Thursday, July 27, 2023

Taasisi zinazotekeleza programu ya kuendeleza kilimo na uvuvi (AFDP) zatakiwa kufanya kazi kwa malengo

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na maswala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama amezitaka taasisi zinazotekeleza Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) kufanya kazi kwa malengo na kwa wakati ili kutekeleza mpango kazi ambao umewekwa katika programu hiyo.

Kauli hiyo ameitoa , alipokuwa katika ziara ya kikazi ya kutembelea Shirika la Uvuvi la Nchini (TAFICO) Jijini Dar es Salaam, ambapo alisema (TAFICO) ni Moja ya taasisi za Serikali iliyopewa majukumu katika programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi, yenye lengo kubwa la kuongeza tija na faida katika mazao yatokanayo na Kilimo na uvuvi ikiwa ni pamoja na ukuzaji wa  mazao yatokanayo na viumbe maji kupitia teknolojia ya kisasa.

Akizitaja Wizara na Tasisi zinazotekeleza Programu hizo chini ya Uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu kuwa  ni pamoja na  Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, (TAFICO) na  (ZAFICO) Waziri Mhagama alitaka Taasisi hizo kuzingatia ubora, na thamani ya fedha katika mradi mzima “Natarajia kila senti itakayowekezwa  katika mradi huu itaenda kujibu na kuleta matokeo halisi tena yakiwa chanya na yatakayosaidia nchi yetu kusonga mbele na kupata maendeleo endelevu kwa wananchi na Taifa kwa Ujumla, Alisisita.”

Akizungumza katika Ziara hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi alisema, Serikali Imeweka mkazo katika kuhakikisha kwamba Nchi inanufaika na Rasilimali maji hasa katika eneo la uvuvi, kupitia mradi wa (AFDP) hivyo “Sisi kama watendaji tupo tayari kuweka msisitizo na kuhahakisha kwamba haya yote yanakamilika kwa wakati na kuleta Tija kwa Taifa letu.” Alisisitiza Dkt. Yonazi

 Kwa Upande wake Afisa Mtendaji mkuu wa Shirika hilo Bw. Dennis Simba alisema kuwa, (TAFICO) imejipanga na ipo tayari katika kuhakikisha kwamba inafungua njia ya kwenda katika uvuvi wa Bahari kuu na mnyororo mzima wa thamani, na kuongeza kuwa miradi kumi na moja (11) iliopo katika programu hii itatekelezwa kwa wakati na kwani Serikali imeonesha nia ya dhati ya kufungua uchumi wa Bluu.

Awali, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya (TAFICO) Dkt. Eliamini Kasembe, alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeamua kufufua Shirika hili kwani lina manufaa makubwa kwa wananchi na Taifa kwa Ujumla, “Nia hii thabiti inaweza kufikia malengo ya uanzishwaji wa Shirika hili ikiwa ni pamoja na kutoa Ajira na kuchangia katika kuinua uchumi wa Taifa hili.” Alibainisha.

 

Read More

Wednesday, July 19, 2023

WAZIRI MHAGAMA ATEMBELEA MNARA WA SHUJAA AHAMAD MZEE

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama ametembelea Mnara wa Shujaa UD 5826 L/CPL AHAMAD MZEE katika kata ya Kitaya Halmashauri ya wilaya ya Nanyamba Mkoani Mtwara.

Waziri ametembelea mnara huo Nanyamba Mkoani Mtwara tarehe 17/07/2023 siku chache kuelekea siku ya Mashujaa ya kitaifa inayotarajiwa kufanyika tarehe 25/08/2023 katika Uwanja wa Mashujaa uliopo Mji wa serikali Mtumba Jijijni Dodoma.

Shujaa Ahmad Mzee alikuwa Muajiriwa wa Jeshi la Wananchi alipokuwa akitekeleza majukumu yake ya kikazi akiwa na umri wa Miaka 21 alipelekwa Mpakani mwa kijiji cha Kitaya akiwa na jukumu la Ulinzi wa Taifa la Tanzania katika nafasi ya Mpiga mzinga wa kuangusha ndege.

