Monday, February 20, 2017

ZIARA YA MAJALIWA BABATI NA MBULU

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama sukari na nishati ya kuni inayotengenezwa kwa kutumia makapi ya miwa inayokamuliwa katika kiwanda cha sukari cha Manyara wakati alipotembelea kiwanda hicho Februari 19, 2017.  Kuni hizo zina ubora unaofanana na ule wa makaa ya mawe na hutumika zaidi katika mitambo inayotumia  nishati ya kuni. Kulia ni Waziri wa  Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba na kulia kwa Waziri Mkuu, ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt. Joel Bendera.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa wilaya mstaafa, Mama Sanka baada  ya kuwasili  kwenye makazi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara  mjini Babati akiwa katika ziara ya mkoa huo, Februari 19, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama sanamu ya binadamu  wakati alipotembelea moja ya darasa  la Chuo cha Uuguzi katika hospitali ya Haydom wilayani Mbulu, Februari 20, 2017.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akipata maelezo kutoka kwa Mtafiti katika hospitali ya Haydom wilayani Mbulu, Rosemary Mshama  (kulia)  wakati alipotembelea Kituo cha Utafiti cha hospitali hiyo Februari 20, 2017.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifurahia ngoma ya asili ya kabila la Wahatzabe wakati alipowasili kwenye hospitali ya Haydom kuanza ziara ya  wilaya ya Mbulu, Februari 20, 2017.

Read More

MSIOGOPE KUKOPA, ASEMA WAZIRI MKUU


*Asisitiza dawa ya deni, kulipa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakulima wakubwa na wadogo wa miwa kwenye kiwanda cha sukari cha Manyara wachukue mikopo kama wanataka kuendeleza kilimo hicho.

Ametoa wito huo jana jioni (Jumapili, Februari 19, 2017) wakati akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda hicho pamoja na wananchi wanaoishi maeneo ya jirani katika kijiji cha Matufa wilayani Babati akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake mkoani Manyara.

“Mkurugenzi wenu amesema hapa kuwa ni vigumu kwa wakulima kupata mikopo na pia mikopo ya benki ina riba kubwa. Napenda niwasisitize kuwa msiogope kukopa kwa sababu hakuna tajiri duniani aliyeendelea bila kukopa,” alisema.

Hata hivyo, Waziri Mkuu aliwakumbusha wakulima hao kwamba wakishakopa, wasisahau kuwa dawa ya deni ni kulipa.

Aliwaeleza kuwa zipo benki ambazo zinatoa mikopo kwa wakulima ambazo ni Benki ya Maendeleo Afrika (ADB), NMB, CRDB, Benki ya Kilimo (TADB) na Benki ya Rasilmali (TIB). “Benki ya Kilimo TADB inatoa mikopo kwa wakulima na pia Benki ya TIB, Kuna TIB Corporate na TIB Development,” alisema.

Aliwataka wakurugenzi wa kiwanda hicho waharakishe uagizwaji wa mitambo mipya ili kiwanda hicho kiweze kuongeza uzalishaji wake. “Napenda niwahakikishie wakurugenzi kuwa Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kulinda viwanda vya ndani. Tunataka muongeze uzalishaji ili kufidia pengo lililopo. Tutaruhusu waagizaji walete suakri kutoka nje baada ya kujiridhisha kuwa uzalishaji wa ndani umejitosheleza,” alisema.

Alisema takwimu za mahitaji ya sukari hapa nchini zinapaswa kupitiwa kwa sababu hazitoi picha halisi. “Tanzania ina watu milioni 50 lakini mahitaji ya sukari tunaambiwa ni tani 420,000 kwa mwaka. Wenzetu wa Kenya wako milioni 45 lakini mahitaji yao ni tani 800,000 kwa mwaka. Tulishawaambia wapiti upya hizi takwimu zao.”

Mapema, akisoma taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Afisa Mahusiano wa kiwanda hicho, Bw. Dipak Odedra alisema kiwanda hicho kilianzishwa mwaka 2006 kikiwa na uwezo mdogo wa kusaga tani 50 za miwa kwa siku lakini sasa kina uwezo wa kusaga tani 500 kwa siku.

