Friday, March 13, 2020

WAZIRI MKUU AFUNGUA MSIKITI WA ANNUR WILAYANI RUANGWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akisalimiana na Masheikh wa Wilaya ya Ruangwa wakati akiwasili kwenye Msikiti wa Annur kushiriki swala ya ijumaa na kuufungua rasmi msikiti huo, uliyojengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Al-Hikma Foundation, wilayani Ruangwa katika Mkoa wa Lindi Machi 13, 2020.

Baadhi ya wananchi waumini wakiwa kwenye Msikiti wa Annur, baada ya swala ya ijumaa wakimsikiliza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, wilayani Ruangwa katika Mkoa wa Lindi Machi 13, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akisikiliza mawaidha, yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Al-Hikma, Sheikh Sharif Abdulqader, kwenye Msikiti wa Annur aliposhiriki swala ya ijumaa na kuufungua rasmi Msikiti wa Annur, uliyojengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Al-Hikma Foundation, wilayani Ruangwa katika Mkoa wa Lindi Machi 13, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akihutubia wananchi, kwenye Msikiti wa Annur, baada ya swala ya ijumaa na baadae kufungua rasmi Msikiti huo uliyojengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Al-Hikma Foundation, wilayani Ruangwa katika Mkoa wa Lindi Machi 13, 2020.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akisikiliza mawaidha, yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Al-Hikma, Sheikh Sharif Abdulqader, kwenye Msikiti wa Annur aliposhiriki swala ya ijumaa na kuufungua rasmi Msikiti wa Annur, uliyojengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Al-Hikma Foundation, wilayani Ruangwa katika Mkoa wa Lindi Machi 13, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiweka jibe la msingi kwenye Msikiti wa Annur, uliyojengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Al-Hikma Foundation, wilayani Ruangwa katika Mkoa wa Lindi Machi 13, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Mwenyekiti wa Taasisi ya Al-Hikma, Sheikh Sharif Abdulqader, kwenye Msikiti wa Annur baada ya kufungua rasmi Msikiti wa Annur, uliyojengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Al-Hikma Foundation, wilayani Ruangwa katika Mkoa wa Lindi Machi 13, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiwasalimia wananchi, kwenye Msikiti wa Annur, baada ya swala ya ijumaa na kufungua rasmi Msikiti huo uliyojengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Al-Hikma Foundation, wilayani Ruangwa katika Mkoa wa Lindi Machi 13, 2020.


Read More

WAZIRI KAIRUKI: MFUKO WA KUKOPESHA WAWEKEZAJI KUKOMBOA WENGI

Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Uswidi na Afrika Mashariki Bw. Jan Furuvald akiwasilisha mada wakati wa kongamano hilo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akiteta jambo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  Dkt. Damas Ndumbaro wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki na Wanachama wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Uswidi na Afrika Mashariki kaika Ukumbi wa Mikutano Serena Hotel Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Machi, 2020.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akiteta jambo na Balozi wa Tanznaia nchini Sweden Mhe. Dkt. Wilibrod Slaa wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki na Wanachama wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Uswidi na Afrika Mashariki kaika Ukumbi wa Mikutano Serena Hotel Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Machi, 2020
Rais wa TCCIA Bw. Paul Koyi akihutubia wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki na Wanachama wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Uswidi na Afrika Mashariki kaika Ukumbi wa Mikutano Serena Hotel Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Machi, 2020
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akiteta jambo na Balozi wa Tanzania nchini Swiden Mhe. Dkt. Wilibrod Slaa  wakati wa kongamano hilo.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania TPSF, Godfrey Sembeye  akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Kipindi cha Supa Breakfast kinachorushwa na Eastafrica radio wakati wa kongamano hilo.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Zungu akieleza mikakati ya ofisi yake katika kuvutia wawekezaji wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki na Wanachama wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Uswidi na Afrika Mashariki kaika Ukumbi wa Mikutano Serena Hotel Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Machi, 2020.
Sehemu ya wajumbe wakifuatilia mada mbalimbali katika Kongamano hilo.
Sehemu ya wajumbe wakifuatilia mada mbalimbali katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki na Wanachama wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Uswidi na Afrika Mashariki kaika Ukumbi wa Mikutano Serena Hotel Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Machi, 2020.

