Tuesday, March 17, 2020

TIMU ZA DHARURA ZA KUKABILI MAGONJWA AMBUKIZI YA MLIPUKO ZATAKIWA KUTUMIA DHANA YA AFYA MOJA



Dhana ya Afya moja ambayo hujikita katika kujumuisha sekta zote za Afya katika kujiandaa, kufuatilia  na kukabili magonjwa yanayomuathiri binadamu imeendelea kufundishwa kwa Wataalamu wa sekta hizo za Afya, ikiwa ni Sekta ya Afya  ya Binadamu, Wanyamapori, Mifugo, Kilimo na Mazingira, ili wataalamu hao watumie dhana hiyo kuimarisha udhibiti wa magonjwa ambukizi kati ya Binadamu na wanyama  ambayo hutokea mara kwa mara katika maeneo ya mipakani kutokana na kuwepo kwa  muingiliano mkubwa kati ya  watu na wanyama katika mazingira yao.

Katika kuimarisha Afya ya binadamu, Shirika la Chakula na Kilimo  la Umoja wa Mataifa (FAO), pamoja  na watalaamu kutoka Wizara ya Mifugo na  Uvuvi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine wamewapa mafunzo wataalamu wa sekta za Afya wanao toka katika Halmashauri za Mkoa wa Kagera, Rukwa, Katavi,  Rukwa na Songwe zilizo mipakani juu ya namna ya kujiandaa na kukabili magonjwa ambukizi ya mlipuko kama  vile Ugonjwa wa Corona na Ebola kwa kutumia Dhana ya Afya  moja.

Akiongea wakati wa kufungua mafunzo hayo leo tarehe 17 Machi, 2020, Jijini Dodoma, Mkurugenzi wa  Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe, amebainisha kuwa ushirikiano wa wataalam na sekta za Afya  kwa kutumia dhana ya Afya Moja hivi sasa ni agenda ya dunia nzima. Aidha, ameeleza kuwa Dhana hiyo imekusudiwa kutumika maeneo ya mipakani   ambapo mwingiliano huo huchochewa na wasafiri kutoka eneo moja kwenda jingine, ongezeko la watu duniani, mabadiliko ya tabia nchi, utandawazi, ongezeko la mahitaji ya maji na chakula.

“Mafunzo haya  ni  muhimu sana nchini kwa kujenga uwezo wa nchi katika utayari wa kukabiliana na magonjwa yanayosambazwa na wanyama na kuathiri wanyama na binadamu.Tanzania tumeabiwa yupo mgonjwa wa Corona19, ambapo Tumeambiwa mgonjwa anaendelea vizuri na matibabu, na serikali inaendelea kuchukua hatua za madhubuti za kuhakikisha ugonjwa huu unadhibitiwa ili usisambae nchini”.

Awali akiongea katika mafunzo hayo, Mkuu wa Ndaki ya Tiba ya  Mifugo, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine-SUA, Profesa, Amandus Muhairwa amebainisha kuwa  sekta za Afya zikishirikiana katika Kudhibiti magojwa zitasaidia kuimarisha Afya ya Binadamu kwa kuwa kila sekta itakuwa inachukuwa tahadhari kwa wakati.

Aidha, Mratibu kutoka FAO wa Mradi wa  ECTAD Tanzania, Fasina Folorunso amabainisha kuwa FAO inaendelea kushirikiana na serikali mya Tanzania kupitia Dawati la  Afya moja katika kujenga uwezo wa kukabiliana na magonjwa ambukizi ya mlipuko kwenye ngazi ya mkoa na wilaya hususani maeneo ya mipakani.


Katika kuhakikisha watalaam hao kutoka sekta za Afya wanaweza kutumia Dhana  hiyo katika kudhibiti magonjwa katika maeneo ya mipakani wameweza kujengewa uwezo wa namna ya kutoa taarifa za milipuko ya magonjwa ambukizi kama vile ugonjwa wa Corona 19 na Ebola  yanapotokea maeneo ya mipakani, namna ya kuunda vikosi vya kufuatilia na kukabili Ugonjwa, Mawasiliano wakati wa kufuatilia na kukabili magonjwa hayo kwa kutumia Dhana ya Afya moja,  pamoja na masuala ya kutumia vifaa Kinga Binafsi vya Kitaalamu.