Katika kutekeleza Majukumu yake tarehe 14 April 1972 wakati ndege za Mreno zikitokea Msumbiji Helicopter na Jet Fighters zilipiga mabomu kijiji cha Kitaya na katika Mapambano hayo Shujaa Ahmad Mzee aliangusha Jet Fighter mbili, moja ilianguka ardhi ya Tanzania Mto Ruvuma na Nyingine ilianguka ardhi ya Msumbiji.

Kwenye Mapambano hayo Shujaa Ahamad Mzee alijeruhiwa baada ya Kupigwa na fighter na alichukuliwa na kukimbizwa Mtwara Ligula Hospitali na huko ndiko alikofia.

Read More

Tuesday, July 18, 2023

SERIKALI YATOA MSAADA WA KIBINADAMU, NANYAMBA NA TANDAHIMBA

 


Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) imetoa misaada ya kibinadamu kwa kaya 184 za kata ya Kitaya Halmashauri ya wilaya ya Nanyamba na kaya 160 kwa kata ya Michenjele Halmashauri ya wilaya ya Tandahimba.

Zoezi hilo limeongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe, Jenista Mhagama Mkoani Mtwara, amesema kwa kutumia sheria no 6 iliyotungwa mwaka 2022 ya usimamizi wa maafa, kazi yetu ni kufanya tathimini na kutoa Mkono wa pole kwenye Majanga yanayohusu binadamu mahali popote.

“Nitoe wito kila yanapotokea majanga na maafa, kwanza liwe jukumu letu kufarijiana kwa karibu; na kutoa taarifa za dalili za majanga yanapotokea, na kuangalia ni mambo gani ya msingi yafanyike ili kurudisha hali katika utaratibu wa kawaida” alihimiza.

Waziri Mhagama amesema, tumepokea tathimini iliyowakilishwa ikionesha madhara yaliyojitokeza kwa wananchi katika eneo hili katika maeneo kadha kwa kadha katika makazi, chakula,na  nyenzo za kufanyia shughuli za kiuchumi

Amefafanua kwamba Serikali imekuja kutoa Mkono ili tuweze kushirikiana na nyie katika kujibadilishia hali katika kipindi hiki chote, “nikweli Serikali imeendelea kuwa na nyie kwa nguvu kubwa na ya ziada zaidi,” alisema Mhe. Waziri

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassani kwa kutushika Mkono wananchi yanapotokea majanga ya kibindamu, yanapotokea mafuriko, na vinapotokea vimbunga, tunajisikia faraja.

Tumepokea magodoro 190 tumepokea ndoo kubwa 380, na ndoo kubwa za lita ishirini 190, tumepokea blanketi za watoto 190 na blanketi za watu wazima 380 na mikeka 380 na mabati 5700 na kaya zinazostahiki ni 184 zilizoordheshwa kwa sasa katika Halmashauri ya wilaya ya Nanyamba.

Kanali Ahmedi ameongeza kusema Halmashauri ya wilaya ya Tandahimba Ilipokea vifaa vya msaada wa kibinadamu kwa waathirika 160, tuna mabati 4800 kuna magodoro 160, mikeka 320 na mablanketi 320, ndoo kubwa za lita ishirini 320 na tayari zimeundwa kamati mbalimbali kwa ajili ya kuhakiki

Naye Mbunge wa Nanyamba Mhe. Abdallah Chikota amesema Tunashukuru kwa msaada wa kibinadamu na kipekee nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassan kwa sababu asiyeshukuru kwa moja hata kumi hawezi kushukuru.

 

Read More

Saturday, July 15, 2023

KAMPENI YA KILL CHALLENGE 2023 KUCHAGIZA JITIHADA ZA KUZIFIKIA SIFURI TATU DHIDI YA VVU NA UKIMWI

 


Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete amepongeza kampeni maalum ya kuchangia fedha katika utekelezaji wa afua za masuala ya  UKIMWI nchini ya Kilimanjaro HIV  & AIDS  Challenge 2023 kwa kuzingatia mchango wake katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI nchini.