Read More

Thursday, March 12, 2020

MAJALIWA: WANAVYUO CHINA WAENDELEA NA MASOMO KWA NJIA YA MTANDAO

WAZIRI MKUU Kassim Mjaliwa amesema wanafunzi wanaosoma katika vyuo vikuu mbalimbali nchini China waliozuiwa kutokana na mlipuko wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona wote wanaendelea na masomo yao kwa njia ya mtandao.

“Tehama sasa imefikia katika hatua nzuri kwa sababu Mhadhili mmoja anaweza kuwafundisha wanafunzi wake wote popote walipo kwa njia ya mtandao. Tehama imewezesha wanafunzi waliozuiwa kurudi nchini China kuendelea na masomo wakiwa nyumbani kwao.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Machi 12, 2020) katika mahafali ya 38 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT), katika uwanja wa Ilulu mjini Lindi. Amesema baada ya virusi vya corona kuikumba China vyuo vilifungwa na sasa vimefunguliwa na wanafunzi wanasomo kwa njia ya mtandao.

Pia, Waziri Mkuu amewaeleza wahitimu wa CKHT kuwa vyeti walivyotunukiwa ni tuzo halali kwa juhudi na jitihada walizoonesha katika masomo yao, hivyo wanaporejea kwenye jamii wahakikishe wanaipatia tuzo ya utendaji bora na ufanisi itakayoakisi viwango vilivyoainishwa kwenye vyeti vyao. 

“Nendeni mkaidhihirishe tuzo hii ya pili katika utendaji wenu na maisha yenu ya kila siku, iwe ni katika sekta rasmi au sekta isiyokuwa rasmi.  Hakikisheni mnaonesha tofauti katika kutafuta majibu ya maswali mbalimbali yanayowakabili Watanzania kuhusu mustakabali mzima wa kujiletea maendeleo.”

Waziri Mkuu amesema amefuatilia kwa karibu maelezo ya Viongozi waliotangulia kuhusu umuhimu na hata mafanikio ya chuo hicho ambapo amewataka watambue kwamba Serikali inakiangalia kwa jicho la karibu sana kwa kuwa kimekaa kimkakati zaidi kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa.

Amesema licha yachangamoto mbalimbali zilizopo, Serikali imeweza kuanzisha chuo hiko na kukiona kikiendelea kutanuka hadi nje ya mipaka ya nchi yetu.  “Haya ni mafanikio makubwa na ya kujivunia. Tunawashukuru waasisi wa Taifa letu kwa maono haya makubwa kuhusu Tanzania.”  

Waziri Mkuu amesema Mwasisi wa Taifa letu, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliona mbali sana wakati akianzisha mchakato wa kuanzisha Chuo hiki kwa kusema angependa kuona taasisi inawawezesha watu wazima wengi waweze kuendelea na elimu ya juu pasipo kuacha kazi zao. 

Vilevile, aliongeza kwa kusema, “Kwa nchi maskini kama Tanzania, hakuna Taasisi nyingine ya elimu ya juu inayoweza kuwa ya msaada zaidi kwa watu wetu”. 

Waziri Mkuu amesema ukweli wa kauli hiyo unaendelea kudhihirishwa siku hadi siku kupitia mafanikio ya chuo hicho. “Tutake tusitake, elimu ya juu inayoweza kusaidia watanzania wengi zaidi ni hii ya kupitia mfumo wa Elimu Masafa na Huria.”

Waziri Mkuu ameongeza kuwa umuhimu na thamani ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na vyuo vingine utakuwa na maana tu pale ambapo vitakuwa na mchango kwenye maendeleo ya nchi. 

“Kwa miaka nenda rudi, chuo kimehitimisha wataalamu lukuki, ambao wengi wameingia kwenye sekta mbalimbali za utumishi na uzalishaji na kutoa mchango muhimu sana kwenye maendeleo ya nchi yetu.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametoa rai kwa uongozi wa CKHT na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TVV) wahakikishe kuwa udahili wa CKHT unatanuliwa kwa sababu hadi sasa chuo kina kozi moja tu ya maandalizi kwa ajili ya kuwaandaa vijana kuingia kwenye Shahada. 

Waziri Mkuu amesema katika kuongeza udahili kwenye elimu ya juu, ameshauri wawe na kozi ama programu za maandalizi kwa wale wanaotaka kusoma stashahada na kwa wale wa cheti pia. 

Amesema matokeo ya programu hizo yataongeza ushiriki wa Watanzania wengi kwenye elimu ya juu. “Wito wangu kwa TCU nchini kuhakikisha inasimimia na kuongoza, kwa kushirikiana na CKHT katika uanzishwaji wa programu hizi kwa kuzingatia viwango vya juu vya ubora wa elimu ya juu.”

Katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 698 walitunikiwa vyeti wakiwemo 20 wa Shahada za Uzamivu (PhD) na wengine 185 Shahada na Stashahada za Uzamili, wengine 344 walitunukiwa Shahada ya Kwanza, 166 walitunikiwa Stashahada na Astashahada mbalimbali. 

Mahafali hayo yamehudhuliwa naWaziri Mkuu Mstaafu na Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania Mizengo Peter Pinda, Mkuu wa Mkoa wa Lindi na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Chuo Mkoani Lindi Godfrey W. Zambi,

Wengine ni Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania, Profesa Rwekaza Mukandala, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania Profesa Elifas Tozo Bisanda na wakuu wa wilaya za mkoa wa Lindi

Read More

WAZIRI MHAGAMA ATOA MAAGIZO MAZITO USIMAMIZI VITALU NYUMBA



Na. OWM, Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama, ametoa maagizo sita kwa  waratibu na wadau wa Programu ya mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba “Greenhouse”na kuwataka kutekeleza, kwa wakati na ufanisi maagizo yake yanayojikita katika  kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa mafunzo hayo ili yawe na ubora zaidi na tija kwa vijana.

Waziri Mhagama ameagiza  kufanyika maamuzi ya haraka yatakayowezesha vijana katika halmashauri ambazo bado mradi huo haujafika wanafikiwa. Aidha, Fedha zote zilizokusanywa na vijana katika awamu ya kwanza ya mafunzo hayo zikaguliwe na vijana washirikishwe ili waweze kutoa taarifa ya idadi ya mazao waliyozalisha na kiwango walichoweza kuuza. 

Akitoa magizo hayo leo,  Machi 11 2020 kwa kikao kilichowakutanisha vijana, Wadau,Waratibu ambao ni Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Kilimo, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na wakandarasi ambao walijenga vitalu nyumba, amewagiza  kuanzishwa mfumo wa ufuatiliaji ambao utakuwa na taarifa ya utekelezaji wa majukumu. 

"Kuanzia sasa  ni lazima mikopo kwa vijana ipatikane kwa wakati,  nataka upatikanaji wa mikopo ambayo itawasaidia vijana hao kuanzisha vitalu nyumba vyao, pia tengenezeni  mfumo wa ukusanyaji mapato na matumizi. Wakandarasi waliojenga vitalu nyumba katika halmashauri 84 awamu ya kwanza fanyeni  marekebisho kwenye  vitalu nyumba ambavyo vimekuwa na matatizo. Nataka usimamizi na uendeshaji wa programu ya mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba “Greenhouse” uwe chachu  ya  kuongeza ajira kwa vijana katika sekta ya kilimo" amesisitiza Mhagama.

Waziri Mhagama amefafanu akuwa,  Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ina nia ya dhati ya kuwawezesha vijana kupitia programu mbalimbali inazoazisha kwa lengo la kuwasaidia vijana kuondokana na changamoto ya ajira.

“Serikali ina lengo la kufikisha ujuzi huo wa kilimo cha kisasa katika halmashauri zote za Tanzania bara kwa kuwa asilimia 63 ya fursa za ajira zinapatikana kwenye kilimo na tena maeneo ya vijijini,” alisema Mhagama 

Waziri Mhagama, amebainisha kuwa,  Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ndio yenye dhamana na masuala ya vijana iliamua kupitia ilani ya uchaguzi ibara ya 6 kifungu (a) inayosema kuhamasisha kilimo kupitia kauli mbiu ya Kilimo Kwanza kwa kuwawezesha wakulima kupata mafunzo ya kilimo cha kisasa, pembejeo, zana za kisasa na wataalamu wa ugani pamoja na mbinu za kuyafikia masoko ya uhakika ya mazao yao, ambao ulipelekea kutambua umuhimu wa mchango wa vijana hasa waliopo vijijini ndipo mradi huu wa Kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba ulianzishwa kwa lengo la kuwezesha vijana,” amesema Mhagama.


“Mataifa makubwa mengi yaliyoendelea wamekuwa wakitumia kilimo cha aina hiyo kwa lengo la kulima kisasa, kuongeza thamani ya mazao, kupata masoko endelevu na la uhakika na kulima kwa tija, hivyo tukiwawezesha vijana wetu watanufaika na kilimo hicho na sekta hiyo italeta tija katika kukuza uchumi wa nchi,” alieleza Mhagama.

