Thursday, November 21, 2024

DKT. YONAZI ASHUKURU MICHANGO INAYOENDELEA KUTOLEWA, AFAFANUA NAMBA SAHIHI YA KUTUMA MICHANGO MAAFA KARIAKOO

 

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera,Bunge na Uratibu  Dkt. Jim Yonazi amewashukuru wadau mbalimbali wanaoendelea kujitolea na kutoa michango kwa ajili ya maafa ya Kuporomoka kwa ghorofa eneo la Kariakoo kusema ni moyo wa upendo unaoneshwa kwa matendo mbalimbali walioguswa na maafa hayo.

Ametoa shukrani hizo wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu hatua zinavyoendelea katika eneo lililopatwa na ajali ya kuporomoko kwa jengo la ghorofa mtaa wa Agrey Kariakoo Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Yonazi ametumia nafasi hiyo kutangaza “Control Number” kwa ajili ya kuwawezesha wananchi ambao wataguswa na maafa hayo kwa kutuma michango yao kwa ajili ya kuendelea kusaidia katika hatua baada ya kutokea maafa hayo.

" Control number ni 987320001709 ambapo namba hii inatumika kwa mitandao yote ,mwananchi anaweza kuchangia kuanzia 1000 na kuendelea na fedha hizi zinaingia moja kwa moja kwenye akaunti ya Maafa au kuchangia kupitia akaunti ya National Relief Fund yenye namba 9921159801 ambayo ipo Benki Kuu ya Tanzania,” amesema Dkt.Yonazi.

Kwa hatua nyingine Dkt. Yonazi amepokea msaada kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) lililokabidhi kiasi cha shilingi za Kitanzania Milioni Ishirini kwa lengo la kusaidia kufuatia maafa hayo.

Akizungumza kabla ya kukabidhi hundi hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya TANAPA, Jenerali mstaafu George Waitara amesema kuwa tukio hilo limesababisha maafa makubwa ikiwemo vifo,uharibifu wa mali pamoja na matatizo ya kisaikolojia kwa waathirika wa tukio hilo.

"TANAPA ni sehemu ya wananchi wa Tanzania,hivyo janga hili tumetugusa tukaona tutoe chochote kusaidia uokoaji wa maafa haya na Watanzania wasiwe na taharuki kwani tumeona shughuli za uokoaji zinakwenda vizuri, kikubwa wawe wanafuatilia taarifa kupitia mamlaka husika na si vyanzo vingine " amesema Jenerali Mstaafu Waitara.











Tuesday, November 19, 2024

SERIKALI YAONGEZA SAA 24 ZA ZIADA ZA UOKOZI KARIAKOO

Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Thobias Makoba, amesema zoezi la uokoaji wa watu walionasa kwenye jengo lililoporomoka Jumamosi ya Novemba 16, 2024 Kariakoo kwenye Mtaa wa Congo na Mchikichi Jijini Dasr es Salaam, litaendelea tena kwa saa 24 za ziada baada ya saa 72 za kawaida za kiwango cha kimataifa kumalizika.

Bw. Makoba ameyasema hayo, wakati akizungumza na waandishi wa habari Kariakoo kwenye eneo la tukio, ambapo amesema kuongezeka kwa saa hizo 24 za ziada, ni agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, alilolitoa kupitia kwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa, katika kikao cha tathmini kuhusu zoezi hilo la uokoaji ambapo amelitaka jeshi la zimamoto na uokoaji, kuendelea na shughuli hiyo ili kunusuru uhai wa watu ambao bado wamekwama kwenye jengo hilo.

“Tukiwa kwenye kikao cha tathmini cha kazi inayoendelea, moja ya ajenda iliyozungumzwa ni kuhusiana na utaratibu wa uokoaji, kulianza kutokea maneno kwenye mitandao ya kijamii kwamba baada ya masaa 72 kwa kawaida kwa viwango vya kimataifa, zoezi la uokoaji kwenye maeneo kama haya linabadilika, na wanaanza kutumia mashine pale inapolazimu, sasa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan muda huu ametoa maelekezo kupitia kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, na maelekezo hayo yaje kwa kikosi chetu cha Zimamoto na Uokoaji kwamba zoezi hili liendelee kwa saa zingine 24 za ziada, ni kwamba wasisitishe, kabla ya kubadili hatua yoyote, kwa hiyo zoezi hili linaendelea, halitasitishwa kama ambavyo wananchi wengine wameanza kuwa na hofu” amesema Bw. Makoba.

Amesema lengo ni kuhakikisha maisha ya watu walioko kwenye jengo hilo yanalindwa na kwamba hakuna kifusi kitakachowaangukia.

“Imempendeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba, tutaendelea kutumia mbinu ambazo zilikuwa zikitumika za weledi na ustadi zaidi katika kuhakikisha kwamba, kwanza tunaridhika kwamba hakuna ambaye aliyepo hai atasumbuliwa au ataangushiwa kifusi huko chini, au kwa namna yoyote ile itamkuta ili kumsababishia kupoteza maisha, baada ya masaa 24 tutatangaza utaratibu unaofuata” amesema Bw. Makoba.

Zoezi la uokoaji wa watu walionaswa kwenye jengo lililoporomoka linaendelea kwa kasi kubwa kwa siku ya nne sasa ambapo Serikali inafanya jitihada zote kuhakikisha hakuna madhara yatakayowapata watu walionasa kwenye jengo hilo.

 

NAIBU WAZIRI UMMY AWASHUKURU RED CROSS NA TPA KWA MISAADA YA VIFAA SAIDIZI MAAFA KARIAKOO


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mheshimiwa Ummy Nderiananga amewashukuru wadau kutoka Shirika la Msalaba Mwekundu (Red Cross Tanzania) pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania TPA kwa kutoa misaada ya vifaa saidizi kwa ajili ya kuendelea kusaidia katika zoezi la uokoaji linaloendelea kufuatia janga la kuporomoka jengo la ghorofa eneo la Congo na Mchikichi Kariakoo Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam.

Ametoa shukrani hizo hii leo na kueleza kuwa miongoni mwa vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na machela tisa (9) mashuka 100 kutoka Shirika la Msalaba Mwekundu (Red Cross Tanzania) Pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania TPA, reflectors pamoja na  cover white.

Naibu Waziri huyo ameendelea kutoa rai kwa wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza kuchangia huku akipongeza namna zoezi la uokoaji linavyoendelea kwa kushirikiana na wadau.








