Thursday, March 5, 2020

SUDANI WAJIFUNZA URATIBU WA URUTUBISHAJI WA VYAKULA TANZANIANa. OWM, DODOMA
Ujumbe wa maafisa waandamizi wa serikali kutoka nchini Sudani umekuja hapa nchini kujifunza masuala ya Uratibu wa Vuguvugu la Lishe  na urutubishaji wa Vyakula. Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikiratibu masuala ya lishe nchini kutokana na mamlaka iliyonayo kikatiba ya kuratibu shughuli zote za Serikali pamoja na masuala mtambuka. Uratibu huo unafanywa kupitia Kamati ya kitaifa ya Lishe chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Dorothy Mwaluko.

Tanzania kupitia Ofisi hiyo imefanikiwa kuandaa Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Masuala ya Lishe ambao hutoa mwongozo wa utekelezaji wa masuala ya Lishe nchini, ikiwemo kupambana na upungufu wa ukosefu wa virutubishi kwa kuongeza virutubishi hivyo kwenye vyakula,  pamoja na    uanzishwaji wa majukwaa mengine ya lishe katika ngazi ya kitaifa hadi ngazi ya mkoa na wilaya likiwemo jukwaa la sekta binafsi linalojikita sana kwenye masuala ya urutubishaji wa vyakula.

Akiongea mara baada ya kikao cha  kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya Urutubishaji wa vyakula,  mjini Dodoma,  Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali,  Ofisi ya Waziri Mkuu, Paul Sangawe,  ambaye pia ni Mratibu wa Vuguvugu la lishe nchini,  amefafanua kuwa Tanzania ilikuwa  miongoni mwa nchi za awali duniani kujiunga na Vuguvugu la Lishe, ambalo linahimiza ushiriki wa sekta zingine na wadau wa lishe kupambana na utapiamlo wa watoto wa chini ya miaka mitano hasa aina ya udumavu, ambapo kwa sasa Tanzania imefanikiwa kupunguza udumavu kutoka 42% mwaka 2010 hadi 32% mwaka 2018.

“Kutokana na utekelezaji mzuri wa Vuguvugu la Lishe tumefanikiwa kuwa na mtandao mzuri  wa Lishe wa kisekta kwa sekta binafsi, lakini pia utashi wa kisiasa umeongezeka hapa nchini ambapo tayari takribani wabunge 55 wamejitanabaisha kujihusisha na masuala ya lishe. Masuala ya lishe tayari yameingizwa kwenye Mpango wa Pili wa  Taifa wa Maendeleo  wa miaka mitano (2016-2021) na Mwongozo wa Mpango na Bajeti ambao umesaidia masuala ya lishe kuingizwa kwenye mipango ya kisekta  ya nchi ” amesisitiza Sangawe.

Aidha, Sangawe amebainisha kuwa tayari Tanzania imefanikiwa kuwa na Kanuni za Urutubishaji wa Vyakula za mwaka 2011, ambapo kanuni hizo zinavihusu viwanda vikubwa vya uzalishaji wa vyakula hususan unga wa ngano na mafuta ya kupikia.

Amesisitiza kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John  Pombe Magufuli, imeendelea kulipa kipaumbele suala la lishe kwa kutoa muongozo kwa Halmashauri zote nchini  kutenga  fedha za lishe kwa kila mtoto, ambapo awali ilikuwa  Shilingi 550/=,  kwa kila mtoto na kwa sasa ni shilingi 1,000/=  kwa kila mtoto.

 “Kwa sasa serikali imefanikiwa kuajiri wataalamu wa masuala ya lishe katika ngazi ya Wizara na Halmashauri ambapo kwa sasa 57% ya Halmashauri 185 zote nchini zimeajiri wataalamu wa masuala ya lishe huku Halmashauri zilizobaki zina maafisa viungo tu wa masuala ya lishe ” Amesisitiza Sangwe.

Amebainisha kuwa serikali imeamua suala la lishe kuwa agenda ya Kitaifa ambapo kwa sasa imeandaa makubaliano maalum (mikataba ya lishe) kwenye ngazi za serikali za mitaa ambayo ni kati ya ngazi hizo na  Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), lengo ni kuongeza uwajibikaji kwenye masuala ya lishe.