Tarehe 13 Februari 2018, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alizindua Dawati la Uratibu la Afya moja chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, likiwa na lengo la kusimamia na kuratibu shughuli za Afya moja nchini. Kwa kutambua umuhimu huo Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia Dawati la Uratibu wa Afya moja  kwa kushirikiana Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) wakishirikiana na USAID, OIE, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine - SUA wakishirikiana na Chuo Kikuu cha Kansas cha nchini Marekani waliandaa na kuratibu mafuzo hayo.

MWISHO.


Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe akisisitiza umuhimu wa kutumia Dhana ya Afya moja ambayo hujikita katika kujumuisha sekta zote za Afya katika kujiandaa, kufuatilia na kukabili magonjwa yanayomuathiri binadamu wakati wa mafunzo kwa timu za dharura za kukabili magonjwa ambukizi ya mlipuko leo, Jijini Dodoma, tarehe 17 Machi, 2020.
Baadhi ya wataalamu wa sekta za Afya kutoka kwa timu za dharura za kukabili magonjwa ya mlipuko kutoka ngazi ya mkoa na wilaya zilizo mipakani, wakifuatilia mafunzo ya kukabili magonjwa ya ambukizi ya mlipuko kwa kutumia Dhana ya Afya moja, wakati wa mafunzo hayo, leo Jijini Dodoma, tarehe 17 Machi, 2020.
Mratibu wa Mradi wa ECTAD Tanzania kutoka FAO, Fasina Folorunso akisisitiza umuhimu wa kuimarisha Afya ya Binadamu kwa sekta za Afya kutumia Dhana ya Afya Moja, wakati wa mafunzo kwa timu za dharura za kukabili magonjwa ya ambukizi ya mlipuko leo, Jijini Dodoma, tarehe 17 Machi, 2020.
Mkuu wa Ndaki ya  Tiba ya Mifugo, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine-SUA, Profesa, Amandus Muhairwa akisisitiza sekta ya Afya ya mifungo na Afya ya Binadamu, kushirikiana katika kujiandaa, kufuatilia na kukabili magonjwa yanayomuathiri binadamu wakati wa mafunzo kwa timu za dharura za kukabili magonjwa ambukizi ya mlipuko kwa kutumia Dhana ya Afya moja  leo, Jijini Dodoma, tarehe 17 Machi, 2020.

Baadhi ya Wakufunzi na wataalamu wa sekta za Afya kutoka kwa timu za dharura za kukabili magonjwa ya mlipuko kutoka ngazi ya mkoa na wilaya zilizo mipakani, wakifuatilia mafunzo ya kukabili magonjwa ya ambukizi ya mlipuko kwa kutumia Dhana ya Afya moja, wakati wa mafunzo hayo, leo Jijini Dodoma, tarehe 17 Machi, 2020.

Mkufunzi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Selemani Makungu, akieleza jambo wakati wa mafunzo kwa  wataalamu wa sekta za Afya kutoka kwa timu za dharura za kukabili magonjwa ya mlipuko kutoka ngazi ya mkoa na wilaya zilizo mipakani, kwa kutumia Dhana ya Afya moja, wakati wa mafunzo hayo, leo Jijini Dodoma, tarehe 17 Machi, 2020.
Baadhi ya Wakufunzi na wataalamu wa sekta za Afya kutoka kwa timu za dharura za kukabili magonjwa ya mlipuko kutoka ngazi ya mkoa na wilaya zilizo mipakani, wakifuatilia mafunzo ya kukabili magonjwa ya ambukizi ya mlipuko kwa kutumia Dhana ya Afya moja, wakati wa mafunzo hayo, leo Jijini Dodoma, tarehe 17 Machi, 2020.

Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu wa sekta za Afya kutoka kwa timu za dharura za kukabili magonjwa ambukizi ya mlipuko kutoka ngazi ya mkoa na wilaya zilizo mipakani, kwa kutumia Dhana ya Afya moja, wakati wa mafunzo hayo, leo Jijini Dodoma, tarehe 17 Machi, 2020.

Read More

Friday, March 13, 2020

MAJALIWA:TUNATAMBUA UMUHIMU WA DINI ZOTE


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inatambua umuhimu wa dini zote katika kuimarisha na kudumisha amani nchini. 