Waziri Mhagama amewataka vijana kutumia ujuzi waliopata katika mafunzo hayo ili waweze kusimamia mradi huo vizuri na wajenge moyo wa kuthubutu katika kuwasaidia vijana wenzao kupata ujuzi wa mafunzo hayo ya kilimo cha kisasa.


Wakati huo huo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw. Andrew Massawe amesema kuwa ameyakupokea maagizo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi ili programu hiyo ya mafunzo ya kilimo cha kisasa iweze kuwa endelevu.


“Ofisi ya Waziri Mkuu iliona umuhimu wa kushirikiana na , Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Kilimo, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, wakandarasi pamoja na Vijana ili kutathmini utekelezaji wa mradi huo na kuona namna ya kukabili changamoto ambazo zilijitokeza, mafanikio yaliyopatikana ili kuona namna bora ya kuimarisha mafunzo hayo,” amesema Massawe.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Ally Msaki ameelezea maazimio waliyofikia pamoja na wadau katika kuimaarisha usimamizi na uendeshaji wa mafunzo hayo

"Pamoja na kuangalia namna bora ya kuendesha mafunzo haya, tumemua kuwa  tutasimamia uwepo wa utaratibu maalum wa makusanyo, utunzaji na matumizi ya fedha, kuwezesha vijana kuwa na ujuzi wa kuongeza thamani ya mazao, kuelezea wananchi mafanikio yaliyopatikana kupitia mradi huo wa kilimo cha Kitalu nyumba,kuwezesha vijana kufanya kilimo biashara na uwepo wa muendelezo wa kutoa mafunzo na kuongeza vitalu nyumba katika kila halmashauri" amesitiza Msaki.

Naye Mmoja wa wanufaika wa Programu hiyo Bw. Festo Masiba ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo yamewajengea ujuzi mkubwa wa kuweza kulima kwa tija.


“Tunaishukuru Serikali kwa kutuamini sisi vijana na kutuwezesha kupata mafunzo ya Kilimo bora kwa kutumia eneo dogo na upatikanaji wa mazao ni mwingi, tumeweza kukua kiuchumi na tunaujuzi wa kuwajengea wadau wengine vitalu nyumba,” alisema Masiba .


MWISHO
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw. Andrew Massawe akieleza jambo wakati wa mkutano huo uliofanyika machi 11, 2020 katika Ukumbi wa Landmark Kilimani, Jijini Dodoma.
Baadhi ya Wakuu wa Idara kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu wakifuatilia mijadala wakati wa mkutano huo.
Sehemu ya vijana wakifuatilia kwa makini hotuba ya Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) walipokutana kujadili namna bora ya kuimarisha mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba.
Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (wa nne kutoka kulia waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wataalamu kutoka ofisi yake, Wadau na Vijana wapokutana kwa lengo la kujadili namna bora ya kuimarisha mafunzo ya Kilimo kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba katika Ukumbi wa Landmark Kilimani, Jijini Dodoma.
Read More