 

Monday, November 18, 2024

MAPITIO YA PROGRAMU YA KUENDELEZA KILIMO NA UVUVI (AFDP), YAWAKUTANISHA WATAALAMU PAMOJA NA UJUMBE KUTOKA- (IFAD) MJINI ZANZIBAR

 


Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali, kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Paul Sangawe ameongoza Kikao cha Ujumbe kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), wakurugenzi wa sekta zinazotekeleza Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu pamoja na timu ya wataalamu.

Pamoja na mambo mengine kikao hicho pia kimehusu mapitio ya Mipango na Bajeti ya Programu kwa kipindi cha miaka minne ya utekelezaji iliyobakia.

Kikao  hicho kimefanyika Zanzibar, katika ukumbi wa Mkutano wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi.



MISAADA KWA AJILI YA WAATHIRIKA WA KUPOROMOKA KWA JENGO KARIAKOO ITOLEWE KWENYE AKAUNTI MOJA- DKT. YONAZI

 


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amesema msaada wa kifedha kwa ajili ya kusaidia walioathirika na kuporomoka kwa jengo la ghorofa Kariakoo Jijini Dar es Salaam unatolewa kwa akaunti maalum ya maafa ya 9921159801 ambayo ipo Benki Kuu ya Tanzania na kushughulikiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Dkt. Yonazi ameyasema hayo leo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu hali inayoendelea katika zoezi la uokoaji.

Amesema akaunti hiyo ni pekee nchini ambayo inakusanya misaada ya kifedha kwa ajili ya maafa.

"Kuna watu wana nia njema kabisa ya kuwasaidia Watanzania, lakini naomba tujizuie kabisa kukusanya michango ya kifedha kutoka kwa mtu yeyote bila kupitia akaunti hii". Amesema Dkt. Yonazi.

Aidha amesema akaunti hiyo ni maalumu imethibitishwa na serikali ili kuweza kuhakikisha misaada inawafikia walengwa na inatimiza malengo ya kutoa misaada hiyo.

Amesema kwa sasa operesheni inaendelea mpaka pale watakapokamilisha zoezi la kuokoa baadhi ya watu ambao bado hawajaokolewa.



Sunday, November 17, 2024

KATIBU MKUU WA CCM DKT. EMMANUEL NCHIMBI AFIKA KARIAKOO, AUNGANA NA VIONGOZI WENGINE WAKATI WA ZOEZI LA UOKOAJI

 


Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Emmanuel Nchimbi afika Kariakoo Leo Novemba 17,2024 na kushuhudia zoezi la uokoaji akiwa ameongozana na viongozi wa Serikali na kujionea zoezi hilo linaloendelea  mara baada ya  kuporomoka kwa jengo la ghorofa Kariakoo kwenye mtaa wa Congo na Mchikichi Jijini Dar es Salaam.

Mawaziri hao ni pamoja na  Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godfrey Mollel, Naibu Waziri wa TAMISEMI Mhe. Zainab Katimba pamoja na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga.



MAWAZIRI WAHAMIA KARIAKOO; KAZI YA UOKOZI INAENDELEA

 


Mawaziri wa kisekta wakiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. William Lukuvi Leo Novemba 17,2024 wamekutana kwa ajili ya kuendelea na zoezi la uokoaji wa watu waliokwama kwenye jengo lililoporomoka Kariakoo kwenye mtaa wa Congo na Mchikichi Jijini Dar es Salaam.

Mawaziri hao ni pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godfrey Mollel, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Khamis na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga.



Thursday, November 14, 2024

TANZANIA YAVUTIA MATAIFA UWEPO WA KITUO CHA UFUATILIAJI WA MAJANGA

 

 

TANZANIA imeendelea kutolewa mfano wa kuwa na Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura (National Emergency Operation and Communication Center Situation Room) na kuelezwa kuwa nchi nyingine ziendelee kuiga mfano wa Tanzania na kuendelea kuwekeza katika mifumo ya tahadhali za mapema -early warning systems kwa kutumia vyanzo vya ndani, kushirikisha jamii na sekta binafsi.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ameyasema hayo 13 Novemba, 2024 wakati wa Mkutano wa 29 wa nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29) unaoendelea mjini Baku, nchini Azerbaijan.

Dkt. Yonazi amesema kuwa,Tanzania imeendelea kuwa kinara katika masuala ya menejimenti ya maafa hususan katika kuzuia, kupunguza kujiandaa na kukabili maafa pindi yanapotokea, huku akitaja mafanikio ya uwepo wa kituo cha ufuatiliaji wa majanga (situation room) ikiwemo ya kurahisisha ufuatiliaji wa mwenendo wa janga lililotabiriwa na kufanya uchambuzi wa kiwango cha madhara kwa jamii, miundombinu na mazingira.

Pia kituo hicho kimesaidia kuandaa taarifa za tahadhari ya mapema ya hatua za kuchukua ili kuzuia, kujiandaa na kukabili maafa, kuandaa taarifa ya mwenendo wa tukio na kusambaza kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya kusaidia uratibu na utekelezaji wa shughuli za kukabili na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea.

Aidha alitumia fursa hiyo kuwahamasisha wadau kuwezesha utekelezaji wa afua za usimamizi wa maafa katika eneo la mifumo ya tahadhali ya mapema.

Dkt. Yonazi ametumia jukwaa hilo kuyakaribisha Mataifa mbalimbali kuja kujifunza Tanzania namna Kituo hicho kinavyofanya kazi katika kuratibu mwenendo wa majanga kwa umahiri wa hali ya juu.

“Uwepo wa kituo hiki umewavutia wadau wengi kuja kujifunza huku wengine wakiahidi kuunga mkono juhudi za Tanzania katika masuala ya menejimenti ya maafa,” alisema Dkt. Yonazi






Tuesday, November 12, 2024

AU YAIPATIA TANZANIA DOLA ZA KIMAREKANI 200,000 MCHANGO WA MAAFA HANANG

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, na Uratibu) Mhe. William Lukuvi ameishukuru Umoja wa Afrika kwa kutoa kibali cha kuichangia nchi ya Tanzania Dola za Kimarekani 200,000 kama ishara ya mshikamano kutokana na maafa makubwa yaliyotokea Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara.