“Dini zinasaidia nchi kuwa tulivu, dini hizi zote ndio zinafanya hata uongozi wa Kitaifa unakuwa rahisi kwani zinaisaidia Serikali katika kuiendesha nchi.“

Ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Machi 13, 2020) baada ya kuzindua msikiti wa Al Nur mjini Ruangwa. Amesesisitiza umuhimu wa viongozi wa dini kushirikiana na Serikali.

“Hakuna siku Serikali itakuja kuitupa dini tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na dini zote nchini na ndio maana Serikali imeridhia uundwaji wa Kamati za Amani.“ 

Kamati za Amani ambazo zimeundwa kuanzia ngazi ya Taifa hadi Kata zinashirikisha viongozi wa dini zote ambao wanakutana na kujadili changamoto zinazowakabili na kuishauri Serikali.

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo ameushukuru na kuupongeza uongozi wa Taasisi ya Al-Hikma kwa kuwajengea nyumba kubwa ya ibada.

Awali, Mwenyekiti wa Taasisi ya Al-Hikma, Sheikh Sharif Abdulkader amesema anamshukuru Mwenyezi Mungu na Serikali ya Awamu ya Tano kwa sababu viongozi wake wanaushirikiano mzuri na taasisi za kidini.

Amesema akiwa nchini Saudia Arabia alikutana na Muft wa Sudan ambaye alipomwambia anatoka Tanzania alionesha kushangazwa na namna kiongozi wa nchi alivyoenda kwenye mashindano ya Quran.

“Nikamwambia hiyo ndio desturi ya Watanzania watu wa dini zote wanashirikiana katika kutunza amani ya nchi, kiongozi yule alitokwa na machozi kwa kuwa kwenye nchi nyingine mambo kama hayo hakuna, hivyo tuendelee kuichunga amani yetu na kushirikiana na Serikali.“

Ameongeza kuwa “Hata Rais (Dkt. John Pombe Magufuli) aliomba hadharani tumjengee msikiti Chato, ni jambo zuri viongozi wanakuwa karibu na watu wa dini zote, hii inaonesha amani tuliyonayo Tanzania. Tuichunge amani yetu na tusisikilize maneno ya watu ambao hawaitakii kheri kwa nchi hii.“

(mwisho)
Read More

WAZIRI MKUU, KASSIM MAJALIWA AKIFURAHIA JAMBO NA WATOTO KIJIJINI KWAKE.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akifurahia jambo na watoto, kijijini kwake Nandagala, wilayani Ruangwa Machi 13, 2020.

Read More

WAZIRI MKUU AFUNGUA MSIKITI WA ANNUR WILAYANI RUANGWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akisalimiana na Masheikh wa Wilaya ya Ruangwa wakati akiwasili kwenye Msikiti wa Annur kushiriki swala ya ijumaa na kuufungua rasmi msikiti huo, uliyojengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Al-Hikma Foundation, wilayani Ruangwa katika Mkoa wa Lindi Machi 13, 2020.

Baadhi ya wananchi waumini wakiwa kwenye Msikiti wa Annur, baada ya swala ya ijumaa wakimsikiliza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, wilayani Ruangwa katika Mkoa wa Lindi Machi 13, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akisikiliza mawaidha, yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Al-Hikma, Sheikh Sharif Abdulqader, kwenye Msikiti wa Annur aliposhiriki swala ya ijumaa na kuufungua rasmi Msikiti wa Annur, uliyojengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Al-Hikma Foundation, wilayani Ruangwa katika Mkoa wa Lindi Machi 13, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akihutubia wananchi, kwenye Msikiti wa Annur, baada ya swala ya ijumaa na baadae kufungua rasmi Msikiti huo uliyojengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Al-Hikma Foundation, wilayani Ruangwa katika Mkoa wa Lindi Machi 13, 2020.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akisikiliza mawaidha, yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Al-Hikma, Sheikh Sharif Abdulqader, kwenye Msikiti wa Annur aliposhiriki swala ya ijumaa na kuufungua rasmi Msikiti wa Annur, uliyojengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Al-Hikma Foundation, wilayani Ruangwa katika Mkoa wa Lindi Machi 13, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiweka jibe la msingi kwenye Msikiti wa Annur, uliyojengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Al-Hikma Foundation, wilayani Ruangwa katika Mkoa wa Lindi Machi 13, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Mwenyekiti wa Taasisi ya Al-Hikma, Sheikh Sharif Abdulqader, kwenye Msikiti wa Annur baada ya kufungua rasmi Msikiti wa Annur, uliyojengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Al-Hikma Foundation, wilayani Ruangwa katika Mkoa wa Lindi Machi 13, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiwasalimia wananchi, kwenye Msikiti wa Annur, baada ya swala ya ijumaa na kufungua rasmi Msikiti huo uliyojengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Al-Hikma Foundation, wilayani Ruangwa katika Mkoa wa Lindi Machi 13, 2020.


