilika kwa soko hilo kutainufaisha halmashauri na wananchi.

Bibi. Ikupa amesema ujenzi wa jengo hilo la soko la ghorofa mbili lililojengwa kwa awamu mbili ulianza mwaka 2011 na umekamilika Septemba 2018, umegharimu sh. bilioni 1.1.

Amesema halmashauri itanufaika kwa kupata ushuru na wananchi ambao wengi wao ni wakulima wa mboga na matunda watakuwa na sehemu ya uhakika wa kufanyia biashara.

“Wakulima 35,000 wa kata ya Malindi na kata jirani za Lukozi, Manolo na Shume wanaozalisha wastani wa tani 5,900 za mboga na matunda kwa mwaka watanufaika.”

Naye, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema Serikali imefanya kazi kubwa katika kuboresha huduma za afya nchini.

Amesema bajeti ya dawa katika halmashauri hiyo imeongezeka kutoka sh milioni 183 za dawa zilizokuwa zinatolewa awani na sasa imefikia sh milioni 565.

Mbunge wa jimbo la Mlalo, Bw. Rashid Shangazi ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa kuwasaidia wananchi wa halmashauri kuongeza thamani ya mazao yao kabla ya kuuza.

Awali,Waziri Mkuu alizindua jengo la utawala la Halmashauri ya wilaya ya Lushoto lililogharimu sh. bilioni 4.3. Kukamilika kwa jengo hilo kutaboresha huduma kwa wananchi.

 (mwisho)
Read More

ZIARA YA MAJALIWA WILAYANI LUSHOTO

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati alipozindua Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto  akiwa katika ziara ya Mkoa wa Tanga Oktoba 31, 2018. Kulia ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na wapili kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba. Wapili kulia ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Tanga, Henry Shekifu, watatu kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela. na kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Lushoto, Ikupa Harrison Mwasyoge.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akimsikiliza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Ikupa Harrison Mwasyoge wakati alipotembelea ofisi mpya za Halmshauri hiyo baada ya kuzindua jengo la utawala, Oktoba 31, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Soko la Kisasa la mbogamboga na matunda linalojengwa na Serikali katika kijiji cha Malindi wilayani Lushoto, Oktoba 31, 2018. Alikuwa katika ziara ya Mkoa wa Tanga.  Wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi wa kijiji cha Lukozi wilayani Lushoto wakati alipowasili kijijini hapo akiwa katika ziara ya Mkoa wa Tanga, Oktoba 31, 2018. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi wa kijiji cha Lukozi katika Jimbo la Mlalo wilayani Lushoto akiwa katika ziara ya Mkoa wa Tanga,  Oktoba 31, 2018.

Read More

Tuesday, October 30, 2018

KIKOSI KAZI CHA KITAIFA CHA MPANGO WA SERIKALI KUHAMIA DODOMA CHATEMBELEA UWANJA WA NDEGE WA DODOMA

Katibu wa Kikosi kazi cha Kitaifa cha kuratibu Mpango wa Serikali kuhamia Dodoma Bw.Meshach Bandawe akiuliza jambo kwa Kaimu Meneja wa Uwanja wa Ndege Dodoma Bi.Bertha Bankwa walipotembelea kukagua hali ya upanuzi na ukarabati wa baadhi ya maeneo ikiwa ni sehemu ya kuboresha huduma za usafiri kwa wananchi ,Oktoba 29, 2018.

Katibu wa Kikosi kazi cha Kitaifa cha kuratibu Mpango wa Serikali kuhamia Dodoma Bw.Meshach Bandawe akizungumza jambo na Msimamizi wa Mradi wa ukarabati wa baadhi ya maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Dodoma Kutoka NHC Bw.Hassan Bendera walipotembelea kuangalia ukarabati huo, Oktoba 29, 2018.