Waziri Lukuvi ametoa shukrani hizo leo katika Ofisi za Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu zilizopo Jijini Dodoma na kubainisha kuwa mchango huo ni muhimu kwa kuwa utasaidia juhudi zinazofanywa na Serikali za kurejesha hali ikiwemo ujenzi wa shule, kituo cha afya na soko katika eneo lililoathirika.

 Akipokea mchango wa fedha hizo kutoka kwa Mheshimiwa Balozi Tabelelo Alfred Boang, Balozi wa Jamhuri wa Muungano wa Botswana nchini Ethiopia na Mwakilishi wa kamati ya Mabalozi (Permanent Representative Sub Committee on refugees, Returnees and IDPs), Mhe. Lukuvi amemweleza kuwa, mwaka 2023/2024 Tanzania ilikumbwa na El-Niño ambayo ilisababisha kuwepo kwa mvua kubwa zilizofululiza kwa kipindi kirefu na kusababisha mafuriko, upepo mkali, maporomoko ya tope na udongo.

Ameeleza, pamoja na juhudi zilizofanywa na Serikali katika kuzuia na kupunguza madhara, bado El-Niño ilileta madhara makubwa ikiwemo maafa ambayo yaliyosababisha vifo, kuharibu makazi ya watu na miundombinu muhimu.

 “Maporomoko ya tope wilayani Hanang’ yaliathiri maisha ya watu, miundombinu, shughuli za kiuchumi na kijamii, takwimu zinaonesha kuwa watu wapatao 89 walipoteza maisha na watu wapatao 139 waliumia kutokana na maporomoko hayo. Aidha, tathmini iliyofanyika inaonesha jumla ya nyumba 261 ziliathirika kwa namna moja au nyingine ambapo nyumba 95 zilibomoka kabisa na zingine kuzungukwa na tope, Watu wapatao 1576 kutoka 526 waliachwa bila makazi katika kipindi cha tukio” ameeleza Mhe. Lukuvi.

 Aidha, ameongeza kuwa, katika kukabiliana na maafa, Serikali ilifanya juhudi za kurudisha hali ambapo mpaka sasa imewezesha kujengwa nyumba 108 za makazi ya watu, kati ya nyumba hizo 73 zimejengwa kwa fedha za Serikali na nyumba 35 zimejengwa na Shirika la Msalaba Mwekundu, ujenzi wa nyumba hizo 108 umekamilika. 

 “Ninaelewa kuwa ujumbe wako utatembelea Wilaya ya Hanang’ tarehe 14 Novemba, 2024, katika safari yenu mtashuhudia juhudi kubwa za Serikali kwa kushirikiana na wadau zinazoendelea za kurejesha hali ikiwemo miundombinu muhimu kama vile barabara, umeme, maji na ujenzi wa nyumba 108 za makazi, ameeleza Mhe. Lukuvi.

Kwa upande wake Mheshimiwa Balozi Tabelelo Alfred Boang, Balozi wa Jamhuri wa Muungano wa Botswana nchini Ethiopia na Mwakilishi wa kamati ya Mabalozi (Permanent Representative Sub Committee on refugees, Returnees and IDPs), ameeleza kuwa, ujumbe huo umeagizwa na Kamati ya Mabalozi kufanya tathmini ya uharibifu uliotokea katika maeneo yaliyoathiriwa ikiwa dhamira kubwa ni Mkoa wa Manyara, aidha muhimu zaidi ni kusikia kutoka kwenye mamlaka na ndio maana wamekutana na Mheshimiwa Waziri na timu yake.

 “Muhimu zaidi kama Umoja wa Afrika kwa hakika kila kidogo tulicho nacho huwa tunainuka tunajivunia kuwa tumejitolea na kusema tunaenda kutafuta suluhu ya Afrika, matatizo au changamoto za Afrika” amebainisha Balozi Tabelelo.



Wednesday, November 6, 2024

UJUMBE WA MFUKO WA KIMATAIFA WA MAENDELEO YA KILIMO "IFAD" WATEMBELEA PROGRAMU YA KUENDELEZA KILIMO NA UVUVI "AFDP" TANZANIA


Ujumbe kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) ukiwa umeambatana na watumishi wa Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), kutoka  Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) pamoja na watekelezaji wa programu hiyo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Wizara ya Uchumi wa Buluu na uvuvi Zanzibar  wamekitembelea Kikundi cha Ufugaji wa samaki kiitwacho UWASAMO, katika kata ya Mzinga Mtaa wa Konga Manispaa ya Morogoro, ili kuona mafanikio ya ufugajiwa samaki kwa wanakikundi baada ya kupata mafunzo ya Ufugaji samaki, biashara na utunzaji wa kumbukumbu kutoka  kituo cha Kingolwira.

Ziara hiyo imefanyika leo tarehe 6/11/2024 kwenye Kituo kinachojishughulisha na utoaji mafunzo ya ufugaji samaki, pamoja na uuzaji wa vifaranga vya samaki.

Akizungumza kwa niaba ya wanakikundi ndugu Asungushe Patrick Msugupakulya amesema, wao kama kikundi wanaishukuru serika kwa kuwaletea mradi wa IFAD, ambao umewasaidia katika kuunda ushirika wao ambao mpaka sasa wanaendelea kupata msaada wa Elimu ya ufugaji wa samaki kwa wakati.

Pamoja na hayo wanakikundi cha UWASAMO, wamefurahishwa na ziara ya viongozi, ambapo wanaamini kwa kutembelewa huko, misaada zaidi watapata ili kuendeleza mtaji wao wa ufugaji wa samaki na kuleta maendeleo yenye tija kwa familia na Tanzania kwa ujumla wake.





TUONGEZE NGUVU YA PAMOJA KATIKA KUTEKELEZA DHANA YA AFYA MOJA - DKT. YONAZI

 


SERIKALI imedhamiria kuendelea kushirikiana na wadau  katika kutekeleza dhana ya Afya Moja nchini hasa maeneo ya kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na milipuko ya magonjwa na hatari nyingine za afya zinazohitaji ushiriki wa sekta zaidi ya moja na taaluma mbalimbali.

Akizungumza leo Jumatano Novemba 6, 2024 wakati akifunga Mkutano wa Afya Moja uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa wa Arusha (AICC) Jijini Arusha, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi amesema lengo la Dhana ya Afya Moja ni kupanua na kuimarisha ushirikiano baina ya sekta pamoja na taaluma mbalimbali katika hatua zote za kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na milipuko ya magonjwa na hatari nyingine za afya zinazohitaji ushiriki wa sekta zaidi ya moja na taaluma mbalimbali  katika kutekeleaji wa Afua hizo.