Read More

WAZIRI KAIRUKI: MFUKO WA KUKOPESHA WAWEKEZAJI KUKOMBOA WENGI

Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Uswidi na Afrika Mashariki Bw. Jan Furuvald akiwasilisha mada wakati wa kongamano hilo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akiteta jambo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  Dkt. Damas Ndumbaro wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki na Wanachama wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Uswidi na Afrika Mashariki kaika Ukumbi wa Mikutano Serena Hotel Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Machi, 2020.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akiteta jambo na Balozi wa Tanznaia nchini Sweden Mhe. Dkt. Wilibrod Slaa wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki na Wanachama wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Uswidi na Afrika Mashariki kaika Ukumbi wa Mikutano Serena Hotel Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Machi, 2020
Rais wa TCCIA Bw. Paul Koyi akihutubia wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki na Wanachama wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Uswidi na Afrika Mashariki kaika Ukumbi wa Mikutano Serena Hotel Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Machi, 2020
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akiteta jambo na Balozi wa Tanzania nchini Swiden Mhe. Dkt. Wilibrod Slaa  wakati wa kongamano hilo.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania TPSF, Godfrey Sembeye  akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Kipindi cha Supa Breakfast kinachorushwa na Eastafrica radio wakati wa kongamano hilo.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Zungu akieleza mikakati ya ofisi yake katika kuvutia wawekezaji wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki na Wanachama wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Uswidi na Afrika Mashariki kaika Ukumbi wa Mikutano Serena Hotel Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Machi, 2020.
Sehemu ya wajumbe wakifuatilia mada mbalimbali katika Kongamano hilo.
Sehemu ya wajumbe wakifuatilia mada mbalimbali katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki na Wanachama wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Uswidi na Afrika Mashariki kaika Ukumbi wa Mikutano Serena Hotel Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Machi, 2020.

Read More

Thursday, March 12, 2020

MAJALIWA: WANAVYUO CHINA WAENDELEA NA MASOMO KWA NJIA YA MTANDAO

WAZIRI MKUU Kassim Mjaliwa amesema wanafunzi wanaosoma katika vyuo vikuu mbalimbali nchini China waliozuiwa kutokana na mlipuko wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona wote wanaendelea na masomo yao kwa njia ya mtandao.

“Tehama sasa imefikia katika hatua nzuri kwa sababu Mhadhili mmoja anaweza kuwafundisha wanafunzi wake wote popote walipo kwa njia ya mtandao. Tehama imewezesha wanafunzi waliozuiwa kurudi nchini China kuendelea na masomo wakiwa nyumbani kwao.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Machi 12, 2020) katika mahafali ya 38 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT), katika uwanja wa Ilulu mjini Lindi. Amesema baada ya virusi vya corona kuikumba China vyuo vilifungwa na sasa vimefunguliwa na wanafunzi wanasomo kwa njia ya mtandao.

Pia, Waziri Mkuu amewaeleza wahitimu wa CKHT kuwa vyeti walivyotunukiwa ni tuzo halali kwa juhudi na jitihada walizoonesha katika masomo yao, hivyo wanaporejea kwenye jamii wahakikishe wanaipatia tuzo ya utendaji bora na ufanisi itakayoakisi viwango vilivyoainishwa kwenye vyeti vyao. 

“Nendeni mkaidhihirishe tuzo hii ya pili katika utendaji wenu na maisha yenu ya kila siku, iwe ni katika sekta rasmi au sekta isiyokuwa rasmi.  Hakikisheni mnaonesha tofauti katika kutafuta majibu ya maswali mbalimbali yanayowakabili Watanzania kuhusu mustakabali mzima wa kujiletea maendeleo.”