WAZIRI KAIRUKI: MFUKO WA KUKOPESHA WAWEKEZAJI KUKOMBOA WENGI

NA. MWANDISHI WETU
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imewezesha kuanzisha mfuko maalum wa kukopesha watu wenye nia ya kuwekeza kwenye viwanda vya kati na vikubwa lengo likiwa ni kuwanufaisha Watanzania waliokosa mitaji na wenye nia ya kuwekeza nchini.
Mfuko huo ulioanzishwa Februari 22 mwaka huu utakuwa ukikopesha Watanzania kuanzia kiwango cha shilingi  milioni 8 hadi 50 kwa wenye nia ya kuwekeza viwanda vya kati na shilingi milioni 50 hadi 300 kwa wenye nia ya kuwekeza kwenye viwanda vikubwa.
Aidha, ofisi hiyo inashirikiana na taasisi nyingine kuendesha mfuko huo ikiwepo Mfuko wa Hifadhi za Jamii (NSSF), Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Shirika la Viwanda Vidogo Tanzania (SIDO) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Hayo yamebainishwa hii leo (Machi 12, 2020) Jijini Dar Es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angellah Kairuki wakati akizungumza na Waandishi wa Habari  mara baada ya kufungua Kongamano la pili la Biashara na Uwekezaji la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Sweden linaloendelea kwa siku mbili Jijini humo.
Kairuki amesema Tanzania hivi sasa imeimarisha Mazingira ya Uwekezaji ambapo tangu kuingia kwa Rais Magufuli Madarakani hakuna kodi yoyote iliyoongezwa kwenye biashara na uwekezaji huku kodi zaidi ya 168 zikifutwa katika kipindi cha miaka miwili zikiwepo kodi 105 za kilimo.
Wakati akifungua Kongamano hilo Waziri Kairuki aliwataka Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza nchini Tanzania kwa kueleza kuwa Sera, Sheria na miundombinu yake imeboreshwa kwa kiwango kikubwa.
"Tunazo fursa nyingi za uwekezaji hapa Tanzania, tuna fursa kwenye Kilimo cha mazao ya chakula na biashara pamoja na mnyororo wake wa thamani kwenye sekta hiyo, tunahitaji uwekezaji wa viwanda mbalimbali vikiwepo vya Dawa na  vifaa tiba, mafuta ya kula na vinginevyo vingi" alisema Waziri Kairuki.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dkt Wilbrod Slaa amesema Wafanyabiashara wa NORDIC wameisifu Serikali ya Tanzania  kwa kuondoa rushwa na kuimarisha utendaji wa wazi Serikalini suala ambalo awali lilikuwa likuwapa changamoto kubwa.
"Nimekuwa nakutana na wafanyabiashara na wawekezaji wengi wa Sweden jambo kubwa nililolipata kutoka kwao ni kwamba wanashukuru tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilivyoingia madarakani mambo ya chini ya meza hayapo tena, angalau sasa wanafanya biashara juu ya meza wengine walifikia hatua ya kufunga biashara zao, lakini pia naomba nishauri tu vibali vya wawekezaji viharakishwe ili kwenda na wakati", alisema Dkt. Slaa.
Kongamano hilo ambalo kwa mara ya kwanza lilifanyika Stockhom Sweden mwaka 2012 lilikuja ma naadhimio kadhaa ya kushirikiana katika kuimarisha uchumi wa nchi hizo kibiashara na uwekezaji lilileta matokeo chanya kufuatia kuwepo kwa wawekezaji wengi wa Sweden kuwekeza kwenye nchi za Afrika Mashariki.
Mkutano huo umehudhuriwa na zaidi ya makampuni makubwa 20 toka Sweden kupitia Chama chao cha Wafanyabiashara na Wawekezaji wa Afrika Mashariki (SWEACC) ambapo Mwenyekiti wake Bw. Jan Furuvald amesema uwekezaji kwenye nchi hizo umekuwa na manufaa kutokana na kuwa na soko kubwa la watumiaji wa bidhaa zao na kuwataka wawekezaji wengine kutoka nchini kwake kuja kuwekeza Afrika Mashariki.
"Sisi Wafanyabiashara na wawekezaji mara nyingi tunaangalia mazingira mazuri ya uwekezaji, kuwekeza kwenye nchi za Afrika Mashariki kunatuhakikishia soko kubwa kwani licha ya kuwa kwenye jumuiya hii pia kuna fursa nyingine za SADC", alisema Furuvald.
Kongamano hilo lenye kauli mbiu ya "Green Solutions in East African Cities" Suluhisho la Kijani kwenye Majiji ya Afrika Mashariki linalenga kuimarisha mazingira ya uwekezaji kwenye majiji yaliyopo kwenye Jumuiya hiyo ambapo kwa Tanzania, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Mussa Zungu amesema ili kukabiliana na hali hiyo hatua kadhaa zimechukuliwa.
Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja  na kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki ambayo ilikuwa ikichafua mazingira na kuharibu mazalia ya viumbe hai ambapo pia kwa sasa Serikali inahamasisha matumizi ya gesi viwandani, majumbani na kwenye magari ili kuepukana na uchafuzi wa mazingira na ukataji miti hivyo kwa ajili ya matumizi ya nishati za mkaa na kuni.
Waziri Zungu amesema katika kuhakikisha nishati mbadala inapatikana kwa urahisi Serikali inajenga Bwawa kubwa la kufua umeme la Nyerere ili kuwe na umeme wa uhakika.
Aidha Zungu aliwataka wawekezaji wote waliokwama kupata vibali vya mazingira kutokana na mazingira ya rushwa kufika ofisini kwake kwa ajili ya kupata vibali hiyo.
"Kwa Wawekezaji waliokwama kupata vibali vya mazingira wanione, tutawapatia vibali vyao bila kuhangaika, hakuna jambo baya Duniani kama kumnyima mtu haki yake ili upate pesa, tunathamini wawekezaji na tunathamini uwekezaji katika nchi yetu" alisema Zungu.
Naye, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stellah Manyanya akasema Serikali ya Tanzania imekuwa ikiweka mazingira mazuri ya biashara kwa kuimarisha miundombinu Sera na miundombinu ambapo kwa sasa ujenzi mkubwa wa Reli ya Kisasa ya Standard Gauge unaendelea lengo likiwa ni kuzifanya nchi hizo kunufaika kwa usafirishaji kauli inayoungwa mkono na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro.
"Kazi ya Serikali yetu ni kuweka mazingira mazuri ya Biashara na Uwekezaji yakiwepo ya Sera, Sheria na Miundombinu, kuimarisha Blue print na hali ya kisiasa ambayo ina tija kubwa kiuchumi", alisema Mhandisi Manyanya.
=MWISHO=
Read More