“Ni wakati sahihi kuendelea kushirikiana kwa pamoja na wadau wengine ikiwemo jamii, kwa kuongozwa na wizara za msingi ambazo ni Afya ya Binadamu, Wanyama (Mifugo na Wanyama Pori), Mazingira na Kilimo katika ngazi zote ili kuhakikisha nguvu ya pamoja inatuvusha hapa tulipo na kuendelea kuipa nguvu dhana ya afya moja,” alisema Dkt. Yonazi

Aliongezea kuwa, Dawati la Uratibu wa Afya Moja lipo chini ya Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo utekelezaji wa majukumu yake unaongozwa na Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa ya Mwaka 2004 inayoweka umuhimu katika usalama wa maisha ya watu na mali zao kwa kupunguza athari za kiuchumi na kijamii katika kuipa nguvu Sera ya Usimamizi wa Maafa ya mwaka 2004, Serikali ilitunga Sheria ya Usimamizi ya Maafa Namba 7 ya Mwaka 2015 inayosimamia utekelezaji wa shughuli za idara.

Dkt. Yonazi alizikumbusha sekta zote kuendelea kushirikiana katika kutatua changamoto ya magonjwa ya zoonotiki, usalama wa chakula, mabadiliko ya tabia nchi na usugu wa dawa dhidi ya vimelea vya magonjwa.

Aidha ameyataja maeneo ya kuimarisha ushirikiano kwa sekta pamoja na wadau wote wanaotekeleza Dhana hiyo ikiwemo ya kuongeza ushiriki wa sekta ya mazingira na sekta ya kilimo katika utekelezaji wa dhana ya Afya Moja, kuandaa miongozo ya namna sekta zitakavyobadilishana taarifa za magonjwa na matukio yenye athari kwa binadamu, wanyama na mazingira chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na kuhuisha orodha ya magonjwa ya kizoonotoki na kutekeleza miongozo na mipango mbalimbali ya kudhibiti magonjwa hayo.

Maeneo mengine ni kuendelea kuzijengea uwezo Kamati za Usimamizi wa Maafa kuhusu uratibu na utekelezaji wa dhana ya Afya Moja, kuendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa Afya Moja (2022-2027) katika maeneo yote pamoja na kuendelea kushiriki katika tafiti na uchunguzi wa pamoja kuhusu milipuko ya magonjwa na matukio mbalimbali nchini.

Kwa hatua nyingine Dkt. Yonazi amepongeza washiriki wote ikiwemo wawasilisha mada kwa siku zote na kueleza kuwa zitaendelea kuongeza tija katika miradi mbalimbali nchini ikiwemo ya kichaa cha mbwa, kimeta  na homa ya bonde la ufa.

“Mmetoa michango mingi na mizuri hakika itatufaa katika utekelezaji wa dhana ya Afya Moja na kuboresha afya za binadamu, wanyama, mimea na mifumo yaikolojia ,”alieleza Dkt. Yonazi.

Aidha amewashukuru wadau waliofanikisha kufanyika kwa mkutano huo muhimu huku akiwasihii kuendelea kuimarisha mashirikiano yaliyopo ili kuendelea kuipa nguvu Dhana ya Afya Moja na kuyafikia malengo yake.

“Kipekee niwashukuru COHESA, FAO, USAID na One Health Society kwa kusaidia na kufanikisha mkutano huu. Aidha, niwapongeze USAID kupitia mradi wao wa Breakthrough Action, MDH, Chuo cha Nelson Mandela kupitia mradi wa CEREBLAM, AFROHUN, KCMC/KCRI na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa kushiriki kikamilifu katika maonesho ya Mkutano huu,” Alisisitiza

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Ndugu Missaile Musa ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuratibu Mkutano huo wenye tija kwa Mkoa na Taifa kwa ujumla huku akisema mkutano huo umefanikiwa kukutanisha wadau na kujengewa uwezo pamoja na kuweka mikakati itakayowezesha kuyafikia malengo yaliyokusudiwa.

“Malengo na mkutano huu yamefanikiwa sana, kama mkoa tunaamini kuwa yote yaliyowasilishwa hapa yanamchango katika kuimarisha afya zetu pamoja na za wanyama, tutaendelea kuwa salama endapo haya tutayapa kipaumbele hivyo tuendelee kuwalinda na kujilinda kuwa na jamii salama,”alisema Missaile

Katika Mkutano huo uliofanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia  Novemba 4  hadi 6, 2024 na kuhudhuriwa na zaidi ya washiriki 320 kutoka ndani na nje ya nchi ikiwemo; Kenya, Uganda, Zimbabwe, Namibia, Rwanda, Nigeria, Ghana, Sudani ya Kusini, Cameroon, Senegal, Scotland na Ujerumani umekuwa ni muhimu sana.



Monday, November 4, 2024

NAIBU WAZIRI NDERIANANGA AMETEMBELEA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA VIONGOZI WA MKOA WA ARUSHA

 



Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshugulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mheshimiw Ummy Nderiananga amewasili kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha na kupokelewa na Katibu Tawala wa Mkoa huo Missaille Albino Musa leo Novemba 4, 2024.

Mhe. Nderiananga licha ya kusaini kitabu cha wageni amefanya mazungumzo na Katibu Tawala huyo kuhusu masuala ya menejimenti ya maafa pamoja na uwajibikaji na utekelezaji wa shughuli za Serikali mkoani humo.

Aidha, Mhe. Nderiananga yuko mkoani Arusha kwa lengo la kuhudhuria Mkutano wa Afya Moja Tanzania unaofanyika katika Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC) ukumbi wa Nyasa.

Mkutano huo unafanyika kuanzia tarehe 04 hadi 06 Novemba, 2024.




Thursday, October 31, 2024

"UTATUZI WA CHANGAMOTO ZA VIJANA BALEHE NI MSINGI WA TAIFA BORA"-DKT YONAZI.