Ametoa pongezi hizo mapema wakati wa hafla ya kuwaaga wapanda Mlima Kilimanjaro na waendesha baiskeli kuzunguka mlima huo katika lango la Machame Mkoani Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya kampeni hiyo kwa mwaka huu.

Mhe. Dkt. Kikwete alisema kampeni hiyo ina mchango mkubwa katika kufikia Kampeni ya Kitaifa ya kufikia malengo ya SIFURI TATU, yaani Sifuri ya maambukizo mapya ya Virusi vya UKIMWI, Sifuri ya Unyanyapaa na Ubaguzi kwa watu wanaoishi na VVU na Sifuri ya vifo vitokanavyo na UKIMWI kwa kuzingatia mchango wa kifedha unaopatikana na kusaidia utekelezaji wa afua za UKIMWI nchini.

“Kazi iliyofanywa na ndugu zetu GGM wameonesha njia wanastahili kuungwa mkono, hivyo basi, niziombe Jumuiya za wafanyabiashara, makampuni na sekta binafsi pamoja na Watanzania wote kwa ujumla, kuunga mkono kampeni ya Kill Challenge kwa miaka ijayo,”alisema

Akieleza uzoefu wa ushiriki wake katika kampeni hiyo alisema ni jambo muhimu kwa kuzingatia mchango wa tukio hilo katika masuala ya Afua za UKIMWI na linamatokeo mengi mazuri ikiwemo la kujijenga kiafya, kuchochea hali ya uzalendo kwa nchi yetu pamoja na kuimarisha mahusiano kati yetu na mataifa mengine kwani wapo washiriki wa mataifa mengine ikiwemo Afrika Kusini.

“Binafsi ninafarijika kuendelea kuwa sehemu ya mafanikio haya, kwani leo ninashiriki kwa mara ya tatu tukio kama hili adhimu ambapo niliwahi kushiriki pia mara ya kwanza tarehe 2 Mei, 2014 na tarehe 21 Julai, 2016, hivyo naipongeza TACAIDS pamoja na Geita Gold Mining Limited ambao ndio waanzilishi na waratibu wa program hii ya Kilimanjaro Challenge Against HIV and AIDS, ni jambo la kuungwa mkono na kupongezwa, hongereni sana,”alisema.

Aidha aliipongea  Serikali katika kupambana na maambuzi ya VVU na UKIMWI ambapo kupitia program hii wadau wanapata fursa kuchangia fedha kwa ajili ya kusaidia jitihada za Serikali na wananchi katika mapambano haya.

“Kwa namna ya kipekee kabisa naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ilivyojipanga kuongeza nguvu ya mapambano haya kwa kuendelea kutenga fedha nyingi  kwa ajili ya utekelezaji wa afua za masuala ya UKIMWI Nchini.

Alitumia nafasi hiyo kuwaasa washiriki kutimiza malengo kwa kushikamana, upendo na kuwa na umoja katika zoezi hilo ili kukamilika kwa namna lilivyokusudiwa.

“Washiriki wote 61 ikiwemo wapanda mlima (Climbers) thelathini na sita na wanaouzunguka kwa baiskeli ishirini na tano mmeonesha ushujaa wa hali ya juu kwa kujitoa kwenu na kuwa tayari kupanda mlima na wengine kuendesha baiskeli mmefanya jambo kubwa na zuri la kuigwa,”.

Aliongezea kuwa, kushiriki zoezi hili ambalo si jepesi imedhihirisha kuwa bado ipo dhamira ya dhati miongoni mwa Watanzania na wadau ya kuendeleza mapambano haya, na yatafanikiwa iwapo pataendelea kuwa na dhamira ya dhati kwa kila mmoja wetu na ushirikiano wa pamoja kufikia ushindi unaoutarajia.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga alipongeza namna zoezi lilivyoratibiwa na kutoa wito kwa washiriki wote kuendelea kujitoa kwa kadiri inavyobidi huku akimshukuru Rais Mtaafu Dkt. Jakaya Kikwete kwa kukubali kuwa mgeni rasmi wa program hiyo na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano na wadau mbalimbali wanaoshughulika na afua za masuala ya VVU na UKIMWI nchini.