“Kuongezeka kwa uzalishaji na kukua kwa kiwanda kumechangiwa na mikataba ya kuwashirikisha wakulima wadogo kuwakopesha mitaji tangu kutayarisha mashamba, kupanda mbegu, usafiri na utaalamu lengo likiwa kununua miwa yao inapokuwa tayari kuvunwa,” alisema.

Alisema mpango huo shirikishi wa kupanda miwa unahusisha vijiji zaidi ya 10 ambapo jumla ya ekari 1,150 zinalimwa na wakulima wadogo waliohamasika na kuona faida za kilimo hicho.

Alisema mwaka jana kiwanda hicho kilisaga tani 64,584 za miwa na kuweza kuzalisha tani 4,251 za sukari. “Kwa msimu ujao baada ya kufunga mitambo ya kisasa, tumepanga kuongeza uzalishaji ili tuweze kusaga tani za miwa 650 kwa siku kutoka tani 500 za sasa. Na mwaka kesho (2018) tunataraji kufikisha tani 750 za miwa kwa siku,” aliongeza.

Akigusia changamoto zinazowakabili, alisema wanaiomba Serikali iwawezeshe kupata mikopo yenye riba nafuu ili waweze kufikia malengo yao kwa haraka zaidi na akagusia sula la wakulima wadogo kunyimwa mikopo kutoka benki za biashara.


Read More

Sunday, February 19, 2017

MAJALIWA AKERWA NA KIWANDA CHA MBOLEA CHA MINJINGU KUWEKA MBOLEA KWENYE MIFUKO INAYOONYESHA KUWA MBOLEA YA KIWANDA HICHO IMEZALISHWA KENYA

Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akionyesha mfuko wa kubebea mbolea ya kiwanda cha Minjingu mkoani Manyara wenye maandishi yanayoonyesha kuwa mbolea hiyo imetengenezwa nchini Kenya. Jambo hilo lilimkera sana Waziri Mkuu na aliuagiza uongozi wa kiwanda hicho kuandika barua ya kumuaomba radhi Rais  John Pombe Magufuli kwa kitendo hicho.
Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa akionyesha mfuko wa kubebea mbolea ya kiwanda cha Minjingu mkoani Manyara wenye maandishi yanayoonyesha kuwa mbolea hiyo imetengenezwa nchini Kenya. Jambo hilo lilimkera sana Waziri Mkuu na aliuagiza uongozi wa kiwanda hicho kuandika barua ya kumuaomba radhi Rais  John Pombe Magufuli kwa kitendo hicho.
Waziri  Mkuu,Kassim Majaliwa akionyesha mfuko wa kubebea mbolea ya kiwanda cha Minjingu mkoani Manyara wenye maandishi yanayoonyesha kuwa mbolea hiyo imetengenezwa nchini Kenya. Jambo hilo lilimkera sana Waziri Mkuu na aliuagiza uongozi wa  kiwanda hicho kuandika barua ya kumuaomba radhi Rais John Pombe Magufuli kwa kitendo hicho. Kushoto ni Waziri wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi, Dkt,Charles Tizeba na wapili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara,Dkt. Joel Bendera.

Read More

WAZIRI MKUU AKERWA MBOLEA YA MINJINGU KUPEWA LEBO YA KENYA


*Ataka waandike barua ya kuomba radhi kwa Rais Magufuli
*Aagiza Waziri wa Biashara aje na timu yake

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema haridhiki na hali aliyoikuta kwenye kiwanda cha kutengeneza mbolea cha Minjingu baada ya kubaini kuwa wanatumia mifuko yenye lebo ya Kenya wakati mbolea hiyo inazalishwa hapa nchini.

Kutokana na hilo, Waziri Mkuu amewataka wamiliki wa kiwanda hicho waandike barua kwa Mheshimiwa Rais Dk. John Pombe Magufuli kabla hajamaliza ziara yake Jumatano, Februari 22, 2017 apate nakala ya barua hiyo.

Ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Februari 19, 2017) baada ya kutembelea kiwanda hicho kilichopo wilaya Babati akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake mkoani Manyara. Waziri Mkuu amerejea Babati leo akitokea Dar es Salaam ambako alikuwa na ratiba za kitaifa.

“Nilikuja kukagua kiwanda baada ya kupokea malalamiko kuwa mbolea hii haikubaliki huko vijijini. Watafiti wameonyesha kuwa ikitumika inasaidia kutoa mazao mengi. Lakini wakati niko kiwandani nimekerwa kukuta mifuko ya kupakia mbolea hii ina anuani ya Nairobi, Kenya wakati mali ghafi inatoka Tanzania,” amesema.

“Ni kwa nini mifuko hii ina anuani ya Kenya? Hapa tulipaswa tuone anuani ya Babati! Je mlipata kibali kutoka serikalini? Tena kuna lebo ya TBS. Kwa nini Tanzania haionekani? Kwani malighafi iko Kenya? Haiwezekani, ni lazima uandike barua na uombe radhi kwa Mheshimiwa Rais Magufuli. Yeye anahimiza ujenzi wa viwanda ndani ya nchi, halafu ninyi mnafanya hivyo?”

Akiwa ndani ya kiwanda hicho, Waziri Mkuu alikuta baadhi ya mifuko ya mbolea ikiwa imeandikwa: ‘County Government of Bungoma’, ina nembo ya Serikali ya Kenya, na anuani ikionesha kuwa mbolea hiyo imetengenezwa na kiwanda cha mbolea cha Minjingu lakini anuani inasomeka P. O Box 2941 – 00200 Nairobi, Kenbro Industrial Park, Mombasa Road; namba ya simu +254-20-6000-970 lakini mifuko hiyo pia ina muhuri wa TBS.

Baadhi ya mifuko ilikuwa ikipakiwa ndani ya lori tayari kwa kusafirishwa kwenda kwa wateja.

Pia amesema atamwagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage aje hapa na wanasheria wake na wataalamu kutoka Tume ya Ushindani wa Kibiashara (FCC) ili waje kuangalia hatua gani zinapaswa kuchukuliwa.

“Kwa staili hii hii tumeona watu wakinunua kahawa yetu na kwenda kuipakia upya huku wakiweka lebo za kwao. Leo hii hata Tanzanite pia inasemwa imetengenzwa India. Hatuwezi kukubali hali hii iendelee,” amesisitiza.

“Tukiruhusu hali hii, watu watajuaje kuwa mbolea hii ambayo ni first class duniani kuwa inapatikana Tanzania? Kiwanda chetu, ardhi yetu, suala la kutangaza nchi yetu kwa kutumia bidhaa zetu litafanikiwa kwa njia hii kweli?”

“Nataka wakati namaliza ziara nipate taarifa ya hili jambo pamoja na nakala ya barua ambayo imetumwa kwa Mheshimiwa Rais,” amesisitiza.

Akitoa maelezo kuhusu hali hiyo, Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Bw. Tosky Hans alimweleza Waziri Mkuu kwamba wametumia lebo hiyo kutokana na makubaliano na wanunuzi jibu ambalo Waziri Mkuu hakulikubali na kusisitiza kuwa anapaswa aombe radhi.

Waziri Mkuu kesho anaendelea na ziara yake wilayani Mbulu ambako atatembelea hospitali ya Haydom, kuzungumza na watumishi wa wilaya hiyo na kuzindua shule ya sekondari Singland.

Read More

Friday, February 17, 2017

OLE MILLYA AIPONGEZA SERIKALI KUTATUA KERO ZA WANANCHI

MBUNGE wa Simanjiro, Mheshimiwa James Ole Millya ametoa pongezi kwa viongozi wa serikali ya awamu ya tano kwa jinsi wanavyojali na kuwahudumia wananchi.

Ametoa pongezi hizo jana (Alhamisi, Februari 16, 2017) kwenye mikutano miwili ya hadhara iliyofanyika Orkesumet na Mererani wilayani Simanjiro, Manyara, baada ya kupewa nafasi asalimie wananchi kabla Waziri Mkuu Kassim Majaliwa hajazungumza na wakazi wa maeneo hayo.