 


Serikali imejidhatiti kutatua changamoto zinazowakumba vijana balehe kwa kuweka mazingira salama na rafiki kwa vijana kupitia afua mbalimbali zinazowawezesha vijana kufikia malengo yao na utimilifu wao kwa ujumla.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera ,Bunge na Uratibu Dkt.  Jim Yonazi akifungua mkutano wa wadau wanaotekeleza Afua za Vijana Balehe nchini (NAIA)kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum unaofanyika kuanzia 31Oktoba hadi 01 Novemba ,2024 Mkoani Dodoma.

Dkt. Yonazi amefafanua kwamba Ajenda ya Kitaifa ya kuwekeza katika Afya na Maendeleo ya Vijana Balehe nchini  iliyozinduliwa Aprili 17,2021  ilikua na lengo ni kuharakisha utekelezaji wa maeneo ya kipaumbele vinavyohusu afya na maendeleo ya vijana balehe katika Mikoa 13 yenye viashiria visivyoridhisha kuhusu afya na maendeleo ya vijana balehe nchini.

“Utekelezaji wa Ajenda umejikita katika nguzo kuu 6 za ambazo ni kuzuia maambukizi ya VVU, kutokomeza mimba za utotoni, kutokomeza ukatili wa kimwili, kingono na kisaikolojia, kuboresha hali ya lishe, kuhakikisha wavulana na wasichana wanabaki shule kukamilisha mzunguko wao wa elimu, na kuwaendeleza vijana katika ujuzi na ufundi ili wapate fursa ya kujiari na kuajiriwa.” amesema Dkt. Yonazi

Vile vile Dkt. Yonazi ametoa rai kwa wadau wote wanaohusika na masuala ya vijana balehe kufahamu kwamba ili kuwa na Taifa imara la leo na baadae ni vema kuwekeza katika kutatua changamoto za vijana balehe leo ikiwa na maana  ya kutatua changamoto za vijana kwa ajili ya kupata taifa imara.

“Kaulimbiu  ya mkutano huu inayosema Utatuzi wa Changamoto za Vijana balehe kwa taifa imara inachechemua utekelezaji wa Ajenda hii kwa upana wake kwa kuwa ndiyo pekee yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto hizo za vijana kwa sasa hivyo ni matumaini yangu kuwa kupitia mkutano huu, mtapata fursa ya kujadili kwa undani kuhusu changamoto zinazohusu vijana balehe kwa kutumia uzoefu wa utekelezaji wa Ajenda hii kwa kipindi cha miaka mitatu.” amesema Dkt. Yonazi.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju ametambua juhudi za  Mashirika ya Kimataifa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yaliyoanzisha miradi mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Vijana Balehe wanapata huduma rafiki za afya, elimu ya afya ya uzazi na kupata ujuzi na maarifa ya kuwafanya vijana wamudu maisha yao.

“Mafanikio haya hayajaja hivi hivi, bali ni jitihada kubwa mlizofanya ninyi Wadau wa Maendeleo kwa kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyeunda Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, hivyo nachukua  fursa hii kuwapongeza kwa dhati kwa ushirikiano huo mlioonesha na kufanikisha malengo ya Ajenda hii.” amesema Wakili Mpanju

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu  Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Wilson Mahela amewakumbusha vijana  kujitunza kwa kuzingatia mila na tamaduni za kitanzania zinazofaa na kuepukana kuiga kila wanachokiona kwenye mitandao ya kijamii.

Kwa niaba ya wadau, Mwakilishi kutoka Shirika linaloshughulikia masuala ya Watoto (UNICEF), Edgar Lungu ameishukuru Serikali kwa kuwezesha wadau kuweza kutekeleza afua zao na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuweza kufanikisha kusudio la Serikali kuwa na taifa lililo na vijana imara na taifa imara.

 


Friday, October 25, 2024

TANZANIA YAPIGIWA MFANO, KUKABILI MAAFA, MATUMIZI SAFI YA NISHATI YA KUPIKIA YATAJWA

Serikali ya Tanzania imeendelea kuonesha umahiri wake katika masuala ya menejimenti ya maafa nchini kwa kuzingatia mifumo sahihi ya kukabiliana na maafa na matumizi ya teknolojia ya kisasa pamoja na miongozo, kanuni na sheria mbalimbali zinazoongoza katika uratibu wa maafa hayo.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mheshimiwa Ummy Nderiananga wakati akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa Nane wa Ngazi ya Viongozi  kuhusu masuala ya kupunguza athari za maafa pamoja na Kikao cha Tisa cha Jukwaa la Kanda la Afrika la Kupunguza Athari za Maafa na vilivyofanyika jijini Windhoek nchini Namibia   kwa muda wa  siku nne kuanzia Oktoba 21 hadi 24 2024.

Mhe.Nderiananga ameeleza kuwa, uwekezaji mkubwa umefanywa na Serikali ya Tanzania hususan katika kuhakikisha teknolojia inavusha Taifa katika kukabili maafa ambapo Serikali ilianzisha Kituo cha Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Majanga  katika Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura nchini Tanzania ambacho kimeifanya nchi  kuwa mahiri katika masuala ya menejimenti ya maafa hususan katika kuzuia, kupunguza kujiandaa na kukabili maafa pindi yanapotokea.

Katika hatua nyingine Mhe.Nderiananga amezungumzia kuhusu mkakati wa miaka kumi wa Nishati safi ya Kupikia ambao utekelezaji wake umeanza mwaka 2024 hadi 2034,  ameeleza kuwa unalenga kuhifadhi mazingira, kulinda afya kwa kuzuia matumizi ya kuni na mkaa ili kuepuka athari za mabadiliko ya tabia nchi.

“Suala ya mabadiliko ya tabia nchi linaathiriwa na ukataji wa miti inayopelekea uharibifu mkubwa wa mazingira na kuchagiza ukosefu wa mvua za kutosha, uwepo wa ukame unaoathiri uzalishaji wa chakula, tunampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuzindua mkakati huo,”alisema

Amesema moja ya mikakati ambayo Tanzania imejiwekea ni kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.

"....Kama nchi tumejipanga kuhakikisha Taasisi za Serikali na Mashirika binafsi yanawekeza ipasavyo katika matumizi ya nishati safi kwa maslahi mapana ya mazingira safi na salama, Afya zetu na Afrika kwa ujumla " amesisitiza Mhe.Nderiananga

Kufuatia hatua huyo Mhe.Nderianga ametoa  wito kwa Mataifa mbalimbali duniani kufuata nyayo za Tanzania kwa kuhakikisha zinaweka mikakati madhubuti ya muda mfupi na mrefu ya Nishati safi ya Kupikia ili kuifanya Dunia kuwe mahali safi na salama pa kuishi.

