Tuesday, March 3, 2020

WALIOFUJA MALI ZA MKONGE KUCHUKULIWA HATUA-MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itawachukulia hatua watu wote waliohusika na ubadhilifu wa mali zikiwemo nyumba za Mamlaka ya Mkonge Tanzania.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali itafanya uchunguzi katika  mashamba yote ya mkonge ili kubaini yameendelezwa kwa kiasi gani na sehemu ambazo hazijaendelezwa zitachukuliwa na kugawiwa kwa wananchi ili walime  mkonge.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo(Jumanne, Machi 3, 2020) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa kata za Segera na Kabuku akiwa katika ziara yake ya kikazi wilaya ya Handeni, Tanga.
Machi 1, mwaka huu Waziri Mkuu alipokea taarifa ya uchunguzi wa tuhuma mbalimbali katika tasnia ya kilimo cha mkonge mkoani Tangana kuagiza mapendekezo yaliyotolewa na timu hiyo yakiwemo ya kurejeshwa Serikalini kwa nyumba na. 176 eneo la Bombo ambayo ilimilikishwa kwa Bw. Salum Shamte yafanyiwe kazi.

Nyumba nyingine zilizopendekezwa kurejeshwa Serikalini ni pamoja na nyumba kumi zilizoko ndani ya Jiji la Tanga katika maeneo ya Raskazone, Bombo, Nguvumali na Market street ambazo zilinunuliwa na watumishi hao kwa udanganyifu.

Timu hiyo maalum ya uchunguzi iliundwa na Waziri Mkuu na ilifanya uchunguzi mkoani Tanga kuanzia tarehe 29/11/2019 hadi tarehe 07/02/2020. Timu hiyo iliyokuwa na  wajumbe 13 ilihusisha maafisa kutoka ofisi mbalimbali za Serikali.

Waziri Mkuu amesema kwa kuwa katani ndio zao la biashara mkoani Tanga Serikali itahakisha watu wote wenye mashamba makubwa ya mkonge ambayo wameshindwa kuyaendeleza itayachukua na kuyarejesha kwa wananchi.
Wakati huo huo,Waziri Mkuu amesema Serikali imejenga vituo 352 vya afya nchi nzima vikiwemo viwili vilivyojengwa Handeni, kutokana na mahitaji makubwa ya huduma hiyo kata ya Segera itapewa kipaumbele katika awamu ya pili ya ujenzi.
Kadhalika, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe ahakikishe wananchi wanaokwenda kufuata huduma za matibabu katika vituo vya afya na zahanati wanapatiwa dawa badala ya kuelekezwa kwenda kununua kwenye maduka ya watu binafsi.
Alisema Serikali imeongeza bajeti ya dawa kutoka sh. bilioni 37 hadi sh bilioni 269, hivyo hakuna sababu ya mwananchi kwenda kwenda eneo la kutolea huduma ya afya na kukosa dawa. 
Pia, Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Handeni ahakikishe kila kijiji kinapata huduma ya maji safi na salama kwa kusimamia uchimbaji wa visima kupitia fedha za makusanyo ya ndani.
Waziri Mkuu amesemaSerikali kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao. 
Kuhusu suala la umeme, Waziri Mkuu amesemamaeneo ya wilaya hiyo ambayo bado hayajapata umeme yote yatasambaziwa umeme kupitia Mradi wa Nishati Vijijini (REA) na wananchi hawatowajibika kulipia gharama za nguzo.

Amesema Rais Dkt. Magufuli anataka kuona nyumba ya kila Mtanzania inawaka umeme tena kwa gharama nafuu ya sh. 27,000, hivyo amewataka waendelee kuwa na imani na Serikali yao.

 (mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.