Wednesday, March 11, 2020

TIMU YA WATAALAM YA KUKABILIANA NA UGONJWA WA CORONA KUTOKA TANZANIA BARA IMETEMBELEA VISIWANI ZANZIBAR

Timu ya wataalam ya kukabiliana na ugonjwa wa corona kutoka tanzania bara imetembelea visiwani Zanzibar. Timu hiyo itatembelea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Karume,hospitali ya mnazi mmoja,eneo maalumu la matibabu iwapo watatokea wahisiwa liliopo  Kidimni wilaya ya kati-Unguja pamoja na bandarini.Timu hiyo inahusisha wataalam kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee ma Watoto, TAMISEMI, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kikanda, pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu- Idara ya Menejimenti ya Maafa,  leo 11 Machi, 2020.

Read More

WAGANGA WAKUU WA MIKOA WAPENI ELIMU YA KUJIKINGA NA CORONA WANANCHI - DKT.CHAULA

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto-Idara kuu afya Dkt. Zainab Chaula akiongea na waganga wakuu wa mikoa(hawapo pichani) wakati wa mkutano wa kujadili utayari wa kukabiliana na tishio la mlipuko wa virus  vya corona kwenye ukumbi wa mkutano wa hospitali ya taifa muhimbili-mloganzila


Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia afya kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Dorothy Gwajima akiongea na waganga wakuu wa mikoa



Mratibu wa Masuala ya Maafa, Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Harrison Chinyuka,  ambaye alimwakilisha  Mkurugenzi wa idara hiyo,  amewasisitiza waganga wakuu wa mikoa kutoa elimu ya magonjwa ya mlipuko  kwa wataalam wengine hususan timu za maafa kwenye mikoa yao
Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula akiwa na Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI Dkt. Dorothy Gwajima pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhammad Bakari Kambi wakati wa mkutano huo
Mkuu wa huduma za afya jeshini-JWTZ Kanali Moses Mlula akiongea na waganga wakuu wa mikoa ambapo alisema kama wataalam wanatakiwa kutoa mchango kwa serikali ili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kwa kuangalia nchi zingine wanafanya nini.
Afisa kutoka kitengo cha magonjwa ya milipuko wizara ya afya Dkt. Vida Makundi akitoa mada kwenye mkutano wa waganga wakuu wa mikoa
Baadhi wa waganga wakuu wa mikoa na maofisa kutoka wizara ya afya walioshiriki mkutano wa kujadili tishio la ugonjwa wa Corona

Na. WAMJW - Dar es Salaam

Wananchi wanatakiwa kupewa elimu ya jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaoletwa na kirusi wa Corona (COVID-19) ili kuepusha usisambae endapo atatokea muhisiwa wa ugonjwa huo hapa nchini.
Maelekezo hayo yametolewa leo na Katibu Mkuu - Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto: Idara Kuu Afya Dkt. Zainab Chaula, wakati wa Mkutano wa Kitaifa wa Waganga Wakuu wa Mikoa (RMOs) wa kujadili utayari, changamoto na hatua za kukabiliana  na tishio la mlipuko wa COVID-19 uliofanyika kwenye ukumbi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Mloganzila jijini Dar es slaam , tarehe 10 Machi 2020.

