Monday, November 26, 2018

SERIKALI YAZINDUA VIZA NA VIBALI VYA UKAAZI VYA KIELEKTRONIKI

  
*Yawataka watakaopewa kufanya shughuli zilizoelekezwa kwenye vibali vyao

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amezindua huduma za viza na vibali vya ukaazi vya kielektroniki na amewataka watu wote watakaopewa vibali hivyo kutii sheria kwa kufanya shughuli ambazo wameelekezwa kwa mujibu wa vibali vyao na si vinginevyo.

Amesema utoaji wa huduma hizo ni miongoni mwa jitihada za Serikali katika kuvutia uwekezaji, hususan katika sekta ya viwanda kwani hatua hiyo itarahisisha upatikanaji wa vibali hivyo kwa raia wa kigeni na kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Novemba 26, 2028) wakati akizindua huduma za viza na vibali vya ukaazi vya kielektroniki katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na kwamba hatua hiyo itasaidia kuondoa urasimu na ucheleweshwaji wa huduma pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi.

Amesema Idara ya Uhamiaji inatarajia kuanza kutoa huduma tajwa kwa raia wa kigeni muda wowote kuanzia sasa na kwa kupitia huduma hiyo, raia wa kigeni wataweza kuomba vibali hivyo kwa njia ya kielektroniki wakati wowote na mahali popote walipo.

Waziri Mkuu amesema watakaopewa vibali wanatakiwa kufanya shughuli zao kwa mujibu wa vibali vyao kwa sababu kufanya shughuli tofauti na ilivyoainishwa kwenye kibali ni kosa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Uhamiaji.

Amesema matumizi ya mtandao katika utoaji wa huduma za viza na vibali vya ukaazi ni hatua ya mfano, kwani inakwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia na sera ya Serikali ya matumizi ya TEHAMA katika shughuli za Serikali (e-government).

Amesema Serikali inatarajia kuwa, matumizi ya mifumo hiyo itaongeza ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa kuwa mteja ataweza kulipia huduma hizo mwenyewe moja kwa moja pasipo kupitia kwa mawakala au mtu yeyote.

“Natoa wito kwa Maafisa, Askari pamoja na Watumishi wote wa Idara ya Uhamiaji kuhakikisha kuwa mifumo hiyo inatunzwa pamoja na kuendeleza miundombinu yote ya kiutendaji.” 

Waziri Mkuu amesema kwa kuzingatia ahadi ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ya kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na raia wa kigeni, Maafisa Uhamiaji wanatakiwa kutoa huduma hiyo kwa wakati, weledi na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Uhamiaji.

Amesema mfumo wa huduma hizo utaunganishwa na mifumo mingine ya Serikali, ambayo inatoa huduma kwa wananchi na wageni kama vile Mifumo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Idara ya Kazi – Ofisi ya Waziri Mkuu, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mfumo wa Malipo ya Serikali Kimtandao (GePG). 

 (mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.