Wananchi waliokumbwa na
athari za maafa ya Maporomoko ya tope na mawe kutoka Mlima Hanang wametoa
shukrani za dhati kwa Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
wema aliowatendea kwa ujenzi wa nyumba za makazi zilizojengwa katika eneo la Waret
Wilaya ya Hanang' Mkoa wa Manyara.
Wametoa salamu hizo katika kikao cha ndani
walichokutana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala
ya Sera Bunge na Uratibu Mheshimiwa William Lukuvi leo katika ukumbi wa
Halmashauri Hanang' ikiwa ni maandalizi ya kuwakabidhi wananchi nyumba 109
zilizojengwa na Serikali tukio litakaloongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.
Bw, Kizito Joackimu Mkazi wa Katesh "A"
amesema Serikali iliweka jitihada kubwa kusimamia urejeshaji wa hali
wakishirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama nchini na kazi imefanyika kwa
ubora na weledi.
“Mama Samia ni zaidi ya Mama hakulazimishwa na mtu
kututendea wema alioufanya kwa wananchi wa Hanang', angeweza kutoa salamu za
pole lakini akaona haitoshi, atoe vyakula vya kutosha, magodoro, matibabu ndugu
zetu wametibiwa kwa kiwango kikubwa,” alieleza Bw, kizito.
Alifafanua, kwamba Kuna wananchi nyumba zao
zilizoharibika zikiangaliwa thamani yake hazilingani na hizi zilizojengwa kwa
ubora na kwa kuzingatia upatikanaji wa huduma muhimu za kibinadamu.
"nyumba hizi zitatufaa sana na kimsingi kuna watu
walikuwa hawana ndoto za kuwa na nyumba zilizokatika mtaa mmoja wenye maji
wenye umeme na eneo la biashara, tumebebwa sana na Serikali lazima tuwe na moyo
wa shukrani," alisisitiza.
Wakitoa neno la shukrani wakati wa kikao hicho Bi.
Fausta Magasa Mkazi wa Katesh, "A"amesema jambo hilo limewaletea
furaha katika maisha yao na kusema ni la neema na baraka ambalo hawakulitegemea
kutokea.
“Tunapenda kutoa shukrani za dhati kwa Rais wetu Dkt.
Samia Suluhu Hassan kwa mbegu ya upendo aliyoipanda kwa watu 109 ambayo itazaa
vizazi na vizazi" alieleza Bi, Magasa.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri Mkuu
(Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi amesema wananchi watakaopewa
funguo za nyumba kesho wataamua wao wenyewe siku watakayohamia kwenye
nyumba zao walizojengewa na serikali.
“Nimepokea Salamu za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania nitaziwasilisha lakini naamini muwakilishi wenu atasema salamu zenu
pia kesho wakati mnapokea hati ya nyumba, funguo za nyumba zenu na majiko ya
gesi" alieleza Waziri Lukuvi.