Thursday, October 11, 2018

ATAKAYEDOKOA MALI YA UMMA HATOVUMILIWA-MAJALIWA

*Awasisitiza watumishi wa umma wawe waadilifu waaminifu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema vitendo vya udokozi wa mali ya umma havitavumiliwa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, hivyo amewataka watumishi wawe waadilifu na waaminifu wanapotekeleza majukumu yao.

Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Oktoba 11, 2018) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo akiwa katika ziara mkoani Dodoma.

Waziri Mkuu amesema Serikali haitamvumilia watumishi wa umma ambaye si muadilifu, mvivu na wala rushwa hawana nafasi, hivyo ni lazima wajibike na ambao watashindwa kutekeleza majukumu yao watapa shida kwenye Serikali hii. “Hakuna mchezo kwenye Serikali hii, watumishi wa umma wanapaswa kulitambua hili.” 

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka watumishi hao kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kufuata maelekezo yaliyotolewa kwenye Ilani ya uchaguzi Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2015/2020.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watumishi hao wahakikishe wanapanga ratiba ya kwenda kuwatembelea wananchi hususani waishio vijijini na kushirikiana nao katika kutatua kero zinazowakabili si kukaa ofisni.

Waziri Mkuu amesema kila mtumishi kwenye idara yake anapaswa kwenda kwa wananchi, kama ana siku tano za kufanyakazi kwa wiki basi siku tatu azitumie kwenda kwa wananchi kutatua changamoto zao na kama ana siku sita, siku nne azitumike kuwafikia wananchi.

Akizungumzia kuhusu idara ya kilimo, Waziri Mkuu amesema Maafisa Kilimo wote wanatakiwa kwenda vijijini kufanyakazi na si kubaki ofisini na alishatoa agizo hilo alipokutana nao jijini Dodoma. “Wakulima huko vijijini wanahangaika peke yao huku maafisa kilimo wamekaa ofisini.” 

Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma wazingatie itifaki, mipaka ya madaraka yao pamoja na kuheshimu viongozi. Amesema hata kama ni mkuu wa idara pia anapaswa kumheshimu mtumishi aliyekuwa chini yake.

Awali,Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kongwa, aliishukuru Serikali kwa kutatua kero mbalimbali ikiwemo changamoto ya ukosefu wa maji pamoja na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Mbande hadi Kongwa ambapo aliomba ujenzi huo uendelee hadi Mpwapwa. 

Aidha, aliiomba serikali kugawa kwa vipande eneo la Rachi ya Taifa lililopo wilayani hapo kwa wafungaji kwa kuwa limekuwa halitumiki. “Napendekeza wananchi wapewe vitalu kisha wafuge kwa njia ya kisasa kwa kupatwa mbegu bora. Hii itasadia kuzalisha bidhaa bora za nyama na maziwa pamoja na wananchi kupata ajira.”

NayeMkuu wa  Wilaya ya Kongwa, Deo Ndejembi aliishukuru Serikali kwa kuwapatia fedha za kutekeleza miradi mbalimbali wilayani humo, hadi sasa wameshapokea zaidi ya sh. bilioni tatu kwa ajili ya miradi ya maji.

Kuhusu upatikanaji wa dawa kwenye wilaya hiyo alisema umefikia zaidi ya asilimia 90 na  wananchi wanapata huduma ya matibabu kwa ubora. 

“Pia Kongwa hakuna njaa. Tumeweza kuhamasisha kilimo cha mtama kwenye vijiji 89 ambapo Mbunge (Ndugai) alitoa sh. milioni saba kwa ajili ya mbegu ambapo sasa tumeweza kufikia ziada ya tani laki mbili.”

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge alisema mafanikio ya Kongwa ni matokeo ya uwepo wa amani na utulivu kwenye eneo hilo.

Hata hivyo, alimuomba Waziri Mkuu baada ya rais kusaini sheria ya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi ni muhimu ikapewa kipaumbele pamoja na miji mingine midogo inayozunguka jiji la Dodoma kupata fedha za kupima maeneo.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.