Thursday, March 12, 2020

WAZIRI MHAGAMA ATOA MAAGIZO MAZITO USIMAMIZI VITALU NYUMBANa. OWM, Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama, ametoa maagizo sita kwa  waratibu na wadau wa Programu ya mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba “Greenhouse”na kuwataka kutekeleza, kwa wakati na ufanisi maagizo yake yanayojikita katika  kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa mafunzo hayo ili yawe na ubora zaidi na tija kwa vijana.

Waziri Mhagama ameagiza  kufanyika maamuzi ya haraka yatakayowezesha vijana katika halmashauri ambazo bado mradi huo haujafika wanafikiwa. Aidha, Fedha zote zilizokusanywa na vijana katika awamu ya kwanza ya mafunzo hayo zikaguliwe na vijana washirikishwe ili waweze kutoa taarifa ya idadi ya mazao waliyozalisha na kiwango walichoweza kuuza. 

Akitoa magizo hayo leo,  Machi 11 2020 kwa kikao kilichowakutanisha vijana, Wadau,Waratibu ambao ni Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Kilimo, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na wakandarasi ambao walijenga vitalu nyumba, amewagiza  kuanzishwa mfumo wa ufuatiliaji ambao utakuwa na taarifa ya utekelezaji wa majukumu. 

"Kuanzia sasa  ni lazima mikopo kwa vijana ipatikane kwa wakati,  nataka upatikanaji wa mikopo ambayo itawasaidia vijana hao kuanzisha vitalu nyumba vyao, pia tengenezeni  mfumo wa ukusanyaji mapato na matumizi. Wakandarasi waliojenga vitalu nyumba katika halmashauri 84 awamu ya kwanza fanyeni  marekebisho kwenye  vitalu nyumba ambavyo vimekuwa na matatizo. Nataka usimamizi na uendeshaji wa programu ya mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba “Greenhouse” uwe chachu  ya  kuongeza ajira kwa vijana katika sekta ya kilimo" amesisitiza Mhagama.

Waziri Mhagama amefafanu akuwa,  Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ina nia ya dhati ya kuwawezesha vijana kupitia programu mbalimbali inazoazisha kwa lengo la kuwasaidia vijana kuondokana na changamoto ya ajira.

“Serikali ina lengo la kufikisha ujuzi huo wa kilimo cha kisasa katika halmashauri zote za Tanzania bara kwa kuwa asilimia 63 ya fursa za ajira zinapatikana kwenye kilimo na tena maeneo ya vijijini,” alisema Mhagama 

Waziri Mhagama, amebainisha kuwa,  Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ndio yenye dhamana na masuala ya vijana iliamua kupitia ilani ya uchaguzi ibara ya 6 kifungu (a) inayosema kuhamasisha kilimo kupitia kauli mbiu ya Kilimo Kwanza kwa kuwawezesha wakulima kupata mafunzo ya kilimo cha kisasa, pembejeo, zana za kisasa na wataalamu wa ugani pamoja na mbinu za kuyafikia masoko ya uhakika ya mazao yao, ambao ulipelekea kutambua umuhimu wa mchango wa vijana hasa waliopo vijijini ndipo mradi huu wa Kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba ulianzishwa kwa lengo la kuwezesha vijana,” amesema Mhagama.


“Mataifa makubwa mengi yaliyoendelea wamekuwa wakitumia kilimo cha aina hiyo kwa lengo la kulima kisasa, kuongeza thamani ya mazao, kupata masoko endelevu na la uhakika na kulima kwa tija, hivyo tukiwawezesha vijana wetu watanufaika na kilimo hicho na sekta hiyo italeta tija katika kukuza uchumi wa nchi,” alieleza Mhagama.

Waziri Mhagama amewataka vijana kutumia ujuzi waliopata katika mafunzo hayo ili waweze kusimamia mradi huo vizuri na wajenge moyo wa kuthubutu katika kuwasaidia vijana wenzao kupata ujuzi wa mafunzo hayo ya kilimo cha kisasa.


Wakati huo huo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw. Andrew Massawe amesema kuwa ameyakupokea maagizo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi ili programu hiyo ya mafunzo ya kilimo cha kisasa iweze kuwa endelevu.


“Ofisi ya Waziri Mkuu iliona umuhimu wa kushirikiana na , Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Kilimo, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, wakandarasi pamoja na Vijana ili kutathmini utekelezaji wa mradi huo na kuona namna ya kukabili changamoto ambazo zilijitokeza, mafanikio yaliyopatikana ili kuona namna bora ya kuimarisha mafunzo hayo,” amesema Massawe.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Ally Msaki ameelezea maazimio waliyofikia pamoja na wadau katika kuimaarisha usimamizi na uendeshaji wa mafunzo hayo

"Pamoja na kuangalia namna bora ya kuendesha mafunzo haya, tumemua kuwa  tutasimamia uwepo wa utaratibu maalum wa makusanyo, utunzaji na matumizi ya fedha, kuwezesha vijana kuwa na ujuzi wa kuongeza thamani ya mazao, kuelezea wananchi mafanikio yaliyopatikana kupitia mradi huo wa kilimo cha Kitalu nyumba,kuwezesha vijana kufanya kilimo biashara na uwepo wa muendelezo wa kutoa mafunzo na kuongeza vitalu nyumba katika kila halmashauri" amesitiza Msaki.

Naye Mmoja wa wanufaika wa Programu hiyo Bw. Festo Masiba ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo yamewajengea ujuzi mkubwa wa kuweza kulima kwa tija.


“Tunaishukuru Serikali kwa kutuamini sisi vijana na kutuwezesha kupata mafunzo ya Kilimo bora kwa kutumia eneo dogo na upatikanaji wa mazao ni mwingi, tumeweza kukua kiuchumi na tunaujuzi wa kuwajengea wadau wengine vitalu nyumba,” alisema Masiba .


MWISHO
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw. Andrew Massawe akieleza jambo wakati wa mkutano huo uliofanyika machi 11, 2020 katika Ukumbi wa Landmark Kilimani, Jijini Dodoma.
Baadhi ya Wakuu wa Idara kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu wakifuatilia mijadala wakati wa mkutano huo.
Sehemu ya vijana wakifuatilia kwa makini hotuba ya Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) walipokutana kujadili namna bora ya kuimarisha mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba.
Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (wa nne kutoka kulia waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wataalamu kutoka ofisi yake, Wadau na Vijana wapokutana kwa lengo la kujadili namna bora ya kuimarisha mafunzo ya Kilimo kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba katika Ukumbi wa Landmark Kilimani, Jijini Dodoma.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.