Awali akifungua mkutano huo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Kazi na Uchukuzi Nchini Namibia Mhe. John Mutorwa amesema mikutano hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa ambapo awamu hii imefanyika nchini Namibia na kuwakutanisha wadau zaidi ya elfu moja wa  maafa kwa nchi za Afrika  wakiwemo wataalamu kutoka  katika ngazi za kitaifa, Serikali za mitaa, Mashirika ya Umoja wa Kitaifa na Kimataifa, Asasi za Kiraia, sekta binafsi, taasisi za elimu na utafiti na wanahabari, na hii imetajwa kuwa ni mafanikio makubwa kwa bara la Afrika.

“Tunashukuru kwa namna nchi zilivyojitokeza kushiriki mikutano hii muhimu katika kuhakikisha masuala ya maafa yanakabiliwa na kuwa na Afrika stahimilivu katika maafa, tunawashukuru sana Mawaziri mlioweza kushiriki mikutano hii, nasi tumepata heshima kama nchi, na tunaahidi kuendelea kuimarisha mashirikiano yetu kama Bara la Afrika,”alisema Mhe. Mutorwa

Aidha, alitoa rai kwa kila nchi kuona umuhimu wa kujipanga kukabili maafa bila kujali utofauti na hali za Mataifa ya Afrika, lengo kuyafikia na kuyaishi malengo na kuwa tayari kusimamia masuala haya.

“Maafa si jambo la kulifurahia, yanapaswa kupewa mwitikio mkubwa na mikakati yenye mashiko na inayotekelezeka lengo ni kulinda jamii zetu na kuweza kuifanya Dunia sehemu salama ya kuishi,hili litafanikiwa tukiendelea kushikamana kwa umoja wetu wa Afrika” alisisitiza




 

Thursday, October 24, 2024

SERIKALI YAPONGEZWA KUENDELEA KUONGEZA AFUA ZA UKIMWI

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Elibariki Emmmanuel Kingu ameipongeza Serikali na wadau wa maendeleo wanaoshirikiana na Serikali katika kutoa afua mbalimbali kukabiliana na ugonjwa wa Virusi vya UKIMWI.

Kauli hiyo ameitoa katika Ukumbi wa Bunge, Jijini Dodoma wakati kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI walipokutana mashirika yasiyo ya kiserikali ya Medical Reseach International(HJMFRI), International Centre for AIDS Care and Treatment Progaram (ICAP) na Management and Development for Health (MDH) yanayofanya kazi chini ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) katika semina ya kujengea uwezo kamati.

Ameeleza umuhimu wa Semina hiyo katika kutambua wadau wanaoshirikiana na Serikali kwa karibu na kuishauri serikali katika kuongeza muitikio wa kisiasa wa kuendelea kushawishi wadau hao kuwa na mkakati  stahimilivu katika kusaidia afua za UKIMWI.



Wednesday, October 23, 2024

DKT. YONAZI ATEMBELEA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI NAMIBIA

 


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ametembelea Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Namibia, ikiwa ni ziara yake ya kikazi nchini humo, lengo ni kushiriki Kikao cha Tisa cha Jukwaa la Kanda la Afrika la Kupunguza Athari za Maafa na Mkutano wa Nane wa Ngazi ya Viongozi (High Level Meeting) kuhusu masuala ya kupunguza athari za maafa vinavyofanyika Windhoek nchini Namibia.

Dkt. Yonazi ameambatana na Timu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwemo Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi hiyo Brig. Jenerali Hosea Ndagala, Mkurugenzi wa Tathmini na Ufuatiliaji Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Charles Msangi, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, Bw. January Kitunsi pamoja na Afisa Habari wa Ofisi hiyo Bi. Nyamagory Kitwara.

Aidha, katika mazungumzo na mwenyeji wake ambaye ni Afisa Mambo ya Nje Mkuu na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Namibia Bw. Elias Tamba ameeleza kuwa, nchi ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Naminia katika masuala mbalimbali kwa kuzingatia urafiki uliopo baina ya Mataifa hayo mawili toka kipindi ya Uhuru wa Namibia ambapo Tanzania inakumbukwa kwa mchango wake.



TANZANIA YANG’ARA KIMATAIFA KWA KUWA NA KITUO CHA UFUATILIAJI MAJANGA, WADAU WA MAAFA WAVUTIWA



Tanzania imetajwa kuwa  nchi ya kwanza barani Afrika kwa kuwa na Kituo cha Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Majanga na Tahadhari ya Mapema (National Emergency Operation and Communication Center Situation Room) katika Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura nchini Tanzania ambacho kimeifanya nchi  kuwa kinara  katika masuala ya menejimenti ya maafa hususan katika kuzuia, kupunguza kujiandaa na kukabili maafa pindi yanapotokea.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ametoa kauli hiyo jijini Windhoek nchini Namibia wakati akiwasilisha  mada katika Kikao cha Tisa cha Jukwaa la Kanda la Afrika la Kupunguza Madhara ya Maafa na Mkutano wa Nane wa Ngazi ya Viongozi kuhusu masuala ya kupunguza madhara ya maafa.

Akizungumzia umuhimu wa kituo hicho, Dkt. Yonazi amesema kituo hicho  kimeendelea kutumika  kufanya ufuatiliaji wa uwezekano wa kutokea kwa majanga kwa kutumia mifumo ya kiteknolojia ya kijiografia kwa majanga yanayotokana na hali ya hewa na haidrolojia kwa kutumia jukwaa la kielektroniki la MyDEWETRA.

“Mfumo huu umerahisisha ufuatiliaji wa mwenendo wa janga lililotabiriwa na kufanya uchambuzi wa kiwango cha madhara kwa jamii, miundombinu na mazingira, kuandaa taarifa za tahadhari ya mapema ya hatua za kuchukua ili kuzuia, kujiandaa na kukabili maafa, kuandaa taarifa ya mwenendo wa tukio na kusambaza kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya kusaidia uratibu na utekelezaji wa shughuli za kukabili na kurejesha hali,” Amesema  Dkt. Yonazi

Dkt. Yonazi amesema kuwa uanzishwaji wa kituo hicho cha ufuatiliaji wa majanga na tahadhari ya mapema umefanikiwa kutokana na mradi ulioanzishwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Madhara ya Maafa katika Kanda ya Afrika na  kufadhiliwa na Serikali ya Nchi ya Italia kupitia Shirika la Maendeleo la Italia (Italian Agency for Development Cooperation) ambapo Taasisi ya CIMA Research Foundation ya Italia imesadia kutoa utaalam wa utekelezaji wa shughuli zote.