“Serikali hii ina viongozi wachapakazi akiwemo Waziri Mkuu. Kwa mara ya kwanza katika jimbo hili, wananchi watapata maji safi kupitia mradi wa maji kutoka mto Ruvu unaoendelea kujengwa hivi sasa,” alisema kwenye mkutano wa hadhara wa Orkesumet.

Alitumia fursa hiyo kumuomba Waziri Mkuu afuatilie suala la ujenzi wa hospitali ya wilaya kwani sasa hivi wanategemeakituo cha afya na hali ikibadlika inabidi mgonjwa apeekewe Arusha mjini ambako ni umbali wa km. 150 kutoka Orkesumet yalipo makao makuu ya wilaya hiyo.

Pia aliomba ijengwe barabara ya lami ya kuunganisha wilaya hiyo pamoja wilaya jirani za Hai na Kiteto.

Akiwa Mererani, Bw. Ole Millya aliipongeza Serikali kwa kujenga barabra ya lami kutoka uwanaja wa ndege wa KIA hadi Mererani. Hata hivyo, aliiomba serikali iongeze juhudi ili barabara hiyo iweze Mererani na Orkesumet.

Akihibu hoja hizo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimpongeza mbunge huyo kwa uungwana wake wa kutambua juhudi ambazo Serikali imezifanya kwa wananchi wa jimbo lake.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Manyara, aliwaambia wakazi hao kwamba Serikali itaendelea kufanya nao kazi bila kumbagua mtu yeyote kwa sababu ya itikadi za kisiasa.

“Mmempa yeye dhamana ya kuwawakilisha kama mbunge wenu lakini dhamana ya kuongoza nchi mmempa Mheshimiwa Rais Dk. John Pombe Magufuli kwa kuwapigia kura. Kwa hiyo, kazi yetu ni kuwatumikia ili tutatue kero zinazowakabili wana-Simanjiro,” alisema.

Akizungumzia sekta ya afya, Waziri Mkuu alisema kituo cha afya cha Orkesumet kimepokea sh. milioni 49 kati ya sh. milioni 57 zilizoombwa ili kukiimarisha katika utoaji wa huduma za tiba.

“Tumeshatuma fedha nyingine sh. milioni 163 kati ya sh. milioni 190 zilizoombwa ili kununulia dawa, vifaa tiba na vitendanishi. Pia kun ash, milioni 483 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya vijijini,” alisema.

“Nia yetu ni kujenga hospitali kubwa ya wilaya lakini ni lazima tuimarishe miundombinu ya utoaji tiba ili wananchi wapate huduma stahiki. Ombi la hospitali ya wilaya nimelipokea na nitafuatilia kujua limefikia hatua gani,” alisema.

Kuhusu ujenzi wa barabara za kuunganisha wilaya, Waziri Mkuu alisema Serikali itaanza kufanya upembuzi na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka Arusha – Kiteto – Kongwa ili ijengwe kwa kiwango cha lami.

Kuhusu migogoro ya ardhi iliyotajwa na wananchi kwenye mabango yao, Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Eng. Zephania Chaula aende na mbunge huyo kwenye maeneo yanayolalamikiwa na wananchi ili akabaini chanzo cha migogoro na aitafutie ufumbuzi.

Kuhusu umeme, Waziri Mkuu alisema vijiji 18 katika ya 57 vya wilaya vimeshapatiwa umeme na vilivyoakia vimeshaingizwa kwenye mpango wa serikali wa kuvipatia umeme vijiji 8,000.

Aliwaonya wakazi wa Mererani wachukue tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwani takwimu zinaonyesha kuwa kasi ya maambukizi katika mji huo iko asilimia 18 kiwango alichosema ni kikubwa kuliko kiwango cha kitaifa.

