Friday, October 26, 2018

PROF.KAMUZORA: JAMII INAPASWA KUTOKOMEZA MILA NA DESTURI ZINAZOWAKANDAMIZA WANAWAKE NA WATOTO NCHINI.

NA MWANDISHI WETU
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera na Uratibu Prof.Faustin Kamuzora ameiasa jamii kutokomeza mila na desturi potofu zinazokwamisha maendeleo ya wanawake na watoto sambamba na kuwapatia fursa ya kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Wito huo ameutoa Oktoba 26, 2018 wakati akifungua mkutano wa Kamati Elekezi ya Taifa ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto uliohusisha Wizara 11 pamoja na wadau mbalimbali wa masuala ya wanawake na watoto nchini walipokutana mkoani Morogoro kujadili na kupitia Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto.
“Jamii inapaswa kuwa mstari wa mbele katika kupinga mila na desturi potofu zinazokandamiza makundi haya na badala yake kutumia muda mwingi katika kuzalisha mali na kujishughulisha katika masuala ya maendeleo ili kuondokana na umasikini na kujiletea maendeleo”.alisema Kamuzora
Aidha Kamuzora aliongezea kuwa, jamii inapaswa kuendelea kusaidia jitihada za Serikali katika kutokomeza mila na desturi potofu kwa kuunga mkono mipango mikakati iliyopo na kuendelea kutoa elimu kwa umma juu ya masuala ya Haki na Usawa katika jamii.
“Tujitathimini na kuona namna bora ya kuondokana na mila na desturi zote zinazomkandamiza wanamke na mtoto ili kuendelea kusimamia zile zinazoiwezesha jamii kuwa na usawa na haki katika makundi yote bila kuwa na ubaguzi”
Naye Mkurugenzi wa Sera na Mipango Idara ya Maendeleo ya Jamii Bw.Atupele Mwambene alieleza kuwa, Serikali imejikita kuhakikisha inamaliza changamoto za wanawake na watoto kwa kuhakikisha Mpango Kazi huo unawawezesha katika maeneo nane ya kipaumbele ikiwemo; kutokomeza mila na desturi zilizopitwa na wakati, Uwezeshaji wa uchumi wa Kaya, kuhakikisha mazingira salama hususan mazingira ya umma na kuwa na malezi bora kuanzia ngazi ya familia.
Aliongezea kuwa Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa maendelea, hususan wanaoshirikiana katika masuala ya watoto na wanawake itaendelea kushirikiana ili kuwa na nguvu ya pamoja na kuhakikisha jamii inakuwa sehemu salama kwa makundi yote.
“Tumekutana pamoja ili kuhakikisha tunahuisha nguvu kwa pamoja ili kuhakikisha mila na desturi zinazochochea ukatili dhidi ya makundi haya unatokomezwa kwa kuwa na mipango inayotekelezeka.
Naye Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.John Njingu alieleza kuwa, jamii inapaswa kubadili mitazamo katika kupashana habari na kuvitumia vyombo vya habari kama nafasi pekee yenye mchango mkubwa katika kuifikia jamii kupitia elimu kwa umma juu ya utokomezaji wa vitendo vya ukatili katika makundi haya.
“watumiaji wa vyombo vya habari wawajibike na kuhakikisha taarifa zinazotolewa katika jamii zisiwe zenye athari kwa watoto na wanawake badala yake tutumia vyombo vya habari kwa matumizi yenye tija katika jamii zetu”.alisisitiza Dkt.Njingu
AWALI
Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) unatarajiwa kuwezesha na kuondoa ukatili dhidi ya wanawake kwa asilimia 50 kufikia mwaka 2022; na kuondoa ukatili dhidi ya watoto kwa asilimia 50 kufikia mwaka huo, na hivyo kuleta mabadiliko makubwa kwa kuwa na familia salama, na jamii yenye utulivu.Katika kufikia malengo mpango unaelekeza nafasi ya kila mdau kuanzia ngazi ya familia, jamii, halmashauri, Mikoa, Wizara, SektaBbinafsi, Asasi za Kiraia na wabia wa maendeleo Mpango umeweka mfumo fungamanishi wa uratibu, ufuatiliaji na tathmini ambao utaratibiwa katika ngazi ya Taifa na Ofisi ya Waziri Mkuu, ngazi ya mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa, na ngazi ya Halmashauri na Wakurugenzi Watendaji.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt.Laurean Ndumbaro akizungumza wakati wa kikao cha Kamati elekezi ya Taifa ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto kwa ajili ya kujadili Utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto kilichofanyika Mkoani Morogoro Oktoba 26, 2018 kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw.Amoni Mpanju.
Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Afya (Maendeleo ya jamii) Bw.Mwambene Atupele akichangia jambo wakati wa kikao hicho.
Mkurugenzi Msaidizi (Mipango na Tafiti) kutoka Wizara ya Viwanda Bi.Zaytun Bagholleh akifafanua jambo wakati wa kikao kazi hicho.
Mjumbe kutoka UNICEF Bi.Maud Droogleever akichangia jambo kuhusu ushirikishwaji wa Taasisi zisizokuwa za Kiserikali katika mapambano dhidi ya Utatili wa wanawake na watoto wakati wa kikao kazi hicho.


Mratibu wa Taifa wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bi.Happiness Mugyabuso pamoja na Mratibu wa MTAKUWWA Bw.Seto Ojwando wakifuatilia uwasilishwaji wa mada wakati wa kiako kazi hicho.
Sehemu ya wajumbe wa kikao wakifuatilia mada zinazowasilishwa wakati wa kikao kazi hicho.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw.Amoni Mpanju akichangia hoja ya masuala ya sheria za watoto wakati wa kikao kazi hicho.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Prof.Faustin Kamuzora akizungumza na waandishi wa habari kuhusu jitihada za Serikali katika kuhakikisha inatokomeza changamoto za ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto Nchini mara baada ya ufunguzi wa kikao kazi hicho.




EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.