Ameongeza kuwa  uwepo wa kituo hicho umesaidia sana Tanzania kuendelea kuwa kinara namba moja katika kukabiliana na  maafa kabla hayajaleta madhara.

Kufuatia umuhimu wa kituo hicho, Dkt. Yonazi ametoa wito kwa  Nchi  wanachama  pamoja na  mataifa mengine kuja Tanzania kwa lengo la  kujifunza na kubadilishana uzoefu kwa kuzingatia umuhimu wake.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoshiriki katika Kikao hicho cha siku nne ambacho kinatajia kumalizika   Oktoba 24, 2024 ambapo kikao hicho kimefanikiwa kuwakutanisha wadau zaidi ya elfu moja wa  maafa kwa nchi za Afrika  wakiwemo wataalamu kutoka  katika ngazi za kitaifa, Serikali za mitaa, Mashirika ya Umoja wa Kitaifa na Kimataifa, Asasi za Kiraia, sekta binafsi, taasisi za elimu na utafiti na wanahabari.



 

Monday, October 21, 2024

ENDELEENI KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA VIRUSI VYA UKIMWI” MHE. NDERIANANGA


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga ameihimiza jamii kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI nchini kwa kuendelea kuzingatia elimu inayotolewa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) ili kuunga mkono jitihada za Serikali dhidi ya mapambano hayo na kuyafikia malengo yaliyopo.

Mhe. Nderiananga ametoa wito huo wakati akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa ya utekelezaji wa Mkakati wa Tano wa Taifa wa kudhibiti UKIMWI wa mwaka 2021/22 hadi 2025/26 iliyowasilishwa katika ukumbi wa Bunge, jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo Dkt. Jerome Kamwele katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI.

Alisema, jamii haina budi kuendelea kujilinda na kuwalinda wengine kwa kuzingatia ushauri na elimu inayotolewa ili kuhakikisha hali ya maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI nchini ipungue na kuyafikia malengo ya kuzifikia sifuri tatu ifikapo 2030.

“Suala la UKIMWI siyo la TACAIDS na Ofisi ya Waziri Mkuu peke yake, Wizara ya Afya inapambania kuboresha huduma ya mama na Mtoto, Ofisi ya Rais TAMISEMI ndio imejenga miundombinu  na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewekeza Ujenzi hadi ngazi ya Kata kuna vituo Vya afya yote hii ni kusogeza huduma karibu na wananchi na uwekezaji huu tutaona matunda yake katika mapambano dhidi  ya VVU,”Alieleza Mhe. Nderiananga.

Pia aliishukuru TACAIDS kwa kufanya kazi nzuri ya kuifikia jamii kwa njia ya elimu huku akiwahimiza kuendelea kuongeza nguvu kwa vijana kwani ndilo kundi linaloongoza kwa maambukizi bila kusahau ni kundi muhimu katika uzalishaji na kujiletea maendeleo.

Awali akiwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa Mkakati wa Tano wa Taifa wa kudhibiti UKIMWI wa mwaka 2021/22 hadi 2025/26 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo Dkt. Jerome Kamwele alieleza kwamba, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi Oktoba 2024, tume hiyo imefanikiwa kuratibu kwa ufanisi utekelezaji wa mkakati katika sekta zote ndani ya Serikali na sekta binafsi, Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Taasisi za dini na wadau mbalimbali.

“Tume pia tumefanikiwa kupunguza maambukizi mapya ya VVU kutoka maambukizi 61,281 mwaka 2020 hadi maambukizi 60,000 mwaka 2023, kupungua kwa vifo vitokanavyo na UKIMWI kutoka vifo 32,639 mwaka 2020 hadi vifo 25,000 mwaka 2023 na kupungua kwa kiwango cha ubaguzi na unyanyapaa unaogokana na VVU kutokana na elimu ambayo imeendelea kutolewa kwa jamii na wadau,” alieleza Dkt. Kamwele.

Alifafanua kwamba mafanikio mengine ni pamoja na kufikia lengo la utekelezaji wa shabaha za Kimataifa 95-95-95 zinazohusu kupima na kutibu ifikapo 2026 ambapo asilimia 98 ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI  (WAVIU) wameanza tiba huku utafiti ukionyesha mwelekeo mzuri wa kufikia shabaha ya asilimia 95 ya tatu inayohusu kufubaza Virusi vya UKIMWI na kusisitiza ushirikiano wa pamoja kufikia asilimia 95 ya kwanza inayohusu watu wote wanaoishi na VVU kupima na kujua hali zao.

“Serikali inaendelea kuweka mkazo katika utekelezaji wa afua zinazolenga kupunguza kasi ya maambukizi mapya ya VVU hasa makundi maalum, kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha watu kupima kujua hali zao, kuongeza nguvu kuyafikia makundi maaalum hasa vijana, wanawake, wanaume, Watoto, watu wenye ulemavu na wanaoishi katika mazingira hatarishi,” alifafanua.

Aidha Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Bernadeta Mushashu aliipongeza TACAIDS kwa jitihada zake ikishirikiana na wadau kuhakikisha wananchi wanafanya shughuli zao za kiuchumi wakiwa katika hali njema ya kiafya.

Sunday, October 13, 2024

TANZANIA YAADHIMISHA SIKU YA MAAFA DUNIANI OKTOBA 13.

Tanzania imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya Maafa Duniani ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo Oktoba 13 ili kuendelea kukabiliana na kupunguza madhara yatokanayo na maafa nchini,

Akitoa Tamko la maadhimisho hayo katika Uwanja wa CCM Kirumba leo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema maafa usababisha madhara mbalimbali ikiwemo vifo, ulemavu wa kudumu, upotevu ,uharibifu wa mali, miundombinu na mazingira huku watoto na vijana wamekuwa wakikabiliwa na athari mbaya zaidi ikiwemo kukatizwa masomo, upungufu wa lishe, athari za kiafya, ulinzi na usalama.