“Katika mkoa wewe mganga mkuu wa mkoa ndio mtaalam namba moja wa afya kwenye mkoa wako ambalo ndilo eneo lako la kazi, hivyo mnatakiwa kushauri viongozi katika kukabiliana na ugonjwa huu”. Amesisitiza  Dkt. Chaula

Amesema upashanaji elimu juu ya kujikinga na maambukizi kwa wananchi ni jambo muhimu sana kwani jamii inapaswa kuwa na uelewa wa pamoja wa namna ya ugonjwa huo unavyoambukizwa pamoja na dalili zake ili kila rika iweze kuwa na ufahamu na hivyo itasaidia kuepusha magonjwa ya mlipuko yasiingie nchini.

“Kama nchi za Afrika hivi sasa hatupo kwenye hatua ya utayari bali kwenye hatua ya kukabiliana. Kwani utaona ugonjwa huu umezikumba nchi nyingine, hivyo kama nchi lazima wataalam wote tujiandae kukabiliana na virusi hivi vya Corona ili endapo tutapata mgonjwa basi vyanzo vyote vya maambukizi vinatakiwa kudhibitiwa ili usienee.

Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - TAMISEMI anayeshughulikia afya Dkt. Doroth Gwajima amesema kuwa TAMISEMI wapo tayari kupokea maelekezo na mafunzo yote ya kisekta ili kutimiza lengo tarajiwa la Serikali la kudhibiti na kukabiliana ugonjwa huo.

Dkt. Gwajiama amesema kuwa mkutano huu utasaidia waganga wakuu wa mikoa nchini kutoka na mkakati wa pamoja wa namna ya kukabiliana na ugonjwa huu hususan mikoa ya mipakani kama Kagera, Katavi, Songwe, Kigoma, pamoja na mikoa mingine ambayo ipo kwenye hatari ya kuingia kwa magonjwa ya mlipuko.

Hata hivyo Naibu Katibu Mkuu huyo amewataka waganga wakuu hao kutoa mafunzo kwa wataalam wengine wa chini yao na viongozi wa mikoa na halmashauri ili kwenda pamoja katika kukabiliana na magonjwa wakati wa dharura.
Kwa upande wake Mratibu wa Masuala ya maafa, Idara ya Menejimenti ya Maafa, ofisi ya Waziri Mkuu, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara hiyo amefafanua kuwa, katika ngazi ya mkoa na wilaya hadi kwenye vijiji zipo Kamati za maafa hivyo wataalamu hao hawanabudi kuwap elimu ili waweze kuwelimisha wananchi walionao katika ngazi zao na hatimaye uwezo wa kukabiliana na ugonjwa huo utakuwa umeimarika.

-MWISHO-

Read More

Tuesday, March 10, 2020

WAZIRI MKUU AKAGUA DARAJA LA MUDA LA KIYEGEYA

*Abaini Meneja wa TANROADS Mkoa bado hajateuliwa
*Aliyemhamisha akutwa bado yuko ‘site’ sababu ni mtaalamu wa madaraja

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa barabara ya muda kwenye eneo la daraja la Kiyegeya na kusema kazi inaenda vizuri sababu hakuna tena msongamano wa magari kama ilivyokuwa wiki iliyopita.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa Mameneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wa mikoa yote nchini wanapaswa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa madaraja yote siyo kwa juu tu bali hadi chini ya madaraja ili kujiridhisha na usalama wake.

“Nilitoa agizo kwa mameneja wa TANROADS ambao wana highways, wazikague kila mara kwa sababu hatuhitaji kuwa na highways zilizobomoka.”

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Machi 10, 2020) wakati akizungumza na watendaji wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na viongozi wa Mkoa wa Morogoro, mara baada ya kutembelea eneo hilo na kukagua ujenzi wa barabara ya muda ili kurejesha mawasiliano na mikoa mingine.

“Nimekuja kuona kazi inaendeleaje, nimekuta msongamano wa magari hakuna kama ilivyokuwa wiki iliyopita. Ile diversion (barabara ya mchepuko) imesaidia kuondoa msongano uliokuwepo,” amesema Waziri Mkuu.

“Mahitaji yetu ni kuwa na daraja la kudumu, kwa hiyo mharakishe ujenzi wa daraja hilo, Mmesema sasa hivi mnapanga kuweka daraja la zege ili maji yakija kwa wingi yaweze kupita juu ya hii barabara ya muda, msisitizo ni kukamilisha kazi ya daraja la kudumu,” amesema wakati akizungumza na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale.

Katika ukaguzi huo, Waziri Mkuu alibaini kuwa Meneja wa TANROADS, mkoa wa Morogoro, Mhandisi Godwin Andalwisye ambaye aliagiza arejeshwe wizarani na nafasi yake ijazwe na mtu mwingine, bado alikuwepo kwenye eneo la tukio akiendelea na kazi.

