WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuboresha maslahi ya watumishi wote wa umma wakiwemo wa kada ya afya kupitia Bodi ya Mishahara na Motisha baada ya kukamilisha uhakiki wa taarifa za kiutumishi.
Amesema kukamilika kwa uhakiki huo wa taarifa za kiutumishi kwa watumishi wa umma kutaiwezesha Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kupanga upya mishahara na motisha kwa watumishi.
Waziri Mkuu alitoa taarifa hiyo jana jioni (Alhamisi, Novemba 29, 2018) alipozungumza na watumishi wa Kituo cha Afya cha Ushirombo wilayani Bukombe baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi mradi wa uboreshaji miundombinu wa kituo hicho uliogharimu sh. milioni 500.
Alisema Serikali inaendelea kushughulikia maslahi ya watumishi, hivyo aliwataka waendelee kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi bila ya ubaguzi wa aina yoyote. “Tunataka mwananchi akifika kwenye maeneo ya kutolea huduma apokelewe, asikilizwe na ahudumiwe.”
Kadhalika, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Bukombe kwa kutekeleza kwa vitendo agizo la Serikali la kujenga Zahanati katika kila kijiji kwa kuwa wilaya hiyo imebakisha vijiji 2 kati ya 52 kumalizia ujenzi huo.
Waziri Mkuu alisema kwa sasa wananchi wa Ushirombo hawana sababu ya kusafiri umbali mrefu hadi Geita mjini au wilayani Kahama kwa ajili ya kufuata huduma za afya kwa kuwa huduma zote zitakuwa zikipatikana kituoni hapo.
Alizitaja huduma ambazo zitakuwa zikipatikana kwenye Kituo cha Afya cha Ushirombo kuwa ni pamoja na za mama na mtoto, huduma za upasuaji wa aina zote mdogo na mkubwa, maabara, chumba cha kuhifadhia maiti.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Bukombe, Dionis Myinga alisema ukarabati wa Kituo cha Afya cha Ushirombo ulianza Juni 22, mwaka huu na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka huu.
Alisema lengo la mradi huo ni kukiwezesha Kituo cha Afya cha Ushirombo kutoa huduma bora za upasuaji wa dharura kwa akinamama wajawazito pindi wapatapo matatizo yatokanayo na uzazi. Majengo yote ya kipaumbele yamekamilika kwa asilimia 99.
“Mradi huu ambao tunaujenga kwa kutumia force account, pamoja na lengo la kutatua matatizo yatokanayo na uzazi kwa akinamama mradi huu utakapokamilika, Kituo cha Afya cha Ushirombo kitaweza kuhudumia watu wapatao 54,271.”
Mkurugenzi huyo alisema mradi wa ukarabati wa kituo hicho cha afya unakadiriwa kutumia sh. milioni 436.933 hadi utakapokamilika na sh. milioni 63.066 zilizosalia kwenye ukarabati huo zitatumika kujenga njia za kuunganisha wodi na kukarabati majengo ya zamani.
(mwisho)