Waziri Mkuu amesema amefuatilia kwa karibu maelezo ya Viongozi waliotangulia kuhusu umuhimu na hata mafanikio ya chuo hicho ambapo amewataka watambue kwamba Serikali inakiangalia kwa jicho la karibu sana kwa kuwa kimekaa kimkakati zaidi kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa.

Amesema licha yachangamoto mbalimbali zilizopo, Serikali imeweza kuanzisha chuo hiko na kukiona kikiendelea kutanuka hadi nje ya mipaka ya nchi yetu.  “Haya ni mafanikio makubwa na ya kujivunia. Tunawashukuru waasisi wa Taifa letu kwa maono haya makubwa kuhusu Tanzania.”  

Waziri Mkuu amesema Mwasisi wa Taifa letu, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliona mbali sana wakati akianzisha mchakato wa kuanzisha Chuo hiki kwa kusema angependa kuona taasisi inawawezesha watu wazima wengi waweze kuendelea na elimu ya juu pasipo kuacha kazi zao. 

Vilevile, aliongeza kwa kusema, “Kwa nchi maskini kama Tanzania, hakuna Taasisi nyingine ya elimu ya juu inayoweza kuwa ya msaada zaidi kwa watu wetu”. 

Waziri Mkuu amesema ukweli wa kauli hiyo unaendelea kudhihirishwa siku hadi siku kupitia mafanikio ya chuo hicho. “Tutake tusitake, elimu ya juu inayoweza kusaidia watanzania wengi zaidi ni hii ya kupitia mfumo wa Elimu Masafa na Huria.”

Waziri Mkuu ameongeza kuwa umuhimu na thamani ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na vyuo vingine utakuwa na maana tu pale ambapo vitakuwa na mchango kwenye maendeleo ya nchi. 

“Kwa miaka nenda rudi, chuo kimehitimisha wataalamu lukuki, ambao wengi wameingia kwenye sekta mbalimbali za utumishi na uzalishaji na kutoa mchango muhimu sana kwenye maendeleo ya nchi yetu.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametoa rai kwa uongozi wa CKHT na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TVV) wahakikishe kuwa udahili wa CKHT unatanuliwa kwa sababu hadi sasa chuo kina kozi moja tu ya maandalizi kwa ajili ya kuwaandaa vijana kuingia kwenye Shahada. 

Waziri Mkuu amesema katika kuongeza udahili kwenye elimu ya juu, ameshauri wawe na kozi ama programu za maandalizi kwa wale wanaotaka kusoma stashahada na kwa wale wa cheti pia. 

Amesema matokeo ya programu hizo yataongeza ushiriki wa Watanzania wengi kwenye elimu ya juu. “Wito wangu kwa TCU nchini kuhakikisha inasimimia na kuongoza, kwa kushirikiana na CKHT katika uanzishwaji wa programu hizi kwa kuzingatia viwango vya juu vya ubora wa elimu ya juu.”

Katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 698 walitunikiwa vyeti wakiwemo 20 wa Shahada za Uzamivu (PhD) na wengine 185 Shahada na Stashahada za Uzamili, wengine 344 walitunukiwa Shahada ya Kwanza, 166 walitunikiwa Stashahada na Astashahada mbalimbali. 

Mahafali hayo yamehudhuliwa naWaziri Mkuu Mstaafu na Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania Mizengo Peter Pinda, Mkuu wa Mkoa wa Lindi na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Chuo Mkoani Lindi Godfrey W. Zambi,

Wengine ni Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania, Profesa Rwekaza Mukandala, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania Profesa Elifas Tozo Bisanda na wakuu wa wilaya za mkoa wa Lindi

Read More

WAZIRI MHAGAMA ATOA MAAGIZO MAZITO USIMAMIZI VITALU NYUMBA



Na. OWM, Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama, ametoa maagizo sita kwa  waratibu na wadau wa Programu ya mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba “Greenhouse”na kuwataka kutekeleza, kwa wakati na ufanisi maagizo yake yanayojikita katika  kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa mafunzo hayo ili yawe na ubora zaidi na tija kwa vijana.

