Saturday, November 3, 2018

WIZARA, MIKOA ONDOENI VIKWAZO UJENZI WA VIWANDA-MAJALIWA


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka Wizara zinazohusika na masuala ya viwanda, Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na sekta binafsi watambue na waondoe vikwazo na urasimu dhidi ya ujenzi na ustawi wa viwanda nchini.

Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage ampelekee taarifa ya hatua iliyofikiwa juu ya kampuni ya Budget Motors walioomba kibali cha kutengeneza na kuunganisha bodi za mabasi tangu mwaka jana na hawajajibiwa.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Novemba 3, 2018) wakati akifunga wiki ya maonesho ya viwanda yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Sabasaba katika kata ya Picha ya Ndege, Kibaha mkoani Pwani. Amesena uwepo wa viwanda nchini unatoa ajira nyingi.

“Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imeamua kujenga uchumi wa viwanda utakaokuwa mhimili mkuu wa maendeleo ya Taifa na wananchi, hivyo itaendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha ajenda ya ujenzi wa viwanda inafanikiwa.”

Amesema katika kupunguza vikwazo na kuboresha sera nchini, Rais Dkt. Magufuli ameweka msukumo wa kutosha ili kurahisisha na kuondoa ukiritimba kwenye shughuli zote za kibiashara, lakini pia katika kuboresha sera za Taifa za kodi ili kulinda viwanda vya ndani

Waziri Mkuu amesema umuhimu wa viwanda umetokana na Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015/2020 ambayo inaielekeza Serikali kuweka nguvu katika ujenzi wa viwanda ili kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025.

Amesema kwa msingi huo, Rais Dkt. Magufuli alitoa msukumo wa sekta binafsi nchini kuanzisha viwanda vinavyotumia malighafi zinazozalishwa nchini kutokana na mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na maliasili, vikiwemo viwanda vya nguo, sabuni, korosho na matunda.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa uwepo wa viwanda nchini utasaidia kuongeza wigo wa mapato ya Serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali. “Huu ndio mwelekeo wa Serikali ya awamu ya tano unaolenga kuifikisha nchi kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.”

Kuhusu suala la kampuni ya Budget Motors, Wiziri Mkuu amesema ifikapo Ijimaa (Novemba 9, 2018) Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji awasilishe taarifa kuhusu suala hilo la kibali. “Huu ni urasimu, ni bora apewe atengeneze na akikosea arekebishwe.”

Kampuni ya Budget Motors inadai kuwa iliomba kibali cha kuwa na uthibitisho wa kutengeneza na kuunganisha bodi za mabasi kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kwa takribani mwaka mmoja bila ya kujibiwa. Walitoa malalamiko hayo kwa Waziri Mkuu alipotembelea banda lao.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa rai kwa taasisi zenye miradi mbalimbali nchini pamoja na wananchi kuthamini na kuzitumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya hapa nchini zikiwemo na za viwanda vya mkoa wa Pwani kwani zina viwango vya ubora.

“Wakati natembelea mabanda kwenye maonesho haya nimeshuhudia bidhaa nyingi nzuri na zenye ubora. Nimeona wazalishaji wa saruji, mabati, nondo, marumaru, mabomba ya plastiki, chuma, zana za kilimo, vyakula, vinywaji na vifungashio.”

Waziri Mkuu amesema kupitia maonesho hayo ya viwanda vilivyopo katika mkoa wa Pwani vimeudhihirishia umma kuwa vina uwezo mkubwa wa kuzalisha bidhaa zilizo bora na hata kuzidi zile zinazoingizwa kutoka nje, amewahamasisha wananchi kutumia bidhaa za ndani.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo ameiagiza mikoa yote nchini kuhakikisha inatumia bidhaa zinatengenezwa na viwanda vya ndani katika miradi mbalimbali ya ujenzi wanayoitekeleza kama ujenzi wa hospitali za wilaya na vituo vya afya.

Amesema Wakuu wa Mikoa ni lazima wahakikishe bidhaa kama saruji, nondo, marumaru, mabati zinavyotumika katika ujenzi ziwe vimezalishwa na viwanda vya ndani kwa sababu vina viwango vya ubora unaotakiwa na pia itasaidia kuondoa tatizo la soko la bidhaa hizo.

Naye,Waziri Mwijage amewataka watendaji wanaohusika na masuala ya viwanda kutoweka vikwazo kwa wawekezaji ambao wanakwenda katika ofisi zao kwa ajili ya kutafuta maeneo ya kuwekeza kwenye viwanda au wanaohitaji vibali kwani jambo hilo halina tija.


(mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.