Kaimu Meneja wa Uwanja wa Ndege Dodoma Bi.Bertha Bankwa akitoa maelezo kuhusu ukarabati  unaoendelea katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma kwa kikosi kazi cha kuratibu mpango wa  Serikali kuhamia Dodoma walipotembelea Oktoba 29, 2018.

Katibu wa Kikosi kazi cha Kitaifa cha kuratibu Mpango wa Serikali kuhamia Dodoma Bw.Meshach Bandawe akionesha nyumba zilizovunjwa kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege Dodoma wakati walipotembelea kuona hali halisi ya kazi ya upanuzi wa eneo hilo inavyoendelea.
Katibu wa Kikosi kazi cha Kitaifa cha kuratibu Mpango wa Serikali kuhamia Dodoma Bw.Meshach Bandawe (wa kwanza kushoto) akizungumza jambo na Msimamizi wa Mradi wa kukarabati baadhi ya maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Dodoma  Kutoka NHC Bw.Hassan Bendera wakati wa ziara hiyo.


Kaimu Meneja wa Uwanja wa Ndege Dodoma Bi.Bertha Bankwa akitoa maelezo kuhusu upanuzi wa sehemu ya Ukumbi wa abiria wanaoondoka(departure waiting Lounge) kwa Katibu wa Kikosi kazi cha Kitaifa cha kuratibu Mpango wa Serikali kuhamia Dodoma Bw.Meshach Bandawe walipotembelea ili kuona kazi za upanuzi zinavyoendelea uwanjani hapo.

Muonekano wa baadhi ya nyumba zilizobomolewa katika eneo la Uwanja wa ndege Dodoma ili kupisha zoezi la upanuzi wa uwanja wa ndege huo.
Mhandisi wa Uwanja wa Ndege wa Dodoma, Dickson Mmbando akitoa ufafanuzi kwa Katibu wa Kikosi kazi cha Kitaifa cha kuratibu Mpango wa Serikali kuhamia Dodoma Bw.Meshach Bandawe walipotembelea kukagua upanuzi wa baadhi ya maeneo katika Uwanja huo.


Read More

NIMERIDHISHWA NA HATUA ZA AWALI ZA UWEKEZAJI MKINGA-MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea eneo la mradi wa ujenzi wa viwanda 11 katika kijiji cha Mtimbwani wilayani Mkinga, ambapo amesema ameridhishwa na hatua za awali za uwekezaji huo.

Katika eneo hilo vinatarajiwa kujengwa viwanda mbalimbali kikiwemo cha saruji cha Hengya, kiwanda cha vioo, kiwanda cha vifaa vya kisasa vya ujenzi, uzalishaji wa umeme kwa kutumia makaa ya mawe.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Oktoba 30, 2018) wakati akizungumza na wananchi katika kijiji cha Mtimbwani wilayani Mkinga akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Tanga.

Amesema uwekezaji huo unatarajiwa kulinufaisha Taifa na wananchi wakazi wa wilaya ya Mkinga kwa kuwa kinatarajiwa kuajiri zaidi ya watu 8,000, hivyo amewaomba wananchi hao waendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji hao.

Kuhusu wananchi ambao eneo lao limechukuliwa na wawekezaji na bado hawajalipwa fidia Waziri Mkuu amewataka wawe na subira kwa kuwa wote watalipwa. “Muwekezaji amenihakikishia kwamba atawalipa wananchi wote wanaodai fidia.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuuamewataka watumishi wa umma kutenga siku tatu katika wiki na kuwafuata wananchi waishio maeneo ya vijijini kwa ajili ya kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi.

Amesema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kuwatumikia wananchi bila ya ubaguzi wa kidini, kisiasa, rangi  na kimapato, hivyo amewataka watumishi hao wafanye kazi kwa bidii.

