Thursday, July 27, 2023

Taasisi zinazotekeleza programu ya kuendeleza kilimo na uvuvi (AFDP) zatakiwa kufanya kazi kwa malengo

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na maswala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama amezitaka taasisi zinazotekeleza Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) kufanya kazi kwa malengo na kwa wakati ili kutekeleza mpango kazi ambao umewekwa katika programu hiyo.

Kauli hiyo ameitoa , alipokuwa katika ziara ya kikazi ya kutembelea Shirika la Uvuvi la Nchini (TAFICO) Jijini Dar es Salaam, ambapo alisema (TAFICO) ni Moja ya taasisi za Serikali iliyopewa majukumu katika programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi, yenye lengo kubwa la kuongeza tija na faida katika mazao yatokanayo na Kilimo na uvuvi ikiwa ni pamoja na ukuzaji wa  mazao yatokanayo na viumbe maji kupitia teknolojia ya kisasa.

Akizitaja Wizara na Tasisi zinazotekeleza Programu hizo chini ya Uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu kuwa  ni pamoja na  Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, (TAFICO) na  (ZAFICO) Waziri Mhagama alitaka Taasisi hizo kuzingatia ubora, na thamani ya fedha katika mradi mzima “Natarajia kila senti itakayowekezwa  katika mradi huu itaenda kujibu na kuleta matokeo halisi tena yakiwa chanya na yatakayosaidia nchi yetu kusonga mbele na kupata maendeleo endelevu kwa wananchi na Taifa kwa Ujumla, Alisisita.”

Akizungumza katika Ziara hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi alisema, Serikali Imeweka mkazo katika kuhakikisha kwamba Nchi inanufaika na Rasilimali maji hasa katika eneo la uvuvi, kupitia mradi wa (AFDP) hivyo “Sisi kama watendaji tupo tayari kuweka msisitizo na kuhahakisha kwamba haya yote yanakamilika kwa wakati na kuleta Tija kwa Taifa letu.” Alisisitiza Dkt. Yonazi

 Kwa Upande wake Afisa Mtendaji mkuu wa Shirika hilo Bw. Dennis Simba alisema kuwa, (TAFICO) imejipanga na ipo tayari katika kuhakikisha kwamba inafungua njia ya kwenda katika uvuvi wa Bahari kuu na mnyororo mzima wa thamani, na kuongeza kuwa miradi kumi na moja (11) iliopo katika programu hii itatekelezwa kwa wakati na kwani Serikali imeonesha nia ya dhati ya kufungua uchumi wa Bluu.

Awali, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya (TAFICO) Dkt. Eliamini Kasembe, alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeamua kufufua Shirika hili kwani lina manufaa makubwa kwa wananchi na Taifa kwa Ujumla, “Nia hii thabiti inaweza kufikia malengo ya uanzishwaji wa Shirika hili ikiwa ni pamoja na kutoa Ajira na kuchangia katika kuinua uchumi wa Taifa hili.” Alibainisha.

 


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.