Monday, September 29, 2025

DKT. YONAZI: TUIMARISHE LISHE, TUPUNGUZE MAGONJWA SUGU

 


KATIBU Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi amewataka wadau kushirikiana na Serikali katika kuimarisha hali ya lishe nchini ili kupunguza kasi ya kuenea kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Amesema ulaji usio faa na mitindo mibaya ya maisha vimechangia kuongezeka kwa magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza jambo linalohatarisha maendeleo ya Taifa.

Dkt. Yonazi ameyasema hayo jijini Dar es salaam leo katika Mkutano Mkuu wa 11 wa Wadau wa Lishe unaoendelea katika kituo cha mikutano cha APC Bunju.

 Dkt. Yonazi amesema tafiti zinaonesha kuwa uzito uliozidi na uliokithiri ni chanzo kikuu cha magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza yakiwemo  kisukari, moyo, figo na baadhi ya saratani.

“Napenda kukumbusha wadau, taasisi na wataalam kushirikiana na serikali kufanya tafiti zitakazosaidia kuleta majibu ya changamoto za lishe, pamoja na kusaidia watu kubadili tabia za ulaji na mtindo wa maisha ili kuzuia magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza yanayohusiana na ulaji usiofaa na ambayo ni tishio kwa Taifa letu,”alisema Dkt. Yonazi

Dkt.Yonazi ameongeza kuwa  Takwimu zinaonesha  licha ya hali ya lishe nchini kuendelea kuimarika bado kuna changamoto hususani kwenye uzito uliozidi na kiriba tumbo hii kutokana maendeleo tunayoyapata na mabadiliko ya mtindo wa maisha hususani  ulaji usiofaa hivyo jitihada za pamoja kati ya wadau na serikali zinahitajika ili kukabiliana na tatizo hili.

Akizungumza kuhusu mkutano huo Dkt. Yonazi amesema lengo ni kupokea na kujadili hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa afua za lishe kwa kipindi cha Mwaka wa Tatu 2024/2025 katika maeneo mahsusi yaliyoanishwa kwenye Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe (2021/22-2025/26).

Vilevile amesema mkutano huo unatoa fursa kwa wadau wote wa lishe kujadili namna utekelezaji ulivyofanyika, changamoto na mikakati ya kufanikisha utekelezaji katika kipindi kilichobaki cha utekelezaji wa mpango huo hususan mwaka 2025/26.

Kwa mujibu wa Dkt. Yonazi mkutano huo unatazamiwa kuongeza msukumo mpya wa utekelezaji wa afua za lishe miongoni mwa wadau kama moja ya nguzo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

“Uwepo wenu hapa, ni uthibitisho tosha wa ushirikiano mlionao na utayari wenu katika kuhamasisha uboreshaji wa hali ya lishe kwa Watanzania, hususani makundi yanayoathirika zaidi ambayo ni watoto wadogo na wachanga, watu wenye mahitaji maalum, wanawake wajawazito na wale walio katika umri wa uzazi,”amesema Dkt. Yonazi.

Dkt. Yonazi amewashukuru  wadau wote walitoa mchango wa fedha na ushauri wa kitaalamu katika kufanikisha maandalizi ya mkutano huo na amewahakikishia kuwa serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za wadau ili kuhakikisha Taifa linapata mafanikio dhidi ya mapambano ya tatizo la utapiamlo.

 


Read More

Thursday, September 25, 2025

DKT. YONAZI ATOA WITO WATUMISHI KUBEBA MAONO YA DIRA YA TAIFA 2050

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi, ametoa wito kwa Viongozi, Menejimenti na Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake kubeba malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 kama sehemu ya wajibu wao wa kitaifa ili kuweza kufikia maono yaliyopo kufikia mwaka 2050.

 Dkt. Yonazi ametoa wito huo wakati ufunguzi wa Kikao cha Mazingativu ya Menejimenti, Wakuu wa taasisi na Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu na taasisi zake kinachofanyika leo Jijini Arusha.

 “Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 tayari imeshazinduliwa, Dira hii ni ramani ya mustakabali wa nchi yetu, ikitupa taswira ya nchi ambayo tunaihitaji kuwa nayo katika ndani ya miaka 25 ijayo, ili kufanikisha maono haya kila mmoja wetu anawajibu na anajambo la kulifanya, ni wajibu wetu kujiuliza kwamba nitachangia nini kuhakikisha nchi yangu inafikia maono haya kufikia mwaka 2050” ameeleza Dkt. Yonazi.

 Aidha, amebainisha kuwa, kila mmoja mahali pake pa kazi anawajibu kwa kuhakikisha nchi ya Tanzania inakuwa nchi bora na mahali bora pa kuishi kwa kuweka misingi bora ifikapo mwaka 2050.