“Uamuzi niliochukua wa kumhamisha Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro ulikuwa sahihi kwa sababu huyu Bwana anaonekana hawezi kazi ya kusimamia wengine. Fedha ya ukaguzi ipo, ya ujenzi ipo, halafu kazi haifanyiki. Kazi ya kusupervise haiwezi, kwa hiyo, ateuliwe Meneja mwingine,” alisisitiza.

“Nilimuuliza meneja aliyekuwepo kama wana fedha za ukaguzi, akasema anayo. Nikamuuliza kama anayo fedha ya spot maintenance, akasema anayo. Fedha hizi zote zilipaswa zitumike kwa kazi iliyopangwa, lakini hilo halikufanyika.”

Akijibu hoja hiyo, Mhandishi Mfugale alisema amemuacha Mhandisi Godwin Andalwisye aendelee kuwepo pale site kwa sababu ya utalaamu wake kweye madaraja. “Ulishatoa maelekezo kuwa aondolewe, na wa kumhamisha ni mimi, tunatumia tu utaalmu wake.

Alipoulizwa kama ameshateua Meneja mwingine wa Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Mfugale alikiri kwamba bado hajamteua mtu mwingine.

Jumatano iliyopita, (Machi 4, 2020) Waziri Mkuu alikatisha ziara yake mkoani Tanga na kutembelea eneo hilo ambako alishuhudia mlundikano wa magari na abiria hali ambayo haikumfurahisha.

Aliagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Morogoro, Mhandisi Godwin Andalwisye arejeshwe wizarani na nafasi yake ijazwe na mtu mwingine mara moja kwa sababu ya kuzembea kutimiza wajibu wake.

Waziri Mkuu ambaye alisafiri kwa magari kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, pia alisimama Morogoro na kukagua ujenzi wa uzio wa makaburi ya Kola Hill ambako walizikwa wahanga wa ajali ya lori la mafuta lililopinduka na kulipuka Agosti 10, 2019 na kuua watu 115, kati yao wanaume walikuwa ni 109 na wanawake ni sita.

Akiwa makaburini hapo, Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa Manispaa ya Morogoro uweke utaratibu wa kuwa na mtu maalum atakayesimamia masuala ya mazishi yote yatakayofanyika kwenye makaburi ya Kola Hill.

Amesema mtu huyo ahakikishe makaburi yote yanachimbwa katika utaratibu na mpangilio utakaoliwezesha eneo hilo kuwa na nafasi ya kuzika watu wengi. “Utaratibu wa sasa wa kuchimba makaburi kiholela utalifanya eneo hili lijae haraka huku likiwa halina mpangilio maalum.”

Waziri Mkuu pia aliridhia maombi ya uongozi wa mkoa wa Morogoro ya kutaka akubali makaburi hayo yajengewe ili yawe na muonekano mzuri kazi ambayo itagharimu zaidi ya sh. milioni 12.

Uongozi huo pia uliomba rdhaa ya Waziri Mkuu kutengeneza mandhari ya ndani ya uzio (Landscaping) kazi ambayo itagharimu sh. 1,682,500/- pamoja na kujenga mnara wa kumbukumbu kwa gharama ya sh. 4,173,125/-.

(mwisho)
Read More

MAJALIWA AKAGUA UJENZI WA BARABARA YA MUDA KATIKA ENEO LA KIYEGEYA WILAYANI KILOSA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akikagua  kazi ya ujenzi wa ukuta  wa kuzunguka makaburi  ya wahanga wa moto katika eneo la Kolahill mjini Morogoro, Machi 10, 2020.  Kulia ni Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa barabara ya muda katika eneo la Kiyegeya wilayani Kilosa, Machi 10, 2020. Wa tatu kushoto ni mkewe, Mary na kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Rota Sanare.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patric Mfugale  (mwenye kofia) wakati alipokagua ujenzi wa barabara ya muda  katika eneo la Kiyegeya wilayani Kilosa Machi 10, 2020. Kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Kalobelo.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patric Mfugale  (mwenye kofia) wakati alipokagua ujenzi wa barabara ya muda  katika eneo la Kiyegeya wilayani Kilosa Machi 10, 2020. Kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Kalobelo.
Kazi ya ujenzi wa barabara ya muda katika eneo la Kiyegeya wilayani Kilosa Machi 10, 2020. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  amekagua ujenzi huo leo.


Read More