Awali, Mbunge wa jimbo la Mkinga, Dastan Kitandula ameishukuru Serikali kwa niaba ya wananchi wa Mkinga baada ya Serikali kufuta hati ya shamba la moa na kuirudisha ardhi hiyo kwa wananchi, pia ameomba ifute hayi za mashamba mengine yaliyotekelezwa katika Tarafa ya Maramba.

 (mwisho)
Read More

WAZIRI MKUU AAGIZA ENEO LA KIOMONI LITATHMINIWE


*Ni baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya kutoridhishwa na fidia

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atamuagiza Mthamini Mkuu wa Serikali Bibi. Evelyne Mugasha kwenda katika Kata ya Kiomoni kufanya tathmini ya ardhi ya wananchi ili kubaini thamani halisi ya maeneo hayo ili wananchi waweze kufidiwa.

Hatua hiyo inakuja baada ya wananchi hao kumlalamikia Waziri Mkuu kuhusu kutoridhishwa na fidia ya maeneo yao yaliyochukuliwa na kampuni ya Neelkanth inayomiliki kiwanda hicho cha kuzalisha chokaa.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana jioni (Jumanne, Oktoba 30, 2018) wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Kiomoni katika mtaa wa Kiomoni wilayani Tanga akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Tanga.

Alisema atamtuma Mthamini Mkuu aende kubaini nani anadai nini na anamiliki nini ili atoe kibali cha ulipwaji ili muwekezaji aweze kupewa kibali cha kuwalipa fidia yao.”Tunataka jambo hili liishe kabla ya mwishoni mwa mwaka huu kila kitu kiwe kimekamilika na hakuna mwananchi hata mmoja atakayepoteza haki yake ya msingi.”

Waziri Mkuu aliongeza kuwa uwekezaji huo ni muhimu kwa kuwa ni sehemu ambayo viwanda mbalimbali vya saruji nchini vinategemea kwa kupata malighafi, hivyo alimpongeza muwekezaji na kumshauri aongeze uzalishaji kadiri anavyoweza.

Alisema wawekezaji katika sekta ya viwanda ni muhimu kwa sababu wanaunga mkono mkakati wa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ya kukuza uchumi kutoka wa chini hadi wa kati ifikapo 2025 kwa kupitia sekta ya viwanda.

Alisema fursa ya uwepo wa kiwanda hicho utawezesha kukuza uchumi Taifa na wananchi kwa ujumla kwa sababu kiwanda kitakapokamilika kitatoa ajira ya watu zaidi ya 2,000 wakiwemo wakazi wa eneo hilo.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Bw. Thobias Mwilapwa Mkinga leo (Jumatano, Oktoba 31, 2018) akutane na wananchi wa kijiji hiko na kusikiza kero mbalimbali zinazowakabili na kushirikiana nao katika kuzipatia ufumbuzi.

Waziri Mkuu alisema Serikali imeelekeza nguvu kubwa katika kuwatumikia wananchi na kutatua kero zao, hivyo itasimamia kuhakikisha kila mtumishi anawajibika kwa kiwango kinachostahili, ambapo aliwataka viongozi wa wilaya hiyo kwenda kwa wananchi.

“Watendaji hamuendi kuwatembelea wananchi na kusikiliza matatizo yao, haiwezekana wawe wanawasubiri viongozi wa juu na kuwasilisha kero zao, sasa jipangeni haya mabango yote mtakuja kuyajibu kwa sababu hoja zote ni za ngazi ya halmashauri,” alisema.


(mwisho)
Read More

MAJALIWA AWASILI TANGA KWA ZIARA YA KAZI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Tanga, Henry Shekifu wakati alipowasili kwenye uwanja wa Ndege wa Tanga kuanza ziara  ya kazi mkoani humo, Oktoba 30, 2018. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela wakati alipowasili kwenye uwanja wa Ndege wa Tanga kuanza  ziara ya  kazi mkoani humo Oktoba 30, 2018. 

Read More

Saturday, October 27, 2018

TUTAENDELEA KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI-MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inathamini uwepo wa sekta binafsi nchini na kwamba inaendelea kushirikiana nayo katika kuboresha maendeleo ya Taifa.

Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Oktoba 27, 2018) wakati alipokutana na bodi mpya ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania kwenye makazi wa Waziri Mkuu, jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu ampongeza Mwenyekiti wa taasisi hiyo Bw. Salum Shamte na wajumbe wa bodi hiyo kwa kuchaguliwa kuingoza taasisi hiyo. Bodi hiyo mpya ilikwenda kujitambulisha.

“Serikali inadhamira ya dhati ya kushirikiana na taasisi hii kwa sababu ndio muwezeshaji wa kuifanya Tanzania kufikia uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda ifikapo 2025,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa taasisi hiyo Bw. Shamte amesema sekta binafsi inatambua juhudi za Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara nchini Tanzania.

“Sisi tupo tayari kushirikiana na Serikali kwa kuwabana wafanyabiashara ambao wanaenda kinyume na maadili na sheria, ila tunaomba Serikali ishirikiane nasi katika utekelezaji wake.”

Pia, Bw. Shamte ameiomba Serikali iendelee kutoa vivutio kwa biashara zinazoanza ili kuhamasisha uwekezaji kwa kuwa baadhi yake zimeonesha gharama kubwa za uzalishaji.

(mwisho)
Read More

MAJALIWA AKUTANA NA BODI YA TAASISI YA SEKTA BINAFSI TANZANIA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wajumbe wa Bodi Mpya ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kwenye Makazi ya Waziri Mkuu jijini Dsr es salaam Oktoba 27, 2018.  Kushoto kwake ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Profesa Faustin Kamuzora na kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Salum Shamte.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi Mpya ya Taasisi  ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) baada ya mazungumzo kwenye Makazi ya Waziri Mkuu, jijini Dar es salaam, Oktoba 27, 2018. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Profesa Faustin  Kamuzora  na kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Salum Shamte.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na Mwenyekiti wa Bodi Mpya ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Salum Shamte  baada ya kukutana na wajumbe wa Bodi hiyo kwenye Makazi ya Waziri Mkuu jijini Dar es salaam, Oktoba 27, 2018.

Read More

Friday, October 26, 2018

PROF.KAMUZORA: JAMII INAPASWA KUTOKOMEZA MILA NA DESTURI ZINAZOWAKANDAMIZA WANAWAKE NA WATOTO NCHINI.