Kwa upande wake, Kiongozi wa ujumbe wa Maafisa Waandamizi kutoka nchini Sudani, Kutoka Wizara ya Afya nchini Sudani, Huda Kambal, amefafanua kuwa wamechagua kuja Tanzania kujifunza uratibu wa kisekta wa masuala ya lishe na Urutubishaji wa vyakula hususani kwenye unga wa ngano na mafuta ya kupikia.
“Sisi katika nchi ya Sudani hatuna huu Uratibu wa kisekta katika masuala ya lishe na Urutubishaji wa vyakula. Lengo la kuja hapa ni kujifunza na kutaka kupata uzoefu wa namna ya kuratibu na kutekeleza shughuli za Urutubishaji wa Vyakula hasa kwa wazalishaji wakubwa wa vyakula ili twende tukaboreshe nchini kwetu shughuli hizo” Amesisitiza Kambal
 Amebainisha kuwa katika kuhakikisha wanafanikiwa kwenye kuanzisha Utaratibu huo wanatarajia kujifunza na kupata uzoefu katika maeneo ya Udhibiti na Usimamizi wa vyakula vilivyorutubishwa, ushiriki wa sekta binafsi kwenye masuala ya lishe, ufuatiliaji wa mara kwa mara na mawasiliano kwa umma juu ya masuala ya lishe.
Kikao  hicho kilihudhuriwa na maafisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa Shughuli za serikali, Taasisi ya Lishe Tanzania, Shirika la Viwango Tanzania pamoja na maafisa waaandamizi kutoka nchini Sudani ambao wametoka Wizara ya Afya,  Shirika la Chakula Duniani, Shirika la Afya Duniani, Mamlaka ya Viwango na Ubora Sudani, Mamlaka ya utafiti na Viwanda, Wizara ya Viwanda na Shirika la Biashara Sudani
Mnamo mwaka 2012 Tanzania ilikuwa ni miongoni mwa nchi za kwanza Duniani kujiunga kwenye Vuguvugu la Lishe Duniani, ambapo mnamo mwaka 2011 aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kipindi hicho , Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa ni miongoni mwa viongozi wa kwanza kuingia kwenye kikundi cha viongozi wa Vuguvugu la Lishe Duniani. Kuanzia Kipindi hicho Agenda ya kitaifa ya masuala ya lishe ilianza kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kama Ofisi yenye dhamana ya kuratibu shuguli za Serikali kwa mujibu wa sheria.

MWISHO.


Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali,  Ofisi ya Waziri Mkuu, Paul Sangawe,(Mwenye tai)  na Kiongozi wa ujumbe wa Maafisa Waandamizi kutoka nchini Sudani, Kutoka Wizara ya Afya nchini Sudani, Huda Kambal (mwenye Ushungi), wakifuatilia kikao cha kubadilishana uzoefu kuhusu uratibu wa masuala ya Urutubishaji wa vyakula nchini, maafisa hao wamekuja kujifunz hapa nchini kuhusu masuala hayo, tarehe 3 Machi 2020 Jijini Dodoma.

Baadhi ya maafisa waandamizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na maafisa waandamizi kutoka nchini Sudani, wakifuatilia kikao cha kubadilishana uzoefu kuhusu uratibu wa masuala ya Urutubishaji wa vyakula nchini, yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, tarehe 3 Machi 2020 Jijini Dodoma.
Baadhi ya maafisa waandamizi kutoka nchini Sudani, wakifuatilia kikao cha kubadilishana uzoefu kuhusu uratibu wa masuala ya Urutubishaji wa vyakula nchini,yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Machi 2020 Jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali,  Ofisi ya Waziri Mkuu, Paul Sangawe (Mwenye tai), akiwa katika picha  ya pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka nchini Sudani  mara baada ya kumaliza kikao cha kubadilishana uzoefu kuhusu uratibu wa masuala ya Urutubishaji wa vyakula nchini, Machi 2020 Jijini Dodoma.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.