Thursday, October 18, 2018

SERIKALI IMEDHAMIRIA KUTOKOMEZA CHANGAMOTO ZA UKATILI KWA WANAWAKE NA WATOTO NCHINI

NA.MWANDISHI WETU
Serikali imedhamiria kumaliza changamoto za ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto kwa kushirikia na wadau wanaohusika na masuala ya wanawake na watoto nchini.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw.Patrick Golwike alipokuwa akifungua kikao kazi cha Kamati Tendaji ya Taifa ya ulinzi wa wanawake na watoto kilichofanyika Oktoba 17, 2018 Jijini Dodoma kujadili utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya makundi hayo.
Kamati hiyo imekutana kujadili Utekelezaji wa Mpango Kazi huo unaolenga kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA) na changamoto zinazotokana na vitendo hivyo.
Aidha, Miongoni mwa maeneo muhimu yaliyojadiliwa katika mpango kazi huo ni pamoja na kuhakikisha maeneo nane ya kimkakati yanafikiwa ili kufukia malengo ya kupunguza aina zote  za ukatili kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2020, na kuwataka wadau wote kushirikiana katika kukabiliana na vita ya ukatili kwa wanawake na watoto.
Maeneo ya utekelezaji yaliyoainishwa ni pamoja na; uimarishaji wa uchumi wa Kaya, kupinga mila na desturi zinazomkandamiza  mwanamke na mtoto, kuhakikisha mazingira salama sehemu za umma, kuimarisha mahusiano mema na kuziwezesha familia katika malezi bora, utekelezaji na usimamizi wa sheria, utoaji huduma kwa waathirika wa ukatili pamoja na mazingira salama shuleni na stadi za maisha.
“Wajibu wa wadau wote wenye kutekeleza afua za kuzuia na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto kutumia mwongozo huu katika maeneo mnayosimamia kwani utarahisisha katika utekelezaji wa majukumu yetu na kuhakikisha maeneo nane yaliyoainishwa yanafikiwa kikamilifu”.Alisisitiza Golwike
Aliongezea kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali katika kukabiliana na vitendo vya ukatili nchini kupitia Sera, Sheria, Kanuni, Miongozo na Mipango ya Kisekta ikiwemo uanzishwaji wa madawati ya Jinsia na watoto katika kila Wizara na katika vituo vya polisi 417, kuandaliwa kwa sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000) na Sera ya Mtoto ya mwaka 2008.
Jitihada nyingine ni pamoja na uanzishwaji wa mifumo ya ulinzi wa mtoto katika Halmashauri 63 nchini pamoja na uanzishwaji wa Mahakama za kusimamia kesi za watoto katika Halmashauri 131.
Kwa upande wake Mratibu wa Taifa wa Dawati la Jinsia na Watoto Bi.Happiness Mugyabuso aliongezea kuwa ili kufikia malengo ya kutokomeza ukatili kwa makundi hayo ni vyema mpango kazi huo ukatekelezwa kwa vitendo ili kutorudisha nyuma jitihada za Serikali.
“Ni vyema sasa mpango kazi huu ukajadiliwa kwa kina ili kufikia malengo na kuwa miongozo mizuri itayotoa utaratibu wa uratibu, usimamizi na ufuatiliaji”.alisistiza Mugyabuso
Aidha, alieleza kuwa wadau wanaotekeleza mpango huu ni pamoja na  Wizara, Idara na Wakala za Serikali, Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa wanaoshughulikia masuala ya wanawake  na watoto, Mashirika ya Kimataifa , Asasi zisizo za Kiserikali, Sekta Binafsi, Taasisi za Dini na Wanawake kwa pamoja wamekuwa ni chachu katika vita dhidi ya ukatili kwa wanawake na watoto nchini.
=MWISHOI=


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.