Ameeleza kuwa siku hiyo ilianzishwa kwa Azimio namba 64/200 lililopitishwa na Baraza la Umoja wa Mataifa Disemba 21 mwaka 2009 , huadhimishwa kila mwaka, ili kuunganisha juhudi za kuwalinda watoto na vijana dhidi ya athari za majanga ambapo mikakati mbalimbali imewekwa ikiwemo kutoa mafunzo ya kujikinga na maafa,elimu ya hali ya hewa na jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,kuendeleza tafiti kuhusu madhara ya maafa na kutoa taarifa kwa umma ili kuongeza uelewa.

Akirejea taarifa iliyotolewa na serikali kupitia kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi zote kufuatia mwelekeo wa mvua za vuli katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2024 uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA) imeonyesha maeneo  mengi ya nchi yanayopata mvua hizo hayatapata mvua za kutosha hivyo wamejiandaa kuzuia, kupunguza madhara, kujiandaa kukabili na hali hiyo sambamba na  kurejesha hali nzuri.

Akitaja hatua sita za kuzingatia kukabiliana na hali hiyo amezitaka Mamlaka husika ziendelee kuhamasisha na kuwezesha matumizi ya mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi pamoja na utunzaji wa chakula cha binadamu na malisho ya mifugo, mamlaka husika ziimarishe utoaji taaluma ya matumizi ya mbinu za kilimo zinazohitaji maji kidogo pia taasisi za umma ikiwemo za elimu, afya na ofisi mbalimbali ziwe mfano wa kuweka mifumo ya kuvuna, kuhifadhi na kutumia maji ya mvua.

Ameongeza kuwa hatua zingine ni kuimarisha mikakati ya kuzuia milipuko ya magonjwa yanayoweza kujitokeza kutokana na upungufu wa upatikanaji wa maji safi na salama,taasisi husika zishirikiane na taasisi za elimu na mashirika ya maendeleo ili kutoa mafunzo kwa wananchi kuhusu jinsi ya kukabiliana na ukame na Wizara yenye dhamana ya elimu na taasisi zake kuhakikisha wanaendelea kuimarisha mitaala ya elimu ili ijumuishe masuala ya usalama shuleni, kupunguza hatari, na uelewa wa majanga na wakihakikisha mafunzo kwa walimu kuhusu mbinu za kufundisha masuala hayo kwa wanafunzi.

 

"Kaulimbiu ya mwaka huu ni "Elimu ni msingi katika kulinda na kuwawezesha vijana kwa mustakabali wa baadae usio na maafa" ili kuungana na kaulimbiu serikali imeendelea kushirikiana na wadau wa kitaifa na kimataifa kuimarisha mifumo ya elimu inayolenga kutoa maarifa na ujuzi wa kupunguza madhara ya maafa kwa watoto na vijana " anaeleza Mhe.Majaliwa

Pia serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya hali ya hewa nchini ikiwemo kufunga miundombinu ya kisasa ya hali hewa, mafunzo kwa watumishi kwa kuzingatia vigezo vya kitaifa na kimataifa, na kuweka mifumo wezeshi ya usambazaji wa taarifa ya hali ya hewa pamoja na kuimarisha mifumo ya uhakiki wa ubora wa huduma huku uwekezaji wa miundombinu unajumuisha ununuzi wa rada za hali ya hewa.

"Ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, Tanzania itakuwa na rada saba ambapo ni kiwango kikubwa cha rada katika nchi za Afrika Mashariki na kati nitumie fursa hii kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan,  kwa uwekezaji mkubwa katika eneo hilo pia kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwa makundi maalumu na kuweka mikakati thabiti inayolenga kuwawezesha vijana kiuchumi na kijamii pamoja na kuhakikisha Serikali inatoa elimu kwa wigo mpana na kuwezesha vijana kuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto za majanga na kujenga jamii iliyo na ustawi endelevu." anaeleza Mhe.Majaliwa.

Aidha aliwahimiza wananchi wote, taasisi za elimu, na wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwajengea uwezo vijana kupitia elimu itakayowasaidia kujenga stahimilivu dhidi ya majanga kwa sababu elimu ina nafasi kubwa katika kuhakikisha kizazi cha leo kinakuwa na mbinu za kulinda mazingira, kuzuia uharibifu wa maliasili, na kuhakikisha kuwa tunakuwa na mfumo thabiti wa kukabiliana na majanga.

Saturday, October 12, 2024

VIONGOZI WAHIMIZWA KUWEKA MKAZO, WATU KUJITOKEZA KUJIANDIKISHA

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe William Lukuvi ametoa rai kwa viongozi wa vyama vya siasa viongozi wa dini viongozi wa kimila na viongozi wengine kushirikiana katika kuhimiza wananchi kwenda kujiandikisha kwa sababu ni haki yao.

Wito huo umetolewa leo wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa uliofanyika katika Ukumbi wa LAPF Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi wa vyama Siasa.

Ameeleza kwamba haki ya mtu kujiandikisha inabaki pale pale awe mwanachama wa chama cha siasa au bila kuwa mwanachama wa chama cha siasa.

Waziri Lukuvi amesema, “tukijumlisha wanachama wetu wote kuna watu wanabaki  ambao hawako kwenye fungu lolote  katika vyama hivi vya siasa 19, lakini bado tunao ushawishi wa kutumia sauti zetu kuhimiza  wananchi wote wenye umri wa kujiandikisha wajiandikishe  na hatimae watumie nafasi hiyo kupiga kura”

Tunaowajibu kama viongozi wa vyama vya siasa kwa pamoja kuufanya uchaguzi huu uwe mzuri.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha (UDP) Mhe. John Cheyo amesema kuna changamoto moja ya matumizi wa mhuri wa chini ambao bado haieleweki vizuri, nadhani sisi kama wadau wa siasa tunayo nafasi kukubaliana kwa kuwa na kauli moja ya kusimamia uchaguzi kulingana na kanuni na sheria ambazo tumejiwekea.

“Tunadhamira ya kuwa na uchaguzi huru na haki kwa kila mmoja wetu na kama ilivyoelezwa na Waziri Lukuvi na hiyo ndiyo dhamira ya Mhe, Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassani,” alisema Mhe. Cheyo

Awali Makamu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, Joseph Selasini amesema huu ni mkutano ambao umeandaliwa tukiwa tunaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kujipanga katika maandalizi ya chaguzi zinazoendelea.