NA MWANDISHI WETU
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera na Uratibu Prof.Faustin Kamuzora ameiasa jamii kutokomeza mila na desturi potofu zinazokwamisha maendeleo ya wanawake na watoto sambamba na kuwapatia fursa ya kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Wito huo ameutoa Oktoba 26, 2018 wakati akifungua mkutano wa Kamati Elekezi ya Taifa ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto uliohusisha Wizara 11 pamoja na wadau mbalimbali wa masuala ya wanawake na watoto nchini walipokutana mkoani Morogoro kujadili na kupitia Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto.
“Jamii inapaswa kuwa mstari wa mbele katika kupinga mila na desturi potofu zinazokandamiza makundi haya na badala yake kutumia muda mwingi katika kuzalisha mali na kujishughulisha katika masuala ya maendeleo ili kuondokana na umasikini na kujiletea maendeleo”.alisema Kamuzora
Aidha Kamuzora aliongezea kuwa, jamii inapaswa kuendelea kusaidia jitihada za Serikali katika kutokomeza mila na desturi potofu kwa kuunga mkono mipango mikakati iliyopo na kuendelea kutoa elimu kwa umma juu ya masuala ya Haki na Usawa katika jamii.
“Tujitathimini na kuona namna bora ya kuondokana na mila na desturi zote zinazomkandamiza wanamke na mtoto ili kuendelea kusimamia zile zinazoiwezesha jamii kuwa na usawa na haki katika makundi yote bila kuwa na ubaguzi”
Naye Mkurugenzi wa Sera na Mipango Idara ya Maendeleo ya Jamii Bw.Atupele Mwambene alieleza kuwa, Serikali imejikita kuhakikisha inamaliza changamoto za wanawake na watoto kwa kuhakikisha Mpango Kazi huo unawawezesha katika maeneo nane ya kipaumbele ikiwemo; kutokomeza mila na desturi zilizopitwa na wakati, Uwezeshaji wa uchumi wa Kaya, kuhakikisha mazingira salama hususan mazingira ya umma na kuwa na malezi bora kuanzia ngazi ya familia.
Aliongezea kuwa Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa maendelea, hususan wanaoshirikiana katika masuala ya watoto na wanawake itaendelea kushirikiana ili kuwa na nguvu ya pamoja na kuhakikisha jamii inakuwa sehemu salama kwa makundi yote.
“Tumekutana pamoja ili kuhakikisha tunahuisha nguvu kwa pamoja ili kuhakikisha mila na desturi zinazochochea ukatili dhidi ya makundi haya unatokomezwa kwa kuwa na mipango inayotekelezeka.
Naye Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.John Njingu alieleza kuwa, jamii inapaswa kubadili mitazamo katika kupashana habari na kuvitumia vyombo vya habari kama nafasi pekee yenye mchango mkubwa katika kuifikia jamii kupitia elimu kwa umma juu ya utokomezaji wa vitendo vya ukatili katika makundi haya.
“watumiaji wa vyombo vya habari wawajibike na kuhakikisha taarifa zinazotolewa katika jamii zisiwe zenye athari kwa watoto na wanawake badala yake tutumia vyombo vya habari kwa matumizi yenye tija katika jamii zetu”.alisisitiza Dkt.Njingu
AWALI
Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) unatarajiwa kuwezesha na kuondoa ukatili dhidi ya wanawake kwa asilimia 50 kufikia mwaka 2022; na kuondoa ukatili dhidi ya watoto kwa asilimia 50 kufikia mwaka huo, na hivyo kuleta mabadiliko makubwa kwa kuwa na familia salama, na jamii yenye utulivu.Katika kufikia malengo mpango unaelekeza nafasi ya kila mdau kuanzia ngazi ya familia, jamii, halmashauri, Mikoa, Wizara, SektaBbinafsi, Asasi za Kiraia na wabia wa maendeleo Mpango umeweka mfumo fungamanishi wa uratibu, ufuatiliaji na tathmini ambao utaratibiwa katika ngazi ya Taifa na Ofisi ya Waziri Mkuu, ngazi ya mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa, na ngazi ya Halmashauri na Wakurugenzi Watendaji.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt.Laurean Ndumbaro akizungumza wakati wa kikao cha Kamati elekezi ya Taifa ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto kwa ajili ya kujadili Utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto kilichofanyika Mkoani Morogoro Oktoba 26, 2018 kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw.Amoni Mpanju.
Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Afya (Maendeleo ya jamii) Bw.Mwambene Atupele akichangia jambo wakati wa kikao hicho.
Mkurugenzi Msaidizi (Mipango na Tafiti) kutoka Wizara ya Viwanda Bi.Zaytun Bagholleh akifafanua jambo wakati wa kikao kazi hicho.
Mjumbe kutoka UNICEF Bi.Maud Droogleever akichangia jambo kuhusu ushirikishwaji wa Taasisi zisizokuwa za Kiserikali katika mapambano dhidi ya Utatili wa wanawake na watoto wakati wa kikao kazi hicho.


Mratibu wa Taifa wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bi.Happiness Mugyabuso pamoja na Mratibu wa MTAKUWWA Bw.Seto Ojwando wakifuatilia uwasilishwaji wa mada wakati wa kiako kazi hicho.
Sehemu ya wajumbe wa kikao wakifuatilia mada zinazowasilishwa wakati wa kikao kazi hicho.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw.Amoni Mpanju akichangia hoja ya masuala ya sheria za watoto wakati wa kikao kazi hicho.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Prof.Faustin Kamuzora akizungumza na waandishi wa habari kuhusu jitihada za Serikali katika kuhakikisha inatokomeza changamoto za ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto Nchini mara baada ya ufunguzi wa kikao kazi hicho.