Read More

Thursday, February 16, 2017

RED CROSS YAKABIDHI KADI ZA UANACHAMA IDARA YA MAAFA


Mratibu wa Maafa Idara ya Uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Bw.Charles Msangi akipokea kadi ya uanachama wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania kutoka kwa Katibu wa chama hicho Bw. Julius Kejo Februari 16, 2017 katika Ofisi za Idara hiyo Dar es Salaam.
Rais wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania Bw. Mwadini Jecha (katikati) akiweka saini kitabu cha wageni Idara ya Uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu walipotembelea Idara hiyo na kukabidhi Kadi za Uanachama kwa Idara  hiyo, tarehe 16 Februari, 2017.
Mkurugenzi wa Chama Cha Msalaba Mwekundu Tanzania Bw.Renatus Mkaruka (wa kwanza kulia) akizungumza jambo wakati wa zoezi la kukabidhi kadi za Uanachama wa chama hicho kwa Idara ya Uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Februari 16, 2017 katika Ofisi ya Waziri Mkuu Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Brig.Jenerali Mbazi Msuya (kulia) akipokea kadi ya uanachama wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania kutoka kwa Rais wa Chama hicho Bw. Mwadini Jecha Februari 16, 2017 katika Ofisi za Idara hiyo Dar es Salaam.

Read More

Wednesday, February 15, 2017

MAJALIWA AHUTUBIA MKUTANO WA HADHARA MJINI KITETO

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea  kutoka Mzee Mbambire Oloi Kurukur, jani la mti ikiwa ni ishara ya amani ya kukomesha mapigano kati ya wakulima na wafugaji wilayani Kiteto kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa michezo wa  Kiteto, Februari 15, 2017.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa hadhara kwenye  uwanja wa michezo wa Kiteto  akiwa katika ziara ya mkoa wa Manyara, Februari 15, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea  kutoka kwa  Katibu wa Baraza la Amani la  Kiteto,  Salum Mambo, jembe la asili  ikiwa ni ishara ya kukoma kwa mauaji kati ya wakulima na wafugaji wilayani Kiteto katika mkutano wa hadhara aliouhutubi kweye uwanja wa michezo wa Kiteto, Februari 15, 2017.

Read More

Tuesday, February 14, 2017

MAJALIWA APOKEA MADAWATI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akipokea mchango wa sh.  milioni 5.5 kutoka kwa Mhasibu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Rose Makange (katikati)ukiwa ni mchango wa watumishi wa TAMISEMI kwa ajili ya madawati wilayani Ruangwa. Makabidhiano hayo yalifanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu, mjini Dodoma Februari 14, 2017. Kulia ni Rose Nyoni.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) baada ya kupokea  Sh. milioni 5.5 ukiwa ni mchango wa watumishi wa Ofisi hiyo kwa ajili ya madawati wilayani Ruangwa. Makabidhiano  hayo yalifanyika, Ofisini kwa Waziri Mkuu mjini Dodoma Februari 14, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) baada ya kupokea mchango wa watumishi hao wa sh. milioni 5.5 kwa ajili ya madawati wilayani Ruangwa. Makabidhiano hayo yalifanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu mjini Dodoma  Februari 14, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na  baadhi ya watumishi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) baada ya kupokea mchango wa watumishi hao wa sh. milioni 5.5 kwa ajili ya madawati wilayani Ruangwa. Makabidhiano hayo yalifanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu mjini Dodoma  Februari 14, 2017.

Read More

MAMA MAGUFULI NA MAMA MAJALIWA WATEMBELEA GEREZA TABORA


MKE wa Rais Mheshimiwa Mama Janeth Magufuli pamoja na Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa wametembelea Gereza la Mahabusu Tabora na kutoa zawadi mbalimbali kwa wafungwa na mahabusu gerezani hapo.

Wake wa viongozi wametembelea gereza hilo leo (Jumanne, Februari 14, 2017)  wakiwa katika ziara  mkoani Tabora, ambapo Mama Janeth amesema wameamua kuwatembelea wafungwa na mahabusu hao kwa nia ya kuwafariji kwa kuwa wao ni sehemu ya jamii.

“Vitabu vitakatifu vinasema kwamba ukiwasaidia watu wenye mahitaji utakuwa umetoa sadaka kubwa kwa Mwenyezi Mungu, hivyo tumeamua kuja kutembea  wafungwa na mahabusi kwenye gereza hili na kuwapa zawadi kwa kuwa nanyi mnahitaji faraja,” amesema.

