Thursday, November 29, 2018

WAZIRI MKUU ACHUKIZWA NA WANAFUNZI KUKATISHWA MASOMO


*Ni baada ya wanafunzi 72 wa kike kupewa ujauzito wilayani Nyang’hwale

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amechukizwa na vitendo vya watoto wa kike kukatisha masomo yao kwa kupata ujauzito wilayani Nyang’hwale ambapo jumla ya wanafunzi 72 wamepata ujauzo katika kipindi cha miaka mitatu cha kuanzia mwaka 2016 hadi 2018.

Kutokana na wilaya hiyo kuwa na idadi kubwa ya watoto wa kike wanaokatisha masomo kutokana na ujauzito, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale Hamim Gwiyama kufanya operesheni katika kila kijiji na kubaini waliowapa wanafunzi ujauzito na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana jioni (Jumatano, Novemba 28, 2018) alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Sabasaba,kijiji cha Kalumwa wilaya ya Nyang’hwale, akiwa katika ziara yake mkoani Geita.

“Jambo lingine litakalowawezesha kukabiliana na tatizo la ujauzito kwa wanafunzi wa kike ni kuanzisha miradi ya ujenzi wa mabweni ili watoto wa kike waweze kusoma bila ya kupata vishawishi vinavyosababisha wao kupata ujauzito.” 

Waziri Mkuu alisema Serikali haiwezi kuacha jambo hilo likiendelea, hivyo aliwataka wananchi washirikiane katika kuwalinda watoto wa kike na Serikali itawachukulia hatua watendaji wote ambao katika maeneo yao watoto wa kike watabainika kuwa na ujauzito.

 “Watoto wa kike lazima waheshimiwe waachwe wasome bila ya usumbufu na atakayekatisha masomo adhabu yake ni kali. Tukikukuta umesimama na binti katika kona isiyoeleweka tutakukamata. Ole wenumtakaobainika kuwapa ujauzito wanafunzi, adhabu yake ni miaka 30 jela.”

Waziri Mkuu pia, alitoa onyo kwa wazazi au walezi watakaowaozesha watoto kike ambao bado ni wanafunzi na kwa upande wa wazazi watakaomsindikiza mtoto wao wa kiume kwenda kuoa mwanafunzi wote watachukuliwa hatua za kisheria.

Katika kuoneshwa kuchukizwa na jambo hilo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mwita Waitara ambaye anashughulikia elimu, amemueleza Waziri Mkuu kwamba Novemba 30, 2018 yeye arudi wilayani hapo kwa  ajili ya kuwashughulia wote wanaokatisha masomo wanafunzi kike. Ametoa namba ya simu ili wananchi waanze kumpa taarifa za wahusika.

Katika hatua nyingine,Waziri Mkuu alisemaSerikali imedhamiria kusambaza umeme katika vijiji vyote ambavyo bado havijaunganishiwa nishati hiyo nchini vitaunganishiwa katika awamu ya tatu ya Mradi wa Nishati Vijijini (REA).

“Rais wetu Dkt. John Magufuli anataka kuona nyumba ya kila Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote nchini. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu.”

Kuhusu suala la gharama za kulipia nguzo, Waziri Mkuu alisema wananchi hawatowajibika tena katika kulipia gharama za nguzo pamoja na zile za fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme kwa sababu tayari gharama hizo zimeshabebwa na Serikali.

Awali, Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kuchenjua dhahabu cha Nyamigogo ambapo alikagua miundombinu ya kiwanda hicho na kisha aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda hicho, ambacho muwekezaji wake ni mzawa.
(mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.