 Akizungumza kuhusu kikao hicho, Dkt. Yonazi amebainisha kuwa, kikao hicho ni sehemu ya utamaduni wa Ofisi ya Waziri Mkuu kutenga muda kila mwaka kwa ajili ya kujitafakari, kujifunza na kujipanga upya kwa lengo la kuboresha utendaji katika kutekeleza majukumu ya Ofisi hiyo.

 Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha CPA. Amos Makalla ametoa wito kwa Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuwa wabunifu katika kufikiri na kutekeleza majukumu yao, ili kuweza kutoa huduma zinazokidhi mahitaji na matarajio ya wananchi kwa ufanisi zaidi.

“Dunia ya sasa inabadilika kwa kasi kubwa na changamoto zake zinahitaji mbinu mpya za kuzikabili, ni wajibu wetu kuwa wabunifu katika kufikiri na kutekeleza majukumu yetu, ili tuweze kutoa huduma zinazokidhi mahitaji na matarajio ya wananchi kwa ufanisi zaidi. Hivyo, kubadilika kulingana na wakati ni muhimu ili kuendana na mabadiliko ya kidunia, kitaifa na kijamii, tukizingatia misingi hii, tutakuwa na Ofisi yenye weledi, inayothamini maendeleo endelevu na inayokabiliana na changamoto kwa mafanikio” alisema.

 Aidha, Mkuu wa Wilaya huyo amebainisha kuwa “Kwa kuwa jukumu la uratibu, ufuatiliaji na tathmini ya shughuli zote za Serikali lipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, nitumie fursa hii kutoa rai kuwa tuendelee kulitekeleza jukumu hili kwa ufanisi wa hali ya juu. Kila taasisi inapaswa kuonesha matokeo halisi katika maeneo yake ya utekelezaji, tuweke mkazo zaidi katika kuhakikisha kwamba kazi zetu zinajikita kwenye matokeo yanayogusa maisha ya wananchi, badala ya kuishia kwenye michakato au utekelezaji usioonesha matokeo”.

Mbali na hayo Mhe. Mkude ametoa wito wa kushiriki uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kwani Uchaguzi huo ni fursa ya kipekee kushiriki katika kuimarisha misingi ya demokrasia na utawala bora.

 “Kila Mtanzania anatakiwa kutimiza haki na wajibu wake wa kikatiba kwa kupiga kura, ili kuchagua viongozi watakaoliongoza Taifa letu katika ngazi zote, aidha, ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha tunadumisha amani, mshikamano na utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi, ili Tanzania iendelee kubaki kuwa mfano bora wa utulivu, mshikamano na demokrasia barani Afrika” ameongeza.

 Kikao hicho kinaendelea Jijini Arusha, na mada mbalimbali zitawasilishwa ikiwemo ikiwemo Matumizi ya Akili Unde (AI) mahala pa kazi na mustakabali wa ajira kutokana na maendeleo ya kasi ya sayansi na teknolojia, masuala ya afya ya akili, fursa za uwekezaji kwa watumishi na maandalizi ya maisha baada ya kustaafu, masuala ya itifaki na ustaarabu na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ili kuweza kujiimarisha katika nyanja mbalimbali kitaaluma, kimaisha na kiutumishi.



Read More

Sunday, September 21, 2025

UBUNIFU UENDELEZAJI MAKAO MAKUU, MJI WA SERIKALI WAHITAJIKA- DKT. YONAZI

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi amesisitiza ubunifu katika uendelezaji wa Makao Makuu na Mji  Serikali ili kuweza kuvutia watalii wa ndani na nje.

Dkt. Yonazi ametoa msisitizo huo wakati wa ziara yake nchini Malaysia alipotembelea Mji Mkuu wa Utawala wa Malaysia uitwao Putrajaya.

"Ni muhimu wataalam kuzingatia masuala yanayofanya mji wa Serikali kuwa kivutio kwa wananchi na watalii kutoka nje. Masuala hayo ni ubunifu katika majengo, utunzaji wa mazingira na miundombinu na huduma muhimu hasa nyumba za ibada, huduma za fedha na maeneo ya kupumzika" amesema Dkt. Yonazi.

Aidha, Dkt.  Yonazi ameahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi za Kimataifa ili kubadilishana uzoefu na kujifuza masuala ambayo yataongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla.

Katika ziara hiyo Dkt. Yonazi ameambata na Balozi wa Tanzania nchini Malaysia Mhe. Dkt. Mahadhi Maalim, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali Bw. Paul Sangawe, Wataalam kutoka Ubalozi wa Tanzania Nchini Malaysia na kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.


Read More

Tuesday, September 16, 2025

DKT. YONAZI ATANGAZA FURSA ZILIZOPO MAKAO MAKUU YA MJI WA SERIKALI DODOMA NCHINI KOREA.


 Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi leo tarehe 16 Septemba, 2025 ameshiriki Mkutano wa Kimataifa wa Uendelezaji Miundombinu unaofanyika Jijini Seoul nchini Korea.

Katika Mkutano huo Dkt. Yonazi amepata fursa ya kuwasilisha mada kuhusu hatua iliyofikiwa katika zoezi lakuhamisha Makao Makuu na fursa za uendelezaji wa Jiji la Dodoma pamoja na Mji wa Serikali.

Aidha, Dkt. Yonazi amekutana na Mwenyekiti wa KFINCO na taasisi inayoratibu uendelezaji wa Mji wa Serikali Korea (National Agency For Administrative City Construction of KOREA-NA ACC) kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano baina Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) na Taasisi ya NAACC.

Katika mkutano huo, Dkt. Jim Yonazi ameongozana na Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali Bw. Paul Sangawe na wajumbe wengine kutoka Tanzania.



Read More

Saturday, September 6, 2025

AFDP YADHAMIRIA KUONGEZA UPATIKANAJI WA MBEGU BORA NCHINI

 


Ujumbe wa Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) kwa kushirikiana na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), umesema utaendelea kuwekeza katika uzalishaji na upatikanaji wa mbegu bora ili kuongeza tija kwa wakulima nchini.

Kauli hiyo imetolewa na kiongozi wa ujumbe huo, Bi. Nester Mashingaidze, alipozungumza na wakulima wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, alipokuwa akikagua utekelezaji wa programu hiyo inayolenga kuongeza uzalishaji wa mahindi, alizeti, maharage na mimea jamii ya mikunde.

“Tunalenga kuongeza upatikanaji wa mbegu bora kwa kushirikiana na taasisi kama TARI, ASA, na TOSCI ili kuwafikia wakulima wengi zaidi kwa wakati,” alisema Bi. Mashingaidze.

Kwa upande wake, Bw. Salum Mwinjaka – Mratibu wa Programu hiyo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, alisema AFDP inatekelezwa katika mikoa 11 ya Tanzania Bara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba. Alibainisha kuwa programu inajikita katika kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi, lishe na usawa wa kijinsia.

Naye, Mhandisi Enock Nyanda kutoka TAMISEMI, alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wizara za kisekta kufikisha huduma kwa wananchi kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo.

Wakulima waliopokea mafunzo kutoka kwenye programu hiyo wamesema imewasaidia kuachana na kilimo cha mazoea na kuhamia kwenye kilimo chenye tija kwa kutumia mbegu bora na za kisasa.



Read More

Tuesday, September 2, 2025

WAZALISHAJI WA MBEGU MKALAMA WAOMBA SERIKALI KUIMARISHA UFUNGASHAJI

 


Wazalishaji wa mbegu za alizeti katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, mkoani Singida, wameiomba Serikali kuongeza juhudi katika kuwawezesha kuandaa vifungashio bora vya mbegu ili kuongeza thamani ya mazao yao sokoni. 

 Wito huo umetolewa  wakati wa ziara ya ujumbe wa Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) kwa kushirikiana na wawakilishi kutoka IFAD katika Kijiji cha Ilunda, waliokuja kufuatilia utekelezaji wa programu hiyo. 

Bw. Athumani Ramadhani, mzalishaji wa mbegu aina ya Record, alisema: “Tunaomba Serikali itupe msaada wa kitaalamu kuandaa vifungashio bora vitakavyotangaza mbegu zetu na kuongeza thamani sokoni.” 

Naye Bi. Aziza Ramadhani aliongeza kuwa uzalishaji huo umeimarisha ushirikiano wao na taasisi za Serikali kama ASA na TOSCI, zinazopima ubora kabla ya mbegu kuingia sokoni. 

 Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mkalama, Bi. Asia, alisema Serikali inalenga kuifanya Mkalama kuwa mfano bora katika utekelezajiwa Programu ya Kilimo na Uvuvi (AFDP), huku akisisitiza umuhimu wa kuongezwa nguvu katika sekta hiyo.

 


Read More

Monday, September 1, 2025

DKT. KILABUKO: OFISI YA WAZIRI MKUU ITAENDELEA KUSHIRIKIANA NA IFAD

 


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. James Kilabuko, amesema Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) katika utekelezaji wa miradi ya kilimo na uvuvi nchini. 

Ametoa kauli hiyo Jijini Dodoma wakati wa kikao na ujumbe wa IFAD waliopo nchini kufuatilia utekelezaji wa mradi wa programu ya kuendeleza sekta ya Kilimo na uvuvi (AFDP). 

“Nawahakikishia kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ipo tayari kutoa ushirikiano wote unaohitajika ili kuhakikisha miradi mnayoitekeleza inaleta matokeo chanya,” amesema Dkt. Kilabuko.



Read More