Read More

SERIKALI YAITAKA WIZARA YA KILIMO IJITATHMINI


*Yaagiza Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Koroshokurudishwa wizarani


RAIS Dkt. John Magufuli ameitaka Wizara ya Kilimo ijitathmini kutokana na suala la mauzo ya zao la korosho linavyoendelea pamoja na utendaji wa Bodi ya Korosho Tanzania.

Pia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo kumrudisha wizarani Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Prof. Wakuru Magigi baada ya kutoridhishwa na utendaji wake.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Oktoba 26, 2018) katika kikao chake na wakuu wa mkoa ya inayolima korosho kilichofanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.

“Haturidhishwi na utendaji wa bodi ambao amekiuka maelekezo ya msingi ya Serikali katika kusimamia mfumo mzima wa zao la korosho uliopelekea kuvurugika kwa minada.”

Kutokana na hali hiyo Waziri Mkuu amesema Serikali imesitisha minada yote ya korosho nchini kuanzia leo na kuwataka wakulima wawe watulivu wakati ikishughulikia suala hilo.

Kiongozi huyo wa Bodi ya Korosho analalamikiwa kwa kufanya kazi bila ya kushirikisha ushirika wa zao hilo na kutotambua mamlaka zilizowekwa kisheria kama mkuu wa mkoa.

Mbali na malalamiko hayo pia anadaiwa kuendesha operesheni kwa kutumia silaha na askari  dhidi ya viongozi wa ushirika kinyume cha taratibu za nchi. 

Hivyo, Waziri Mkuu amemuagiza Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Lindi na wa  Mtwara wahakikishe gari lenye namba T 814 DDM pamoja na dereva wake linatafutwa popote.

Waziri Mkuu amesema gari hilo ndilo linalodaiwa kutumika katika kuwakamata viongozi wa ushirika waliokuwa wanawasimamia wananchi waliokataa kuuza korosho kwa bei ndogo.

Amesema baada ya dereva wa gari hilo kukamatwa ahojiwe na aeleze askari hao alikuwa anawatoa wapi na nani aliyemtuma. Ameagiza askari wote waliohusika watafutwe.

“Bodi imekuwa ikiwatisha na kuwalazimisha wakulima na viongozi wa ushirika kukubali kuuza korosho kwa bei ya chini jambo ambalo Serikali haiwezi kulikubali.”

Waziri Mkuu amesema Serikali haiwezi kulifumbia macho suala hilo kwa sababu limekuwa likiipaka matope kwani mkurugenzi huyo alikuwa anaingiza askari katika mikoa hiyo bila ya mamlaka kuwa na taarifa.

Kadhalika Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Kilimo kutokaa kimya pindi zinapotokea changamoto kama hizo na badala yake watoe taarifa mapema. “Mambo kama haya yanatokea alafu wizara mmekaa kimya tu.” 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli anawapongeza wakulima wa korosho kwa uamuzi wao wa kukataa kuuza kwa bei ndogo na kwamba yuko pamoja nao.

“Rais Dkt. Magufuli ameitaka Wizara ya Kilimo ijitathmini katika suala la mauzo ya zao la korosho linavyoendelea,” amesema Waziri Mkuu.

Pia Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli anataarifa kwamba kuna baadhi ya watendaji Serikalini wanatumia vibaya jina lake kwamba lazima wahusika wote watachukuliwa hatua. 

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Bw. Gelasius Byakanwa na Mkuu wa mkoa wa Lindi Bw. Godfrey Zambi walilalamikia kitendo cha Prof. Magigi kuvuruga mfumo wa uuzaji wa korosho.

