Saturday, November 10, 2018

PROF. KAMUZORA AWATAKA WAKULIMA WA KASULU KUZALISHA KWA TIJA


NA.MWANDISHI WETU
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera na Uratibu Prof.Faustin Kamuzora amewataka wakulima wa Wilaya ya Kasulu kulima kwa tija ili kuondokana na changamoto wanazokabiliana nazo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa masoko.
Ametoa kauli hiyo Novemba 08, 2018 alipofanya ziara katika maeneo ya Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara Local Investment Climate (LIC) ikiwemo Mradi wa Umwagiliaji wa Tittye Wilayani Kasulu mkoani Kigoma ili kukagua na kujiridhisha ubora na faida zitokanazo na mradi huo.
“Wakulima wa Wilaya ya Kasulu hamna budi kubadili mitazamo katika uzalishaji kwa kuanza kuweka mikakati ya kuzalisha kwa tija ili kuondokana na changamoto za kukosa masoko ya mazao ikiwemo Mpunga na mihogo hivyo ni wakati muafaka kuwatumia maafisa kilimo waliopo ili kupata mbinu mbadala za matumizi mazuri ya pembejeo za kisasa ili kuzalisha kwa tija”.Alisema Prof.Kamuzora
Aliongezea kuwa wakulima wanapaswa kuondokana na dhana potofu ya kilimo cha asili kinachohusisha dhana ya kulima kwa dawa za kienyeji ambazo wamekuwa wakizitumia kwa muda mrefu bila kuleta matunda wanayotarajiwa.
“Ni vyema sasa kuachana na kilimo cha matumizi ya dawa za kienyeji na hatimaye muone namna bora ya kuwatumia wataalam wa masuala ya kilimo ili  kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ili kuzalisha kwa tija.”Alisisitiza Prof.Kamuzora
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Mhe.Kanali Simon Anange aliahidi kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Katibu Mkuu huyo pamoja na kutoa rai kwa wakulima wa Kasulu kuendelea kuzalisha kwa tija ili kuendana na soko lililopo.
Aidha alipongeza juhudi za Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Mradi wa LIC kwa kuendelea kuwawezesha wakulima wa wilaya yake kwa kuwapatia elimu na kuboresha miundombinu ikiwemo ujenzi wa mfereji wa umwagiliaji katika mashamba ya mpunga ya Titye na kukiri ongezeko la uzalishaji toka mradi ulipoanza mwaka 2014 hadi sasa.
“Mradi wa umwagiliaji umekomboa wakulima 750 katika Wilaya yangu ya Kasulu hivyo, niwatake sasa wakuliwa kuendelea kuutumia mradi huu wa kuboresha mazingira ya biashara kwa kuhakikisha tunazalisha kwa tija pamoja na kushirikiana na sekta binafsi”.alisisitiza Kanali Anange.
Kwa upande  wake mmoja wa wanufaika wa mradi huu Bi.Evelyne Reuben alishukuru Serikali kwa jitihada za kuwafikia wakulima kwa kutoa elimu ya kilimo cha kisasa pamoja na uboreshaji wa mazingira ya kilimo na kuomba jitihada hizo ziendelee ili kumaliza changamoto za kukosekana kwa masoko na kuiomba serikali kuendelea kuleta pembejeo za kilimo kwa wakati.
“Ninaipongeza Serikali kwa kutukumbuka wana Kasulu ila ombi letu kama wakulima ni kupatiwa pembejeo za kilimo kwa wakati pamoja na kuendelea kupewa elimu ya kilimo cha kisasa ili kuwa na uzalishaji wenye tija zaidi”.Alieleza Evelyne.
=MWISHO=
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Mhe.Kanali Simon Anange akizungumza jambo wakati wa kikao cha pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Prof.Faustin Kamuzora alipotembelea ofisini kwake kwa lengo la kupata taarifa za miradi inayotekelezwa chini ya uratibu wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC).

Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara Bi.Oliver Ligula akichangia jambo wakati wa kikao na Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Mhe.Kanali Simon Anange pamoja na baadhi ya Watendaji wa Wilaya hiyo walipotembelea kukagua utekelezaji wa Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara ( Local Investment Climate -LIC) katika Wilaya hiyo.

Afisa wa Baraza la Biashara la Taifa na Mratibu wa shughuli za Mabaraza ya Biashara Kigoma Bw. Ano Mwamsiku akieleza mafanikio ya mabaraza ya biashara kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Prof.Faustin Kamuzora (hayupo pichani) wakati wa kikao cha pamoja na Watendaji wa Wilaya ya Kasulu walipotembelea kupata taarifa za utekelezaji wa miradi ya LIC.

Baadhi ya wajumbe wa kikao cha kupokea taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya Umwagiliaji ya mashamba ya mpunga ya Titye inayofadhiliwa na Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (Local Investment Climate -LIC) Wilayani Kasulu Mkoani  Kigoma.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Prof.Faustin Kamuzora (mwenye koti jeusi) akipokea maelezo kutoka kwa Fundi Sanifu Bw.Godfrey Rwekiza kuhusu mfereji wa umwagiliaji wa Titye unaotoa maji kutoka mto ruchugi wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa mradi wa umwagiliaji katika mashamba ya mpunga ya Titye Wilayani Kasulu mkoani Kigoma Nobemba 8, 2018.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Prof.Faustin Kamuzora (mwenye koti jeusi) akipokea maelezo kutoka kwa Fundi Sanifu Bw.Godfrey Rwekiza kuhusu banio la maji la mfereji wa umwagiliaji wa Titye unaotoa maji kutoka mto ruchugi wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa mradi wa umwagiliaji katika mashamba ya mpunga ya Titye Wilayani Kasulu mkoa wa Kigoma.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Prof.Faustin Kamuzora akuzungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara yake katika mradi wa Umwagiliaji wa Titye Wilayani Kasulu Kigoma.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.