Waziri Mhagama ameagiza  kufanyika maamuzi ya haraka yatakayowezesha vijana katika halmashauri ambazo bado mradi huo haujafika wanafikiwa. Aidha, Fedha zote zilizokusanywa na vijana katika awamu ya kwanza ya mafunzo hayo zikaguliwe na vijana washirikishwe ili waweze kutoa taarifa ya idadi ya mazao waliyozalisha na kiwango walichoweza kuuza. 

Akitoa magizo hayo leo,  Machi 11 2020 kwa kikao kilichowakutanisha vijana, Wadau,Waratibu ambao ni Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Kilimo, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na wakandarasi ambao walijenga vitalu nyumba, amewagiza  kuanzishwa mfumo wa ufuatiliaji ambao utakuwa na taarifa ya utekelezaji wa majukumu. 

"Kuanzia sasa  ni lazima mikopo kwa vijana ipatikane kwa wakati,  nataka upatikanaji wa mikopo ambayo itawasaidia vijana hao kuanzisha vitalu nyumba vyao, pia tengenezeni  mfumo wa ukusanyaji mapato na matumizi. Wakandarasi waliojenga vitalu nyumba katika halmashauri 84 awamu ya kwanza fanyeni  marekebisho kwenye  vitalu nyumba ambavyo vimekuwa na matatizo. Nataka usimamizi na uendeshaji wa programu ya mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba “Greenhouse” uwe chachu  ya  kuongeza ajira kwa vijana katika sekta ya kilimo" amesisitiza Mhagama.

Waziri Mhagama amefafanu akuwa,  Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ina nia ya dhati ya kuwawezesha vijana kupitia programu mbalimbali inazoazisha kwa lengo la kuwasaidia vijana kuondokana na changamoto ya ajira.

“Serikali ina lengo la kufikisha ujuzi huo wa kilimo cha kisasa katika halmashauri zote za Tanzania bara kwa kuwa asilimia 63 ya fursa za ajira zinapatikana kwenye kilimo na tena maeneo ya vijijini,” alisema Mhagama 

Waziri Mhagama, amebainisha kuwa,  Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ndio yenye dhamana na masuala ya vijana iliamua kupitia ilani ya uchaguzi ibara ya 6 kifungu (a) inayosema kuhamasisha kilimo kupitia kauli mbiu ya Kilimo Kwanza kwa kuwawezesha wakulima kupata mafunzo ya kilimo cha kisasa, pembejeo, zana za kisasa na wataalamu wa ugani pamoja na mbinu za kuyafikia masoko ya uhakika ya mazao yao, ambao ulipelekea kutambua umuhimu wa mchango wa vijana hasa waliopo vijijini ndipo mradi huu wa Kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba ulianzishwa kwa lengo la kuwezesha vijana,” amesema Mhagama.


“Mataifa makubwa mengi yaliyoendelea wamekuwa wakitumia kilimo cha aina hiyo kwa lengo la kulima kisasa, kuongeza thamani ya mazao, kupata masoko endelevu na la uhakika na kulima kwa tija, hivyo tukiwawezesha vijana wetu watanufaika na kilimo hicho na sekta hiyo italeta tija katika kukuza uchumi wa nchi,” alieleza Mhagama.

Waziri Mhagama amewataka vijana kutumia ujuzi waliopata katika mafunzo hayo ili waweze kusimamia mradi huo vizuri na wajenge moyo wa kuthubutu katika kuwasaidia vijana wenzao kupata ujuzi wa mafunzo hayo ya kilimo cha kisasa.


Wakati huo huo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw. Andrew Massawe amesema kuwa ameyakupokea maagizo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi ili programu hiyo ya mafunzo ya kilimo cha kisasa iweze kuwa endelevu.


“Ofisi ya Waziri Mkuu iliona umuhimu wa kushirikiana na , Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Kilimo, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, wakandarasi pamoja na Vijana ili kutathmini utekelezaji wa mradi huo na kuona namna ya kukabili changamoto ambazo zilijitokeza, mafanikio yaliyopatikana ili kuona namna bora ya kuimarisha mafunzo hayo,” amesema Massawe.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Ally Msaki ameelezea maazimio waliyofikia pamoja na wadau katika kuimaarisha usimamizi na uendeshaji wa mafunzo hayo

"Pamoja na kuangalia namna bora ya kuendesha mafunzo haya, tumemua kuwa  tutasimamia uwepo wa utaratibu maalum wa makusanyo, utunzaji na matumizi ya fedha, kuwezesha vijana kuwa na ujuzi wa kuongeza thamani ya mazao, kuelezea wananchi mafanikio yaliyopatikana kupitia mradi huo wa kilimo cha Kitalu nyumba,kuwezesha vijana kufanya kilimo biashara na uwepo wa muendelezo wa kutoa mafunzo na kuongeza vitalu nyumba katika kila halmashauri" amesitiza Msaki.