Amesema wameamua kwenda kuwaona wafungwa na mahabusu hao kwa lengo la kuwafariji na kuwatia moyo kwa sababu wanaimani kwamba wakitoka watakuwa raia wema na hayo wanayopitia ni sehemu ya kufanya marekebisho ya tabia.

“Ni siku kubwa kwangu, nimejifunza mengi baada ya kufika hapa. Kitendo cha kwenda kuwaona wenye mahitaji wakiwemo wagonjwa, wafungwa ni jambo jema tunaamini hizi zawadi tulizozitoa zitawasaidia kwa sababu tunajua mnamahitaji mengi,” amesema.

Katika gereza hilo wake hao wa viongozi wamekabidhi zawadi mbalimbali kwa wafungwa na mahabusu, ambapo mwakilishi wa wafungwa hao Deo Kitave aliwashukuru kwa niaba ya wenzake. “Tunawashukuru kwa kutukumbuka, tunamuomba Mwenyezi Mungu muendelee kuwa na moyo huo,”.
Read More

Monday, February 13, 2017

WAZIRI MKUU AAGIZA MAENEO YA MAGEREZA YA PIMWE


*Ataka karakana za ujenzi, useremala zianzishwe kupunguza gharama
*Asisitiza ufyatuaji matofali kukabili upungufu wa nyumba za askari

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamishna Mkuu wa Magereza, Dk. Juma Malewa asimamie zoezi la upimaji wa maeneo yanayomilikiwa na Magereza kote nchini na kuhakikisha yanawekewa mipaka. 

Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumatatu, Februari 13, 2017) katika kikao baina ya Kamishna huyo mpya na Maafisa Magereza wa Mikoa yote na maafisa wanaoshughulikia kilimo na viwanda alichokiitisha ofisini kwake mjini Dodoma.

“Magereza yetu mengi yako kwenye maeneo ambayo hayajapimwa. Baadhi ya maeneo kuna migogoro kwa sababu wananchi wamejenga karibu kabisa na maeneo ya Magereza. Lazima tupime maeneo yote na kuyawekea alama mipakani ili kubainisha maeneo yetu,” amesisitiza.

Mbali ya maeneo ya Magereza, Waziri Mkuu amesema, jeshi hilo lina mashamba makubwa ambayo pia hayajapimwa hali ambayo amesema imechangia baadhi ya wananchi kulima ndani ya maeneo ya jeshi hilo.

“Natambua kuwa jeshi hili lina mashamba makubwa lakini nayo pia hayajapimwa. Kila RPO ni mjumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wake, tumieni wapima ardhi kutoka kwenye Halmashauri zenu na mhakikishe kuwa maeneo hayo yanapatiwa hati,” amesema. 

Amesema umefika wakati sasa kila gereza litambue na kuainisha fursa walizonazo ili waweze kuamua ni kwa kiasi gani wanaweza kujitegemea kwa uzalishaji. “Kama ni kilimo, ufugaji, au uzalishaji wa umeme, tuangalie ni kipi kinaweza kuvutia uwekezaji, lakini cha msingi zaidi ni lazima tuwe na hati za maeneo tuliyonayo,” amesema.

Waziri Mkuu amesema kuna baadhi ya magereza yalikuwa maarufu kwa kilimo lakini hivi sasa hakuna hata moja lenye trekta na kama yapo ni moja au mawili tu. “Sasa hivi teknolojia ya kilimo imebadilika, ni lazima tutumie zana za kilimo ili kwenda na kilimo cha kisasa.

Akizungumzia kuhusu ufugaji na uvuvi wa samaki, Waziri Mkuu aliagiza jeshi hilo litumie maafisa wake waliobobea kwenye sekta hizo, watumike kuendeleza na kuhamisha ujuzi wao kwa wafungwa wanaotumikia vifungo ili wanapotoka gerezani, wawe na ujuzi ambao utawasaidia kujikimu kimaisha wanaporudi kuishi vijijini.

“Nimetembelea maonesho ya Nanenane na Sabasaba huko nimekuta wamejenga banda la kuku juu ya bwawa la samaki. Hii ina maana kuku wanakula na kinyesi chao kinakuwa ni chakula kwa wale samaki walioko bwawani,” amesema.

