Monday, October 22, 2018

USHIRIKIANO WA TAASISI ZA DINI NA SERIKALI NI MUHIMU-MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ushirikiano mzuri baina ya taasisi mbalimbali za dini nchini na Serikali ni jambo la muhimu katika kuboresha na kuimarisha amani.

Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Oktoba 22, 2018) alipowasili jijini Mwanza akiwa njiani kwenda mkoani Simiyu ambako kesho anatarajia kufungua maonesho ya wajasiriamali.

Alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza, Waziri Mkuu amepokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella na viongozi mbalimbali wa mkoa huo wakiwemo wa Serikali na wa dini mbalimbali.

Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua mkakati wa viongozi wa dini wa kuunda kamati za amani nchini ambapo walianzia kwenye ngazi ya mkoa na sasa wamefikia katika kata.

“Viongozi wa dini mnadhamana kubwa katika kulifanya  Taifa liendelee kudumisha amani, utulivu na mshikamano, hivyo ushirikiano wenu na   Serikali ni muhimu.”

Amesema viongozi wa Serikali wakati wote wamekuwa tayari kufanyakazi na viongozi pamoja na taasisi mbalimbali za dini, lengo ni kuimarisha amani na utulivu uliopo nchini.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mwanza inawajibu wa kuhakikisha kwamba maeneo ya mkoa huu yanaendelea kuwa salama.

Pia, Waziri Mkuu amempongeza Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Sheikh Hassan Bin Mussa Kabeke kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo.

“Nakupongeza kaimu sheikh wa mkoa kwa kuteuliwa na ninakutakia kila la heri katika kazi yako na kwamba dhamana yako kubwa ni kuwaunganisha waislamu na waumini wa dini zote.” (mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.