Naye Mmoja wa wanufaika wa Programu hiyo Bw. Festo Masiba ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo yamewajengea ujuzi mkubwa wa kuweza kulima kwa tija.


“Tunaishukuru Serikali kwa kutuamini sisi vijana na kutuwezesha kupata mafunzo ya Kilimo bora kwa kutumia eneo dogo na upatikanaji wa mazao ni mwingi, tumeweza kukua kiuchumi na tunaujuzi wa kuwajengea wadau wengine vitalu nyumba,” alisema Masiba .


MWISHO
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw. Andrew Massawe akieleza jambo wakati wa mkutano huo uliofanyika machi 11, 2020 katika Ukumbi wa Landmark Kilimani, Jijini Dodoma.
Baadhi ya Wakuu wa Idara kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu wakifuatilia mijadala wakati wa mkutano huo.
Sehemu ya vijana wakifuatilia kwa makini hotuba ya Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) walipokutana kujadili namna bora ya kuimarisha mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba.
Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (wa nne kutoka kulia waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wataalamu kutoka ofisi yake, Wadau na Vijana wapokutana kwa lengo la kujadili namna bora ya kuimarisha mafunzo ya Kilimo kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba katika Ukumbi wa Landmark Kilimani, Jijini Dodoma.
Read More

WAZIRI KAIRUKI: MFUKO WA KUKOPESHA WAWEKEZAJI KUKOMBOA WENGI

NA. MWANDISHI WETU
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imewezesha kuanzisha mfuko maalum wa kukopesha watu wenye nia ya kuwekeza kwenye viwanda vya kati na vikubwa lengo likiwa ni kuwanufaisha Watanzania waliokosa mitaji na wenye nia ya kuwekeza nchini.
Mfuko huo ulioanzishwa Februari 22 mwaka huu utakuwa ukikopesha Watanzania kuanzia kiwango cha shilingi  milioni 8 hadi 50 kwa wenye nia ya kuwekeza viwanda vya kati na shilingi milioni 50 hadi 300 kwa wenye nia ya kuwekeza kwenye viwanda vikubwa.
Aidha, ofisi hiyo inashirikiana na taasisi nyingine kuendesha mfuko huo ikiwepo Mfuko wa Hifadhi za Jamii (NSSF), Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Shirika la Viwanda Vidogo Tanzania (SIDO) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Hayo yamebainishwa hii leo (Machi 12, 2020) Jijini Dar Es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angellah Kairuki wakati akizungumza na Waandishi wa Habari  mara baada ya kufungua Kongamano la pili la Biashara na Uwekezaji la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Sweden linaloendelea kwa siku mbili Jijini humo.
Kairuki amesema Tanzania hivi sasa imeimarisha Mazingira ya Uwekezaji ambapo tangu kuingia kwa Rais Magufuli Madarakani hakuna kodi yoyote iliyoongezwa kwenye biashara na uwekezaji huku kodi zaidi ya 168 zikifutwa katika kipindi cha miaka miwili zikiwepo kodi 105 za kilimo.
Wakati akifungua Kongamano hilo Waziri Kairuki aliwataka Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza nchini Tanzania kwa kueleza kuwa Sera, Sheria na miundombinu yake imeboreshwa kwa kiwango kikubwa.
"Tunazo fursa nyingi za uwekezaji hapa Tanzania, tuna fursa kwenye Kilimo cha mazao ya chakula na biashara pamoja na mnyororo wake wa thamani kwenye sekta hiyo, tunahitaji uwekezaji wa viwanda mbalimbali vikiwepo vya Dawa na  vifaa tiba, mafuta ya kula na vinginevyo vingi" alisema Waziri Kairuki.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dkt Wilbrod Slaa amesema Wafanyabiashara wa NORDIC wameisifu Serikali ya Tanzania  kwa kuondoa rushwa na kuimarisha utendaji wa wazi Serikalini suala ambalo awali lilikuwa likuwapa changamoto kubwa.