Pia walisema licha ya kumshauri kiongozi huyo juu ya namna bora ya kuendesha minada ya uuzaji wa korosho hakuwasikiliza na kwamba hakuwa tayari kushirikiana nao na pia alikuwa akidharau mamlaka zao. 

Pia alikuwa akiingiza askari na kuwatisha na kukamata viongozi wa ushirika bila ya wao kujua jambo ambalo walisema limezua taharuki kwa watendaji wa ushirika.
Read More

MAJALIWA AKUTANA NA WAKUU WA MIKOA YA LINDI, MTWARA, PWANI NA RUVUMA NA VIONGOZI WA BODI YA KOROSHO KUJADILI BEI YA KOROSHO

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza  na  Wakuu wa Mikoa  ya Mtwara, Lindi, Pwani na Ruvuma  ambayo inalima  korosho na  imeanza kuuza zao hilo, wakuu  wa wilaya za mikoa hiyo, Wenyeviti  wa Vyama Vikuu vya Ushirika katika mikoa hiyo na Viongozi wa Juu wa Bodi ya Korosho Tanzania  kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Oktoba 26, 2018. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi na kushoto ni  aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Profesa Wakuru Magigi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na  Wakuu wa Mikoa  ya Lindi, Mtwara, Pwani na Ruvuma  ambao mikoa yao imeanza kuuza korosho, Wenyeviti wa Vyama Vikuu vya Ushirika na Watendaji Wakuu wa Bodi ya Korosho kwenye ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Oktoba 26, 2018. Kulia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba.
 Washirki wa Mkutano ulioitishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  uliowajumuisha Wakuu wa Mikoa  ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Pwani ambao mikoa yao imeanza kuuza korosho, Wenyeviti wa Vyama Vikuu vya Ushirika na Watendaji Wakuu wa Bodi ya Korosho wakimsikiliza Waziri Mkuu wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Oktoba 26, 2018.



Read More

MAJALIWA ASHIRIKI KATIKA TAMASHA LA UTAMADUNI WA MTANZANIA KWA JAMII YA WATU WA MKAO WA LINDI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mwadhama  Polycarp Kardinali Pengo wakati alipowasili kwenye kijiji cha Makumbusho jijini Dar es salaam kushiriki katika  Tamasha la Utamaduni wa Mtanzania kwa Jamii ya Watu wa Mkoa wa Lindi, Oktoba 26, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza  na Mwadhama  Polycarp Kardinali Pengo wakati alipowasili kwenye kijiji cha Makumbusho jijini Dar es salaam kushiriki katika  Tamasha la Utamaduni wa Mtanzania kwa Jamii ya Watu wa Mkoa wa Lindi, Oktoba 26, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa amekaa katika mazingira ya asili wakati aliposhiriki katika  Tamasha la Utamaduni wa Mtanzania kwa Jamii ya Watu wa Mkoa wa Lindi lililofanyika  kwenye kijiji cha Makumbusho jijini Dar es salaam, Oktoba 26, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama vyakaula vya asili wakati aliposhiriki katika Tamasha la Utamaduni wa Mtanzania  kwa Jamii ya Watu wa Mkoa wa Lindi  lililofanyika kwenye kijiji cha Makumbusho jijini Dar es salaam, Oktoba 26, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama vyakaula vya asili wakati aliposhiriki katika Tamasha la Utamaduni wa Mtanzania  kwa Jamii ya Watu wa Mkoa wa Lindi  lililofanyika kwenye kijiji cha Makumbusho jijini Dar es salaam, Oktoba 26, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipanda mti wa asili wakati aliposhiriki katika Tamasha la Utamaduni wa Mtanzania  kwa Jamii ya Watu wa Mkoa wa Lindi  lililofanyika kwenye kijiiji cha Makumbusho jijini Dar es salaam, Oktoba 26, 2018.

Read More