Awali akieleza kuhusu kampeni hiyo Kaimu Mtendaji Mkuu wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Nchini Dkt. Jerome Kamwela alisema Tanzania imeendelea kuwa na mikakati madhubuti katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI na kueleza takwimu zinaonesha maambukizi yamepungua kufikia asilimia 4.7 ambapo ni ishara kuwa jamii imekuwa na mwamko na uelewa mpana kuhusu masuala haya.

 

Read More

Sunday, July 2, 2023

WAZIRI MHAGAMA AKABIDHIWA KIPANDE CHA SEHEMU YA UJENZI WA UWANJA WA MASHUJAA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama, amekabidhiwa kipande cha sehemu ya ujenzi wa uwanja wa mashujaa, katika Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma mapema Julai 2, 2023.

Ujenzi huo unaotekelezwa na kampuni ya SUMA JKT,Umekamilisha kipande cha  sehemu ya kwanza ya ujenzi wa uwanja wa Gwaride ambao unategemewa kutumika katika Maadhimisho ya Siku ya kumbukumbu ya Mashujaa.

Akiwa kiwanjani hapo Waziri Mhagama alisema, Serikali pamoja na kuhamia Dodoma imejenga miundombinu yenye hadhi ya makao Mkuu ya Serikali, na jamii inashuhudia majengo ya Serikali makubwa na miondombinu mingine ikiendelea kukamilishwa.

Akiongelea Ujenzi wa Uwanja huo, Waziri Mhagama alisema, ujenzi utakapo kamilika utakuwa ni wa mfano Barani Afrika.

"Eneo hili ni sehemu ya kwanza ya ujenzi wa eneo la maadhimisho ya uwanja wa mashujaa, (Parade Ground) ambayo itakuwa na Mnara wa Mashujaa, wenye ubora na viwango vya juu kabisa.” Alieleza Mhe. Mhagama

Aliendelea kusema kuwa, awamu ya pili itakuwa na bustani kubwa, ambayo itakuwa na mvuto wa aina yake, na tayari Taasisi mbali mbali za Serikali zimeonesha nia ya kuwekeza na kushirikiana, kuhakikisha kutakuwa na bustani hiyo yenye migahawa, viwanja vya michezo na burudani mbalimbali, ambazo zitakuwa katika eneo hilo ambao leo amekabidhiwa kipande kidogo tuu kama sehemu ya kwanza ya ujenzi.

Alifafanua zaidi kuwa, sehemu ya tatu itahusisha ujenzi wa mnara mrefu wa zaidi mita 110 ambao utakuwa mnara wa kwanza Barani Afrika, ambao utakuwa ni kivutio kwa watalii na kuongeza pato la Taifa.

Kwa Upande Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Dkt. Jim Yonazi alisema uwanja huo utakapokamilika utaongeza uzuri na ubora wa Jiji la Dodoma na Serikali itahakikisha kwamba mnara pamoja na uwanja wake unakuwa wa kupendeza na kuwa na mvuto wa kipekee huku akizishuruku sekta nyingine zilizoonesha ushirikiano katika utekelezaji wa ujenzi huo na kuhakikisha miundombinu muhimu inapatikana kwa wakati.

Awali akizungumza katika makabidhiano hayo, Katibu wa Kikosi kazi cha Taifa cha kuratibu Serikali kuhamia Dodoma Bw. Meshach Bandawe, alisema ujenzi huo umezingatia suala la mpango kabambe wa ujenzi wa Mji wa Serikali na kazi ya ubunifu wa awali ilifanywa kwa kina na wataalam kutoka chuo kikuu cha Ardhi, TPA, NHC  na SUMA JKT.

Naye Mwakilishi wa kampuni ya Ujenzi kutoka SUMA JKT kanda ya Kati Meja Samweli Jambo, alisema ujenzi huo umefuata taratibu zote za upimaji na viwango.

 “Tulifanya kazi usiku na mchana kuhakikicha tunatekeleza maelekezo ya Mhe. Waziri ya kukabidhi kipande hiki kwa wakati.” Alieleza Samweli

Read More