Wednesday, October 24, 2018

TANZANIA HAKUNA UBANAJI WA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI-MAJALIWA

*Asisitiza kwa  atakayeenda kinyume na sheria, Serikali itamuwajibisha

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kwamba nchini Tanzania hakuna ubanaji wa uhuru wa vyombo vya habari wala taasisi zisizo za kiserikali.

Amesema jambo hilo linadhihirishwa na uwepo wa jumla ya vituo vya redio 152, ambavyo kati yake ni vituo vitatu tu ndivyo vinavyomilikiwa na Serikali.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Oktoba 24, 2018) katika maadhimisho ya siku ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

“Tunapenda kuwahakikishia kuwa, Serikali ya Tanzania inaongozwa na katiba na sheria za nchi ambazo zinatoa uhuru wa kujieleza na kupata habari,” amesisitiza.

Waziri Mkuu amesisitiza kwamba mwananchi yeyote atakayeenda kinyume na sheria, Serikali itamuwajibisha kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.

Amesema Serikali imeridhia mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na ule wa haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni. 

Sambamba na kusimamia haki hizo, Serikali imeendelea kutekeleza wajibu wake katika kuiwezesha jamii kuishi salama kwa amani na utulivu kwa kuzingatia sheria za nchi.

Amesema kukuza, kuimarisha na kulinda haki za binadamu ni wajibu wa Serikali na kwa kuzingatia umuhimu huo mwaka 1984 iliingiza sheria ya haki za binadamu katika katiba.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kuwa zoezi la kuwarejesha wakimbizi wa Burundi nchini kwao lilikuwa ni la hiari na limetekelezwa baada ya hali ya amani kurejea.

Amesema hakuna sababu ya kuendelea kuwahifadhi wakimbizi ambao kwa hiari yao wameamua kurejea nchini kwao ili wakaendelee na shughuli za kulijenga Taifa lao.

“Nasisitiza kuwa zoezi hili ni la hiari. Tangu mwezi Septemba mwaka jana, Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Burundi na UNHCR imekuwa ikiwarejesha wakimbizi hao kwao.”

Amesema zoezi hilo limekuwa likifanyika kwa kuzingatia usalama na utu wa wakimbizi hao. Wakimbizi 52,283  wa Burundi wamerejea nchini kwao kati 81,281 waliokwisha jiandikisha.
Waziri Mkuu ameyasema hayo baada Serikali kupokea shutuma katika siku za hivi karibuni kutoka kwa baadhi ya jamuiya ya kimataifa kuhusu uendeshaji wa zoezi hilo.

Hivyo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa na washirika wengine wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa mujibu wa mkataba wa UN wa mwaka 1967 wa kuwahudumia wakimbizi ili kufanikisha zoezi hilo la kuwarejesha makwao kwa hiari na kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu.

Maadhimisho hayo ya siku ya Umoja wa Mataifa ambao umetimiza miaka 73 tangu uanzishwe yalihudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro.

Wengine ni Mratibu wa Mkaazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bw. Alvaro Rodrigues pamoja na mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao nchini.



EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.