"Nimekuwa nakutana na wafanyabiashara na wawekezaji wengi wa Sweden jambo kubwa nililolipata kutoka kwao ni kwamba wanashukuru tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilivyoingia madarakani mambo ya chini ya meza hayapo tena, angalau sasa wanafanya biashara juu ya meza wengine walifikia hatua ya kufunga biashara zao, lakini pia naomba nishauri tu vibali vya wawekezaji viharakishwe ili kwenda na wakati", alisema Dkt. Slaa.
Kongamano hilo ambalo kwa mara ya kwanza lilifanyika Stockhom Sweden mwaka 2012 lilikuja ma naadhimio kadhaa ya kushirikiana katika kuimarisha uchumi wa nchi hizo kibiashara na uwekezaji lilileta matokeo chanya kufuatia kuwepo kwa wawekezaji wengi wa Sweden kuwekeza kwenye nchi za Afrika Mashariki.
Mkutano huo umehudhuriwa na zaidi ya makampuni makubwa 20 toka Sweden kupitia Chama chao cha Wafanyabiashara na Wawekezaji wa Afrika Mashariki (SWEACC) ambapo Mwenyekiti wake Bw. Jan Furuvald amesema uwekezaji kwenye nchi hizo umekuwa na manufaa kutokana na kuwa na soko kubwa la watumiaji wa bidhaa zao na kuwataka wawekezaji wengine kutoka nchini kwake kuja kuwekeza Afrika Mashariki.
"Sisi Wafanyabiashara na wawekezaji mara nyingi tunaangalia mazingira mazuri ya uwekezaji, kuwekeza kwenye nchi za Afrika Mashariki kunatuhakikishia soko kubwa kwani licha ya kuwa kwenye jumuiya hii pia kuna fursa nyingine za SADC", alisema Furuvald.
Kongamano hilo lenye kauli mbiu ya "Green Solutions in East African Cities" Suluhisho la Kijani kwenye Majiji ya Afrika Mashariki linalenga kuimarisha mazingira ya uwekezaji kwenye majiji yaliyopo kwenye Jumuiya hiyo ambapo kwa Tanzania, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Mussa Zungu amesema ili kukabiliana na hali hiyo hatua kadhaa zimechukuliwa.
Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja  na kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki ambayo ilikuwa ikichafua mazingira na kuharibu mazalia ya viumbe hai ambapo pia kwa sasa Serikali inahamasisha matumizi ya gesi viwandani, majumbani na kwenye magari ili kuepukana na uchafuzi wa mazingira na ukataji miti hivyo kwa ajili ya matumizi ya nishati za mkaa na kuni.
Waziri Zungu amesema katika kuhakikisha nishati mbadala inapatikana kwa urahisi Serikali inajenga Bwawa kubwa la kufua umeme la Nyerere ili kuwe na umeme wa uhakika.
Aidha Zungu aliwataka wawekezaji wote waliokwama kupata vibali vya mazingira kutokana na mazingira ya rushwa kufika ofisini kwake kwa ajili ya kupata vibali hiyo.
"Kwa Wawekezaji waliokwama kupata vibali vya mazingira wanione, tutawapatia vibali vyao bila kuhangaika, hakuna jambo baya Duniani kama kumnyima mtu haki yake ili upate pesa, tunathamini wawekezaji na tunathamini uwekezaji katika nchi yetu" alisema Zungu.
Naye, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stellah Manyanya akasema Serikali ya Tanzania imekuwa ikiweka mazingira mazuri ya biashara kwa kuimarisha miundombinu Sera na miundombinu ambapo kwa sasa ujenzi mkubwa wa Reli ya Kisasa ya Standard Gauge unaendelea lengo likiwa ni kuzifanya nchi hizo kunufaika kwa usafirishaji kauli inayoungwa mkono na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro.
"Kazi ya Serikali yetu ni kuweka mazingira mazuri ya Biashara na Uwekezaji yakiwepo ya Sera, Sheria na Miundombinu, kuimarisha Blue print na hali ya kisiasa ambayo ina tija kubwa kiuchumi", alisema Mhandisi Manyanya.
=MWISHO=
Read More