Thursday, December 19, 2024

WANANCHI WA HANANG' WAMSHUKURU RAIS SAMIA

 


Wananchi waliokumbwa na athari za maafa ya Maporomoko ya tope na mawe kutoka Mlima Hanang wametoa shukrani za dhati kwa Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wema aliowatendea kwa ujenzi wa nyumba za makazi zilizojengwa katika eneo la Waret Wilaya ya Hanang' Mkoa wa Manyara.

Wametoa salamu hizo katika kikao cha ndani walichokutana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu Mheshimiwa William Lukuvi leo katika ukumbi wa Halmashauri Hanang' ikiwa ni maandalizi ya kuwakabidhi wananchi nyumba 109 zilizojengwa na Serikali tukio litakaloongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.

Bw, Kizito Joackimu Mkazi wa Katesh "A" amesema Serikali iliweka jitihada kubwa kusimamia urejeshaji wa hali wakishirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama nchini na kazi imefanyika kwa ubora na weledi.

“Mama Samia ni zaidi ya Mama hakulazimishwa na mtu kututendea wema alioufanya kwa wananchi wa Hanang', angeweza kutoa salamu za pole lakini akaona haitoshi, atoe vyakula vya kutosha, magodoro, matibabu ndugu zetu wametibiwa kwa kiwango kikubwa,” alieleza Bw, kizito.

Alifafanua, kwamba Kuna wananchi nyumba zao zilizoharibika zikiangaliwa thamani yake hazilingani na hizi zilizojengwa kwa ubora na kwa kuzingatia upatikanaji wa huduma muhimu za kibinadamu.

"nyumba hizi zitatufaa sana na kimsingi kuna watu walikuwa hawana ndoto za kuwa na nyumba zilizokatika mtaa mmoja wenye maji wenye umeme na eneo la biashara, tumebebwa sana na Serikali lazima tuwe na moyo wa shukrani," alisisitiza.

Wakitoa neno la shukrani wakati wa kikao hicho Bi. Fausta Magasa Mkazi wa Katesh, "A"amesema jambo hilo limewaletea furaha katika maisha yao na kusema ni la neema na baraka ambalo hawakulitegemea kutokea.

“Tunapenda kutoa shukrani za dhati kwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mbegu ya upendo aliyoipanda kwa watu 109 ambayo itazaa vizazi na vizazi" alieleza Bi, Magasa.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi amesema wananchi watakaopewa funguo za nyumba kesho wataamua wao wenyewe siku watakayohamia kwenye nyumba  zao walizojengewa na serikali.

“Nimepokea Salamu za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nitaziwasilisha lakini naamini muwakilishi wenu atasema salamu zenu pia kesho wakati mnapokea hati ya nyumba, funguo za nyumba zenu na majiko ya gesi" alieleza Waziri Lukuvi.






EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.