Amemtaka Dk. Malewa aangalie uwezekano wa kuanzisha karakana na ujenzi kwenye kila gereza ili maafisa na wafungwa waliopo kule watumike kufanya kazi kwenye karakana hizo. “Nimetembelea gereza la Isanga, nikakuta kuna milango haina komeo. Kwa vile hakuna karakana, inabidi atafutwe fundi kutoka mtaani ili aje kutengeneza kitasa au komeo. Tuanzishe karakana na tuziboreshe,” amesisitiza.

Amesema uwepo wa karakana hizo ziwe ni za umeme, ujenzi au useremala, utasaidia kupunguza gharama za uendeshaji kwa jeshi la magereza kwa matengenezo madogo madogo yatafanywa na watu wa kwenye karakana badala ya kutumia watu wa nje.

Amesema ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa nyumba za askari, kila afisa magareza wa mkoa hana budi kuandaa matofali ya kutoka kwani timu za wafyatuaji wanazo na nguvukazi wanayo pia. 

“Badala ya kutegemea wazabuni, kule kwenye udongo mzuri, tafuteni vifaa mfyatue matofali ya hydraform. Kule kwenye mchanga, fyatueni ya saruji. Kuweni na matofali ya kutosha kulingana na mahitaji yenu, mtakuwa mmepunguza gharama za ujenzi wa nyumba za askari kwa kiasi kikubwa,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu huyo, Dk. Malewa amesema atafuatilia suala la upimaji wa maeneo ya magereza kwa sababu wanao wapimaji na vifaa wanavyo. Amesema kuna magareza 11 yenye migogoro ya maeneo na wananchi.

“Pia tutafuatilia upimaji wa maeneo ya mashamba ya magereza. Tumeanzisha mashamba makubwa ya kilimo na tutahakikisha maeneo hayo yote yanapimwa na kuwekewa alama za mipaka,” amesema.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Mwigulu Nchemba; Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Bw. William Tate Ole Nasha; Kamishna Jenerali wa Magereza, Makatibu Wakuu wa Wizara ya Kilimo wanaoshughulikia Kilimo na Mifugo pamoja na Katibu Mkuu wa Mambo ya Ndani.

Read More

MAJALIWA AKUTANA NA MAOFISA WA MAGEREZA

Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa  akisalimiana na Kamishina Mwandamizi  wa Magereza na Mkuu wa Magereza wa Mkoa wa Lindi, Tusikile Mwaisabira baada ya kikao  chake na Maofisa wa Magereza kutoka Makao ya Magereza  na  Maofisa Magereza wa Mikoa, kilichofanyika Ofisini kwake mjini Dodoma   Februari 13,2017
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiongoza  kikao  kati yake na  Maofisa wa Magereza kutoka makao Makuu ya Magereza , pamoja na Makamanda wa Magereza wa Mikoa  yote nchini, ofisini kwake  mjini Dodoma  Februari 13, 2017.
 Waziri Mkuu, Kassim  Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Watalaamu na Wasimamizi wa Mkiradi ya Jeshi la Mgereza, baada ya kikao  chake na Maofisa wa Magereza kutoka Makao ya Magereza  na Wakuu wa Magereza wa Mikoa kilichofanyika Ofisini kwake mjini Dodoma   Februari 13,2017.    Kulia kwake ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba.
Waziri Mkuu, Kassim  Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Maofisa wa  Jeshi la Magereza Wanawake  baada ya kikao  chake na Maofisa wa Magereza kutoka Makao ya Magereza kilichofanyika Ofisini kwake mjini Dodoma   Februari 13,2017.   Kulia kwake ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya  Nchi, Mwigulu Nchemba.
Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa  akisalimiana na Kamishina Jenerali wa Magereza,  Dr Juma Malewa baada ya kikao  chake na Maofisa wa Magereza kutoka Makao ya Magereza kilichofanyika Ofisini kwake mjini Dodoma   Februari 13,2017.   Katikati ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya ndani Meja Jenerali  Projest  Rwegasira.

Read More